Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumatatu, 21 Aprili 2008 21:29

Yunus 57-61

Bismillahir Rahmanir Rahim. Tunamshukuru Mwenyezi Mungu mtukufu kwa kutuwafikisha kukutana tena katika darsa yetu hii. Sura ya 10 ya Yunus ndiyo tunayoizungumzia kwa sasa, na hii ni darsa ya 317 tunayoianza kwa aya za 57 na 58 ambazo zinasema:
Enyi watu Yamekujieni mawaidha kutoka kwa Mola wenu, na poza kuponyesha yaliyomo vifuani, na uwongofu, na rehema kwa waumini.
Sema: Kwa fadhila ya Mwenyezi Mungu na rehma yake! Basi nawafurahi kwa hayo. Haya ni bora kuliko hayo wanayoyakusanya.
Roho ya mwanadamu wapenzi wasikilizaji kama ulivyo mwili wake huzongwa na mashaka na magonjwa mbali mbali ya kinafsi na hivyo nayo pia huhitajia dawa. Maradhi ya kiroho kama vile kiburi, ghururi, ubakhili, uhasidi na riya, kama hayatopatiwa dawa huweza kumfanya mtu aishie kwenye ukafiri na unafiki na kumtoa kwenye njia ya uongofu. Na kwa hivyo quran kutokana na mawaidha na maonyo yake ya mara kwa mara huweza kumkinga mtu na kumwezesha kuepuka madhambi mbali mbali. Kwa upande mwingine kwa kubainisha adhabu iliyoandaliwa na Mwenyezi Mungu kwa ajili ya waovu, kitabu hicho cha mbinguni humzindua na kumtanabahisha mwanadamu na matendo yake maovu ili achukue hatua ya kuisafisha na kuitakasa roho yake. Ni wazi kwamba nafsi zilizo safi ndizo zinazoweza kupata taufiki ya kuufikia uongofu wa Allah sw. Hivyo Mola Mwenyezi anamtaka Mtume wake awaeleze waumini kwamba rasilimali bora kabisa kwao ni hiyo imani yao kwa kitabu cha Allah na kushikamana kwao na kitabu hicho, na kwa kweli wana kila sababu ya kufurahia kupata neema hiyo kubwa na si kupaparikia vyeo na utajiri wa kidunia. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kuwa quran ndiyo ponya na dawa bora kabisa kwa nyoyo zenye maradhi na nafsi zilizo chafu kimaadili. Aidha kutokana na aya hizi tunabaini kuwa quran ndiyo hazina na kito chenye thamani kubwa zaidi kuliko utajiri wa aina yoyote ile wa kidunia. Kwa hakika fukara hasa ni yule mtu aliyekosa mafundisho matukufu ya kitabu hicho, hata kama atakuwa amejikusanyia mali na kila aina ya utajiri. Na kinyume chake tajiri na aliye mkwasi hasa ni yule anayeishi maisha ya kiquran hata kama kwa mtazamo wa kimaada na kidhahiri hatokuwa na mali wala utajiri wowote.
Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya za 59 na 60 ambazo zinasema:
"Sema: Je! Mwaonaje zile riziki alizo kuteremshieni Mwenyezi Mungu, nanyi mkafanya katika hizo nyengine haramu na nyengine halali. Sema:Je! Mwenyezi Mungu amekuruhusuni, au mnamzulia Mwenyezi Mungu tu?"
"Na nini dhana ya wanaomzulia Mwenyezi Mungu kwa Siku ya Kiyama? Hakika Mwenyezi Mungu ana fadhila juu ya watu, lakini wengi wao hawashukuru."
Aya zilizotangulia zimezungumzia rehma na uongofu wa quran. Zikiendeleza yale yaliyokuja katika aya hizo aya hizi zinasema yule ambaye amejiweka mbali na quran hutumbukia kwenye mkumbo wa kufuata mambo ya uzushi na kubuni na kanuni zisizo na mashiko, ambayo yenyewe ni chanzo cha masaibu na matatizo mbali mbali yanayowatinga watu katika maisha yao. Kama ilivyo katika aya nyingine, quran tukufu inaashiria hapa tabia waliyokuwa nayo washirikina ya kujiharamishia kula wanyama wa miguu mine na baadhi ya mazao ya kilimo na badala yake wakivichukua vitu hivyo na kuviweka nadhiri kwa ajili ya masanamu yao. Katika aya tulizosoma quran tukufu inawaambia washirikina hao kuwa riziki yenu nyinyi inatoka kwa Mwenyezi Mungu, na hivyo ni yeye ndiye mwenye haki ya kuamua kipi kiwe halali na kipi kiwe haramu kula, na wala sio nyinyi; vinginevyo muonyeshe kama mumepata idhini kutoka kwake yeye Allah sw ya kufanya hayo, hali ya kuwa nyinyi hamjapewa haki hiyo. Hivyo basi mjiandae kwenda kujieleza siku ya Kiyama kuhusu uzushi na uwongo huo mliojitungia. Aya zinaendelea kubainisha kuwa neema za Mwenyezi Mungu kwa waja ni kielelezo cha fadhila na ukarimu wake Mola lakini wanaadamu si washukurivu wa neema hizo ambazo huwaondokea kutokana na kuzusha kwao aina kwa aina za mambo ya upotofu na yasiyo na msingi. Baadhi ya mambo tunayojifunza kutokana na aya hizi ni kuwa neema zote zinatoka kwa Mwenyezi Mungu na hivyo ni yeye ndiye mwenye haki ya kuhalalisha na kuharamisha vitu, na si wanadamu kutokana na utashi na matamanio yao ya kinafsi wajiamulie watakavyo kuhalalisha hiki na kuharamisha kile. Aidha aya zinatutaka tuelewe kuwa aliye na mamlaka ya kuweka sheria kwa ajili ya wanadamu ni Allah pekee, na hivyo sheria yeyote inayotungwa na wanadamu ikakinzana na sheria yake ni bidaa na haina itibari.
Aya ya 61 ndiyo inayotuhitimishia darsa yetu hii. Aya hiyo inasema:
"Na huwi katika jambo lolote, wala husomi sehemu yoyote katika Quran, wala hamtendi kitendo chochote ila Sisi huwa ni mashahidi juu yenu mnapo shughulika nayo. Na hakifichikani kwa Mola wako Mlezi chenye uzito hata wa chembe katika ardhi na katika mbingu, wala kidogo kuliko hicho wala kikubwa ila kimo katika Kitabu kilicho wazi."
Aya hii inaashiria elimu isiyo na mpaka ya Allah sw iliyo na utambuzi wa hali na harakati zote za mwanadamu, na kuelewa kila tendo litendwalo, liwe kubwa au dogo, la siri na la dhahiri, linalojiri kila mahala na katika kila sekunde, iwe ni katika ulimwengu wa mbinguni au wa ardhini na kuyahifadhi yote hayo katika lauhim mahfuudh. Kwa hakika matendo yote ya waja, mbali na kushuhudiwa moja kwa moja na yeye Mola Karima yanaandikwa na kuhifadhiwa pia na malaika wake ambao huwa pamoja na waja ili kushuhudia na kuyanakili mazuri yote na mabaya yote wanayotenda. Baadhi ya nukta za kuzingatiwa katika aya hii ni kuwa matendo yetu yote bali hata yale yanayotupitikia akilini na katika nafsi zetu yanashuhudiwa na kujulikana na Mwenyezi Mungu sw pamoja na malaika wake. Na kwa kweli hakuna chochote kinachofichika kwao. Wapenzi wasikilizaji darsa yetu ya juma hili inaishia hapa. Tunamwomba Mola atulinde na hatari ya kuhalalisha vile alivyoviharamisha yeye na kuharamisha vile vilivyohalalishwa na yeye Mola Karima. Amin. Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.
Zaidi katika kategoria hii: « Yunus 62-67 Surat Yunus 50-56 »

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)

Hadithi ya Uongofu (39)

Ni matarajio yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji na tunakutana tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. …

Ufeministi, Itikadi na Misingi yake (26)

Assalaamu Alaykum wafuatiliaji wa kipindi hiki na karibuni kuwa nasi katika sehemu nyingine ya kipindi hiki kinachokosoa itikadi ya ufeministi …

Ulaji wa Lishe Bora katika Kipindi Chote cha Maisha

Wataalamu wa Afya wanasema kuwa, awamu mbalimbali za maisha zinahitajia ulaji wa chakula wa aina tofauti. Iwapo wewe ni mtoto, …

Maua mawili ya Mtume wa Allah (31) Sauti

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh Karibuni wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili Radio Tehran na wasomaji wa mtandao …