Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumatatu, 21 Aprili 2008 21:33

Yunus 93-97

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh. Karibuni katika mfululizo huu wa 323 wa darsa ya quran, tukiwa tunaendelea kuizungumzia sura ya 10 ya Yunus. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 93 ambayo inasema:
"Na hakika tuliwaweka Wana wa Israili makazi mazuri, na tukawaruzuku vitu vizuri. Nao hawakukhitalifiana mpaka ilipowafikia ilimu. Hakika Mola wako atahukumu baina yao Siku ya Kiyama katika yale waliyokuwa wakikhitalifiana."
Katika aya hii Mwenyezi Mungu sw ameashiria neema kadha wa kadha alizowapa Bani Israil na kusema kuwa baada ya miaka na miaka ya kutangatanga na kutokuwa na pa kukaa tuliwapa Bani Israil eneo lenye hali nzuri kabisa ya hewa, na lenye rutuba na ustawi huko Sham na kuwaruzuku riziki zilizo bora kabisa. Lakini badala ya kushukuru kwa hayo na kuwa watiifu wa kushikamana na maamrisho tuliyowateremshia wakaanza kufarikiana na kutengana na kila mmoja akaamua kufuata njia yake. Hivyo kila mmoja atatakiwa kuja kuutolea maelezo mwenendo huo muovu aliokuwa nao atakaposimamishwa mbele ya mahakama ya uadilifu siku ya Kiyama. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kuwa katika mafundisho ya Mitume, mbali na kuzingatiwa suala la kuwalea na kuwajenga watu kiroho na kimaanawi, yanazingatiwa vile vile mahitaji yao ya kimaada kwa kuwapa uhuru, fursa na suhula za kimaisha za kupatia riziki safi na za halali. Aidha aya hii inatuonyesha kuwa hitilafu na mifarakano hutokana na kujiweka mbali watu na mafundisho ya mbinguni na hilo huwa sababu ya kuondokewa na neema za Mola wao.
Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya za 94 na 95 ambazo zinasema:
"Na kama unayo shaka juu ya hayo tuliyokuteremshia, basi waulize wasomao kitabu kabla yako. Kwa yakini imekwisha kujia haki kutoka kwa Mola wako. Basi usiwe miongoni mwa wenye shaka."
"Na kabisa usiwe miongoni mwa wale wanaozikanusha ishara za Mwenyezi Mungu usije ukawa miongoni mwa wenye khasara."
Aya hizi wapenzi wasikilizaji zinawahutubu wale waliokuwa na shaka kama yale aliyokuja nayo Bwana Mtume Muhammad saw ni maneno ya haki au la na kuwaambia kwamba ikiwa mtavirejea vitabu vya mbinguni vilivyotangulia mtaona humo bishara na alama za Mtume Muhammad SAW. Mbali na hayo mtashuhudia pia kuwa zimezungumzwa na vitabu hivyo hatima za kaumu nyingi zilizotangulia zilizotajwa pia ndani ya Quran kama vile bani Israil, na hivyo kukubainikieni kwamba hii Quran pia ni kitabu cha haki kinachotoka kwa Mwenyezi Mungu sw. Ni wazi kuwa kama shaka yenu itaondolewa baada ya kubaini hayo na kutambua kuwa Quran ni kitabu cha haki, kukadhibisha kwenu kitabu hicho baada ya kubainikiwa na hayo kutakuwa ni kwa madhara yenu yenyewe kutokana na kujinyima fursa ya kuufikia uongofu hapa duniani. Ijapokuwa kidhahiri matamshi ya aya hizi wapenzi wasikilizaji yanaonekana kumhutubu Bwana Mtume, lakini ni wazi kwamba si yeye anayesemezwa hapa, kwa sababu ni jambo lililo muhali na lisiloingia akilini kwamba Bwana Mtume awe na shaka na wahyi alioteremshiwa na Mola wake. Hivyo anaowahutubu Allah katika aya hii ni mushirikina na Ahlul Kitab, lakini kama ilivyo katika aya nyingi za Quran lugha iliyotumika inaonyesha kuwa mhutubiwa ni bwana Mtume wakati kumbe mlengwa hasa ni watu wengine wa kawaida. Pamoja na mambo mengine aya hizi zinatuelimisha kuwa shaka na hati hati ni vitu vya kawaida vinavyoweza kumtokea kila mtu. La muhimu ni kujivua na hali ya shaka kwa kurejea kwa maulamaa na wanazuoni wa kidini na kufikia kwenye daraja ya utambuzi kamili na yakini. Funzo jengine tunalopata hapa ni kuwa endapo mtu ataendelea kubakia katika hali ya shaka na kutochukua hatua ya kuiondoa shaka aliyonayo si hasha akajikuta anaishia kwenye kukadhibisha na kuikataa moja kwa moja haki.
Aya za 96 na 97 ndizo zinazotuhitimishia darsa yetu ya juma hili. Aya hizo zinasema:
"Hakika wale ambao neno la Mola wako limekwisha thibitika juu yao hawataamini."
"Ijapokuwa itawajia kila ishara mpaka waione adhabu inayoumiza."
Watu wamegawika makundi matatu katika suala la namna wanavyoamiliana na ukweli wa mafundisho ya dini. Kundi la kwanza ni la wale wasioitambua haki na wala hawajishughulishi kutaka kuijua. La pili ni la wale ambao haki hawaijui lakini wanaamua kufanya juhudi za kuitafuta hadi kuifikia. Ama kundi la tatu ni la wale ambao wameitambua haki lakini kwa kuwa inagongana na maslahi yao ya kimaada ya hapa duniani, hawako tayari kuifuata. Aya tulizosoma zinawalenga watu wa kundi hili la tatu ambao nyoyo zao zimepiga weusi na kufanya kutu kutokana na inadi na ukaidi wao na ambao hakuna tena matumaini ya nyoyo zao kubadilika na kuiamini haki. Watu wa aina hii huwa ni katika wale walioghadhibikiwa na Mwenyezi Mungu; kwani hawawi tayari kuamini na kujisalimisha kwa Mola wao kama haijafikia hatua ya kuiona adhabu ya Mwenyezi Mungu kwa macho yao. Tatizo la watu hao si kutopewa hoja za kiakili wala kutoonyeshwa muujiza, ambao hata kama wataonyeshwa pia hawatouamini. Tatizo lao ni kwamba hawaa na matamanio yao ya nafsi hayawaruhusu kuungama kile ambacho wamepata utambuzi wake. Hivyo kama tutaona watu wengi hawaiamini haki, hilo lisitufanye tukautilia shaka ukweli wa maneno ya Mitume na vitabu vya mbinguni walivyokuja navyo. Bali tuelewe kwamba kuna watu ambao nafsi zao zimekubuhu kwa maovu na kuharibika kimaanawi kiasi kwamba hakuna chochote kile cha kuweza kuwaathiri wakabadilika. Watu hao ni mithili ya mpira ambao kama utautupa baharini hakuna hata moja la maji litakalopenya na kuingia ndani yake. Hali ambayo ni matokeo ya kuziba kwa mpira tu vinginevyo bahari iko pale pale na maji yake yako kwa ajili ya kila mtu. Baadhi ya nukta za kuzingatiwa katika aya hizi ni kuwa tusiwe na matumaini kwamba watu wote wataiamini haki, bali tujue kwamba maovu na madhambi ni mambo yanayofanya utandu juu ya moyo wa mtu unaomfanya asiwe tayari kuikubali haki. Nukta nyingine ya kuzingatiwa katika aya hizi ni kuwa iko siku hata wale waliotopea katika kukadhibisha haki watabaini hakika hiyo lakini wakati huo watakuwa wamechelewa na kuikubali kwao haki wakati huo hakutowasaidia kitu.
Darsa ya 323 imeifikia tamati. Tunamwomba Allah atuonyeshe haki na kutuwafikisha kuifuata na atuonyeshe batili na kutupa taufiki ya kuiepuka. Amin. Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh
Zaidi katika kategoria hii: « Yunus 98-100 Yunus 87-92 »

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)

Hadithi ya Uongofu (39)

Ni matarajio yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji na tunakutana tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. …

Ufeministi, Itikadi na Misingi yake (26)

Assalaamu Alaykum wafuatiliaji wa kipindi hiki na karibuni kuwa nasi katika sehemu nyingine ya kipindi hiki kinachokosoa itikadi ya ufeministi …

Ulaji wa Lishe Bora katika Kipindi Chote cha Maisha

Wataalamu wa Afya wanasema kuwa, awamu mbalimbali za maisha zinahitajia ulaji wa chakula wa aina tofauti. Iwapo wewe ni mtoto, …

Maua mawili ya Mtume wa Allah (31) Sauti

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh Karibuni wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili Radio Tehran na wasomaji wa mtandao …