Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumatatu, 21 Aprili 2008 21:34

Yunus 98-100

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh. Karibuni katika mfululizo mwingine wa darsa ya quran. Hii ni darsa ya 324, na tukiwa tunaendelea kuizungumzia sura ya 10 ya Yunus, tunaianza darsa yetu kwa aya ya 98 ambayo inasema:
"Kwa nini usiwepo mji mmoja ukaamini na imani yake ikawafaa isipokuwa kaumu Yunus? Waliamini na sisi tukawaondolea adhabu ya hizaya katika maisha ya dunia, na tukawasterehesha kwa muda."
Kama ambavyo tumewahi kuashiria katika darsa zetu za huko nyuma, ni kwamba utaratibu aliojiwekea Allah sw kuhusiana na waja wake ni kuwapa fursa na muhula wa kutubia madhambi yao na kutenda amali njema ili kufidia waliyoyatanguliza huko nyuma. Lakini pia kama tulivyowahi kueleza ni kwamba mlango wa toba uko wazi madamu mtu bado hajafikia lahadha ya kufikwa na mauti au kuteremkiwa na adhabu ya Mwenyezi Mungu. Kwani kutubia katika lahadha mbili hizo au kuiamini haki katika wakati huo hakuwi na faida yoyote kwa mtu, na sababu ni kwamba imani na toba ya lahadha hizo hutokana na khofu ya mauti na adhabu na si kwa hiyari yake mtu. Suala hilo la fursa na muhula wa kutubia na kuiamini haki hauishii kwa mtu binafsi tu, bali Allah ameuweka pia kwa kaumu na umma mzima wa watu. Kwa upande wa kaumu, ni ile ya Nabii Yunus tu (AS) ndiyo ambayo watu wake walipoiona adhabu waliiamini haki na kujisalimisha kwa Mwenyezi Mungu, naye Mola Mrehemevu akaikubali imani yao na kuwapa fursa nyingine. Historia inasimulia kwamba baada ya miaka mingi ya kazi ya tablighi aliyoifanya Nabii Yunus as kuwalingania watu wake lailaha illa llah ni watu wawili tu ndiyo walioukubali wito wa uongofu. Akiwa katika siku za mwisho za uhai wake, na kutokana na kukata tamaa kwa watu wake kuiamini haki, Mtume huyo wa Allah aliwaapiza watu wa kaumu yake na kisha akaamua kuondoka na kwenda zake. Kama ilivyo kawaida ni kwamba dua za Mitume huwa hazirudi, na kwa hivyo ilipasa watu wa kaumu yake wateremkiwe na adhabu. Hata hivyo mtu mmoja mtambuzi na mwenye hekima kati ya wale wawili waliomuamini Mtume huyo alipoona Nabii Yunus ameshatoa tamko la kuwaapiza watu wake waliokataa kuamini haki aliwaendea watu hao na kuwaambia:" Sasa subirini mshukiwe na adhabu ya Mwenyezi Mungu, la kama mnataka mpate rehma zake Mola basi tokeni nje ya mji, na mutenganishe baina yenu na watoto wenu wadogo ili sauti za vilio vya watoto na za maombolezo ya mama zao waliotenganishwa nao ziweze kupanda na kusikika, na nyote pamoja mtubie kwa mliyoyafanya huko nyuma na kumwomba maghufira Allah sw. Asaa kwa njia hiyo mkaweza kusamehewa. Hivyo watu hao wakaufuata wasia huo na hivyo adhabu haikuteremshwa tena, naye Nabii Yunus akarejea kwa watu wake. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na ayah ii ni kuwa miongoni mwa kaumu zilizopita, ni kaumu ya Yunus tu ndiyo iliyotubia kwa wakati na kabla ya kushuka adhabu na toba yao ikapokelewa na kuamini kwao kukakubaliwa. Funzo jengine tunalopata katika ayah ii ni kwamba hatima na majaaliwa ya watu yako mikononi mwao wenyewe, na hivyo kwa kuomba dua na kushtakia waja hali zao hiyo inaweza ikawa sababu ya kuzuia balaa lisiwashukie na rehma za Mola ziwamiminikie.
Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya 99 ambayo inasema:
"Angelitaka Mola wako wangeliamini wote waliomo katika ardhi. Je wewe utawalazimisha watu kwa nguvu mpaka wawe waumini?"
Moja ya kati ya mambo ambayo Mwenyezi Mungu sw amejifunga nayo mwenyewe ni kuwafikishia waja wake uongofu. Hata hivyo Mola Mwenye hikima hakutaka watu waiamini haki kwa nguvu na kulazimishwa. Bali ametaka waamue kwa hiyari yao waja, ima kuiamini au kuikufuru haki. Tabaan baada ya kuchagua kwa hiyari yake mtu ima kuamini au kukufuru ajiweke tayari pia kwa jaza na malipo atakayopata kutokana na chaguo lake. Kwa kuzingatia kwamba sifa moja kubwa ya Bwana Mtume Muhammad saw kama ilivyoelezwa na quran ni kwamba alikuwa na hamu kubwa ya kuona watu wa umati wake wanaiamini haki na akiumia na kuungulika mno kwa kuwaona wamezama katika dimbwi la upotofu, lakini kwa kuwa Allah sw ametaka imani ya waja itokane na hiyari yao hivyo anamhutubu Mtume wake kwa kumwambia kwamba pamoja na hamu kubwa uliyonayo usifikirie kuwafanya watu waumini hata kwa kuwateza nguvu, kwani lau Mola wako angetaka iwe hivyo wanaadamu wote wangeiamini haki. Moja ya nukta za kuzingatiwa katika ayah ii ni kuwa imani huwa na thamani inapotokana na hiyari ya mtu, ama ikiwa itatokana na kulazimishwa haiwezi kuwa na faida kwa mtu.
Darsa ya 324 inahitimishwa na aya ya 100 ambayo inasema:
"Na hawezi mtu kuamini ila kwa idhini ya Mwenyezi Mungu. Naye hujaalia adhabu iwafike wasiotumia akili zao."
Kama tujuavyo, watu hawalazimishwi kuiamini haki, na kuamini kwa kulazimishwa hakuna thamani yoyote. Pamoja na hayo ni taufiki ya Mola ndiyo inayoufanya moyo wa mtu uikubali na kuiamini haki kwa hiyari na ukunjufu. Kwani ni yeye ndiye anayetukamilishia suhula zote kuanzia za kutufikia uongofu wenyewe kupitia kwa Mitume wake, pamoja na kutupa akili timamu ya kuchanganua na kupambanua zuri na baya, la kheri na la shari na lile la kimantiki na lisiloingia akilini. Hivyo mtu asije akaingiwa na ghururi na kumpitikia kwamba ni uhodari wake ndio uliomfanya kuitambua haki na kuifuata. Na kwa hakika kila mtu anapojiona amepata taufiki ya kushikamana barabara na kamba ya uongofu, basi amshukuru sana Mola wake na kuomba taufiki ya kudumu katika kushikamana na mambo ya kheri. Amin. Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.
Zaidi katika kategoria hii: « Yunus 101-106 Yunus 93-97 »

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)

Hadithi ya Uongofu (39)

Ni matarajio yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji na tunakutana tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. …

Ufeministi, Itikadi na Misingi yake (26)

Assalaamu Alaykum wafuatiliaji wa kipindi hiki na karibuni kuwa nasi katika sehemu nyingine ya kipindi hiki kinachokosoa itikadi ya ufeministi …

Ulaji wa Lishe Bora katika Kipindi Chote cha Maisha

Wataalamu wa Afya wanasema kuwa, awamu mbalimbali za maisha zinahitajia ulaji wa chakula wa aina tofauti. Iwapo wewe ni mtoto, …

Maua mawili ya Mtume wa Allah (31) Sauti

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh Karibuni wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili Radio Tehran na wasomaji wa mtandao …