Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumatatu, 21 Aprili 2008 21:28

Surat Yunus 45-49

Bismillahir Rahmanir Rahim. Tunamshukuru Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa kutuwafikisha kukutana tena katika darsa yetu hii. Sura ya 10 ya Yunus ndiyo tunayoizungumzia kwa sasa, na hii ni darsa ya 315 tunayoianza kwa aya ya 45 ambayo inasema:
"Na siku atakapowakusanya, itakuwa kama kwamba hawakukaa (duniani) ila saa moja tu ya mchana. Watatambuana. Hakika wamekhasirika wale waliokanusha kukutana na Mwenyezi Mungu, wala hawakuwa wenye kuongoka."
Ijapokuwa makafiri wamekadhibisha na kukanusha kuwepo kwa siku ya kiyama, hata hivyo watake wasitake ni kwamba wao pia kama ilivyo kwa wanaadamu wote watafufuliwa tu na kuishuhudia siku hiyo. Uzito wa siku hiyo utakuwa hauna mfano wake kiasi cha kuwafanya wale waliokufuru wahisi kwamba umri wao wote walioishi hapa duniani, pamoja na kipindi chote cha maisha ya barzakh huko makaburini, ulikuwa ni sawa na muda wa saa moja tu ya mchana mzima. Pamoja na wanaadamu kupitiwa na miaka bali pengine karne nyingi za baada ya kufa kwao, lakini watahisi kana kwamba wameamka tu kutoka kwenye usingizi wa kawaida. Katika hali hiyo watu watatambuana vizuri na wala hawatokumbwa na usahaulifu. Ni wazi kwamba katika lahadha hiyo wale ambao hapa duniani walikanusha kuwepo kwa kiyama, wakati kweli itakapodhihiri na kujiona wamesimamishwa katika uwanja wa siku ya kiyama, hapo ndipo watakapobaini kuwa wao ni watu waliokhasirika kwa kufika mahala hapo wakiwa mikono mitupu, huku kukiwa hakuna tena fursa ya kurudi walikotoka. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kuwa umri tunaoishi hapa duniani ni mfupi, kiasi kwamba siku ya kiyama mtu atajuta na kujihisi amekhasirika na kupata hasara kubwa kwa kutoitumia fursa hiyo ya uhai wa kupita aliojaaliwa hapa duniani. Halikadhalika inatubainikia kutokana na aya hii ni kuwa hasara ya kweli ni ile ya mtu kuhitari na kufadhilisha starehe za kupita za hapa duniani kwa raha na neema za milele za huko akhera.
Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya 46 ambayo inasema:
"Na vyovyote vile, tukikuonyesha baadhi ya tunayowaahidi au tukakufisha kabla yake, marejeo yao ni kwetu. Kisha Mwenyezi Mungu ni shahidi wa wanayoyafanya."
Aya hii inamliwaza Bwana Mtume na waumini kwa kuwaambia kuwa ikiwa mnaona Mwenyezi Mungu hawashushii adhabu kamili makafiri hapa duniani ni kwa sababu malipo hasa ya waja iwe ni adhabu ya moto au neema ya pepo wataipata huko akhera pale wote watakaporejea kwa Mola wao. Hata hivyo sio kwamba adhabu ya kila ovu itasubiri huko akhera tu bali baadhi ya adhabu zitawashukia wakanushaji hapo papa hapa duniani, nawe Mtume utashuhudia kwa macho yako; na baadhi ya adhabu zitawashukia hata baada ya wewe kuaga dunia. Funzo mojawapo tunalopata katika aya hii ni kuwa waislamu wasikate tamaa kuona muda unapita bila makafiri kupatwa na adhabu ya Mwenyezi Mungu. Hiyo ni ahadi ya Mwenyezi Mungu, na Mwenyezi Mungu ni mtimizaji wa ahadi anayotoa, tabaan kulingana na hikima yake mutlaki.
Ifuatayo sasa ni aya ya 47 ambayo inasema:
"Na kila umma una Mtume. Alipowajia Mtume wao walihuhukumiwa baina yao kwa uadilifu; wala hawakudhulumiwa."
Mitume wa Mwenyezi Mungu walikuwa katika makundi mawili. Wale waliopewa vitabu na sheria, na wale ambao walikuwa wafikishaji na walinganiaji tu wa risala za Mitume waliopewa vitabu na sheria. Kutokana na aya za quran inabainika kuwa katika kipindi cha historia, na katika umma na kaumu mbali mbali za wanaadamu wamekuwepo watu waliokuwa wakiwafikishia wanadamu wenzao mafundisho ya mitume na yale yaliyokuja katika vitabu vya mbinguni. Na ujumbe mkuu katika risala za manabii ulikuwa ni kusimamisha haki na uadilifu na kupambana na dhulma na uonevu. Na hivyo siku ya kiyama Allah sw ataawafufua watu wa kila kaumu na umati pamoja na Mtume wao na kuwasimamisha na kuwahukumu kwa uadilifu katika mahakama ya siku hiyo ya malipo. Funzo mojawapo tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa hakuna uma au kaumu yoyote ambayo Mwenyezi Mungu ameiwacha vivi hivi bila ya kuhakikisha imefikiwa na ujumbe wa mafundisho ya Mitume wake.
Tunaihitimisha darsa yetu kwa aya za 48 na na 49 ambazo zinasema:
"Na wanasema: Ni lini ahadi hii ikiwa mnasema kweli?"
"Sema: Sijimilikii nafsi yangu shari wala kheri, ila apendavyo Mwenyezi Mungu. Kila umma una muda wao waliowekewa. Ukifika muda wao hawakawii saa moja wala hawatangulii."
Makafiri ambao waliamua kukanusha hakika ya kuwepo kwa siku ya kiyama waliamua kuzusha visingizio vya kila aina alimradi kuutia shaka uhakika huo. Hivyo wakaibuka na suali kwamba ikiwa ni kweli kiyama kitatokea na wewe Muhammad unayoyasema ni kweli kuhusu hilo, tuambie basi kujiri kwake kutakuwa lini hasa! Walizusha hoja hiyo ilhali uhakika wa kutokea jambo haushurutishi kujua wakati halisi wa kutokea kwake. Mfano wa hili ni sawa na mauti. Kila mmoja wetu ana hakika kuwa iko siku ataiaga dunia tu, lakini hakuna yeyote kati yetu ajuaye ni lini hasa atafikwa na mauti. Kwa upande wa Bwana Mtume, naye pia kupitia wahyi alioushushiwa na Mola wake aliwapa khabari watu wa umati wake kwamba baada ya kumalizika dunia itawadia siku ya Kiyama, hata hivyo Allah sw hakumbainishia Mtume wake ni wakati gani hasa litajiri tukio hilo kubwa kabisa la kutikisa nyoyo. Baadhi ya mafunzo tunayoyapata kutokana na aya hizi ni kuwa Mitume walikuwa ni waja wateule wanaozungumza na watu kwa uwazi na ukweli mtupu; na hivyo wakiwaeleza bayana kuwa binafsi hawana nguvu na uwezo usio wa kawaida wala mamlaka ya kujiamulia kupata manufaa fulani au kujilinda na kujiepusha na shari yoyote ile ila kwa uwezo na idhini ya Allah sw. Wapenzi wasikilizaji, kwa haya machache tunaifunga darsa hii ya 315. Inshaallah Mwenyezi Mungu atujaalie kuwa miongoni mwa wanaoyakinisha kiimani juu ya kuwepo kwa siku ya kiyama kutokana na amali zao na matendo yao. Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)

Hadithi ya Uongofu (39)

Ni matarajio yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji na tunakutana tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. …

Ufeministi, Itikadi na Misingi yake (26)

Assalaamu Alaykum wafuatiliaji wa kipindi hiki na karibuni kuwa nasi katika sehemu nyingine ya kipindi hiki kinachokosoa itikadi ya ufeministi …

Ulaji wa Lishe Bora katika Kipindi Chote cha Maisha

Wataalamu wa Afya wanasema kuwa, awamu mbalimbali za maisha zinahitajia ulaji wa chakula wa aina tofauti. Iwapo wewe ni mtoto, …

Maua mawili ya Mtume wa Allah (31) Sauti

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh Karibuni wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili Radio Tehran na wasomaji wa mtandao …