Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumamosi, 23 Januari 2016 20:48

Kiongozi Muadhamu akutana na Rais wa China

Kiongozi Muadhamu akutana na Rais wa China

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa: "Mapatano ya marais wa Iran na China kuhusu 'mpango wa miaka 25 wa uhusiano wa kistratijia' baina ya nchi mbili ni hatua sahihi na yenye hekima.

Ayatullah Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameyasema hayo leo Jumamosi mjini Tehran wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Rais Xi Jinping wa China na ujumbe alioandamana nao. Huku akiashiria historia ndefu ya uhusiano wa kibiashara na kiutamaduni baina ya mataifa ya Iran na China, Kiongozi Muadhamu ameongeza kuwa: "Serikali na watu wa Iran wanataka kustawisha uhusiano na nchi zenye kujitegemea na zenye kuaminika kama China."

Ayatullahil Udhma Khamenei amesema "nishati" au kawi ni kati ya masuala muhimu duniani na kubainisha kuwa: "Iran ni nchi pekee yenye kujitegemea katika eneo ambayo katika sekta ya nishati inaweza kuaminika kwani kinyume cha baadhi ya nchi za eneo, sera za nishati Iran haziathiriwi popote na wasiokuwa Wairani."

Kiongozi Muadhamu ameashiria sera za kibeberu za baadhi ya nchi na muelekeo usio wa kuaminika hasa wa Marekani na kuongeza kuwa: "Katika hali kama hii, nchi zenye kujitegemea zinapaswa kushirikiana zaidi na hivyo mapatano ya China na Iran yamefikiwa katika fremu hii na yanapaswa kufuatilliwa kwa uzito."

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amebainisha kuwa, nchi za Magharibi hazijaweza kuvutia imani ya taifa la Iran na kwamba taifa la Iran kamwe halitasahau ushirikiano wa China wakati nchi hii ikiwa katika zama za vikwazo. Kiongozi Muadhamu ameongeza kuwa, "China Moja" ni sera ya kimsingi na isiyopingika ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Kiongozi Muadhamu pia ameelezea masikitiko yake kutokana na ukosefu wa usalama hivi sasa katika eneo. Amesema hali hii imetokana na sera ghalati za madola ya Magharibi na ufahamu potovu kuhusu Uislamu na kwamba hali hiyo inaweza kuzuiwa kwa ushirikiano wenye busara.

Ayatullah Khamenei amesema baadhi ya nchi za eneo ndio chimbuko asili la fikra potovu na kuongeza kuwa: "Badala ya Wamagharibi kukabiliana na chimbuko asili la fikra hizo pamoja na makundi ya kigaidi, wanawahujumu na kuwashinikiza Waislamu Ulaya na Marekani katika hali ambayo ugaidi unakinzana kikamilifu na fikra sahihi za Kiislamu."

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)