Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumapili, 10 Aprili 2016 19:42

'Vikosi vya Iran ndivyo pekee vyenye umaanawi'

'Vikosi vya Iran ndivyo pekee vyenye umaanawi'

Amirijeshi Mkuu wa vikosi vyote vya ulinzi vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitizia udharura wa kutiliwa nguvu uwezo wa operesheni za kijeshi na misukumo ya kimaanawi na kidini ya vikosi vya ulinzi vya Iran.

Ayatullah Ali Khamenei amesema hayo leo wakati alipoonana na makamanda waandamizi wa vikosi vya ulinzi vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kuongeza kuwa: Katika mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu, jukumu kuu la vikosi vya ulinzi ni kulinda mipaka na usalama wa taifa, hivyo kuna wajibu wa kuongezwa nguvu na uwezo wa kufanya operesheni za kijeshi na misukumo ya kimaanawi ya vikosi hivyo kadiri inavyowezekana.

Amesema, kielelezo cha "utambulisho wa pamoja" wa vikosi vya ulinzi vya Iran ni kuwa, kwa wakati mmoja vikosi hivyo vina "uwezo wa operesheni za kijeshi" na wakati huo huo vina "misukumo na misimamo ya kimaanawi na kidini."

Ameongeza kuwa: Vikosi vya ulinzi vya Iran si mali ya mtu binafsi au chama na mrengo fulani, bali ni mali ya taifa na nchi nzima na vinapaswa kuwa ngao ya ulinzi na usalama pamoja walinzi wa taifa na wananchi wote.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amegusia kuweko vikosi vya aina mbili vya ulinzi vyenye utambulisho maalumu katika nchi nyingi duniani na kuongeza kuwa: Katika baadhi ya nchi duniani, kuna jeshi na polisi wa kimaonesho, kimapambo na kidhahiri tu bila ya kuwa na uwezo wa kufanya operesheni za kijeshi bali kazi kubwa ya vikosi hivyo ni kulinda serikali na usalama wa watawala tu.

Ayatullahil Udhma Khamenei amesisitiza kuwa: Katika eneo letu hili (la Mashariki ya Kati) viko pia vikosi vya namna hiyo ambavyo baadhi yake kwa muda wa zaidi ya mwaka mmoja sasa vinatumia nguvu zao zote kufanya mashambulizi makubwa dhidi ya Yemen na wananchi wake, na pamoja na hayo hadi leo hii vimeshindwa kufanikisha chochote cha maana.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa: Kuna vikosi vingine vya kijeshi ambavyo kijuu juu vinaonekana kuwa na nguvu kubwa za kufanya opereseheni za kijeshi lakini vinapoingia kwenye medani ya opereseheni vinaonesha mabavu ya kijeshi tu na vinafanya mambo yasiyoingilika akilini na yasiyo na chembe ya huruma; na mfano wa wazi wa jambo hilo ni vitendo vya jeshi la Marekani katika nchi za Iraq na Afghanistan, na wakati vikosi kama hivyo vya ulinzi vinaposhindwa katika medani ya mapambano, havisiti hata chembe kutumia vikosi vya watu waliokubuhu katika kutenda jinai kama vile vikosi vya Black Water.

Amirijeshi Mkuu wa vikosi vyote vya ulinzi vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema, vikosi vya ulinzi vya Iran ndivyo vikosi pekee duniani ambavyo vina misukumo ya kimaanawi na kidini na wakati huo huo vinafanya kazi zake kwa umakini na uwezo wa hali ya juu. Ameongeza kuwa, vikosi hivyo vinafanya kazi katika nchi ya Iran ambayo ina uhuru kamili wa kisiasa.

Amirijeshi Mkuu wa vikosi vya ulinzi vya Iran amesisitiza kuwa: Kazi za jeshi ndani ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran si kazi za kimaonesho na kimapambo tu na pia si kazi za kufanya operesheni zisizodhibitiwa au zisizoingilika akili au zisizojali na kuzingatia pande zote kabla ya kuchukua hatua.

 

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)