Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumatano, 29 Disemba 2010 19:57

Surat Yusuf - Aya ya 16-18

Sikiliza

Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Natumai hamjambo wapenzi wasikilizaji wa Darsa ya Qur'ani. Kwa taufiki yake Mola tumekutana tena katika mfululizo mwingine wa kila wiki wa darsa hii ambayo kwa sasa inazungumzia sura ya 12 ya Yusuf. Tunaianza basi darsa yetu hii ambayo ni ya 359 kwa aya ya 16 ambayo inasema:
Wakaja kwa baba yao usiku wakilia.
Katika darsa iliyopita tulisema kuwa kaka zake Yusuf walitekeleza mpango wao waliokuwa wamepanga na hivyo wakamtia ndugu yao ndani ya kisima na kisha wao peke yao wakarudi zao nyumbani kwao. Kama ambavyo ingetarajiwa suala la kwanza ambalo ilitarajiwa Nabii Yaqub awaulize wanawe hao lilikuwa ni kutaka kujua Yusuf yuko wapi. Lakini wakati wanaingia kwao kaka hao walijifanya ni wenye huzuni huku wakitokwa na machozi ili waonyeshe kuwa kutoweka kwa Yusuf kumewauma na kuwahuzunisha kama atakavyokuwa na majonzi baba yao juu ya msiba huo. Aidha kujiliza kwao huko kulikuwa na lengo pia la kufuta ndani ya fikra za baba yao hisia zozote za kushuku kwamba labda kuna jambo baya wamemfanyia ndugu yao. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kuwa si kila aliaye ni mtu wa kuaminika. Kwani si hasha mtu haini na msaliti akajitia kulia na kutoa machozi ya huruma za mamba ili aweze kujitoa hatiani. Funzo jengine tunalopata katika aya hii ni kuwa miongoni mwa mbinu zinazotumiwa na watu waovu ni kucheza na hisia za watu na kutumia nyenzo za kutilisha huruma kama kulia ili kufikia malengo yao.
Ifuatayo sasa ni aya ya 17 ambayo inasema:
Wakasema: Ewe baba yetu! Hakika tulikwenda kushindana na tukamwacha Yusuf penye vitu vyetu. Basi mbwa mwitu akamla. Lakini wewe hutuamini ijapokuwa tunasema kweli.
Kaka zake Nabii Yusuf hawakutosheka na kujiliza kiuwongo bali waliamua kusema na uwongo mkubwa pia kwa kudai kwamba 'wakati sisi tulipokuwa tumekwenda kwenye mchezo wa mashindano, Yusuf yeye alibaki kuangalia vitu vyetu, na kwa kuwa alikuwa peke yake alitokea mbwa mwitu akamla'. Waliyasema hayo huku wakiwa wamesahau kwamba walimtenganisha Yusuf na baba yake kwa hoja kwamba wanataka aende pamoja nao huko jangwani kwa ajili ya burudani na michezo na si kwamba wao waende kucheza na yeye wamweke awalindie vifaa vyao. Kaka hao wakafika mbali zaidi ya uwongo waliotunga kwa kumtuhumua baba yao kwamba hatowaamini pamoja na kuwa wayasemayo ni kweli tupu. Baadhi ya mafunzo yanayopatikana katika aya hii ni kuwa baadhi ya wakati kusema uwongo mmoja huwa sababu ya kusema uwongo mwingine kumi na moja. Katika kujenga hoja kutokana na dhambi waliyotenda kaka zake Yusuf walianza kutapika uwongo mmoja bada ya mwingine bila kuzingatia kwamba matokeo ya kitendo chao hicho yatakuwa ni kuja kufedheheka.
Tunaihitimisha darsa yetu kwa aya ya 18 ambayo inasema:
Wakaja na kanzu yake ina damu ya uwongo. Akasema: Bali nafsi zenu zimekushawishini kutenda kitendo. Lakini subira ni njema; na Mwenyezi Mungu ndiye wa kuombwa msaada kwa haya mnayoyaeleza.
Katika kuendelea na utoaji wao wa ushahidi wa uwongo, kaka zake Yusuf mbali na vilio na maombolezo waliichukua pia kanzu ya ndugu yao waliyoitapakaza damu ya mnyama na kumepelekea baba yao ili iwe kielelezo na kidhibiti madhubuti cha kuthibitishia madai yao kwamba Yusuf alishambuliwa na kuraruliwa na mbwa mwitu. Hata hivyo Nabii Yaaqub ambaye alikuwa mtume wa Mwenyezi Mungu aliyekuwa na utambuzi wa hakika ya yaliyoko nyuma ya pazia alitambua kuwa Yusuf yuko hai, na hivyo hakutekwa wala kuzikubali hila na hadaa za wanawe na hivyo akawaambia:" hayo yote ni matokeo ya husda na matashi yenu ambayo yamekufanyeni mumtendee uovu mliomtendea ndugu yenu Yusuf, na hivyo kututenganisha mimi na yeye. Nyinyi mlidhani kuwa kwa kumweka Yusuf mbali na macho yangu mutakuwa mumemkomoa yeye tu, hali ya kuwa mbali na yeye, mumeniumiza na mimi pia kwa kunifanya nipatwe na huzuni na majonzi ambayo hayatonitulia wala kunifanya nipoe ila kwa auni na msaada wa Mwenyezi Mungu. Yamkini pengine ndoto aliyokuwa ameota Yusuf na kumsimulia baba yake yaani Nabii Yaqub ndiyo iliyomfanya mzazi huyo asichukue hatua yoyote dhidi ya wananwe wala kuhangaika kumtafuta Yusuf mwenyewe. Ndoto ambayo ilimfanya atambue kuwa mwanawe bado yu hai na amesalimika na kila aina ya hatari na kwamba ahadi ya Mwenyezi Mungu iko pale pale ya kuwa atamfikisha kwenye hadhi na daraja ya juu. Na ndiyo maana alizungumzia juu ya majonzi na huzuni zilizompata yeye mwenyewe tu na kusema kuwa 'namwomba Mwenyezi Mungu anipe subra ya kuweza kuvumilia hali hii ya kutengana na mwanangu'. Baadhi ya mafunzo yanayopatikana katika aya hii ni kuwa nafsi iliyochafuka kwa uovu humfanya mtu aione dhambi na ovu alilotenda kuwa ni kitu kizuri na hata kumtayarishia mazingira ya kutafuta hoja ya kuhalalisha dhambi hiyo. Funzo jengine tunalopata katika aya hii ni kuwa matukio yoyote yale yanayotokea kwa namna fulani huwa ni mtihani wa Mwenyezi Mungu na hivyo lazima mtu ajiandae kwayo na kuwa na subra na uvumilivu anapopatwa na masaibu hayo. Kadhalika aya inatuelimisha kuwa subra iliyo njema ni ile ambayo pamoja na moyo wa mtu kuumia na hata kububujikwa na machozi lakini hafikii mahali pa kukufuru neema kwa majaribu yaliyompata, bali humuelekea Mwenyezi Mungu kwa msaada. Kwa haya machache tunaifunga darsa yetu hii. Tunamwomba Mola azijaze nyoyo zetu subra na kutujaalia kuwa washukurivu wa neema zake. Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)

Hadithi ya Uongofu (39)

Ni matarajio yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji na tunakutana tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. …

Ufeministi, Itikadi na Misingi yake (26)

Assalaamu Alaykum wafuatiliaji wa kipindi hiki na karibuni kuwa nasi katika sehemu nyingine ya kipindi hiki kinachokosoa itikadi ya ufeministi …

Ulaji wa Lishe Bora katika Kipindi Chote cha Maisha

Wataalamu wa Afya wanasema kuwa, awamu mbalimbali za maisha zinahitajia ulaji wa chakula wa aina tofauti. Iwapo wewe ni mtoto, …

Maua mawili ya Mtume wa Allah (31) Sauti

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh Karibuni wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili Radio Tehran na wasomaji wa mtandao …