Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Alkhamisi, 21 Aprili 2016 09:23

Ushirikiano wa Marekani na Saudi Arabia dhidi ya Hizbullah ya Lebanon

Ushirikiano wa Marekani na Saudi Arabia dhidi ya Hizbullah ya Lebanon
Gazeti la al-Akhbar linalochapishwa nchini Lebanon liliandika jana Jumatano kwamba sheria ya kuiadhibu Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya nchi hiyo Hizbullah iliyopitishwa na Congress ya Marekani na kuidhinishwa na Rais Barrack Obama wa nchi hiyo mwaka mmoja uliopita imeanza kutekelezwa.

Licha ya kuwa chuki ya Marekani na watawala vibaraka wa nchi za Kiarabu dhidi ya Hizbullah ya Lebanon si jambo geni lakini kushadidishwa kwa chuki na uadui wa watawala hao dhidi ya harakati hiyo ya Kiislamu katika mazingira ya hivi sasa ni jambo la kuzingatiwa. Hizbullah ni moja ya makundi yaliyo na athari kubwa katika mapambano ya harakati za Kiislamu dhidi ya maadui wa Uislamu. Wapinzani wakuu wa Hizbullah wakiongozwa na Marekani na Saudi Arabia daima wamekuwa wakitekeleza njama za kukabiliana na kundi hilo la Kiislamu lililo na athari kubwa katika matukio ya Mashariki ya Kati. Chuki na uadui wa nchi hizo dhidi ya Hizbullah umeongezeka sana katika siku za hivi karibuni kufuatia hatua ya harakati hiyo ya Kiislamu ya kuiunga mkono serikali halali ya Rais Bashar al-Asad wa Syria na juhudi zake za kuisaidia isiangushwe na magaidi wanaoungwa mkono na nchi za kigeni. Hivi karibuni Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi na Jumuiya ya Nchi za Kiarabu ambapo Saudi Arabia ina ushawishi mkubwa katika jumuiya mbili hizo, ziliiweka Hizbullah katika orodha ya eti makundi ya kigaidi. Kufuatia hatua hiyo shirika la setalaiti la Nilesat la Misri lilifungamana na jumuiya mbili hizo katika kusimamisha urushaji wa vipindi vya televisheni ya al-Manar inayomilikiwa na Hizbullah. Vilevile Saudi Arabia ambayo ina ushawishi mkubwa katika Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu OIC ambayo ina makao makuu yake huko mjini Jeddah Saudia, ilichochea na kuingiza kipengee cha uadui dhidi ya Hizbullah katika taarifa ya mwisho ya jumuiya hiyo huko mjini Istanbul Uturuki.

wakati huohuo Wizara ya Mambo ya Ndani ya Saudia ilitangaza mwezi Machi uliopita kwamba kila mtu atakayeficha mfungamano wa watu na Hizbullah atachukuliwa kuwa ni gaidi. Kwa mujibu wa sheria iliyotangazwa na wizara hiyo kila mtu anayeishi Saudia na kupatikana kuwa na uhusiano na Hizbullah atafukuzwa nchini humo. Sambamba na kutekelezwa sheria hiyo ya uadui dhidi ya Hizbullah na Saudi Arabia na washirika wake wa Kiarabu katika eneo, Marekani nayo imechukua hatua kama hiyo dhidi ya harakati hiyo ya Kiislamu. Obama hivi sasa yuko ziarani Saudi Arabia kwa ajili ya kuimarisha uadui huo dhidi ya Hizbullah. Kwa mujibu wa sheria ya kuiadhibu Hizbullah, hakuna mtu anayeruhusiwa kuiunga mkono kifedha au vingine harakati hiyo ya Lebanon na ikiwa atapatikana na kosa hilo basi atawekwa kwenye orodha ya watu wanaopaswa kuadhibiwa. Baadhi ya makamanda na viongozi wa ngazi za juu wa Hizbullah akiwemo Sayyid Hassan Nasrullah, Katibu Mkuu wa harakati hiyo na vilevile mashirika ya harakati hiyo na wafanyabiashara wanaotuhumiwa na Marekani kuwa wanashirikiana na Hizbullah, wote wamewekwa kwenye orodha ya watu wanaopasa kuadhibiwa. Televisheni ya al-Manar, Radio Nuru, taasisi na mashirika ya kandarasi, jumuiya za misaada na hata maduka ya mauzo jumla yamewekwa kwenye orodha hiyo, ambapo baadhi ya mashirika hayo yako katika nchi kama vile Brazil, Paraguay, Chile, China, Hong Kong, Lebanon, Marekani, Gambia, Nigeria na Iraq. Wakati huohuo Wizara ya Hazina ya Marekani imezipa baadhi ya taasisi za nchi hiyo jukumu la kufuatilia na kuhakikisha kwamba sheria hiyo inatekelezwa vilivyo na kisha kutoa ripoti kwa Congress ya Marekani.

Kwa kutekeleza sheria hiyo dhidi ya Hizbullah, Marekani imechukua hatua nyingine ya kuiridhisha Saudi Arabia na bila shaka kupata fursa ya kuuzia utawala huo wa Aal Soud silaha zaidi na hivyo kujidhaminia pato la kuendeshea shughuli zake. Licha ya kuzidishwa uadui huo dhidi ya Hizbullah ya Lebanon lakini kama alivyosema Ayatullah Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran, pamoja na kuwepo vitisho vya kimatendo na propaganda chungu nzima dhidi ya Hizbullah leo hii harakati hiyo ya Kiislamu imeimarisha uepo na dhihirisho lake lililokomaa katika ulimwengu wa Kiislamu, na wala kulaaniwa kwake katika karatasi isiyo na thamani yoyote na utawala fasidi na kibaraka hakuna umuhimu wowote.

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)

Hadithi ya Uongofu (39)

Ni matarajio yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji na tunakutana tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. …

Ufeministi, Itikadi na Misingi yake (26)

Assalaamu Alaykum wafuatiliaji wa kipindi hiki na karibuni kuwa nasi katika sehemu nyingine ya kipindi hiki kinachokosoa itikadi ya ufeministi …

Ulaji wa Lishe Bora katika Kipindi Chote cha Maisha

Wataalamu wa Afya wanasema kuwa, awamu mbalimbali za maisha zinahitajia ulaji wa chakula wa aina tofauti. Iwapo wewe ni mtoto, …

Maua mawili ya Mtume wa Allah (31) Sauti

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh Karibuni wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili Radio Tehran na wasomaji wa mtandao …