Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumatatu, 21 Aprili 2008 21:33

Yunus 87-92

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh. Karibuni katika mfululizo mwingine wa darsa ya quran. Hii ni darsa ya 322, na tukiwa tunaendelea kuizungumzia sura ya 10 ya Yunus, tunaianza darsa yetu kwa aya ya 87 ambayo inasema:
"Na tukampelekea Musa na ndugu yake wahyi ya kwamba: Watengenezeeni majumba watu wenu katika Misri na zifanyeni nyumba zenu zielekeane, na mshike Sala na wabashirie Waumini."
Ili kuijenga tena jamii ya Bani Israil, baada ya kuikomboa na madhila ya Firaun, Nabii Musa as aliamriwa na Mola wake kuwakusanya watu wa kaumu yake mahali pamoja na kwa msaada wao kujenga nyumba kwa ajili ya makaazi yao. Nyumba hizo zilitakiwa ziweko mahali pamoja zikiwa zimeelekeana na si kutawanyika huku na huko ili iwe rahisi kwao kujumuika pamoja kwa ajili ya kupanga na kuchukua maamuzi mbali mbali ya kijamii, na pia endapo Firauni atataka kuwaangamiza waweze kusimama pamoja na kukabiliana naye. Baadhi ya wafasiri wa quran wanasema, kutokana na kutolewa amri ya sala katika aya hii, muradi uliokusudiwa hapa juu ya neno qibla ni kuzijenga nyumba zao hizo kwa namna ambayo zitakuwa zimeelekea upande wa kibla ili wakiwa ndani ya nyumba zao waweze kutekeleza ibada zao. Pamoja na hayo maana hiyo ni ya kiistilahi, na kimsingi makusudio ya neno qibla kilugha ni maana hiyo hiyo ya kuelekeana. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kuwa mojawapo ya sifa za Mitume ilikuwa ni kuwafikiria watu na hivyo kila wakati wakichukua hatua zinazohitajika kwa ajili ya kuwasaidia watu wa kaumu zao. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa kushughulika na masuala ya kimaada na kimaisha kusitughafilishe na utekelezaji wa sala na kumwabudu Mola wetu. Kutekeleza kwa pamoja yote hayo ndiko kutakakotufanya tupate rehma na baraka za Mola Karima.
Zifuatazo sasa ni aya za 88 na 89 ambazo zinasema:
"Na Musa akasema: Mola wetu! Hakika wewe umempa Firauni na watu wake wakubwa mapambo na mali katika maisha ya dunia. Mola wetu! Hivyo wanapoteza watu na Njia yako. Mola wetu! Ziangamize mali zao na zifunge nyoyo zao, wasiamini mpaka waione adhabu chungu."
"Mwenyezi Mungu akasema: Maombi yenu yamekubaliwa. Basi simameni sawasawa, wala msifuate njia za wale wasiojua."
Katika kuendelea na utekelezaji wa jukumu alilopewa na Mola wake la kupambana na Firaun, Nabii Musa AS alimwomba Allah SW auangamize utajiri uliopindukia mpaka aliokuwa nao Firaun na kutomruhusu aendelee kufanya ufisadi na uharibifu, pamoja na kutumia vibaya nguvu na mamlaka aliyokuwa nayo kutokana na utajiri na neema za kimaada alizoruzukiwa na yeye Mola Karima; mali na neema ambazo alikuwa akizitumia kwa ajili ya kupotosha watu na njia ya Mwenyezi Mungu. Nabii Musa aliomba dua hiyo kwa Mwenyezi Mungu pale ilipofika hadi akawa hana matumaini tena kwamba Firauni ataamini na kuikubali haki. Allah sw aliitakabalia dua ya Mtume wake, na hivyo akamtaka Mussa as na watu wake wao wenyewe kwanza wasimame sawa sawa na kushikamana na njia ya Mola wao; kwani sharti mojawapo la kutakabaliwa dua ni waumini wenyewe kwanza kuwa wameshikamana barabara na njia ya uongofu. Na ndiyo maana kwa mujibu wa hadithi ni kwamba ilichukua muda wa miaka arubaini tokea Nabii Musa alipoomba dua ya kumwapiza Firauni hadi taghuti huyo alipoangamizwa kwa kugharikishwa baharini. Aya hizi pamoja na mambo mengine zinatufunza kwamba, kuwa na utajiri wa mali tu si kipimo cha kuonyesha kuwa Mwenyezi Mungu amemjali na kumpenda mja. Kwani katika dunia hii, hata makafiri nao wamepewa neema nyingi za kimaada. Halikadhalika aya zinatuonyesha kuwa pamoja na sisi kumwomba Mola awaangamize madhalimu, sisi wenyewe pia tujihimu na kutekeleza wajibu wetu ipasavyo.
Darsa ya 322 inahitimishwa na aya za 90, 91 na 92 ambazo zinasema:
"Tukawavusha bahari wana wa Israili, na Firauni na askari wake wakawafuata kwa dhulma na uadui. Hata Firauni alipokuwa anataka kuzama akasema: "Naamini kuwa hapana mungu ila yule waliyemuamini Wana wa Israili, na mimi ni miongoni mwa wanaonyenyekea."
"Ala! Sasa (unaamini hayo)? Na hali uliasi kabla yake na ukawa miongoni mwa mafisadi!"
"Leo basi tutakuokoa kwa kuuweka mwili wako, ili uwe ishara kwa ajili ya walio nyuma yako. Na hakika watu wengi wameghafilika na ishara zetu."
Aya hizi wapenzi wasikilizaji zinabainisha jinsi dua iliyoombwa na Nabii Musa as ilivyotakabaliwa, na kueleza kuwa pale jeshi la Firauni lilipoamua kukuandameni nyinyi kwa lengo la kukuangamizeni, sisi tulikufungulieni njia katika mto Nile na kukupitisheni salama usalimini. Ama Firauni na jeshi lake wao tuliwagharikisha kwenye mto huo na tukaamua kukiibua kutoka majini kiwiliwili cha Firauni tu peke yake, ili hilo liwe funzo na ibra kwa wengine. Nukta yenye kutoa mguso hapa ni kuwa ule utabiri wa Nabii Musa tuliouona katika aya iliyotangulia ulithibiti na kuwa kweli, kwani wakati Firauni alipoiona adhabu ya kugharikishwa imemkabili hapo alitamka kwa unyenyekevu kuwa amemwamini Mola wa haki waliyemuamini Bani Israil. Lakini wapi! jibu alilopata ni kuwa, hivi sasa wakati mauti yamekukabili ndiyo unatubia na kuiamini haki. Hayo ni majuto matupu yaliyopitwa na wakati na majuto ni mjukuu. Miongoni mwa yale tunayojifunza kutokana na aya hizi ni kuwa katika kupambana na mataghuti, tutawakal na kumtegemea Mwenyezi Mungu tu, kwani yeye hatotuacha mkono bali atatufungulia njia ya faraja hata pale tutakapkuwa katika hali ngumu kabisa ya misukosuko. Funzo jengine tunalopata hapa ni kuwa, kama sisi tutasimama imara na bila kutetereka katika njia ya laa ilaha illa llah mataghuti hawatokuwa na jengine la kufanya ghairi ya kupiga magoti na kusalimu amri, na kupata jaza ya maovu yao. Aidha aya zinatuonyesha kuwa kuna umuhimu wa kuzitunza na kuzihifadhi athari na turathi za watu waliotangulia zinazoonyesha uwezo wa Allah sw, ili ziwe funzo na mazingatio kwetu sisi na watakaokuja baada yetu. Kwa haya machache tunaifunga darsa yetu hii, kwa kumwomba Allah atuwafikishe kutubia makosa yetu mara tu tunapoteleza, na kupata maghufira na msamaha wake kabla ya kufikwa na mauti. Amin. Wassalaamu Alaykum Warahmallahi Wabarakaatuh.
Zaidi katika kategoria hii: « Yunus 93-97 Yunus 79-86 »

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)

Hadithi ya Uongofu (39)

Ni matarajio yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji na tunakutana tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. …

Ufeministi, Itikadi na Misingi yake (26)

Assalaamu Alaykum wafuatiliaji wa kipindi hiki na karibuni kuwa nasi katika sehemu nyingine ya kipindi hiki kinachokosoa itikadi ya ufeministi …

Ulaji wa Lishe Bora katika Kipindi Chote cha Maisha

Wataalamu wa Afya wanasema kuwa, awamu mbalimbali za maisha zinahitajia ulaji wa chakula wa aina tofauti. Iwapo wewe ni mtoto, …

Maua mawili ya Mtume wa Allah (31) Sauti

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh Karibuni wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili Radio Tehran na wasomaji wa mtandao …