Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumatano, 29 Disemba 2010 19:42

Surat Yusuf - Aya ya 7-10

Sikiliza
Wapenzi wasikilizaji wa darsa ya Qur'ani Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Tunamshukuru Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa kutuwafikisha kukutana tena katika darsa yetu hii. Sura ya 12 ya Yusuf ndiyo tunayoizungumzia kwa sasa, na hii ni darsa ya 357 tunayoianza kwa aya ya 7 na ya 8 ambazo zinasema:
Kwa yakini katika (kisa cha) Yusuf na nduguze yako mazingatio mengi kwa wanaouliza (mambo wapate kujua).
Pale waliposema (ndugu zake): Hakika Yusuf na nduguye wanapendwa zaidi na baba yetu kuliko sisi, hali sisi ni kikundi chenye nguvu. Hakika baba yetu yumo katika upotofu wa dhaahiri.
Katika darsa iliyopita tulisema kuwa kwa mujibu wa aya ya Qur'ani kisa cha Nabii Yusuf kimeanza kusimuliwa kwa ndoto aliyoota Nabii huyo wakati alipokuwa mdogo. Ndoto hiyo ilibainisha nafasi ya juu ya hadhi na utukufu ambaye angeifikia Yusuf AS katika mustakbali wake. Hata hivyo kufikia kwenye daraja hiyo hakuthibiti kwa wepesi na urahisi bali kuna dhoruba, mawimbi na utafani kali zisizo na kifani ambazo wale watafutao haki na hakika inawabidi wazivuke kwanza na kupata ibra na mazingatio ndani yake. Wapenzi wasikilizaji, yale tuliyoyasikia katika aya za mwanzoni za sura hii yalihusu yake yaliyotokea katika ndoto ya Yusuf, ama yaliyoanza kutokea baada ya ndoto hiyo yalikuwa kinyume na hayo. Kaka zake Yusuf ambao walikuwa ndugu zake wa baba mmoja walikuwa wakimwonea husudu yeye na nduguye Benjamin ambao wote wawili mama yao alikuwa mmoja kutokana na walivypokuwa wakipendwa na baba yao, mpaka wakawa wanaelezana wenyewe kwamba: "Baba anawapenda zaidi wawili wale kuliko sisi hali ya kuwa sisi ni vijana mashababi na wenye nguvu. Kwa kweli baba anakosea katika hili." Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kuwa ndani ya Qur'ani kuna mengi ya kumfanya mtu aelewe hakika ya mambo, hata hivyo wanaoweza kufaidika na hayo ni wale walio na nia ya kweli ya kujua hakika ya mambo. Funzo jengine linalopatikana katika aya hizi ni kuwa tujihadhari na jinsi tunavyoamiliana na watoto wetu kwani endapo baadhi yao watahisi wanabaguliwa, moto wa husuda unaweza kufukuta ndani ya nyoyo zao.
Ifuatayo sasa ni aya ya 9 ambayo inasema:
Muuweni Yusuf, au mtupeni nchi ya mbali ili uso wa baba yenu ukuelekeeni nyinyi. Na baada ya haya mtakuwa watu wema.
Hisia potofu walizokuwa wamejengeka nazo ndani ya nafsi zao kaka zake Yusuf kuhusiana na muamala wa upendo na huruma ambao baba yao alikuwa nao kwa Yusuf na nduguye Benjamin ziliwafanya baadhi ya kaka zake hao wafikie hadi ya kupendekeza kwamba lazima watafute njia yoyote ile wamtokomeza ndugu yao huyo ili nao waweze kupata mapenzi ya baba yao. Na kwamba baada ya kufanya watakalolifanya watatubia, na Mwenyezi Mungu atawaghufikia, nao watakuwa watu wazuri. Waliyawaza hayo hali ya kuwa maana ya toba ni kuonyesha majuto kwa dhambi aliyofanya mtu, na si kupata kisingizio cha kufanyia dhambi. Kwani kama mtu atasema wacha sasa nifanye madhambi kisha nitatubia siku za usoni, huko ni mtu kuihadaa nafsi yake tu. Hiyo si sawa na mtu kusema acha nile hiki chakula chenye sumu, kisha nitakwenda kwa daktari na kupata matibabu. Alaa kulli haal mpango wa kumuua Yusuf au kumwacha peke yake huko jangwani ilikuwa ni fikra ya kishetani iliyobainisha husda kubwa waliyokuwa nayo kaka zake juu yake. Hakika nukta hii ni kengele ya hatari kwa kila familia na tahadhari kwa wazazi wote. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kuwa husda ni kitu hatari mno kinachoweza kumfanya mtu afikie hadi ya kuwa tayari kumuua ndugu yake: na hili haliko katika kisa hiki cha Nabii Yusuf tu na kaka zake, bali hata katika kisa cha Habil na Qabil kama kilivyokuja pia ndani ya Qur'ani tukufu husda ilimfanya Qabil atoe roho ya ndugu yake Habil. Aidha aya inatuelimisha kuwa watoto wanahitajia mapenzi ya wazazi wao, na kukosa mapenzi hayo ni hatari kubwa inayoweza kuwasukuma kwenye mambo ya upotofu.
Tunaihitimisha darsa yetu kwa aya ya 10 ambayo inasema:
Akasema msemaji kati yao:Msimuuwe Yusuf. Lakini mtumbukizeni ndani ya kisima. Wasafiri watakuja mwokota: kama nyinyi mna sharti ya kufanya jambo.
Kutokana na kwamba moto wa husuda uliokuwa ukifukuta ndani ya nyonyo za kaka zake Yusuf ulitofuatiana kati ya mtu na mtu, kwa wengine kuwa mkali na kwa wengine kuwa na wastani, njama ya kumuua ndugu yao huyo ilipingwa na baadhi yao. Hivyo mmoja miongoni mwao akasema: "Hakuna haja ya kumuua Yusuf. Inatosha kumtia kisimani ili kuweza kumaliza mushkili wetu huu' wala hakuna sababu ya kutaka kumwaga damu bure. Yusuf anye atakuwa salama kisimani humo mpaka utakapotokea msafara wa watu watakaokwenda teka maji, ambao watamchukua na kuondoka naye." Wazo la ndugu huyo ndilo lilolokubaliwa na wote na kwa njia hiyo Yusuf akawa amesalimika na njama ya kutaka kumuua. Wapenzi wasikilizaji, kuna baadhi ya wakati ukatazaji wa ovu moja tu unaopelekea kuokoa maisha ya mtu, huwa sababu ya kutokea matukio na mabadiliko makubwa katika historia. Katika kadhia hii kama tulivyoona upinzani wa mmoja tu wa kaka zake Yusuf kwa wazo la kumuua ndugu yao ulinusuru maisha ya Mtume huyo. Naye Yusuf AS bada ya kushika madaraka huko Misri akaja akainusuru nchi hiyo na janga la ukame na upotofu. Kama ambavyo katika kisa kingine ndani ya Qur'ani tunaona hatua ya mke wa Firauni ya kumtaka mumewe asimuue Nabii Musa wakati akiwa mchanga, iliokoa maisha ya Musa. Naye miaka kadhaa baadaye akaja akikomboa na kuiokoa maisha ya Musa. Naye miaka kadhaa baadaye akaja akikomboa na kuiokoa kaumu yake ya Bani Israil na shari ya Firauni. Mifano hii ya wazi ni uthibitisho wa aya tukufu ya Qur'ani isemayo: Wa man ahyaha faka-annama ahya nnasa jamia... Na mwenye kumuokoa mtu na mauti, ni kama amewaokoa watu wote Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kuwa kama hatutokuwa na uwezo wa kuzuia kikamilifu ovu lolote lile, basi tujaribu kadiri ya uwezo wetu walau kupunguza nguvu na athari yake. Kama ambavyo katika kadhia ya Nabii Yusuf mmoja wa kaka zake alishauri badala ya kumuua wakamtie kisimani. Funzo jengine tunalopata hapa ni kuwa unapotaka kuchukuliwa uamuzi usio sahihi, tusisalimu amri kwa hoja ya kukubali sauti ya wengi. Tueleze mawazo na mitazamo yetu asaa ikakubaliwa na kufuatwa wote. Wapenzi wasikilizaji darsa ya 357 inaishia hapa. Tunamwomba Mola ajaalie bora ya amali zetu iwe ni ile tutakayoifanya katika lahadha ya mwisho ya kuondoka duniani, na bora ya siku zetu, iwe ni ile ya kukutana na yeye. Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)

Hadithi ya Uongofu (39)

Ni matarajio yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji na tunakutana tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. …

Ufeministi, Itikadi na Misingi yake (26)

Assalaamu Alaykum wafuatiliaji wa kipindi hiki na karibuni kuwa nasi katika sehemu nyingine ya kipindi hiki kinachokosoa itikadi ya ufeministi …

Ulaji wa Lishe Bora katika Kipindi Chote cha Maisha

Wataalamu wa Afya wanasema kuwa, awamu mbalimbali za maisha zinahitajia ulaji wa chakula wa aina tofauti. Iwapo wewe ni mtoto, …

Maua mawili ya Mtume wa Allah (31) Sauti

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh Karibuni wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili Radio Tehran na wasomaji wa mtandao …