Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumatano, 08 Disemba 2010 18:44

Surat Yusuf - Aya ya 1-3

Sikiliza
Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema ni za Allah SW, mbaye ametupa taufiki ya kukutana tena katika mfululizo mwingine wa darsa hii. Baada ya kumalizika tarjumi na maelezo ya sura ya 11 ya Hud, kuanzia darsa hii ya 355 tutaanza kutoa tarjumi na maelezo kwa muhtasari ya sura ya 12 ya Yusuf ambayo inazungumzia kisa cha maisha ya Nabii huyo yaliyojaa matukio mbalimbali matamu na machungu. Kinyume na zilivyo sura nyingine za Qur'ani ambazo huzungumzia mchanganyiko wa masuala mbalimbali yakiwemo yale ya kiitikadi, kiakhlaki na ya hukumu za dini pamoja na yale yaliyojiri katika maisha ya Mitume mbalimbali na kaumu zao, aya za suratu Yusuf ambayo iliteremshwa Makka na ina jumla ya aya 111, zinazungumzia kisa kimoja tu cha maisha ya Mtume huyo bila ya kuashiria maudhui nyingine yoyote.
Kisa cha maisha ya Nabii Yusuf kimetajwa pia ndani ya Taurat, taba'an kwa namna inayotofautiana katika baadhi ya mambo na vile ilivyozungumziwa katika Qur;ani Tukufu.
Kwa kukitalii kisa cha maisha ya Mtume huyo kupitia ya za Qur'ani Tukufu ndivyo ukweli wa kitabu hicho unapozidi kuwa wazi na opotoshaji uliofanywa ndani ya vitabu vingine vilivyopita kuhusu kisa cha Nabii Yusuf unapodhihirika zaidi. Baada ya utangulizi huo mfupi tunaianza sura yetu hii kwa aya ya kwanza na pili ya sura hiyo ambazo zinasema:
Alif Lam Raa. Hizi ni aya za kitabu kinachobainisha.
Hakika Sisi tumeiteremsha Qur'ani kwa lugha ya Kiarabu ili mpate kuzingatia.
Sura hii kama zilivyo sura nyingine 29 za Qur'ani Tukufu imeanza kwa herufi za mkato ambazo katika moja ya maana zake ni kubainisha sifa ya kimuujiza ilionayo Qur'ani. Kwani katika akthari ya sura zinazoanza kwa herufi hizo baada ya aya ya mwanzo yenye herufi hizo imefuatia aya inayozungumzia Qur'ani yenyewe na adhama yake. Ikiwa na maana ya kuonyesha kwamba, Mwenyezi Mungu ameuteremsha muujiza wake huo kwa kutumia herufi hizi zinazotumiwa na watu wote katika lugha ya Kiarabu, hivyo kama nyinyi mnaoipinga Qur'ani hii mnaweza, tumieni herufi hizo hizo kuleta kitabu mithili ya Qur'ani.
Aya hizo zinaashiria nukta mbili muhimu:
Ya kwanza ni kuwa Qur'ani Tukufu ni kitabu cha muongozo wa nuru ambacho kinabainisha ni njia ipi ya haki; na ni taa ya maisha ambayo mwanga wake humulika kumwezesha mja kufikia kwenye makusudio.
Nukta ya pili ni kwamba watu wote wanatakiwa watadabari na kuzitafakari aya za Qur'ani Tukufu na kufaidika nazo kwa ajili ya kukuza akili na fikra zao. Qur'ani haikuteremshwa kwa ajili tu ya watu kuisoma na kupata thawabu kwa ajili ya akhera, bali imekuja ili watu waitumie pia kama katiba na mwongozo wa kuratibia maisha yao kuanzia mtu binafsi na jamii nzima kwa ujumla.
Miongoni mwa mafunzo tunayoyapata kutokana na aya hizi ni kuwa kiarabu ni lugha ya Qur'ani. Hivyo kuna udharura wa kuielewa lugha hiyo ili kuweza kutadabari na kupata mazingatio ipasavyo kutokana na aya za Qur'ani.
Funzo jingine tunalopata hapa ni kuwa Qur'ani si kitabu cha kuishia kusoma na kupata baraka, bali ni wenzo wa kumfanya mwanadamu akae na kutafakari. QASIDA QASIDA
Aya ya tatu ya sura yetu hii ya Yusuf ndiyo inayotuhitimishia darsa yetu hii. Aya hiyo inasema:
Sisi tunasimulia simulizi nzuri kwa kukufunulia Qur'ani hii, japokuwa kabla ya haya ulikuwa miongoni mwa wasiojua.
Katika aya hii, Mwenyezi Mungu anamweleza bwana Mtume SAW kuwa Sisi tunaokuteremshia wewe wahyi wa hii Qur'ani, tunakusimulia na kukubainishia kwa namna iliyo bora kabisa kuhusu yale yaliyotukia kwa watu waliopita na hiyo ni sehemu ya wahyi wa mbinguni wa kitabu cha Qur'ani. Kimsingi ni kwamba kisa ni kitu chenye nafasi na mchango muhimukatika malezi ya mwanadamu, na hasa kinapohusu matukio ya kweli yaliyojiri kwa kaumu zilizotangulia, na yule anayesimulia akawa hakuvichukilia kuwa ni mambo yaliyobuniwa na mtu tu. Kwa hakika nukta muhimu zaidi katika visa vy Qur'ani Tukufu ni kule kuwa kwake matukio ya kweli. Kitu ambacho leo hii kinajulikana kama tarikh au historia na kupewa umuhimu wa namna mbalimbali katika vyuo vikuu na vituo vingine vya kielimu. Katika barua kwa mwanawe Imamu Hassan as, Imam Ali bin Abi Twalib aliandika hivi: "Ewe mwanangu! Mimi nimeyasoma na kuyatalii yaliyotokea kwa waliotangulia kana kwamba niliishi pamoja nao na kuishi umri kama walioishi wao!" kwa hakika nafasi ya tarikh au historia ndani ya Qur'ani ni kubwa kiasi kwamba kwa mujibu wa badhi ya hadithi, moja kati ya majina ya Qur'ani ni hilo la "Ahsanul Qasas", yaani simulizi nzuri kabisa kama ilivyotajwa katika aya tuliyosoma. Muhimu zaidi ni kuwa Mwenyezi Mungu SW mwenyewe anajitangaza kuwa ndiye msimulizi wa kisa cha Nabii Yusuf as kwa ajili ya bwana Mtume na kukitaja kuwa ni sehemu ya Qur'ni Tukufu. Ikiwa tunaona kisa cha Nabii Yusuf kimetajwa kwenye aya tuliyosoma kuwa ni ‘Ahsanul Qasas' hii ni kwa sababu shakhsia mkuu wa kisa hiki ni kijana ambaye aliipamba nafsi yake kwa sifa njema za usafi wa maadili, uaminifu, subira na imani. Nukta kuu ya kisa chenyewe ni kwamba wakati akiwa kwenye kilele cha rika la ubarobaro, Nabii Yusuf alifaulu katika kupambana na nafsi yake. Vilevile hali mbalimbali zenye sura ya mkinzano zinashuhudiwa kukusanyika pamoja ndani ya kisa hiki. Hali hizo ni kutengana na kisha kuonana tena, huzuni na furaha, ukame na neema, utumwa na ubwana, ubaya na wema na usafi wa maadili na tuhuma.
Katika aya hii kughafilika kwa maana ya kutojua kwa nafsi yake si kitu cha aibu. Kughafilika kuliko kubaya ni kule kunakukuja baada ya mtu kuwa ameshajua kitu. Ni kama vile mtu kughafilika na Allah SA baada ya kuwa anashuhudia athari za adhama yake. Kuhusu bwana Mume SAW ni kuwa hakuwa akijua yaliyotokea katika maisha ya Nabi Yusuf AS, na hivyo akatambulishwa kupitia wahyi wa mbinguni.
Pamoja na mambo mengine aya hii inatuelimisha kuwa, kwa ajili ya kutoa vigezo bora, tunawatambulisha kwa watu shakhsia wa kihistoria na visa vya kweli ambavyo kusimuliwa kwake kuna taathira njema. Kadhalika aya inatutaka tuelewe kuwa yale ambayo Qur'ani inayasimulia kama matukio ya kihistoria, ni matukio ya kweli na ya kiaminika na sababu ni kuwa yamesimuliwa kwetu na Mwenyezi Mungu SA, Mjuzi wa kila kitu na Mwenye hikima.
Kwa haya machache basi tunaifunga darsa yetu ya leo kwa kumuomba Mwenyezi mungu atuwezeshe kukisoma kitabu chake cha Qur'ani kwa namna inayomridhisha yeye, tuyafahamu yaliyoelezwa ndani yake na muhimu zaidi ya yote tuyatekeleze kivitendo katika kila kipengele cha maisha yetu ya kila siku. Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.

 

Unaweza pia kusikiliza kwa kupitia:

 

Zaidi katika kategoria hii: « Surat Yusuf - Aya ya 4-6

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)

Hadithi ya Uongofu (39)

Ni matarajio yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji na tunakutana tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. …

Ufeministi, Itikadi na Misingi yake (26)

Assalaamu Alaykum wafuatiliaji wa kipindi hiki na karibuni kuwa nasi katika sehemu nyingine ya kipindi hiki kinachokosoa itikadi ya ufeministi …

Ulaji wa Lishe Bora katika Kipindi Chote cha Maisha

Wataalamu wa Afya wanasema kuwa, awamu mbalimbali za maisha zinahitajia ulaji wa chakula wa aina tofauti. Iwapo wewe ni mtoto, …

Maua mawili ya Mtume wa Allah (31) Sauti

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh Karibuni wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili Radio Tehran na wasomaji wa mtandao …