Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumatatu, 15 Februari 2016 10:32

Ulimwengu wa Michezo, Feb 15

Ulimwengu wa Michezo, Feb 15

Iran yainyeshea Iraq na kuizaba China katika Futsal

Timu ya taifa ya Iran ya mchezo wa soka ya ukumbini maarufu kama futsal imeendeleza wimbi la mabao wikendi hii katika Mashindano ya Mabingwa wa Futsal nchini Uzbekistan. Ilikuwa mvua ya mabao Jumapili katika Uwanja wa Taifa wa Uzbekistan katika mchuano kati ya Iran na Iraq. Iran iliinyeshea Iraq mabao 13-2, nyota wa mechi hiyo akiwa kiungo Hossein Tayebi aliyetikisa nyavu za Wairaqi mara 4.

Kabla ya kichapo hicho cha mbwa dhidi ya Iraq, Iran awali ilikuwa imeisasambua China mabao 7-0 katika mashindano hayo ya kieneo. Katika mchuano huo wa Ijumaa katika uwanja wa Universal katika mji mkuu wa Uzbekistan, Tashkent, vijana wa Iran ambao siku mbili kabla ya hapo walikuwa wameilaza Jordan mabao 6-0, walionyesha mchezo mzuri katika kipindi chote, huku Muhammad Taheri akifunga bao la mapema zaidi tangu mashindano hayo ya kieneo yaanze, kwa kucheka na nyavu za Wachina sekunde nane baada ya kuanza mchezo.

Wengine waliofunga mabao ya Iran siku hiyo ni Asghar Hassanzadeh, Hamid Ahmad, nahodha Muhammad Keshavarz, Hussein Tavebi huku Ghodrat Bahadori akipiga msumari wa mwisho kwenye jeneza la China. Iran, China, Iraq na Jordan zipo katika Kundi B kwenye mashindano hayo yaliyoandaliwa na Shirikisho la Futsal barani Asia huku kundi A likijumuisha mwenyeji Uzbekistan, Kygyzstan, Lebanon na Saudi Arabia. Timu za Kundi C ni Taipei, Tajikistan, Thailand na Vietnam huku Kundi D ikizileta pamoja Australia, Japan, Malaysia na Qatar. Timu 5 bora zitakazoibuka kidedea katika mashindano hayo ya Asia Futsal Championship yanayofanyika kati ya Februari 10 na 21 nchini Uzbekistan, zitajikatia tiketi ya kushiriki Kombe la Dunia la Futsal baadaye mwaka huu nchini Colombia.

Binti wa Kiirani ateuliwa Mchezaji Bora wa Dunia-Futsal

Huku hayo yakijiri, Fereshte Karimi, bingwa wa mchezo wa futsal wa Kiirani ameteuliwa kuwania tuzo ya Mchezaji Bora wa Kike Duniani wa mchezo huo mwaka jana 2015. Karimi mwenye umri wa miaka 26 ambaye kwa sasa anakipiga katika klabu ya Daneshgah Azad, atalazimika kuchuana na wenzake 9 ili kutwaa taji hilo la kimataifa. Karimi ameteuliwa kwa kufanya vyema katika mashindano ya Wanawake ya Futsal Championship yaliyofanyika nchini Malaysia Septemba mwaka jana 2015.Kwa mujibu wa mtandao wa tuzo za Futsalplanet, wachezaji wengine walioteuliwa kuwania ubingwa wa mchezo huo kwa upande wa wanawake duniani ni Amanda Lyssa (Brazil), Ana Patricia (Ureno), Lucileia Renner (Brazil), Caroline Da Silva (Brazil), Daniela Sofia (Ureno), Aleksandra Samorodova (Russia), Tatiane Debiasi (Brazil), Vanessa Cristina (Italia) na Vanessa Sotelo (Uhispania). Wakati huo huo, Farzaneh Tavasoli ameteuliwa kuwania tuzo ya mlinda lango bora wa kike duniani wa mchezo wa futsal. Wengine ni Ana Catarina Silva Pereira wa Ureno, Mhispania Belén De Uña Marzo, Gabriella Gonçalves wa Italia, raia wa Russia Anastasia Ivanova, Joziane de Oliveira na Missiara Luiza Papst wa Brazil, Karen Julieth Murillo Rey wa Colombia and mchezaji wa Kihispania Vanessa Barberá Martínez. Mataji ya dunia ya Futsalplanet yanahesabiwa kuwa tuzo zenye thamani kubwa zaidi katika mchezo wa futsal.

Kocha wa timu ya soka ya Iran ajiuzulu?

Rais wa Shirikisho la Soka nchini Iran, Ali Kaffashian amesema mkufunzi wa timu ya taifa ya soka ya Iran, Carlos Queiroz hatajiuzulu kama ilivyotangazwa hapo awali na vyombo vya habari vya hapa nchini. Kaffashian amesema Queiroz ataendelea kuwanoa vijana wa Iran ambao wanajiandaa kushiriki michuano ya kufuzu Kombe la Dunia mwaka 2018. Siku ya Ijumaa, kocha huyo wa Kireno alitangaza kujiuzulu wadhifa huo kutokana na kile alichokitaja kuwa 'mashinikizo'. Raia huyo wa Ureno alisema amechukua uamuzi huo ili kulinda jina la Rais wa Shirikisho la Soka Iran, Ali Kafashian; ambaye angelaumiwa na wanasoka na taifa kwa ujumla iwapo angemfuta kazi kocha huyo. Queiroz mwenye umri wa miaka 62 alisema alikabidhi barua yake ya kujiuzulu Jumamosi iliyopita na kwamba ataacha rasmi kuinoa timu ya taifa ya mpira wa miguu ya Iran Aprili 30. Rais wa Shirkisho la Soka la Iran amesema kocha huyo atasalia Melli na kwamba matakwa na maombi yake yatashughulikiwa. Itakumbukwa kuwa, Carlos Queiroz alitangaza kujiuzulu kama kocha wa timu ya taifa ya soka Iran baada ya Iran kufungwa na Bosnia Herzegovina mabao 3-1 katika Kombe la Dunia nchini Brazil mwaka 2014. Carlos Queiroz aliwahi kuwa kocha msaidizi wa Manchester United katika kipindi cha ukocha wa Sir Alex Ferguson mapema katika muongo wa 90. Alichukua uongozi wa Timu ya Taifa ya Iran mwaka 2011 na kuiwezesha kufika fainali za Kombe la Dunia Brazil mwaka 2014. Aidha aliiwezesha timu hiyo kuisasambua Kisiwa cha Guam mabao 6-0 Novemba mwaka jana, katika mchuano wa kuwania kufuzu Kombe la Dunia mwaka 2018.

Kenya yapata msimamizi mpya wa soka

Huenda kiwango cha soka nchini Kenya ambacho kilikua kinazidi kudidimia kikaimarika tena baada ya Shirikisho la Soka nchini humo FKF kupata rais mpya. Nick Mwendwa anakuja kurithi mikoba ya mkuu wa miaka mingi wa FKF, Sam Nyamwea ambaye alijiondoa kwenye kinyang’ayiro cha kutetea kiti chake dakika za mwisho. Mwanaspoti wetu wa Nairobi Suleiman Yeri amefuatilia habari hiyo na kututumia ripoti hii..

Mwandishi wa habari za michezo TZ ala kichapo

February 10 habari za kiungo wa Simba Mwinyi Kazimoto kutuhumiwa kumpiga mwandishi wa habari wa gazeti la MwanaSpoti la Tanzania Mwanahiba Richard zimezidi kuibua gumzo miongoni mwa wanaspoti, wadau wa uanahabari na wananchi kwa jumla. Imearifiwa kuwa, mchezaji huyo wa Simba tayari amefunguliwa kesi baada ya kisa hicho kuripotiwa katika kituo kikuu cha polisi Shinyanga. Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) limelaani kupigwa na kuumizwa kwa mwandishi huyo. Mwenyekiti wa Jukwaa hilo, Theophil Makunga amesema mwandishi huyo alipigwa na mchezaji wa Klabu ya Simba Mwinyi Kazimoto wakati akitimiza majukumu yake Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga Jumatano wiki iliyopita.

Msimamo wa Ligi ya Premier

Kurejea ulingoni kiungo Danny Welbeck ambaye alikuwa anauguza jeraha tangu Aprili mwaka jana, kuliinusuru Arsenal ambayo ilipata ushindi wa dakika za mwisho katika mchuano wa kufana wa Ligi Kuu ya Uingereza Jumapili hii dhidi ya Leicerster. Welbeck aliwapa wabeba bunduki bao hilo la ushindi katika sekunde za mwisho kabla ya kupigwa kipenga cha kumaliza mchezo, ikizingatiwa kuwa mchuano huo ulikuwa unaelekea kumalizika kwa sare ya bao 1-1.

The Foxes ndiyo ilikuwa ya kwanza kucheka na nyavu za mwenyeji wake Arsenali waliokuwa wakiupiga nyumbani Emirates mbele ya mashabiki zaidi ya 60 elfu, kupitia mkwaju tata wa penati uliofungwa na Jamie Vardy.

Theo Walcott hata hivyo alifanya mambo kuwa sare ya 1-1 kunako dakika ya 70. Licha ya kichapo hicho, Leicerster wanasalia kileleni mwa jedwali la Ligi ya Premier wakiwa na pointi 53 huku pointi tatu walizoondoka nazo vijana wa Gunners zikiwafanya kufikisha alama 51 wakiwa katika nafasi ya tatu, ponti ilizonazo Tottenham iliyoko katika nafasi ya pili ingawa ina wingi wa mabao. Vijana wa Spurs waliwatandika Man City mabao 2-1, kichapo ambacho kinawafanya vijana wa City wasalie na pointi 47 wakishikilia nafasi ya nne. Mashetani Wekundu wa Man U ambao walikung’utwa mabao 2-1 na timu nambari 19 kwenye msimamo wa ligi, yaani Sunderland, kwa sasa wanalazimika kurithika na nafasi ya 5 wakiwa na pointi 41.

………………… TAMATI…………………..

 

 

 

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)

Hadithi ya Uongofu (39)

Ni matarajio yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji na tunakutana tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. …

Ufeministi, Itikadi na Misingi yake (26)

Assalaamu Alaykum wafuatiliaji wa kipindi hiki na karibuni kuwa nasi katika sehemu nyingine ya kipindi hiki kinachokosoa itikadi ya ufeministi …

Ulaji wa Lishe Bora katika Kipindi Chote cha Maisha

Wataalamu wa Afya wanasema kuwa, awamu mbalimbali za maisha zinahitajia ulaji wa chakula wa aina tofauti. Iwapo wewe ni mtoto, …

Maua mawili ya Mtume wa Allah (31) Sauti

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh Karibuni wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili Radio Tehran na wasomaji wa mtandao …