Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumatatu, 21 Aprili 2008 21:35

Yunus 107-109

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh. Tunamshukuru Mwenyezi Mungu mtukufu kwa kutuwafikisha kukutana tena katika darsa yetu hii. Sura ya 10 ya Yunus ndiyo tunayoizungumzia kwa sasa, na hii ni darsa ya 326 na ya mwisho inayozungumzia sura hiyo tunayoianza kwa aya ya 107 ambayo inasema:
"Na kama Mwenyezi Mungu akikugusisha dhara, basi hapana wa kukuondolea ila yeye. Na akikutakia kheri basi hapana awezaye kurudisha fadhila zake. Huzifikisha kwa amtakaye katika waja wake. Naye ni Mwingi wa Kusamehe na Mwingi wa Kurehemu."
Katika aya ya mwisho tuliyoisoma katika darsa iliyopita Allah sw alimtaka Bwana Mtume Muhammad saw asimame imara na kuwatangazia kinagaubaga washirikina kuwa njia yake yeye ni ya tauhidi, na wala hatolegeza msimamo kwa sababu ya kuwavutia ao washirikina waukubali Uislamu. Aya tuliyosoma inaendeleza yale yaliyokuja katika aya iliyotangulia na kumwambia Bwana Mtume na Waislamu kwa jumla kwamba, elewa kuwa kheri yoyote utakayopata au dhara yoyote itakayofika iko mikononi mwa Mola wako Allah sw, na hakuna yeyote ghairi ya yeye aliye na uwezo wa kukupa kheri au kukupokonya neema yoyote uliyopewa na yeye Mola. Kama ambavyo bila ya ridhaa yake Mola, hakuna mtu yeyote awezaye kukudhuru, kama ambavyo endapo Mwenyezi Mungu sw atataka dhara yoyote ile impate mja hakuna yeyote aliye na uwezo wa kumkinga mja na dhara hiyo. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kuwa mushirikina na makafiri waelewe kwamba kukataa kwao kuiamini haki hakutawawezesha kutoka nje ya irada ya Allah sw, na kwa hakika kile alichoandika Mola kiwafike ndicho kitakachotokea. Aidha aya inatuelimisha kuwa kheri na neema azipatazo mja zinatokana na ihsani na fadhila zake Mola na wala si kwa kustahiki mja.
Ifuatayo sasa ni aya ya 108 ambayo inasema:
"Sema: Enyi watu haki imekwisha kukujieni kutoka kwa Mola wenu. Basi anayeongoka, anaongoka kwa faida ya nafsi yake, na anayepotea, anapotea kwa khasara ya nafsi yake. Na mimi si mlinzi juu yenu."
Katika aya hii ambayo ni moja kabla ya aya ya mwisho ya suratu Yunus Bwana Mtume Muhammad saw anawahutubu watu wote kwa jumla kwamba mimi nina jukumu la kukufikishieni wito wa wahyi wa Mola wangu na kukulinganieni kuifuata njia yake tu; na wala sina haki ya kukulazimisheni muukubali wito huo. Kila mmoja kati yenu anaweza kuamua kwa hiyari yake kuukubali uongofu na kuongoka, au kuukana na kupotoka. Lakini jueni kwamba kuamini kwenu na kukufuru kwenu hakuna tofauti yoyote kwa Mwenyezi Mungu sw wala mimi Mtume wake, na kwa hakika kama ni kupata faida au madhara na hasara, hilo litakurudieni nyinyi wenyewe. Kwani Mwenyezi Mungu yeye ni mkwasi wala hahitaji chohcote kwenu, nami pia nimetimiza wajibu wangu wa kukulinganieni na kukufikisheni risala ya uongofu kutoka kwa Mola wenu, na hivyo sina dhima yoyote juu ya kuamini au kutoamini kwenu. Baadhi ya nukta za kuzingatiwa katika aya hii ni kuwa Mwenyezi Mungu ameondoa dhima kwa waja wake kwa kuwaonyesha na kuwabainisha njia ya haki. Kufuata au kutofuata hilo liko katika hiyari ya waja wenyewe. Nukta nyengine ya kuzingatiwa katika aya hii ni kuwa jukumu la maulamaa na wale wafanyao tablighi ya dini ni kuwaelimisha na kuwaonyesha njia watu na si kuwalazimisha waikubali na kuifuata.
Darsa ya 326 na sura yetu ya Yunus inahitimishwa na aya ya 109 ambayo inasema:
"Na (nimeambiwa): Fuata yanayofunuliwa kwako kwa Wahyi. Na vumilia mpaka Mwenyezi Mungu ahukumu, na yeye ndiye mbora wa mahakimu."
Aya hii ya mwisho ya sura hii inasisitiza kwa mara nyingine juu ya kushikamana barabara na njia ya haki ya risala ya wahyi utokao kwa Mola Muumba, kwanza kabisa ikimuelekea bwana Mtume mwenyewe na kisha waumini kwa jumla, kwa kuwataka waendelee kuwa na subra hadi ushindi wa haki dhidi ya batili. Kama inavyojulikana mataghuti na madhalimu hufanya kila vitimbi na njama ili kuwakwamisha waumini wa kweli wasiweze kushikamana na kamba ya lailaha illa llah kama inavyostahiki. Na ndiyo maana aya inawataka waumini kusimama kidete dhidi ya njama hizo na kuvumilia tabu na mashaka yote yatakayowapata katika njia hiyo. Alaa kulli haal Mwenyezi Mungu sw anaona kila kinachofanywa na waja wake wote, na siku itafika ambapo atahukumu baina yao kwa uadilifu. Lakini hata hapa duniani pia, pale waumini wanaposimama kidete kukabiliana na madhalimu, mwishowe hupata nusra ya Allah na haki kuishinda batili. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kuwa watu wana hiyari ama kuamini au kukufuru, hata hivyo kukufuru kwao kusitufanye sisi tukaingiwa na shaka katika kufuata njia ya uongofu ya kushikamana na maamrisho ya Mola wetu na kujiweka mbali na makatazo yake. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 326 imefikia tamati na kuhitmisha pia tarjumi na maelezo ya sura ya kumi ya Yunus. Tunamwomba Mwenyezi Mungu atuwafikishe kuyatekeleza kivitendo yale yote tuliyojifunza ndani ya sura hii, Amin. Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.
Zaidi katika kategoria hii: Yunus 101-106 »

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)

Hadithi ya Uongofu (39)

Ni matarajio yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji na tunakutana tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. …

Ufeministi, Itikadi na Misingi yake (26)

Assalaamu Alaykum wafuatiliaji wa kipindi hiki na karibuni kuwa nasi katika sehemu nyingine ya kipindi hiki kinachokosoa itikadi ya ufeministi …

Ulaji wa Lishe Bora katika Kipindi Chote cha Maisha

Wataalamu wa Afya wanasema kuwa, awamu mbalimbali za maisha zinahitajia ulaji wa chakula wa aina tofauti. Iwapo wewe ni mtoto, …

Maua mawili ya Mtume wa Allah (31) Sauti

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh Karibuni wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili Radio Tehran na wasomaji wa mtandao …