Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumatatu, 21 Aprili 2008 21:32

Yunus 74-78

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh. Tunamshukuru Mwenyezi Mungu mtukufu kwa kutuwafikisha kukutana tena katika darsa yetu hii. Sura ya 10 ya Yunus ndiyo tunayoizungumzia kwa sasa, na hii ni darsa ya 320 tunayoianza kwa aya 74 na 75 ambazo zinasema:
"Kisha tukawapeleka Mitume (wengi) baada yake kwa watu wao. Nao wakawajia na hoja waziwazi. Lakini hawakuwa wenye kuamini waliyoyakadhibisha kabla yake." "Namna hivi tunapiga muhuri juu ya nyoyo za watu warukao mipaka."
Kisha baada ya hao tukamtuma Musa na Haruni kwa Firauni na watu wake wakubwa, kwa hoja zetu. Lakini walijivuna, wakawa watu maasi.
Aya tulizosoma zinaashiria utaratibu alioweka Mwenyezi Mungu mtukufu kuhusiana na utumaji wa Mitume mmoja baada ya mwingine kwa ajili ya kuwafikishia waja wake risala ya uongofu na kusema kuwa manabii walikuwa na miujiza mbali mbali kwa ajili ya kuthibitisha ukweli kwamba risala walizokuja nazo zinatoka kwa Mwenyezi Mungu mtukufu. Na kwa hakika ukweli huo uliwathibitikia wale waliofikishiwa risala hizo. Pamoja na hayo akthari ya watu hawakuwa tayari kuikubali haki kutokana na kutopea kwenye ufuska na mambo machafu vitu ambavyo havikubaliani na sifa ya kushikamana na mafundisho ya dini. Ijapokuwa wakati ilipotokea tufani ya gharika katika enzi za Nabii Nuh as makafiri wote waliangamizwa, na ni wale tu waliokuwa wamemwamini Mtume huyo na kuabiri pamoja naye jahazini ndio waliookoka, lakini baada ya Nabii huyo walizuka tena makafiri na mushirikina wengi na hivyo na kupelekea Mwenyezi Mungu kutuma manabii wengine kadhaa wakiwemo Ibrahim, Ismali, Hud, Saleh, Yaaqub, Yusuf n.k. Pamoja na hayo watu waliendelea kuonyesha inadi, ukaidi na upinzani dhidi ya haki na kama walivyokuwa wakanushaji waliowatangulia hawakuwa tayari kuacha maovu ya kiitikadi na kimatendo na kuamini wito wa haki. Baada ya manabii hao, Nabii mwingine mteule yaani Musa as akiwa pamoja na ndugu yake Harun amani ya Allah iwe juu yake, walitumwa kwa Firauni ili kumfikishia wito wa Lailaha illa llah. Lakini naye pia pamoja na watu wake walitakabari na kuipa mgongo haki. Baadhi ya mafunzo tunayoyapata kutokana na aya hizi ni kuwa Allah sw amehakikisha kwamba anawapelekea waja wake Mitume wa kuwalingania uongofu, lakini wakati huo huo amempa mwanadamu uhuru kamili wa kuchagua kati ya kuamini na kuikufuru haki, kwani hakutaka mwanadamu aiamini na kuifuata dini yake ya haki kwa kulazimishwa na kutezwa nguvu.
Zifuatazo sasa ni aya za 76 na 77 ambazo zinasema:
"Basi ilipowajia haki kutoka kwetu walisema: Bila shaka huu ni uchawi dhahiri."
"Akasema Musa: Mnasema (hivi) juu ya haki ilipokujieni? Huu ni uchawi? Na wachawi hawafaulu!"
Mojawapo ya mbinu zilizokuwa zikitumiwa na wapinzani wa Mitume na hasa wale vigogo wa ukafiri na shirki ilikuwa ni kuzusha tuhuma zisizo na msingi kwa waja hao wateule wa Allah. Na ndiyo maana Quran tukufu inaeleza kuwa takriban Mitume wote hawakusalimika na tuhuma za kusingiziwa kuwa ni wachawi, ili miujiza waliyokuja nayo ionekane kuwa ni vitendo vya hila na hadaa na wao wenyewe wachukuliwe kuwa ni watu wajanja na matapeli. Kama aya zinavyoeleza, wakati Firauni alipoona ameshindwa kukabiliana na hoja za kimantiki za wito wa haki wa Nabii Musa aliamuru wachawi wake wote wakusanywe pamoja ili kumfanya Mtume huyo wa Allah aonekane naye pia kuwa ni mchawi tu kama walivyo wachawi wake. Hali ya kuwa alichokuwa akikieleza Nabii Musa ni kwamba nyinyi kina Firauni na watu wenu hamjawahi kunishuhudia hapo kabla nikifanya uchawi au kiini macho, lakini sasa nimekuja na wito wa haki na kuthibitisha ukweli wa Utume wangu kwa kukuonyesheni muujiza mnanisingizia kuwa ni mchawi na maneno yangu nayo mnadai kuwa ni uchawi. Ukweli ni kuwa hicho ni kisingizio tu kwa ajili ya kuipa mgongo haki. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kuwa viongozi wa dini wanatakiwa waelewe kuwa siku zote watakuwepo watu katika jamii watakaowapiga vita na kuipinga haki na hata kutaka haki hiyo ionekane kuwa ni batili.
Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 320 inahitimishwa na aya ya 78 ambayo inasema:
"Wakasema: Je umetujia ili utuachishe tuliyowakuta nayo baba zetu na ili ukubwa uwe wenu nyinyi (wawili) katika nchi (hii)? Wala sisi hatukuaminini nyinyi."
Kwa sababu ya kuonyesha heshima ya wazee wao waliowatangulia watu wengi huwa hawako tayari kuacha mila na desturi walizozioea na kurithi kutoka kwao, na kujenga dhana kwamba kila kilichosemwa na hao mababa na mababu zao kilikuwa sahihi, na mtu yeyote yule hana haki ya kusema kinyume na dhidi ya hayo. Hali ya kuwa kuwaheshimu waliotangulia ni kitu kimoja na kung'ang'ania bila hoja bali kwa taasubi na ukereketwa tu kila lililosemwa na kutendwa na wao, na kuhisi sisi wa baada ya wao tufanye kile kile kilichofanywa na wao hata kama si sahihi, hicho nacho ni kitu kingine kabisa. Na ni kwa mantiki hiyo isiyo sahihi, ndio maana wapinzani wa Mitume walikuwa wakishikilia kwamba maadamu wazee wetu walikuwa wakiabudu masanamu, sisi hatuko tayari kuamini bali hata kusikia kitu kingine ghairi ya hicho. Funzo mojawapo tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa kushikilia kufuata kibubusa itikadi potofu za waliotangulia ni miongoni mwa sababu kuu zilizowafanya watu wengi wapinge risala za Mitume wao. Wapenzi wasikilizaji darsa ya 320 imefikia tamati. Tunamwomba Allah atuonyeshe haki na kutuwafikisha kuifuata, na atuonyeshe batili na kutuwezesha kuiepuka. Amin. Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.
Zaidi katika kategoria hii: « Yunus 79-86 Yunus 68-73 »

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)

Hadithi ya Uongofu (39)

Ni matarajio yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji na tunakutana tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. …

Ufeministi, Itikadi na Misingi yake (26)

Assalaamu Alaykum wafuatiliaji wa kipindi hiki na karibuni kuwa nasi katika sehemu nyingine ya kipindi hiki kinachokosoa itikadi ya ufeministi …

Ulaji wa Lishe Bora katika Kipindi Chote cha Maisha

Wataalamu wa Afya wanasema kuwa, awamu mbalimbali za maisha zinahitajia ulaji wa chakula wa aina tofauti. Iwapo wewe ni mtoto, …

Maua mawili ya Mtume wa Allah (31) Sauti

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh Karibuni wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili Radio Tehran na wasomaji wa mtandao …