Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumatatu, 21 Aprili 2008 21:34

Yunus 101-106

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh. Tunamshukuru Mwenyezi Mungu mtukufu kwa kutuwafikisha kukutana tena katika darsa yetu hii. Sura ya 10 ya Yunus ndiyo tunayoizungumzia kwa sasa, na hii ni darsa ya 325 tunayoianza kwa aya ya 101 ambayo inasema:
"Sema: Angalieni yaliyomo mbinguni na kwenye ardhi! Na ishara zote na maonyo hayawafai kitu watu wasioamini."
Katika aya zilizotangulia tulisema kuwa kutotumia watu akili zao na kutotafakari juu ya alama na ishara za uwezo wa Allah ndiyo sababu ya watu kukufuru na kuikana haki. Aya tuliyosoma inatilia mkazo suala la kutadabari na kubainisha kuwa, kutafakari na kuzingatia kwa kina madhihirisho ya uumbaji wa Allah ni utangulizi wa kumfikisha mtu kwenye imani thabiti na sahihi. Kwa upande mwingine kama tulivyosisitiza katika darsa iliyopita na nyingine kadhaa, imani lazima itokane na hiyari ya mtu na si kwa kulazimishwa na kutezwa nguvu, na ndiyo maana aya hii ya 101 inasisitiza juu ya kutafakari ili kwa kupitia njia hiyo ya uelewa na ufahamu mtu aiamini haki na kuweza kudumu na imani aliyonayo. Bila shaka utafiti sahihi na wa kutafuta ukweli juu ya chungu ya maajabu yaliyomo katika mbingu na ardhi na ulimwengu mzima wa uumbaji humfanya mwanaadamu atambue adhama ya Mola wake na hivyo kunyenyekea na kujisalimisha kwa Muumba asiye na mshirika. Pamoja na hayo bado wanakuwepo watu ambao licha ya kushuhudia ishara za adhama ya Mola Muumba huamua kuikana na kuikataa haki. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kuwa kutafakari na kutadabari juu ya uumbaji ni njia inayoweza kutumiwa na kila mtu kwa ajili ya kumjua Mwenyezi Mungu. Ifuatayo sasa ni aya ya 102 ambayo inasema:
"Basi je wanagojea jingine ila kama yaliyotokea siku za watu waliopita kabla yao? Sema: Basi ngojeni! Nami ni pamoja nanyi katika wanaongojea."
Katika aya zilizotangulia Mwenyezi Mungu amewataka wapinzani wa haki kutafakari na kuzingatia kwa makini ishara za kuwepo Muumba wa ulimwengu katika mbingu na ardhini. Aya tuliyosoma hivi punde inasema wale ambao hawako tayari kutafakari juu ya hayo basi wajiweke tayari kukabili siku ngumu za mashaka na adhabu. Kwani utaratibu aliouweka Allah kuhusiana na uma au jamii za watu mbali mbali ni kwamba kama ilivyo kwa watu mmoja mmoja, majaaliwa na hatima ya jamii nzima ya watu hutegemea mwenendo wa akthari ya watu walioko katika jamii hiyo. Kama wengi wao watakuwa ni watu wema basi jamii nzima huwa na muelekeo wa kutengenea hata kama watu wachache kati yao watakuwa mafasiki; la kama wengi wao watakuwa ni waovu basi jamii nzima itatumubukia kwenye ufisadi na kupatwa na mwisho mbaya hata kama ndani yake baadhi ya watu watakuwa ni waja wema. Historia ya kaumu zilizopita kama zile za Manabii Nuh, Lut na Hud as ni uthibitisho juu ya kutobadilika kwa utaratibu huo wa Allah sw. Hivyo bwana Mtume anatakiwa na Mola awaeleze Mushirikina wa Makka kwamba kama nao pai wataamua kusimama dhidi ya risala ya haki watafikwa na hatima sawa na iliyowapata watu wan kaumu hizo. Miongoni mwa mafunzo tunayoyapata kutokana na aya hii ni kuwa ni historia ya waliotangulia ni funzo na ibra kwa wanaofuatia.
Ifuatayo sasa ni aya ya 103 ambayo inasema:
"Kisha sisi huwaokoa Mitume wetu na walioamini. Ndio kama hivyo, inatustahiki kuwaokoa Waumini."
Ikiendeleza yale yaliyokuja katika aya iliyotangulia kuhusiana na watu kupatwa na adhabu ya papa hapa duniani, aya ya 103 ya suratu Yunus inasema kwa kuwa hailaiki katika uadilifu wa Allah kuwachanganya wema na wabaya katika adhabu, hivyo kila kaumu inayofkia hatua ya kustahiki kufikwa na adhabu ni wale walio waovu na wale waliokuwa hawayajali maovu yanayotendeka katika jamii ndio wanakaopatwa na adhabu ya Allah, ama wale walio waumini Mwenyezi Mungu atawaokoa na adhabu hiyo. Baadhi ya nukta za kuzingatiwa katika aya hii ni kuwa wale walio waumini wa kweli Mwenyezi Mungu huwalinda na adhabu hata ya hapa duniani, japokuwa watakuwa wakiishi katika jamii ya watu mafasiki.
Ifuatayo sasa ni aya ya 104 ambayo inasema:
"Sema: Enyi watu ikiwa nyinyi mnayo shaka katika dini yangu basi mimi siwaabudu mnaowaabudu nyinyi badala ya Mwenyezi Mungu. Lakini mimi ninamwabudu Mwenyezi Mungu anayekufisheni. Na nimeamrishwa niwe miongoni mwa Waumini."
Baada ya aya ziliowahutubu washirikina na kuwabainishia ipi itakuwa hatima yao, aya hii inamtaka Bwana Mtume awaambie watu hao kuwa kama wanadhani kwamba wewe utayumba na kutia shaka katika kufuata njia yako ya haki na pengine kukushawishi ulegeze msimamo katika itikadi yako basi wape jibu zito na la wazi kwamba hutomwabudu mwingine yeyote ghairi ya Mola wako Allah sw na katu hutoyatukuza msanamu yao hayo wanayoyaabudu. Waambie kwamba mimi ninamwabudu Mungu ambaye mauti yangu na yenu yako mikononi mwake na hamuwezi nyinyi abadani kuyakwepa hayo wala hayo masanamu yenu pia hayana uwezo wa kukuepusheni na kifo. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kuwa shaka inayotiwa na wengine juu ya haki hata kama watakuwa wengi namna gani isituyumbishe katika kufuata njia ya uongofu. Aidha aya inatuonyesha kuwa aliye na ustahiki wa kuabudiwa ni yule ambaye uhai wetu na mauti yetu yako mikononi mwake.
Darsa ya 325 inahitimishwa na aya za 105 na 106 ambazo zinasema:
"Na uelekeze uso wako kwenye dini ya kweli wala usiwe katika washirikina."
"Na wala usiwaombe wasiokuwa Mwenyezi Mungu ambao hawakufai kitu wala hawakudhuru. Ukifanya hivyo basi utakuwa miongoni mwa waliodhulumu."
Katika kuwatangazia watu na hasa washirikina yale aliyoamriwa na Mola wake, Bwana Mtume anabainisha katika aya hizi kuwa ni wajibu kuifuata na kushikamana nayo njia iliyonyooka na kuepuka kila aina ya upotofu. Ama kinyume chake, itikadi ya mushirkina imejaa upotofu na mambo ya uzushi chungu nzima na muhimu zaidi ni kuwa hivyo vinavyoabudiwa na washirikina hao yaani masanamu, havina uwezo wa kumdhuru wala kumnufaisha mtu kwa lolote. Hivyo anayevielekea na kuviabudu vitu hivyo huwa ameidhulumu nafsi yake na pia kuifanyia dhulma dini ya haki ya mbinguni.
Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kuwa dini ya kufuata ni ile inayokubaliana na maumbile ya mwanadamu. Aidha aya zinatuonyesha kuwa kila mwenye akili na busara hufanya kitu ambacho ima kitamletea manufaa au kumuepusha na madhara. Lakini kama tujuavyo masanamu na miungu wengine wengine wote bandia hawana uwezo wa hayo. Kwa haya machache basi tunaifunga darsa yetu hii kwa kumwomba Allah atulinde na kila aina ya shirki na kutuwafikisha kumwabudu yeye kwa ikhlasi. Amin. Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.
Zaidi katika kategoria hii: « Yunus 107-109 Yunus 98-100 »

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)

Hadithi ya Uongofu (39)

Ni matarajio yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji na tunakutana tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. …

Ufeministi, Itikadi na Misingi yake (26)

Assalaamu Alaykum wafuatiliaji wa kipindi hiki na karibuni kuwa nasi katika sehemu nyingine ya kipindi hiki kinachokosoa itikadi ya ufeministi …

Ulaji wa Lishe Bora katika Kipindi Chote cha Maisha

Wataalamu wa Afya wanasema kuwa, awamu mbalimbali za maisha zinahitajia ulaji wa chakula wa aina tofauti. Iwapo wewe ni mtoto, …

Maua mawili ya Mtume wa Allah (31) Sauti

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh Karibuni wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili Radio Tehran na wasomaji wa mtandao …