Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumatatu, 08 Februari 2016 11:33

Ulimwengu wa Michezo, Feb 08

Ulimwengu wa Michezo, Feb 08

Kiongozi na Wanamichezo

Mwanzoni mwa wiki hii vyombo vya habari hapa nchini viliangazia habari ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kuonana na waendeshaji wa "Kongamano la Mashahidi Wanamichezo Nchini Iran".
Katika mkutano huo, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei alipongeza ubunifu wa kuvutia wa kuwaenzi mashahidi wanamichezo nchini Iran na kusisitiza kuwa: Ni jambo la lazima kuifanya jamii nchini ielewe ni kwa kiasi gani watu wa kila namna walivyojitolea muhanga maisha yao katika njia ya dini na Mapinduzi ya Kiislamu na kwamba watu hao hawakutoka katika tabaka fulani tu la watu, bali watu wa matabaka yote wameshiriki kwenye jambo hilo adhimu la kimaanawi. Amesema suala la kuwaenzi mashahidi wanamichezo nchini linazitia nguvu nyoyo na kuimarisha fikra ya kimapinduzi na kuongeza kuwa: Kijana mwanamichezo ni kigezo kwa sehemu kubwa ya tabaka la vijana; na maadili, mwenendo na mtindo wake wa maisha unaweza kuwa na taathira kwa vijana na unaweza kuiongoza jamii kuelekea kwenye kuthamini mambo ya kidini, kimaadili na kimaanawi. Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amelitaja neno la lugha ya Kifarsi la "Pahlevan" kuwa ni lakabu yenye ubora wa namna yake katika fasihi ya jadi na ya kitaifa kwa Iran na huku akiwaenzi wanamichezo ambao wanafanya vitendo vizuri katika maeneo yao ya michezo amesisitiza kuwa: Fakhari kubwa zaidi inayopindukia fakhari ya kuimbwa wimbo wa taifa au kupandishwa juu bendera ya nchi baada ya kupatikana ubingwa katika medani fulani ya michezo, ni kitendo cha mwanamichezo ambaye anakataa kupigana mweleka na mpinzani Mzayuni au yule mwanamichezo wa kike ambaye anasimama juu ya jukwaa la ubingwa akiwa amevaa "chadoro" au hijabu kamili ya Kiislamu.

………………… …………… 

Iran: Saudia iache kuweke siasa katika masuala ya michezo

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeitaka Saudi Arabia kukoma kuingiza siasa katika masuala ya michezo yanayohusu nchi mbili hizi. Hussein Amir Abdullahian, Naibu Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran ameikosoa Saudia kwa kujaribu kuanzisha sera ya uhasama kati ya nchi mbili hizi katika mawanda ya spoti. Abdullahian amelitaja kama kisababu lemavu, ombi la Shirikisho la Soka la Saudi Arabia kulitaka Shirikisho la Soka Barani Asia AFC, kuandaa michuano kati ya nchi mbili hizi katika nchi ya tatu. Shirikisho hilo la Saudia lilidai kuwa, huenda michuano yake dhidi ya Iran hapa Iran ikavurugika kutokana na sababu za kiusalama, jambo ambalo Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amelipuuzilia mbali na kusisitiza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ndiyo nchi salama zaidi katika eneo. Shirikisho la Soka barani Asia limezipa pande mbili hizo hadi Machi 15 kuutafutia ufumbuzi mgogoro huo. Iran imetishia kujiondoa kwenye michuano ya AFC, iwapo Saudia itaendelea kuweka siasa kwenye masuala ya spoti. Ni vyema kuashiria hapa kuwa, utawala wa Aal-Saud Januari 3 ulitangaza kukata uhusiano wake wa kidiplomasia na Iran, baada ya kufanyika maandamano nje ya ubalozi wake mjini Iran na ubalozi mdogo mjini Mashhad, kulalamikia hatua ya utawala wa kifalme wa nchi hiyo kumuua shahidi mwanachuoni mashuhuri wa Kiislamu nchini humo, Sheikh Nimr Baqir al-Nimr.

Muirani bingwa wa 'squash' barani Asia

Muirani Alireza Shameli ametangazwa kuwa bingwa wa mchezo wa skwoshi barani Asia, kutokana na rekodi nzuri aliyoonyesha katika Mashindano ya Kimataifa ya Mabingwa wa Squash nchini Malaysia mwaka jana. Shirikisho la Skwoshi la Asia limemtangaza barobaro huyo wa Iran kuwa mwanaspoti bora barani kwa namna alivyong'ara katika duru ya 9 ya mashindano hayo yanayofahamika kama Redtone Squash Championship, yaliyofanyika mjini Kuala Lumpar. Shameli ameteuliwa bingwa wa mchezo huyo kitengo cha vijana wenye umri chini ya miaka 17, kwa kujizolea pointi 1,149.40. Mcheza skwoshi huyo wa Iran anafuatwa na Law Yat Long wa Hong Kong mwenye pointi 1,092.2 huku Eugene Heng wa Malaysia na Kashif Asif wa Pakistan wakishika nafasi za tatu na nne kwa alama 972 na 900 kwa utaratibu huo. Katika kitengo cha vijana wenye umri usiozidi miaka 19, Muirani Sajad Zareian ametangazwa kuwa wa tatu akiwa na pointi 1,149.4 nyuma ya Abhay Sing wa India huku bingwa wa kitengo hicho akiwa Mjapani Ryunouke Tsukue mwenye pointi 1,215. Mashindano ya Kimataifa ya Mabingwa wa Squash nchini Malaysia yaliyowavutia wanakwoshi 500 wa bara hili, yalifanyika kati ya Disemba 1 hadi 6 mwaka jana mjini Kuala Lumpur.

………………….. ………………..

CHAN: DRC Mabingwa wa soka Afrika

Timu ya taifa ya soka ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo imetwaa ubingwa wa Michuano ya Mabingwa wa Soka katika Mataifa ya Afrika maarufu kama CHAN baada ya kuitia skulini Mali kwa kuisasambua mabao 3-0. Katika kitimutimu hicho cha fainali kilichofanyika katika uwanja wa taifa wa Amavubi mjini Kigali, Rwanda, vijana wa DRC walionyesha mchezo mzuri katika takriban kipindi chote na hatimaye kutwaa Kombe la CHAN kwa mara ya pili, tangu michuano hiyo ya kibara ianzishwe mwaka 2009. Nyota wa mchuano huo alikuwa kiungo Mechak Elia ambaye alicheka na nyavu za Mali mara mbili, huku mshambuliaji Jonathan Bolingi akifunga bao moja.

Ushindi huo wa pili kwa Kongo DR chini ya mkufunzi Florent Ibenge kwa wachezaji wanaocheza ligi za ndani ya Afrika umeingia katika madaftari ya kumbukumbu. Huku hayo yakijiri, Kodivaa imemaliza katika nafasi ya tatu katika michuano hiyo baada ya kuichabanga Guinea Mabao 2-1 katika kindumbwendumbwe cha kumtafuta mshindi wa tatu. Rais wa Rwanda Paul Kagame alikuwa katika uwanja wa Amavubi kuwatuza vijana wa DRC, ingawa alitamani taji hilo lingetwaliwa na wenyeji wa mashindano hayo vijana wa Amahoro. Mbali na taji hilo, DRC wametia kibindoni dola laki 7 na elfu 50 za Marekani, huku Mali na Ivory Coast zikiondoka na dola laki 4 na dola laki 2 na nusu za Marekani kwa usanjari huo. Kenya itakuwa mwenyeji wa michuano ijayo ya CHAN mwaka 2018.

………………… ………………

Ligi ya Premier

Ligi Kuu ya Soka ya Uingereza imeendelea kuroroma wikendi hii kwa kushuhudia miamba ya soka ya EPL ikitoana jasho. Mechi mbili muhimu zimepigwa Jumapili hii ya February 7, ambapo Bournemouth walikuwa wenyeji wa wabeba bunduki wa Arsenalkatika uwanja wao wa nyumbani, wakati Chelsea  walikuwa wenyeji wa Man United nyumbani Stamford Bridge. Chelsea ambao bado wapo katika kipindi cha mpito chini ya kocha wao wa muda Guus Hiddink, wamefanikiwa kutoa sare ya goli 1-1, baada ya Man United kufunga goli la uongozi dakika ya 61 kupitia kwa kiungo Jesse Lingard. Wakati Man United wakiwa na matumaini ya kuondoka na point tatu, Chelsea walifanikiwa kusawazisha goli kunanko dakika ya 90 kupitia Diego Costa na mchuano huo kuishia kwa timu hizo kugawana point moja moja.  

Wakati ambapo mashetani wekundu walikuwa wanalazimishwa sare hiyo na the blues, Arsenal ilikuwa inajipatia ushindi laini wa mabao 2-0 dhidi ya Bournemouth katika uwanja wa The Goldsands Vitality. Mabao ya Mesut Ozil la dakika ya 23 na la Oxlade-Chamberlain dakika moja baadaye yaliwatosha vijana wa Wenger kupata alama tatu muhimu na sasa wapo hapa kwa hapa na mahasimu wao wa mjini London Tottenham.

Huku hayo yakijiri, Liverpool ilikuwa inalazimishwa sare ya mabao 2-2 na Sunderland wakati ambapo Everton ilikuwa inainyoa Stoke City bila maji kwa kuicharaza mabao 3-0. Southampton na New Castle zilizishukia Westbrom na Westham bao 1-0 huku Norwich ikikubali kichapo cha mabao 2-0 kutoka kwa Aston Villa. Kwa matokeo hayo, Leicerster ambao waliitandika Man City mabao 3-0 wikendi hii wanasalia kileleni mwa msimamo wa ligi wakiwa na pointi 53 huku Arsenal na Tottenham wakibanana katika nafasi ya pili na tatu wakiwa na pointi 48 kila mmoja ingawa wanatofautiana kwa mabao.Man City kwa sasa hawana budi kuridhika na nafasi ya 4 wakiwa na pointi 47. Man United wapo katika nafasi ya 5 wakiwa na point 41 huku Chelsea ikiwa katika nafasi ya 13 na point 30 wakiwa wamecheza michezo 25 ya EPL.

…………………TAMATI……………….

 

 

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)

Hadithi ya Uongofu (39)

Ni matarajio yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji na tunakutana tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. …

Ufeministi, Itikadi na Misingi yake (26)

Assalaamu Alaykum wafuatiliaji wa kipindi hiki na karibuni kuwa nasi katika sehemu nyingine ya kipindi hiki kinachokosoa itikadi ya ufeministi …

Ulaji wa Lishe Bora katika Kipindi Chote cha Maisha

Wataalamu wa Afya wanasema kuwa, awamu mbalimbali za maisha zinahitajia ulaji wa chakula wa aina tofauti. Iwapo wewe ni mtoto, …

Maua mawili ya Mtume wa Allah (31) Sauti

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh Karibuni wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili Radio Tehran na wasomaji wa mtandao …