Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumatatu, 25 Januari 2016 10:52

Ulimwengu wa Michezo, Januari 25

Ulimwengu wa Michezo, Januari 25

Ahlan wasahlan wa marhaba mpenzi msikilizaji na haswa shabiki wa spoti ni wasaa mwingine tunapojumuika pamoja katika kipindi chako cha Ulimwengu wa Michezo nikupashe yaliyojiri viwanjani wiki hii ndani na nje ya nchi…..

Binti wa Iran ashinda medali Dubai Marathon

Mwanariadha wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Parisa Arab ameshinda medali ya fedha katika mbio za nyika za Dubai Marathon mwaka huu 2016, katika Umoja wa Falme za Kiarabu. Binti huyo wa Iran alishiriki katika kitengo cha wanawake kwenye mbio za kilomita 10 katika barabara ya Umm Suqeim mjini Dubai na kumaliza wa pili kwa kutumia dakika 37.03. Wakati ambapo mbio hizo za kilomita 10 zilikuwa zinafanyika katika barabara ya Umm Suqeim pambizoni mwa jengo mashuhuri la Burj al-Arab, mbio za kilomita 4 zilikuwa zinafanyika katika barabara ya al-Wasl. Mashindano hayo ya Standard Chartered Dubai Marathon yalifanyika Ijumaa ya Januari 22.

Timu ya handiboli ya Iran yaizamisha Imarati

Timu ya taifa ya mchezo wa handiboli ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeicharaza Umoja wa Falme za Kiarabu na kutinga hatua ya muondoano katika Mashindano ya Mabingwa wa Handiboli ya bara Asia nchini Bahrain. Katika mchezo huo wa Jumamosi jioni, kikosi cha wanaume cha Iran kiliichabanga Imarati mabao 34-32 katika mchuano uliopigwa katika Uwanja wa Michezo wa Khalifa mjini Isa.

Ushindi huo ulikuwa wa tatu kwa timu ya taifa ya Iran ya mpira wa mikono katika mashindano hayo ya kieneo. Awali timu hiyo iliichachawiza China mabao 36-18 Januari 19, na siku mbili baadaye, ikaizamisha Lebanon 31-26. Hata hivyo vijana wa Iran wa mchezo wa handiboli walikubali kichapo kutoka Bahrain na Saudi Arabia katika michuano ya mingine ya Kundi B. Fainali ya mashindano hayo ya bara Asia inatazamiwa kutimua vumbi Januari 28.

Medali ya shaba yamuendelea Muirani kwenye Mashindano ya Karate Japan

Bingwa wa karate wa Iran, Hamideh Abbasali ameshinda medali ya shaba katika duru ya 20 ya Mashindano ya Open de Paris ya Ligi Kuu ya Karate nchini Ufaransa. Katika mpambano wa Jumapili, binti huyo wa Kiirani mwenye umri wa miaka 25 aliibuka kidedea kwa upande wa wanawake kwenye uzani wa kilo 68 katika Uwanja wa Pierre de Coubertin mjini Paris. Karateka huyo wa Iran ya Kiislamu alimlemea Sofia Kloucha wa nchi mwenyeji wa mashindano hayo, katika raundi ya kwanza na kumzamisha Valeria Echever wa Ecuador mara 4-0 katika mchezo wake wa fainali na hivyo kutwaa medali ya fedha. Awali bingwa huyo wa karate wa Iran alikuwa amewapeleka mchakamchaka raia wa Italia na Denmark kabla ya kutwaa medali hiyo. Duru ya 20 ya Mashindano ya Open de Paris ya Ligi Kuu ya Karate yalifungua pazia lake Januari 22 na kumalizika Januari 24 katika mji mkuu wa Ufaransa, Paris. Mashindano hayo ya kimataifa yalivutia mabingwa wa karate 1,012 wa kike na wa kiume kutoka nchi 75 duniani.

Muirani atunukiwa fedha Mashindano ya Basikeli Japan

Hossein Jamshidiyan, bingwa wa mchezo wa kuendesha baiskeli wa Jamhuri ya Kiislamu wa Iran ameshinda medali ya fedha baada ya kuibuka wa pili katika duru ya 36 ya Mashindano ya Uendeshaji Baiskeli barani Asia mwaka huu 2016, mjini Izu nchini Japan. Mwendesha baiskeli huyo wa Iran alimaliza katika nafasi ya pili kwa kutumia sekunde 60.25 nyuma ya raia wa Kazakhstan ambaye aliibuka mshindi kwa kutumia sekunde 45.42. Mwakilishi wa mwenyeji Japan katika mashindano hayo alimaliza katika nafasi ya 3 kwa kutumia sekunde 60.34 na kujishindia medali ya shaba. Ujumbe wa wanaspoti 21 kutoka Iran ya Kiislamu unahudhuria mashindano hayo ya kikanda ambayo yalianza Januari 19 na yanatazamiwa kufunga pazia lake Januari 30.  

Afrika: Soka-CHAN

Michuano ya soka ya mataifa ya Afrika iliendelea kurindima wiki hii; baadhi ya timu zikibanduliwa nje ya mashindano hayo ya kieneo huku zingine zikifanikiwa kusonga mbele. Timu ya Kodivaa imezidi kupata mafanikio katika kipute hicho na sasa imetinga robo fainali ya michuano hiyo baada ya kuibamiza Gabon mabao 4-1 siku ya Jumapili. Mali imepata ushindi wa goli 1-0 dhidi ya Zimbabwe katika kundi D, mchuano ambao ulipigwa mjini Rubavu. Goli hilo la dakika ya 82 lilitiwa kimyani na mshambuliaji Moussa Sissoko.

Kwa ushindi huo Mali sasa inaongoza kundi hilo ikiwa na alama 4 kabla ya kutoana kijasho na Uganda yenye alama 1 na Zambia yenye alama 3. Wakati huo huo Zambia imekata tiketi yake ya robo fainali kwa kuishinda Uganda 1-0 mjini Rubavu. Goli hilo la vijana wa Chipolopolo lilifungwa na mwanasoka wa muda mrefu Christopher Katongo kunako dakika ya 41 ya mchezo. Kwa kichapo hicho Uganda imejiweka katika katika mazingira magumu ya kutinga hatua ya mchujo. Uganda italazimika kushinda mechi yake ya mwisho dhidi ya Zimbabwe na kutegemea Zambia kuishinda Mali ilhali Mali itahitaji tu matokeo ya sare. Morocco, ambayo imefungwa na Rwanda mabao 4-1, pamoja na Gabon ambazo zote ni za kundi A, zimeaga michuano hiyo ya CHAN 2016. Morocco inachukua nafasi ya 3, nayo Gabon inachukua nafasi ya 4. Mpaka sasa Rwanda ndio ipo kileleni mwaa kundi A huku Kodivaa ikiwa katika nafasi ya pili katika kundi hili.

Kombe la Premier

Licha ya kuwa ugenini, lakini mabingwa watetezi wa Ligi Kuu ya soka ya Uingereza klabu ya Chelsea imepata ushindi muhimu sana msimu huu ingawaje ulikuwa wa bao 1-0 dhidi ya wabeba bunduki wa London vijana wa Arsenal. Hata hivyo huenda Arsenal walilambishwa chini kwa kuchapwa bao moja la uchungu, kwa kuwa walilazimika kusakata kabumbu hiyo ya Jumapili wakiwa na nakisi ya mchezaji mmoja, baada ya mlinzi wao Per Mertesacker, kulimwa  kadi nyekundu kwa kumchezea visivyo mshambuliaji wa Chelsea Diego Costa. Upungufu huo ulimfanya kocha Arsene Wenger kumtoa mshambuliaji mahiri Oliver Giroud na kumwingiza mlinzi Gabriel Paulista. Bao ya Chelsea lilifungwa na kiungo huyo Diego Coasta.

Hata hivyo kocha wa The Blues Guud Hiddinks anahisi kupawa kadi nyekundu kiungo huyo wa Gunners kulistahili na ilikuwa ni hatua ya mantiki.

Kwa kichapo hicho Arsenal wamedondoka hadi katika nafasi ya tatu ya msimamo wa ligi, wakiwa na alama 44. Man City ambayo ililazimishwa sare ya mabao 2-2 na West Ham ipo katika nafasi ya pili ikiwa na pointi 44 nyuma ya vinara wa ligi kwa sasa Leicester City ambayo ina alama 47 haswa baada ya kuifanyia mauaji ya Stoke City kwa kuicharaza mabao 3-0. Man U pia kama vile Arsenal, walikabiliwa na wakati mgumu pale walipocheza na Southamptom wikendi hii. Mtoka benchi Charlie Austin alifanikiwa kucheka na nyavu za Mashetani Wekundu dakika saba baada ya kuingia uwanjani na kuifanya iridhike na nafasi ya 5 ikiwa na pointi 37. Katikia matokeo mengine ya Ligi ya Premier Ligi wikendi hii, Liverpool iliilaza Norwhich mabao 5-4 wakati ambapo Aston Villa na Westbrom walikuwa wakilazimishana sare ya 0-0. Mchuano wa Sunderland na Bournmouth uliishia kwa sare ya bao 1-1 wakati ambapo Everton ilikuwa ikipokea kichapo cha mabao 2-1 kutoka Swansea.

 

..........................................TAMATI..........................

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)

Hadithi ya Uongofu (39)

Ni matarajio yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji na tunakutana tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. …

Ufeministi, Itikadi na Misingi yake (26)

Assalaamu Alaykum wafuatiliaji wa kipindi hiki na karibuni kuwa nasi katika sehemu nyingine ya kipindi hiki kinachokosoa itikadi ya ufeministi …

Ulaji wa Lishe Bora katika Kipindi Chote cha Maisha

Wataalamu wa Afya wanasema kuwa, awamu mbalimbali za maisha zinahitajia ulaji wa chakula wa aina tofauti. Iwapo wewe ni mtoto, …

Maua mawili ya Mtume wa Allah (31) Sauti

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh Karibuni wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili Radio Tehran na wasomaji wa mtandao …