Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumatatu, 21 Aprili 2008 21:29

Surat Yunus 50-56

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh. Karibuni katika mfululizo huu wa 316 wa darsa ya quran, tukiwa tunaendelea kuizungumzia sura ya 10 ya Yunus. Tunaianza darsa yetu kwa aya za 50 na 51 ambazo zinasema:
"Sema: Mwaonaje ikikufikieni hiyo adhabu yake usiku au mchana, basi kwa nini wenye makosa wanaitake ije haraka?"
"Tena Je! Ikishatokea mtaiamini? Ndio sasa tena? Na nyinyi mlikuwa mkiihimiza."
Aya hizi zinatoa jibu kwa wale wanaokanusha kufufuliwa kwa viumbe ambao walikuwa wakisema, hiyo adhabu ya Mwenyezi Mungu itatokea lini? Ndipo Bwana Mtume akatakiwa awajibu kuwa hivi nyinyi mnaoharakisha mteremshiwe adhabu, kama adhabu hiyo itakushukieni ghafla iwe ni mchana au pengine usiku mkiwa mmelala, mtafanya nini wakati huo? Je mtaweza kupata pa kukimbilia au kuwa na nguvu za kuizuia isikupateni? Kama mnadhani pia kwamba ikiwa mtaiamini haki pale mtakapoanza kuona ishara za kuteremka adhabu na kuwa imani yenu hiyo itaweza kukufaeni, basi dhana yenu hiyo ni batili, kwani pale itakaposhuka adhabu milango ya toba itafungwa na hivyo imani katika lahadha hiyo haitokuwa na taathira yoyote. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kuwa kuamini mtu wakati hatari iko mbele ya macho yake hakuna thamani yoyote, kwani imani ya aina hiyo si ya hiyari wala ya kuitakidiwa moyoni, bali ni imani inayotokana na khofu ya lisilo budi.
Ifuatayo sasa ni aya ya 52 ambayo inasema:
"Kisha waliodhulumu wataambiwa: Onjeni adhabu ya kudumu. Kwani mtalipwa isipokuwa yale mliyokuwa mkiyachuma?"
Katika aya zilizotangulia lilizungumziwa suala la adhabu ya Mwenyezi Mungu ya hapa duniani inayowashukia kwa ghafla waovu na waliomkufuru Mola Aliyetukuka. Aya hii ya 52 inaashiria adhabu ya milele itakayowapata waovu hao siku ya Kiyama kwa sababu ya dhulma waliojitendea wao wenyewe na kuwatendea wanadamu wenzao. Baadhi ya mafunzo tunayoyapata kutokana na aya hii ni kuwa katika mafundisho ya Uislamu mpaka wa dhulma hauishii katika kutenda dhulma kwa wengine tu, lakini hata madhambi anayoyafanya yeye mwenyewe mtu yanahesabika pia kuwa ni dhulma, kwani ufanyaji dhambi huo ni sawa na mtu kujidhulumu nafsi yake na pia kuwafanyia dhulma Mitume wa Allah ambao walitaabika na kupata mashaka mengi kwa ajili ya kuhakikisha uongofu utokao kwa Allah unawafikia waja wake. Aidha aya inatuelimisha kuwa adhabu ya Mwenyezi Mungu itakuwa ya kiadilifu kulingana na amali zake mwenyewe mja, bila kuzidishiwa kitu.
Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya za 53 na 54 ambazo zinasema:
"Na wanakuuliza: Je! ni kweli hayo? Sema: Ehe! Naapa kwa Mola wangu! Hakika hayo ni kweli nanyi hamuwezi kumshinda (Mwenyezi Mungu)."
"Na lau kuwa kila nafsi iliyodhulumu inamiliki kila kilichomo duniani, bila shaka ingelitoa vyote kujikombolea. Na watakapoiona adhabu watajitahidi kuficha majuto yao. Na patahukumiwa baina yao kwa uadilifu nao hawatodhulumiwa."
Baada ya aya zilizotangulia kuelezea juu ya ushukaji wa adhabu ya Allah kwa waovu hapa duniani na ile itakayowapata huko akhera, aya hizi zinasema musiwe na shaka yoyote juu ya kushuka kwa adhabu ya Mwenyezi Mungu, kwani ahadi ya Mola itathibiti tu. Pamoja na kwamba yote aliyokuwa akiyatamka Bwana Mtume Muhammad saw yalikuwa ni hakika na kweli tupu, lakini kutokana na uzito wa suala la kufufuliwa viumbe, hapa anaapa kwa jina la Mola Mwenyezi kuthibitisha kwamba kujiri kwa siku hiyo ya Kiyama hakuna chembe ya shaka, na wala hakuna atakayeweza kuikwepa siku hiyo au kuweza kukabiliana na adhabu yake. Kwa hakika adhabu ya Mwenyezi Mungu siku ya Kiyama itakuwa kali na nzito kiasi kwamba, kila muovu atakuwa tayari kutoa mali na utajiri wote uliopo duniani ili aweze kuokoka na adhabu hiyo. Lakini hiyo itabaki kuwa ni ya laiti ambayo haileti, kwa sababu kujuta wakati huo kwa yale aliyoyatanguliza mtu hakutosaidia kitu kwani mahakama ya Mwenyezi Mungu itatoa na kutekeleza hukumu kwa waja wote kwa msingi wa uadilifu. Funzo mojawapo tunalolipata kutokana na aya hizi ni kuwa katika mahakama ya Mwenyezi Mungu si utajiri wala nguvu na uwezo wa kidunia vitakavyoweza kumsaidia mtu. Ni imani safi na sahihi, na amali njema zilizofanywa kwa ikhlasi, ndivyo vitakamvyomfaa mja siku hiyo.
Darsa hii ya 316 nahitimishwa na aya za 55 na 56 ambazo zinasema:
"Jueni kuwa hakika vyote vilivyomo katika mbingu na katika ardhi ni vya Mwenyezi Mungu. Jueni kuwa hakika ahadi ya Mwenyezi Mungu ni ya haki. Lakini wengi wao hawajui."
"Yeye ndiye anayefufua na anayefisha. Na kwake mtarejeshwa."
Sababu kuu inayowafanya wanaokufuru na kukanusha juu ya kuwepo kwa siku ya Kiyama ni shaka yao juu ya uwezo wa Allah sw. Hivyo aya tulizosoma zinasema kuwa ni nini ikakupitikieni kwamba Mwenyezi Mungu hana uwezo wa kuwafufua waliokufa na kuwalipa kwa waliyotenda? Kwani hamujui nyinyi kuwa kila kitu ni milki yake yeye, na yeye ndiye Muumba na Mmiliki wa ulimwengu, na kwamba uhai wenu na mauti yenu viko mikononi mwake yeye? Kama mnayakubali hayo, yawaje basi mnakuwa na shaka juu ya kiyama? Aya hizi wapenzi wasikilizaji zinatuelimisha kuwa mmiliki halisi wa kila kitu ni Mwenyezi Mungu sw, na umiliki wa wanaadamu kwa kitu chochote kile ni wa kupanga tu. Na ndiyo maana siku ya kiyama wale waliokufuru hawatokuwa na chochote cha kuweza kutoa kama fidia ili waweze kuokoka. Aidha aya zinatuonyesha kuwa uwezo wa Allah wa kutawala kila kitu ni ithbati tosha ya uwezo wake wa kutekeleza kila anachoahidi. Kwa haya machache tunaifunga darsa yetu hii huku tunamwomba Mola atujaalie kuwa miongoni mwa wale watakaopata radhi zake na pepo ya milele, na atulinde na ghadhabu zake na adhabu ya moto, amin, Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.
Zaidi katika kategoria hii: « Yunus 57-61 Surat Yunus 45-49 »

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)

Hadithi ya Uongofu (39)

Ni matarajio yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji na tunakutana tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. …

Ufeministi, Itikadi na Misingi yake (26)

Assalaamu Alaykum wafuatiliaji wa kipindi hiki na karibuni kuwa nasi katika sehemu nyingine ya kipindi hiki kinachokosoa itikadi ya ufeministi …

Ulaji wa Lishe Bora katika Kipindi Chote cha Maisha

Wataalamu wa Afya wanasema kuwa, awamu mbalimbali za maisha zinahitajia ulaji wa chakula wa aina tofauti. Iwapo wewe ni mtoto, …

Maua mawili ya Mtume wa Allah (31) Sauti

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh Karibuni wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili Radio Tehran na wasomaji wa mtandao …