Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumatatu, 21 Aprili 2008 21:28

Surat Yunus 39-44

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh. Karibuni katika mfululizo huu wa 314 wa darsa ya quran, tukiwa tunaendelea kuizungumzia sura ya 10 ya Yunus. Tunaianza darsa yetu kwa aya za 39 na 40 ambazo zinasema:
"Bali wameyakanusha wasiyoyaelewa ilimu yake kabla hayajawajia maelezo yake. Namna hivi walikanusha waliokuwa kabla yao. Basi angalia jinsi ulivyokuwa mwisho wa madhalimu hao."
"Na miongoni mwao wapo wanaoiamini. Na miongoni mwao wapo wasioiamini. Na Mola wako anawajua vyema waharibifu."
Katika darsa iliyopita tulisema kuwa kutokana na dhana tu na bila kuwa na ushahidi mushirikina na makafiri walikuwa walivurumiza tuhuma kuwa Quran ni maneno ya Bwana Mtume na kukanusha kwa kudai kuwa kitabu hicho kitukufu hakina uhusiano wowote na Mwenyezi Mungu. Aya tulizosoma zinasema kuwa kinachofanywa na makafiri na mushirikina hao ni kukariri yale yaliyosemwa na wenzao waliotangulia, kwani mitume wa kabla ya Nabii Muhammad saw walikabiliwa na tuhuma sawa na hizo. Hii ni pamoja na kuwa ukadhibishaji wao hauna mashiko yoyote ya kielimu, hivyo kitendo chao hicho ni sawa na kujidhulumu nafsi zao na pia ni dhulma kwa dini ya haki ya mbinguni na mitume waliotumwa na Allah kuitangaza dini hiyo kwa watu. Lakini katika upande mwingine, kuna watu wanaoitambua na kuiamini haki, na hivyo, kama tulivyowahi kuashiria mara kadhaa, ndivyo alivyokadiria Allah sw, kwamba, kila mtu kwa hiyari mwenyewe aamue ima kuwa muumini au kafiri. Baadhi ya yale tunayojifunza kutokana na aya hizi ni kuwa chanzo cha ukafiri, ukanushaji na ukadhibishaji haki ni kukosa utambuzi wa kuielewa haki hiyo. Kwani wale wanaokusudia kwa dhati kuitafuta na kutaka kuijua haki hufika mahali wakaitambua risala ya tauhidi waliyokuja nayo Mitume wa Mwenyezi Mungu na wakaiamni. Aidha aya zinatuelimisha kuwa kuyakanusha na kuyapa mgongo mafundisho ya manabii wa Allah ndiyo chanzo cha dhulma na ufisadi tunaoushuhudia ulimwenguni.
Ifuatayo sasa ni aya ya 41 ambayo inasema:
"Na wakiendelea kukukadhibisha sema: Mimi nina amali yangu na nyinyi mna amali yenu. Nyinyi hamna dhima kwa niyatendayo, wala mimi sina dhima kwa mnayotenda nyinyi."
Aya hii inabainisha jinsi ya kuamiliana na makafiri na wapinzani wa haki na kueleza kuwa jukumu lenu nyinyi kwa watu hao ni kuwaonyesha tu na kuwatambulisha uongofu; si kuwalazimisha wao waufuate kwa nguvu, wala nyinyi kutaka kuwakumbatia wao ili kiwe kishawishi cha kuwafanya wavutiwe na haki. Ikiwa wao watakuwa wamekaidi na kukataa kata kata kuiamini haki, dhima yenu kwao imeshaondoka, kwani imani ni jambo la moyoni na la hiyari, na hivyo watu hao ni kwamba wameshaamua hawataki kuielewa haki, na kama wameielewa, basi hawataki kuiamini. Katika suala hili hutokezea baadhi ya Waislamu wakahisi kuwa labda ikiwa wao wenyewe wataamua kuacha kushikamana na baadhi ya mambo ya msingi ya dini huenda hilo linaweza kuwavutia wale wanaowalingania waikubali haki. Hali ya kuwa mtu hana haki yoyote ya kufanya hivyo kwa sababu tu ya kutaka kupata idadi kubwa zaidi ya watu walioukubali uongofu. Na ndiyo maana tunaona katika aya hizi Bwana Mtume Muhammad saw anatakiwa awaambie makafiri kwamba, madamu nyinyi hamko tayari kuyaamini maneno yangu, tambueni kuwa mimi najiweka mbali kabisa na matendo yenu na wala sina dhima wala jukumu lolote kwenu. Funzo mojawapo tunalolipata katika aya hii ni kuwa Uislamu ni dini ya hoja, maadili na msimamo. Inatangaza na kuweka wazi msimamo wake; na kama ambavyo haimlazimishi mtu kuifuata, ndivyo vivyo hivyo nayo haiko tayari kulegeza msimamo katika misingi ya mafundisho yake.
Darsa ya 314 inahitimishwa na aya za 42, 43 na 44 ambazo zinasema:
"Na wako miongoni mwao wanaokusikiliza. Je wewe unaweza kuwafanya viziwi wasikie ijapokuwa hawafahamu?"
"Na wapo miongoni mwao wanaokukodolea macho. Je wewe utawaongoa vipofu ingawa hawaoni?"
Hakika Mwenyezi Mungu hawadhulumu watu chochote; lakini watu wenyewe wanajidhulumu nafsi zao.
Katika kuendeleza yale yaliyokuja katika aya zilizotangulia kuhusu jinsi wapinzani wa haki walivyokuwa wakiamiliana na Bwana Mtume, aya hizi zinasema, si hasha baadhi ya wapinzani hao wakawa ni watu wanaohudhuria vikao vya Bwana Mtume, wakimwona kwa macho yao mtukufu huyo na kuyasikia yale anayoyasema; lakini yote hayo hayazipi athari yoyote nafsi zao. Na sababu ni kuwa yote hayo waliyokuwa wakiyashuhudia na kuyasikia hayakuwa yakipenya kweli kwenye masikio yao na kukita kwenye fikra na nyoyo zao. Kana kwamba watu hao walikuwa ni vipofu wasioona au viziwi wasioweza kusikia chochote. Kimsingi ni kwamba kitu kinachompambanua mwanadamu na mnyama ni uwezo wake wa kufikiri na kutafakari, vinginevyo mnyama naye anaona na anasikia, bali hata uwezo na nguvu zake zake za kuona na kusikia ni kubwa zaidi kuliko za binaadamu. Hivyo linalomstahikia mwanadamu ni kuyatia kwenye tafakuri yale ayaonayo na ayasikiayo, kwa kupambanua la haki na la batili, kisha kushikamana na lile la haki na kujiweka mbali na lile la batili. Funzo mojawapo tunalolipata kutokana na aya hizi ni kuwa kuona na kusikia, ni utangulizi wa kutafakari na kuifahamu haki. Wapenzi wasikilizaji darsa yetu ya juma hili inaishia hapa. Tunamwomba Allah atuwafikishe kuitambua haki na kuifuata, na kuielewa batili na kuiepuka. Amin. Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)

Hadithi ya Uongofu (39)

Ni matarajio yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji na tunakutana tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. …

Ufeministi, Itikadi na Misingi yake (26)

Assalaamu Alaykum wafuatiliaji wa kipindi hiki na karibuni kuwa nasi katika sehemu nyingine ya kipindi hiki kinachokosoa itikadi ya ufeministi …

Ulaji wa Lishe Bora katika Kipindi Chote cha Maisha

Wataalamu wa Afya wanasema kuwa, awamu mbalimbali za maisha zinahitajia ulaji wa chakula wa aina tofauti. Iwapo wewe ni mtoto, …

Maua mawili ya Mtume wa Allah (31) Sauti

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh Karibuni wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili Radio Tehran na wasomaji wa mtandao …