Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumatano, 29 Disemba 2010 20:10

Surat Yusuf - Aya ya 19-21

Wapenzi wasikilizaji wa Darsa ya Qur'ani Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Tunamshukuru Allah SW kwa kutuwafikisha kukutana tena katika darsa yetu hii. Sura ya 12 ya Yusuf ndiyo tunayoizungumzia kwa sasa, na hii ni darsa ya 360 tunayoianza kwa aya za 19 na 20 ambazo zinasema:

Ukafika msafara, wakamtuma mchota maji wao, naye akatumbukiza ndoo yake. Alisema: Kheri Inshallah! Huyu hapa mvulana! Wakamficha ili kumfanya ni bidhaa. Na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa wanayoyatenda.
Na wakamuuza kwa thamani duni, kwa akali ya pesa. Wala hawakuwa na haja naye.

Katika Darsa iliyopita tulisema kuwa ndugu zake Yusuf walimtia kisimani ndugu yao huyo na kisha wakaichukua kanzu yake na kuipaka damu ya mnyama. Kisha huku wakijiliza wakaenda kwa baba yao yaani Nabii Yaaqub as na kuonyesha wamepatwa na majonzi makubwa kutokana nay ale yaliyomsibu Yusuf.
Tukirudi huko kisimani alikotiwa Yusuf ni kwamba alibaki humo kwa muda mpaka ukatokea msafara wa watu waliotaka kuteka maji kisimani humo kwa ajili ya kukata kiu yao. Mtu aliyetumwa kwenda kuteka maji hayo alitumbukiza ndoo kisimani. Yusuf alining'inia kamba iliyofungwa na ndoo na kuja juu. Watu hao wa msafara waliomuokota Yusuf walimchukulia mtoto huyo kama mtumwa ambaye walihisi wangeweza kumpeleka kwenye soko la watumwa wakamuuza na kupata pesa nzuri. Kwa hivyo kwa kuchelea asije akatokea mtu mahala hapo akadai kuwa Yusuf ni mtoto wake au milki yake, wakaamua kumficha kwenye bidhaa zao mpaka walipofika kwenye soko la watumwa huko Misri ambako walimuuza kwa bei ya chini kabisa. Na sababu ni kuwa hawakuwa wamesumbuka kumpata mtoto huyo wala kumlipa mtu pesa kwa ajili ya kumchukua. Hakika hivi ndivyo inavyokuwa baadhi ya wakati kwa mtu kukitoa au kukipoteza kirahisi kabisa na bila kukionea uchungu au kujali thamani yake kile ambacho alikipata bila ya kukitokea jasho. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kuwa baadhi ya wakati mtu hutumbukizwa kwenye kisima cha matatizo na mabalaa na watu wake wa damu na wa karibu kabisa, lakini kwa rehma zake Mola akaja akaokolewa na watu baki na wa mbali hata kama pengine bila kukusudia. Funzo jengine tunalopata katika ayah ii ni kuwa baadhi ya watu huwatazama na kuwachukulia wanadamu wenzao kama bidhaa tu na kudharau ile hali ya utu na kiroho ya kiumbe huyo.
Ifuatayo sasa ni aya ya 21 ambayo inasema:

Na yule aliyemnunua huko Misri alimwambia mkewe: Mtengenezee makaazi ya hishima huyu; huenda akatufaa au tukamfanya mwenetu. Na kama hivyo tulimweka Yusuf katika nchi ili tumfundishe kufasiri mambo. Na Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye kushinda katika jambo Lake, lakini watu wengi hawajui.

Wakati watu wa msafara uliomchukua Yusuf walipomnadi mtoto huyo, mjumbe wa mheshimiwa wa Misri akamnunua kijana huyo mwenye sura jamili na kumpelekea bwana wake huyo. Mheshimiwa huyo wa Misri alimchukua kijana huyo hadi nyumbani kwake ili aweze kufanya kazi za nyumbani na pia awe kama kitu cha kumuanisi na kumchangamsha mkewe hapo nyumbani. Sababu ni kuwa hawakuwa na mtoto na hawakuwa na tamaa tena ya kupata mtoto. Mwenyezi Mungu anaeleza kuwa kuja kwa Yusuf nyumbani kwa mheshimiwa wa Misri ulikuwa ndio utangulizi wa kujashika hatamu za utawala kijana huyo na kuthibiti kile alichokiona katika ndoto yake. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kuwa nyoyo za waja ziko mikononi mwa Mwenyezi Mungu. Kwani aliujaza mapenzi ya Yusuf moyo wa mheshimiwa wa Misri kiasi cha kumhisi mtoto huyo kama mwanawe pamoja na kwamba alikuwa mtumwa tu. Funzo jengine tunalopata katika ayah ii ni kwamba si hasha tabu na shida kubwa anazopata mtu mwishowe zikawa na mwisho mwema na kwa hakika huo ndio utaratibu wa Allah sw kwamba 'inna maal usri yusra' au kama walivyosema wahenga'baada ya dhiki si dhiki, baada ya dhiki ya faraji'. Na ndiyo maana Yusuf aliyekuwa ametupwa na kubaki kisimani peke yake na kisha kufanywa mtumwa na kuuzwa Mwenyezi Mungu alimuinua na kumfikisha daraja ya juu ya heshima na utukufu.
Aya ya 21 ndiyo inayotuhitimishia darsa yetu ya juma hili. Aya hiyo inasema:

Na alipo fikilia utu uzima tulimpa hukumu na ilimu. Na kama hivi tunawalipa wanaotenda mema.

Katika kisa cha Nabii Yusuf as Mwenyezi Mungu amezungumzia juu ya hadhi na daraja ya kimaanawi na kueleza kuwa Yusuf alikulia ndani ya nyumba ya mheshimiwa wa Misri. Lakini kutokana na kwamba alikuwa mtu safi, mwema na mwaminifu, wakati alipofikia ukomavu wa kimaanawi na kustahiki kupata rehma mahsusi za Mola kama vile utume na elimu ya mambo ya ghaibu, tulimpa rehma zetu hizo. Huo ndio utaratibu wa Allah sw wa kuwalipa malipo mema waja wema papa hapa duniani. Kwa hakika Mwenyezi Mungu huwachagua mitume wake miongoni mwa watu wa jamii na kuwatahini kwa majaribu na mitihani mbali mbali ili waweze kufikia upeo unaohitajika wa kuweza kubeba na kutekeleza jukumu hilo zito la utume na vile vile ubora na utukufu wao kuweza kudhihirika mbele ya macho ya watu wa jamii zao. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na ayah ii ni kuwa sehemu moja ya elimu walizonazo mitume zinatokana na Mwenyezi Mungu mwenyewe na wala si mambo anayoweza kuyajua mtu kwa kujifunza. Funzo jengine tunalopata hapa ni kuwa kupata hadhi ya kupewa risala ya utume kunategemea ustahiki na daraja anayopasa kufikia mtu ambayo ni Mwenyezi Mungu ndiye ajuaye ni mja wake gani amefikia daraja hiyo. Kadhalika aya inatubainishia kuwa uwezo wa kielimu na kimwili tu havitoshi kumfanya mtu astahiki kupata rehma maalumu za Mwenyezi Mungu. Ni lazima awe mtu mwema pia. Wapenzi wasikilizaji darsa ya 360 inaishia hapa. Tunamwomba Mola atupe yaliyo mema katika dunia hii na atupe yaliyo mema huko akhera na kutulinda na adhabu ya moto.

Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.

Zaidi katika kategoria hii: Surat Yusuf - Aya ya 16-18 »

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)

Hadithi ya Uongofu (39)

Ni matarajio yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji na tunakutana tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. …

Ufeministi, Itikadi na Misingi yake (26)

Assalaamu Alaykum wafuatiliaji wa kipindi hiki na karibuni kuwa nasi katika sehemu nyingine ya kipindi hiki kinachokosoa itikadi ya ufeministi …

Ulaji wa Lishe Bora katika Kipindi Chote cha Maisha

Wataalamu wa Afya wanasema kuwa, awamu mbalimbali za maisha zinahitajia ulaji wa chakula wa aina tofauti. Iwapo wewe ni mtoto, …

Maua mawili ya Mtume wa Allah (31) Sauti

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh Karibuni wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili Radio Tehran na wasomaji wa mtandao …