Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumatatu, 21 Aprili 2008 21:31

Yunus 68-73

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh. Karibuni katika mfululizo huu wa 319 wa darsa ya quran, tukiwa tunaendelea kuizungumzia sura ya 10 ya Yunus. Tunaianza darsa yetu kwa aya za 68, 69 na 70 ambazo zinasema:
"Wamesema: Mwenyezi Mungu amejifanyia mtoto. Ameepukana na hayo. Yeye ni Mkwasi Mwenye kujitosheleza. Ni vyake vilivyomo mbinguni na vilivyomo ardhini. Nyinyi hamna uthibitisho wowote wa haya. Mnamzulia Mwenyezi Mungu msiyoyajua?
Sema: Wale wanaomzulia Mwenyezi Mungu uwongo hawatafaulu."
"Hiyo ni starehe ya katika dunia tu, kisha kwetu ndiyo marejeo yao ni kwetu. Hapo tutawaonjesha adhabu kali kwa sababu ya kukufuru kwao."
Moja kati ya itikadi porofu na ya uzushi ambayo walikuwa nayo watu wa kaumu na uma zilizopita na ambayo inashuhudiwa pia hata hii leo ni kumjaalia Mwenyezi Mungu kuwa na wana na kuwanasibisha na yeye Mola Mwenyezi. Katika historia ya Uyahudi, wafuasi wa dini hiyo walimfanya Uzair mwana wa Mungu, nao wakristo wakatenda hayo hayo kuhusiana na Nabii Issa mwana wa Maryam. Hali ya kuwa kwanza kabisa ni kwamba Mwenyezi Mungu hana mke hata awe na mtoto. Pili ni kuwa Allah hahitaji kuwa na mwana, na tatu ni kwamba mtu ambaye ni kiumbe aliyeumbwa kamwe hawezi kuwa mwana wa Mungu kwa sababu jinsia ya mtoto hutokana na ile ya wazazi wake wawili yaani baba na mama, hali ya kuwa kama tulivyotangulia kusema Mwenyezi Mungu aliyetukuka ametakasika na sifa ya kuwa na mke. Kuhusiana na kauli zote hizo za batili na zisizo na mashiko quran tukufu inasema wale wanaotamka maneno hayo wajue kwamba lazima watawajibika kwayo, na siku ya kiyama watakuja kupata adhabu kali kwa sababu ya uzushi huo waliomnasbishia nao Mwenyezi Mungu sw. Baadhi ya yale tunayojifunza kutokana na aya hizi ni kuwa Mola mtukufu hatishwi na upweke hata ahitajie mwana kwa ajili ya kuuondoa upweke huo. Hahitajii msaada hata na awe na shida ya kuwa na msaidizi, na wala hachelei kuondoka hata iwepo haja ya mrithi wa baada yake. Subhanallah, ametakasika Mola aliyetukuka na kasoro zote hizo bali na nyinginezo. Aidha aya zinatuonyesha kuwa lau mja angelinganisha mapungufu yaliyonayo maisha ya kupita ya dunia na hilaki ya adhabu isiyoweza kukadirika ya akhera basi angechunga na kujiweka mbali na kutamka mengi na kutenda mengi yanayomghadhibisha Mola wake.
Ifuatayo sasa ni aya ya 71 ambayo inasema:
"Wasomee khabari za Nuhu alipowaambia watu wake:"Enyi watu wangu! Ikiwa kukaa kwangu nanyi na kukumbusha kwangu Aya za Mwenyezi Mungu kunakuchukizeni, basi mimi namtegemea Mwenyezi Mungu. Nanyi tengenezeni mambo yenu na hao washirika wenu. Tena shauri lenu hilo lisifichikane kwenu. Kisha nihukumuni.Wala msinipe muhula."
Nabii Nuh AS ni mmoja wa Mitume wateule wa Allah ambaye kwa miaka mingi sana alifanya kazi ya kuwalingania watu wa kaumu yake, lakini ni wachache tu miongoni mwao waliomuamini na akthari yao waliendelea kubaki kwenye shirki na ukafiri. Aya hizi ambazo zilishuka huko Makka zinawaliwaza waislamu ambao walikuwa katika unyonge na hali ngumu ya maisha na kuwataka wawe na imani ya kupata msaada wa Mwenyezi Mungu na kuelewa kwamba Allah sw yuko pamoja na wao na hivyo wasimame imara kama alivyosimama Nabii Nuh as ambaye licha ya vitisho na kila aina ya njama za wapinzani wa haki alisimama peke yake na kubeza nguvu na vitisho vyao kwa kuwaambia jumuikeni pamoja nyote na amueni chochote mnachotaka kuamua juu yangu, lakini jueni kwamba mimi nimetawakal kwa Mwenyezi Mungu na kutegemea nguvu na uwezo wake yeye tu. Aya hii inatuelimisha kuwa historia ya waliotutangulia inabainisha wazi kwamba haki ni yenye kubaki na mwisho wa batili ni kutoweka na kwa hakika kuelewa yaliyojiri huko nyuma kunatoa mwanga wa kuonyesha njia ya huko tunakoelekea.
Aya za 72 na 73 ndizo zinazotuhitimishia darsa yetu ya juma hili. Aya hizo zinasema:
"Lakini mkikengeuka (khiyari yenu). Mimi sikuombeni ujira. Ujira wangu hauko ila kwa Mwenyezi Mungu. Na nimeamrishwa niwe miongoni mwa wanaojisalimisha kwake."
"Lakini walimkadhibisha. Basi tukamuokoa pamoja na waliokuwa naye katika jahazi. Na tukawafanya wao ndio waliobakia. Na tukawazamisha wale waliozikadhibisha Aya zetu. Basi angalia vipi ulikuwa mwisho wa wale walioonywa (wasisikie)."
Katika harakati yao ya kuwalingania watu njia ya Mwenyezi Mungu Mitume sio tu walikuwa tayari kukabiliana na hatari yoyote hata inayotishia maisha yao lakini pia hawakutarajia kupata chumo au mali yoyote ile ya dunia kwa sababu ya kazi hiyo nzito waliyokuwa wakifanya. Kwa maneno mengine ni kuwa hawakuwa wakitarajia chochote kwa watu mkabala wa kheri waliyokuwa wakiwafikishia. Na ndiyo maana walikuwa wakiwaeleza bayana watu wao kwamba msidhani kuwa msipotuamini, kuna hasara tutakayopata kwani hatutarajii kupata ujira au malipo yoyote yale kutoka kwenu; sisi tunafanya yale tu tuliyoamrishwa na Mola wetu. Kisha aya zinaendelea kubainisha mwisho na hatima ya wapingaji haki na kueleza kuwa kwa kuteremka adhabu ya Mwenyezi Mungu na dhoruba kali, maji yalifunika kila kitu na ni wale waliokuwa wamepanda jahazi na Nabii Nuh ndio wao tu waliookoka na wakawa warithi wa ardhi, na kwamba hakuna mwisho mwingine unaowapata wale wanaoonywa wakapuuza zaidi ya huo uliowapata waliomkadhibisha Nauh as. Kwa haya machache wapenzi wasikilizaji ndiyo tumefikia tamati ya darsa hii ya 319 ya quran. Tunamwomba Mwenyezi Mungu atulinde na kila aina ya shirki na kutuwafikisha kumwabudu kwa ikhlasi na kumtakasia dini yake. Amin. Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.
Zaidi katika kategoria hii: « Yunus 74-78 Yunus 62-67 »

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)

Hadithi ya Uongofu (39)

Ni matarajio yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji na tunakutana tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. …

Ufeministi, Itikadi na Misingi yake (26)

Assalaamu Alaykum wafuatiliaji wa kipindi hiki na karibuni kuwa nasi katika sehemu nyingine ya kipindi hiki kinachokosoa itikadi ya ufeministi …

Ulaji wa Lishe Bora katika Kipindi Chote cha Maisha

Wataalamu wa Afya wanasema kuwa, awamu mbalimbali za maisha zinahitajia ulaji wa chakula wa aina tofauti. Iwapo wewe ni mtoto, …

Maua mawili ya Mtume wa Allah (31) Sauti

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh Karibuni wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili Radio Tehran na wasomaji wa mtandao …