Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumatatu, 21 Aprili 2008 21:31

Yunus 62-67

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh. Tunamshukuru Mwenyezi Mungu mtukufu kwa kutuwafikisha kukutana tena katika darsa yetu hii. Sura ya 10 ya Yunus ndiyo tunayoizungumzia kwa sasa, na hii ni darsa ya 318 tunayoianza kwa aya za 62, 63 na 64 ambazo zinasema:
"-Jueni kuwa vipenzi vya Mwenyezi Mungu hawatakuwa na khofu (siku ya Kiyama) wala hawatahuzunika."
"-Nao ni wale ambao waliamini na wakawa wanamcha Mungu."
"-Wao bishara njema katika maisha ya dunia na katika Akhera. Hapana mabadiliko katika maneno ya Mwenyezi Mungu. Huko ndiko kufuzu kukubwa."
Katika darsa kadhaa zilizopita tulisoma aya zilizozungumzia hali ngumu ya adhabu watakayokabiliana nayo wale waliokufuru na kumshirikisha Allah sw. Aya tulizosoma hivi punde zinabainisha hali watakayokuwa nayo waumini wa kweli waliomcha Mwenyezi Mungu, ili kwa kulinganisha hali za makundi mawili hayo iweze kufahamika ni ipi njia ya saada na ipi yenye mwisho mbaya. Utulivu wa roho na kutopatwa na ghamu wala hali yoyote ya huzuni ni miongoni mwa neema kubwa ambazo Allah atawatunuku waja wake wema. Waja ambao kutokana na kujiweka mbali na madhambi na maovu waliweza kujikurubisha kwenye chemchemu ya usafi, mema na mazuri yote yaani Allah sw na kwa taabiri ya quran tukufu kuingia kwenye kundi la mawalii yaani vipenzi vya Mwenyezi Mungu. Ni wazi kuwa nafsi za watu kama hao siku zote humiminikiwa na rehma za bishara njema za Mola Karima na hivyo katu huwa hawapatwi na shaka, ugoigoi au hali ya ulegevu katika kutekeleza majukumu yao ya kidini. Bwana Mtume Muhammad saw amesema:" Kimya cha mawalii wa Mwenyezi Mungu ni dhikri, kutazama kwao ni ibra, maneno yao ni hikima na harakati zao katika jamii, ni sababu ya kupatikana baraka. Naye Imam Ali as amesema: "Usije ukamdunisha mtu yoyote yule, kwani Mwenyezi Mungu ameficha mawalii wake miongoni mwa watu, hivyo si hasha yule umdunishaye akawa ni mmoja wao na wewe usijue". Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kuwa yule ambaye moyo wake unamkhofu Mwenyezi Mungu tu hawezi kumkhofu yeyote mwengine. Aidha aya zinatuonyesha kuwa imani bila taqwa huwa haina athari; muumini wa kweli ni yule ambaye kila wakati anajichunga na kujiweka mbali na maovu na mambo machafu.
Zifuatazo sasa ni aya za 65 na 66 za sura yetu ya Yunus ambazo zinasema:
"-Wala yasikuhuzunishe maneno yao. Hakika utukufu wote ni wa Mwenyezi Mungu.Yeye ndiye asikiaye na ajuaye."
"-Jueni kuwa ni vya Mwenyezi Mungu vyote vilivyomo mbinguni na ardhini. Na wala hawawafuati hao wanaowaomba badala ya Mwenyezi Mungu kuwa ni washirika wake. Wao hawafuati ila dhana tu na hawasemi ila uwongo."
Mushirikina wa Makka walikuwa wakimsingizia Bwana Mtume kila sifa mbovu kama vile kusema kwamba yeye ni mshairi, kuhani na mchawi bali hata mwendawazimu na wakisema: maneno haya ayasemayo Muhammad anafundishwa na watu wengine. Na wakati mwingine wakisema kuwa yeye ni mtu kama wao tu wala lolote la ubora zaidi yao. Katika kuyajibu maneno hayo yasiyo na msingi ya Mushirikina Allah sw anamliwaza Mtume wake kwa kumwambia, irada ya Mola wako imeshakata na kuhukumu kuwa wewe na wafuasi wako muwe na izza na utukufu; nao hao mushirikina hawawezi kufanya lolote kukabiliana na irada hiyo. Na sababu ni kuwa ulimwengu na kila kilichomo ndani yake viko chini ya mamlaka yake Mola wako aliyetukuka, na kwa hivyo wale wanaowaendea waola ghairi ya Mwenyezi Mungu mtukufu si wao wenyewe wala hao waungu wao bandia walio na uwezo wa kufanya lolote. Aya hii pamoja na mambo mengine inatuelimisha kuwa mojawapo ya mbinu zinazotumiwa na maadui wa Uislamu ni kuharibu haiba na shakhsiya ya viongozi wa dini hiyo tukufu. Na hilo halikuishia katika zama za mwanzoni mwa kudhihiri kwa Uislamu bali linaendelea kushuhudiwa hata katika zama zetu hizi. Hata hivyo Allah sw ameshaahidi kuwa maadui hao katu hawatofanikiwa kwa kupitia njia hiyo kulifikia lengo lao hilo.
Tunaihitimisha darsa yetu ya 318 kwa aya ya 67 ambayo inasema:
"-Yeye (Mwenyezi Mungu) ndiye aliyekujaalieni usiku mpate kutulia humo, na mchana wa kuonea. Hakika katika hayo zimo ishara kwa watu wanaosikia."
Aya iliyopita imeashiria utawala mutlaki wa Allah SW katika ulimwengu na kila kilichomo ndani yake. Aya tuliyosoma ya 67 inagusia tadbiri yenye hikima kubwa ya Mola na kueleza kuwa mfumo wa mabadiliko ya usiku na mchana ni mojawapo ya madhihirisho ya uwezo wa Mola Mwenyezi katika uendeshaji wa ulimwengu. Katika aya mbali mbali za quran usiku umetajwa kuwa kitoa utulivu cha mwanadamu. Ni wazi kwamba wakati ambapo utulivu wa kiwiliwili unayumkinika kwa kulala na kupumzika, utulivu wa roho hupatikana kwa dua, minong'ono na kushtakia mja hali yake kwa Mola na Muumba wake. Aya hii pamoja na mambo mengine inatuelimisha kuwa mfumo tuushuhudiao wa ulimwengu haukutokea kwa bahati tu bali ni kitu kilichoumbwa na kuendeshwa kwa lengo na irada maalumu. Kwa haya machache wapenzi wasikilizaji tunaifunga darsa yetu ya juma hili. Inshallah Mwenyezi Mungu atujaalie kuwa miongoni mwa waja wake washukurivu wa neema zake na wanaozingatia na kuyatafakari maumbile ya ulimwengu ili kuweza kuitambua ipasavyo adhama ya Mola wao... Amin. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.
Zaidi katika kategoria hii: « Yunus 68-73 Yunus 57-61 »

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)

Hadithi ya Uongofu (39)

Ni matarajio yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji na tunakutana tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. …

Ufeministi, Itikadi na Misingi yake (26)

Assalaamu Alaykum wafuatiliaji wa kipindi hiki na karibuni kuwa nasi katika sehemu nyingine ya kipindi hiki kinachokosoa itikadi ya ufeministi …

Ulaji wa Lishe Bora katika Kipindi Chote cha Maisha

Wataalamu wa Afya wanasema kuwa, awamu mbalimbali za maisha zinahitajia ulaji wa chakula wa aina tofauti. Iwapo wewe ni mtoto, …

Maua mawili ya Mtume wa Allah (31) Sauti

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh Karibuni wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili Radio Tehran na wasomaji wa mtandao …