Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumatatu, 21 Aprili 2008 21:32

Yunus 79-86

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh. Karibuni katika mfululizo mwingine wa darsa ya quran. Hii ni darsa ya 321, na tukiwa tunaendelea kuizungumzia sura ya 10 ya Yunus tunaianza darsa yetu kwa aya za 79 na 80 ambazo zinasema:
"Na akasema Firauni: Nileteeni kila mchawi mjuzi."
"Basi walipokuja wachawi, Musa aliwaambia: Tupeni mnavyotaka kuvitupa."
Katika darsa iliyopita tulisema kuwa Nabii Musa as alitakiwa na Mola wake aianze kazi yake ya kulingania La ilaha illa llah kwa kumwendea Firauni na kumtaka aikubali tauhidi yaani kumuabudu Mungu mmoja wa haki na pia kuwakomboa Bani Israil na madhila ya Mafirauni. Aya tulizosoma zinasema Firauni, ambaye hakuwa na uwezo wa kukabiliana na huja na burhani alizopewa na Musa as alianza kuutuhumu muujiza alioonyeshwa na Nabii huyo kuwa ni uchawi na hivyo kutoa amri ya kuitwa wachawi wake wote ili kukabiliana na muujiza huo wa Mtume wa Allah Musa as. Lakini Nabii Musa ambaye hakuwa na chembe ya shaka kuwa haki iko upande wake aliwataka wachawi wa Firauni wafanye kila walichonacho cha uchawi na mazingaombwe yao ili watu wajionee wenyewe na kuamua. Hivyo miongoni mwa yale tunayojifunza kutokana na aya hizi ni kuwa mataghuti wa kila zama huamua kuwatumia vibaya wataalamu na taaluma zao ili kuweza kufikia malengo yao maovu. Aidha aya hizi zinatuelimisha kuwa Mitume walikuwa na yakini na risala waliyokuwa wakiilingania, na juu ya kupata nusra na msaada wa Allah sw.
Tunaiendeleza darsa yetu hii kwa aya za 81 na 82 ambazo zinasema:
"Walipotupa, Musa alisema: Mliyoleta ni uchawi; Mwenyezi Mungu sasa hivi ataubatilisha. Hakika Mwenyezi Mungu haitengenezi kazi ya waharibifu."
"Na Mwenyezi Mungu ataithubutisha haki kwa maneno yake, ingawa watachukia hao wabaya."
Kama ilivyoelezwa pia katika suratu Shuaraa, wachawi wa Firauni walitupa kamba zao na vifimbo vyao, na kutamka kuwa kwa utukufu wa Firauni tunaapa kuwa sisi ndio washindi. Hakika ni kuwa wachawi wa Firauni hawakufanya chochote kubadilisha kamba na vifimbo vyao, bali walifanya kiini macho tu na hivyo watu wakahisi kana kwamba vifimbo na kamba hizo zilikuwa zinaonyesha harakati za kutambaa. Na ndiyo maana Nabii Musa aliwatangazia kinagaubaga kuwa Mwenyezi Mungu atauanika hadharani ubatili wa uchawi wao huo na kuithibitisha haki mbele ya macho ya watu. Baadhi ya nukta za kuzingatiwa katika aya hizi ni kuwa hata kama batili itarembwa na kupambwa kwa kila namna ya urembo mwishowe itabainika na kutoweka tu. Nukta nyingine ya kuzingatiwa katika aya hizi ni kuwa nia na njama ya mustakbirina ya kutaka kuizima nuru ya haki haiwezi kufaulu na kusimama mbele ya irada ya Allah SW ambaye ameahidi kuwa nusra na msaada wake hautoacha kuwafikia wale waliosimama upande wa haki.
Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya 83 ambayo inasema:
"Hawakumuamini Musa isipokuwa baadhi ya vijana wa kaumu yake kwa kumuogopa Firauni na wakuu wao, wasiwatese. Kwani hakika Firauni alikuwa jeuri katika nchi. Na kwa yakini alikuwa miongoni mwa (maasi) waliopita mpaka."
Katika awamu ya kwanza ya kazi yake ya kulingania laa ilaha illa llah, Nabii Musa AS alimwendea Firauni na wasaidizi wake kisha katika awamu ya pili akakabiliana na wachawi na kuwashinda . Ama katika hatua ya tatu aliwafuata watu wa Bani Israil ambapo mwanzo wake ni vijana wa kaumu hiyo ndio waliomuamini. Tabaan vijana hao nao waliamini pamoja na kwamba walikuwa wakikabiliwa na mateso na madhila ya Firauni. Miongoni mwa yale tunayojifunza na kutokana na aya hii ni kuwa tabaka la kwanza kumwamini Musa katika Bani Israil lilikuwa ni tabaka la vijana, na hii ni kwa sababu nyoyo ya za vijana huwa safi na bongo zao huwa pia hazijakomazwa na fikra za kitaasubi. Halikadhalika aya hii inatuonyesha kuwa hata katika mifumo inayotawaliwa na mafirauni, mtu anaweza kujivua na upotofu wa mfumo huo na kushikamana na njia ya haki ya akina Musa AS.
Darsa ya 231 inahitimishwa na aya za 84, 85 na 86 ambazo zinasema:
"Na Musa akasema: "Enyi kaumu yangu Ikiwa nyinyi mumemwamini Mwenyezi Mungu, basi mtegemeeni yeye kama nyinyi ni Waislamu kweli."
"Wakasema: Tunamtegemea Mwenyezi Mungu. Ee Mola wetu. Usitufanye wenye kutiwa misukosuko na hao watu madhalimu."
"Na utuokoe kwa rehama yako na hao watu makafiri."
Katika kukabiliana na mateso makali na maudhi na madhila ya akina Firauni, Nabii Musa AS aliwataka watu wa kaumu yake watawakal kwa Mwenyezi Mungu na kuwaonyesha kuwa kutawakkal na kumtegemea Allah tu na kusalimisha muislamu mambo yake yote kwa Mola wa haki ni sharti la imani ya kweli. Nao wale waliokuwa wamemuamini kikweli kweli Musa as waliyasikiliza mawaidha hayo waliyopewa na Mtume wao na kusema, sisi hatuna kimbilio wala egemeo jengine ghairi ya Allah sw na hivyo tunamuelekea yeye na kumwomba atulinde na shari ya madhalimu na makafiri. Baadhi ya mafunzo tunayoyapata kutokana na aya hizi ni kuwa wakati wa masaibu na misukosuko Mola Mwenyezi huwa ndiye tegemeo pekee la mja muumini, na kwa kweli kwa kumtegemea yeye Mola aliye Muweza wa kila kitu na kujisalimisha kwake kwa kushikamana na maamrisho yake na kujiepusha makatazo yake, mja huweza kufaulu katika kukabiliana na misukosuko yoyote inayomkuta. Aidha kutokana na aya hii tunajielimisha kuwa dua na kushtakia hali yake mja kwa Mola, ni miongoni mwa njia za kumnasua mja na mazonge. Kwa haya machache tunaifunga darsa yetu ya juma hili na kumwomba Mola aijaze subra ndani ya nyoyo zetu, athibitshe imani zetu na atunusuru na kila fitna inayoweza kutuweka mbali na dini yetu. Amin. Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.
Zaidi katika kategoria hii: « Yunus 87-92 Yunus 74-78 »

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)

Hadithi ya Uongofu (39)

Ni matarajio yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji na tunakutana tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. …

Ufeministi, Itikadi na Misingi yake (26)

Assalaamu Alaykum wafuatiliaji wa kipindi hiki na karibuni kuwa nasi katika sehemu nyingine ya kipindi hiki kinachokosoa itikadi ya ufeministi …

Ulaji wa Lishe Bora katika Kipindi Chote cha Maisha

Wataalamu wa Afya wanasema kuwa, awamu mbalimbali za maisha zinahitajia ulaji wa chakula wa aina tofauti. Iwapo wewe ni mtoto, …

Maua mawili ya Mtume wa Allah (31) Sauti

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh Karibuni wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili Radio Tehran na wasomaji wa mtandao …