Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumatatu, 01 Februari 2016 11:42

Ulimwengu wa Michezo, Februari 01

Ulimwengu wa Michezo, Februari 01

Kung Fu To'a

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imetwaa taji la Mashindano ya Mabingwa wa Kung Fu mtindo wa To'a Barani Asia mwaka huu 2016, kwa kujizolea jumla ya pointi 87. Katika mipambano ya fainali siku ya Ijumaa, wana-kung fu wa kiume wa Iran waling'ara na kutunukiwa medali ya dhahabu, katika mashindano hayo yaliyofanyika katika ukumbi wa michezo wa Imam Hassan Mujtaba AS, katika mji wa Qasre-Shirin, magharibi wa Iran. Vijana wa Kiafghani wa mchezo huo waliambulia nafasi ya pili kwa kupata jumla ya pointi 41 na kuondoka na medali ya fedha, mbele ya vijana wa Pakistan walioibuka wa tatu kwa pointi 21 na kujishindia medali ya shaba. Kadhalika wapiga Kung Fu mtindo wa To’a wa kike wa nchi hii walitwaa taji hilo kwa upande wa wanawake, wakifuatiwa na Afghanistan na Mongolia. Kwa ujumla, Jamhuri ya Kiislamu imetia kibindoni medali 5 za dhahabu katika mtindo wa Mayana, dhahabu 2 katika kitengo cha Gilma na dhahabu moja na shaba moja katika mtindo wa Stick Fight Forms; na hatimaye kutwaa taji la mashindano hayo. Duru ya kwanza ya mashindano hayo ya kieneo iling'oa nanga Januari 25 na kufunga pazia lake Januari 30. (Makumi ya wanakung fu kutoka nchi 22 za bara hili wameshiriki kwenye mashindano hayo, wakiwemo kutoka Iran, Afghanistan, Syria, Kazakhstan, Lebanon, Pakistan, Mongolia, Syria na Tajikistan. To'a ni mtindo wa Kung Fu ulioasisiwa na bingwa wa mchezo huo Muirani Ibrahim Mirzaei miaka ya 1960 na unajumuisha yoga na Kung Fu mtindo wa Shaolin.

Mieleka

Wanamieleka wa Iran wameshinda medali 5 zikiwemo 2 za dhahabu katika mashindano ya kimataifa ya mchezo huo nchini Bulgaria. Muirani Ali Moujerlou wa kategoria ya kilo 86 mtindo wa freestyle, alimzidi hasimu wake Zbigniew Baranowski wa Poland katika mchezo wa fainali na kutwaa medali ya dhahabu. Amir-Reza Amiri aliipa nchi hii medali ya fedha katika kitengo cha kilo 125, baada ya kushindwa kutamba mbele ya Mchina Deng Shudi katika fainali. Mehdi Ibrahimi wa mtindo wa Greco-Roman aliipa nchi hii dhahabu ya pili katika kitengo cha kilo 80 huku Keyvan Rezaei na Amir Hussein wakitwaa medali ya shaba kila mmoja katika kategoria ya kilo 98. Mashindano hayo ya kimataifa ya mieleka yajulikanayo kama Dan Kolov and Nikola Petrov ya mwaka huu wa 2016 yalifanyika katika mji mkuu wa Bulgaria, Sofia kati ya Januari 29 na 31. (Makumi ya wanamieleka wa kike na wa kiume wa mitindo ya Free style na Greco-Roman kutoka Algeria, Armenia, Bulgaria, Canada, China, Misri, Mongolia, Iran, Poland na Venezuela wameshiriki mashindano hayo).  Wakati huo huo, wanamieleka wa Iran ya Kiislamu wamezoa medali kadhaa katika Mashindano ya Kimataifa ya Mieleka ya Paris mwaka huu 2016 nchini Ufaransa. Mwanamieleka wa Iran wa mtindo wa Free Style Reza Atri amejishindia dhahabu katika kitengo cha kilo 57, baada ya kuwalemea Pedro Jesus Me wa Venezuela, Adama Diatta wa Senegal, Batbold Sodnomdash wa Mongolia na Muhispania Levan Metreveli.  Mwakilishi wa Iran katika kategoria ya kilo 74, Hassan Yazdani alilazimika kuwabwaga Mmarekani Michael Perry na Alberto Martinez wa Uhispania ili kutwaa medali ya fedha. Katika kategoria hiyo hiyo, Muirani mwingine Alireza Ghasemi alilimewa na Mfaransa Zelimkhan Hadjiev na kuridhika na medali ya shaba. Duru ya 3 ya Paris International Tournament iliyoandaliwa na Shirikisho la Mieleka la Ufaransa ilianza Januari 29 na kumalizika Januari 31.

Shabaha

Bingwa wa mchezo wa kulenga shabaha kwa bunduki wa Iran, Najmeh Khedmati amejishindia medali ya dhahabu katika mashindano ya mchezo huo ya Asia mwaka huu nchini India kwa kuzuoa alama 205.9. Siku ya Ijumaa, mwanadada huyo wa Iran mwenye umri wa miaka 19 aliibuka mshindi katika kipute cha fainali cha kulenga shabaha mita 10 kwa upande wa wanawake, kilochofanyika katika uwanja wa Dakta Karni Singh katika mji mkuu wa nchi hiyo New Delhi. Hasimu wake raia wa nchi mwenyeji, Ayonika Paul aliibuka wa pili na kutwaa medali ya fedha. Pooja Ghatkar alimpa mwenyeji medali ya shaba, baada ya kuzoa alama 184.5. Mashindano hayo ya Asian Olympic Shooting Qualifying Tournament yalianza Januari 27 na yanatazamiwa kumalizika Februari 3.

Afrika: CHAN

Nchi 8 zimetinga hatua ya robo fainali ya michuano ya kuwania ubingwa wa soka barani Afrika kwa wachezaji wanaocheza barani humo CHAN, katika kindumbwendumbwe kinachoendelea kurindima nchini Rwanda. Wenyeji Rwanda wamelazimika kuyaaga mashindano hayo baada ya kupokea kichapo cha mabao 2-1 kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo katika mchuano wa robo fainali uliopigwa katika uwanja uliokuwa umefurika mashabiki zaidi ya 30,000 wa Amahoro jijini Kigali wikendi hii. DRC ndio waliokuwa wa kwanza kucheka na nyavu za Rwanda kupitia bao la Doxa Gikanji dakika 10 baada ya kuanza mchezo.

Hata hivyo Rwanda walirekebisha kasoro zilizojitokeza katika kipindi cha kwanza, na kulipiza bao hilo kupitia mchezaji Earnest Sugira dakika 11 baada ya kutoka mapumzikoni. Ilibidi timu hizo ziongezewe dakika 30 baada ya dakika 90 za ada kumalizika kwa sare hiyo ya 1-1, na hapo ndipo kitumbua cha mwenyeji Rwanda kikaingia mchanga baada ya Bompunga kuipa DRC bao la ushindi katika dakika ya 113 na kujikatia tiketi ya nusufainali. Kichapo hicho kilikua pigo jingine kwa soka ya Rwanda, haswa ikizingatiwa kuwa vijana hao wa Amavubi walishindwa kufurukuta mbele ya Uganda katika mchuano wa fainali wa Cecafa mwishoni mwa mwaka jana 2015. Huku hayo yakiripotiwa, Kodivaa pia imejikatia tiketi ya nusu fainali ya CHAN baada ya kuisasambua Cameroon mabao 3-0 katika mchuano mwingine wa robo fainali Jumamosi hii. Mabao yote 3 yalifugwa katika muda wa nyongeza, baada ya dakika 90 za kawaida kumalizika bila timu hizo kufungana. Mabao ya Ivory Coast yalifungwa na Koffi Boua (95), Atcho Djobo (dakika 7 baadaye) na Serge N’Guessan dakika 112.

Kwengineko, mlinda lango wa timu ya mpira wa miguu wa Guinea Abdul Aziz Keita, aliwastaajabisha wengi baada ya kufunga mkwaju wa penalti dhidi ya Zambia katika mchezo mwingine wa robo fainali na hivyo kuikatia timu yake tiketi ya nusu fainali ya michuano hiyo. Katika mchuano huo wa Jumapili, timu hizo zilimaliza dakika 90 bila kufungana na pia kushindwa kuona lango la kila mmoja katika dakika 30 za ziada na hivyo mchuano huo kulazimika kuamuliwa ma mikwaju ya penati. Wakati huo huo, Tunisia ambayo imewahi kutwaa taji hilo imeshindwa kusonga mbele baada ya kulazwa mabao 2-1 na Mali na sasa watakabana koo na Kodivaa katika mchuano wa nusu fainali kati kati ya wiki hii. Mabao ya Mali yalifungwa na Aliou Dieng na Abdoulaye Diarra. Hadi sasa Ahmed Akaichi kutoka Tunisia anaongoza katika safu ya ufungaji mabao kwa kutikisa nyavu mara 4, sawa na Chisom Chikatara kutoka Nigeria ambayo imeaga michuano hii.

Tenisi

Mchezaji tenisi nambari moja duniani kwa upande wa wanaume Novak Djokovic amemlaza Andy Murray na kuibuka mshindi wa taji la Australia Opens. Raia huyo wa Serbia mwenye umri wa miaka 28 aliidhihirishia dunia ugwiji wake wikendi hii baada ya kumtandika Murray seti 3-0 za 6-1,  7-5, na 7-6.

Kichapo hicho ni cha 5 kwa Murray raia wa Uingereza, ambaye sasa ameshindwa katika fainali zote 5 alizowahi kushiriki za mchuano Australia Opens; 4 kati yazo zikinyakulia na mtani wake wa jadi Djokovic. Kwa ushindi huo Djokovic amesajili ushindi wake wa 6 mjini Melbourne na sasa yuko katika safu moja na bingwa wa zamani Roy Emerson kutoka Australia. Murray naye mwenye umri wa miaka 28, sasa ameingia katika madaftari ya kumbukumbu kwa kushindwa katika fainali 5 za Grand Slam za tenis tangu kuasisiwa kwa mashindano hayo ya wazi mwaka wa 1968.

Dondoo

Sasa ni rasmi kuwa nyota wa soka raia wa Tanzania Mbwana Ally Samatta amejiunga na klabu ya KRC Genk ya Ubelgiji baada ya mvutano wa muda mrefu kati yake na Mosie Katumbi, mmiliki wa klabu anayoondoka ya TP Mazembe,ya DRC. Katumbi alimtaka Samatta aende akaichezee klabu ya FC Nantes ya Ufaransa, baada ya kutoridhishwa na dau la awali lililokuwa limetolewa na KRC Genk ya Ubelgiji.

Wakati huo huo,Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt John Magufuli amempongeza Samatta ambaye ndiye nahodha wa timu ya taifa ya soka ya Taifa Stars, kwa kusajiliwa na klabu ya KRC Genk inayocheza Ligi Kuu ya Ubelgiji. Katika salamu hizo alizotoa kupitia kwa Waziri wa Michezo, Nape Nnauye, Rais Magufuli amesema mchezaji huyo ameijengea heshima na kuitangaza Tanzania kimataifa. Hapa tunanukuu sehemu ya salamu hizo za Magufuli kwa Samatta: “Mafanikio ya Samatta kucheza katika ligi kubwa duniani, yanafungua milango ya wanasoka wengine wa Tanzania kujiunga na timu kubwa duniani, ambako licha ya kujipatia ajira zenye kipato kizuri, kunaiwezesha kuinua soko lake,” mwisho wa kunukuu.

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)

Hadithi ya Uongofu (39)

Ni matarajio yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji na tunakutana tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. …

Ufeministi, Itikadi na Misingi yake (26)

Assalaamu Alaykum wafuatiliaji wa kipindi hiki na karibuni kuwa nasi katika sehemu nyingine ya kipindi hiki kinachokosoa itikadi ya ufeministi …

Ulaji wa Lishe Bora katika Kipindi Chote cha Maisha

Wataalamu wa Afya wanasema kuwa, awamu mbalimbali za maisha zinahitajia ulaji wa chakula wa aina tofauti. Iwapo wewe ni mtoto, …

Maua mawili ya Mtume wa Allah (31) Sauti

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh Karibuni wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili Radio Tehran na wasomaji wa mtandao …