Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumatatu, 21 Aprili 2008 21:27

Surat Yunus 34-38

Bismillahir Rahmanir Rahim. Tunamshukuru Mwenyezi Mungu mtukufu kwa kutuwafikisha kukutana tena katika darsa yetu hii. Sura ya 10 ya Yunus ndiyo tunayoizungumzia kwa sasa, na hii ni darsa ya 313 tunayoianza kwa aya za 34 na 35 ambazo zinasema:
"Sema: Je Yupo katika miungu yenu ya ushirikina, aliyeanzisha kuumba viumbe kisha akavirejesha? Sema: Mwenyezi Mungu ameanzisha kuumba viumbe kisha ndiye atakayevirejesha. Huwaje basi mkadanganywa?"
"Sema: Je Yupo katika miugu yenu ya ushirikina anayeongoa kuendea Haki? Sema: Mwenyezi Mungu anaongoa kwendea Haki. Basi je anayestahiki kufuatwa ni yule Mwenye kuongoa kwendea Haki au asiyeongoa ila aongozwe yeye? Basi nyinyi mna nini? Mnahukumu namna gani?"
Zikiendelea kuzungumzia yale yaliyokuja katika aya zilizotangulia kuhusu kutoa changamoto kwa mushrikina ya kuwaonyesha jinsi miungu yao bandia isivyo na uwezo wa kufanya lolote, aya tulizosoma zinasema, ikiwa mtatupia jicho na kuzingatia uumbaji ulivyo mtabaini kuwa hakuna yeyote ghairi ya Mungu Mmoja awezaye kuumba kila kilichopo na kukipa uhai mpya, na hayo masanamu yenu mnayoyaabudu na viumbe vingine vyote vilivyoko, vyote hivyo vimeumbwa na vinamhitajia Muumbaji, basi yawaje vitu hivyo viweze navyo kuwa waumbaji wa ulimwengu? Kama nyinyi ni wenye kutafuta uongofu na kutaka kuifikia saada tambueni kuwa miungu wenu hao wenyewe hawana cha kumuongoza mtu hata muweze kupata muongozo wa kufuata kutoka kwao, na kama ni suala la kupata uongofu, inalazimu wao wenyewe kwanza wawe na sifa hiyo ya kuweza kuufikia huo uongofu kisha ndipo waweze kukuonyesheni nyinyi pia njia ya kuufikia. Hali ya kuwa Mwenyezi Mungu ndiye muongozaji wenu wa kukufikisheni kwenye njia iliyonyooka. Tabaan uongofu wa Mwenyezi Mungu unapatikana kupitia Mitume wake na vitabu vya mbinguni walivyokuja navyo ambavyo kila kilichomo ndani yake ni maneno yake Mola Muumba. Miongoni mwa yale tunayojifunza kutokana na aya hizi ni kuwa kutumia mfumo wa masuali na majibu ni mojawapo ya mbinu bora kwa ajili ya kujadiliana na wapinzani wa kiitikadi na kifikra, mbinu ambayo Allah sw amewafunza Mitume wake. Aidha aya zinatuelimisha kuwa Mwenyezi Mungu si Muumbaji wa ulimwengu tu, bali baada ya kuwaumba viumbe wake hakuwaacha kama walivyo, ila amewaonyesha pia njia yao ya uongofu itakayowafikisha kwenye saada ya duniani na akhera.
Ifuatayo sasa ni aya ya 36 ambayo inasema:
"Na wengi wao hawafuati ila dhana tu. Na dhana haifai kitu mbele ya haki. Hakika Mwenyezi Mungu anajua yote wanayoyatenda."
Aya hii wapenzi wasikilizaji inaashiria chanzo na chimbuko la upotofu wa kifikra la wale wanaomkanusha na kumkufuru Mwenyezi Mungu na kueleza kuwa kufuata dhana na mambo ya udhanifu yasiyo na msingi ambayo kwa hakika ni njozi za kifikra ndiyo yaliyowafanya watu hao waipe mgongo haki na kung'ang'ania fikra na itikadi batili. Hali ya kuwa katika masuala ya kifkra na kiitikadi, dhana na mambo ya udhanifu hayana nafasi wala itibari yoyote, na ukweli ni kuwa hakika na yakini ndiyo mambo yanayoweza kumfikisha mtu kwenye haki. Mbali na hayo chimbuko la itikadi nyingi za zama za ujahilia lilikuwa ni watu kufuata yale waliyowakuta nayo babu zao na kushikilia na kuyanng'ang'ania mambo kwa sababu ya taasubi tu za kikabila, mambo ambayo hayakuwa na thamani wala itibari yoyote ya kielimu na kifikra. Baadhi ya yale tunayojifunza kutokana na aya hii ni kuwa katika masuala ya kiitikadi na kimaadili wingi hauwi kipimo cha kuonyesha haki. Kwani si hasha walio wengi katika watu wakawa wamepotoka kifikra na kimatendo.
Tunaihitimisha darsa yetu ya juma hili kwa aya za 37 na 38 ambazo zinasema:
"Na haiwezekani Qurani hii kuwa imetungwa, na haitoki kwa Mwenyezi Mungu. Bali inayasidikisha yaliyotangulia, na ni mfafanuo wa Kitabu kisicho na shaka ndani yake kutoka kwa Mola wa walimwengu wote."
"Je! Ndiyo wanasema ameizua? Sema:" Hebu leteni sura moja mfano wake na muwaite (kukusaidieni) muwawezao isipokuwa Mwenyezi Mungu ikiwa nyinyi mnasema kweli."
Quran tukufu imetoa changamoto mara kadhaa ya kuthibitisha kuwa ni maneno ya mbinguni na kuonyesha kwamba si majini wala binaadamu walio na uwezo wa kuleta kitu kilicho mfano wake. Bali ikafika mbali zaidi na kueleza kwa kujiamini kwamba, si kuleta mfano wa Quran yote au moja ya sura zake tu, bali kama wana uwezo, wapinzani wa muujiza huo wa Mtume wa mwisho wa Mwenyezi Mungu na walete walau aya moja tu iliyo mfano wa Quran. Hata hivyo licha ya maadui na wapinzani wengi ambao Uislamu na Quran imekabiliana nao katika kipindi cha karne 14 zilizopita, hadi leo hii hakuna aliyethubutu kujitokeza kukabiliana na changamoto hiyo iliyotolewa na kitabu hicho cha Mwenyezi Mungu. Magwiji wa kila zama wa nahau na balagha pamoja na fani nyinginezo za lugha ya kiarabu wasio waislamu, wote hao wameshindwa kubuni walau aya moja tu iliyo na sifa za aya ya Quran tukufu. Wapenzi wasikilizaji quran tukufu ina miujiza na maajabu ya aina kwa aina, machache kati ya hayo ni haya yafuatayo. Kwanza ni utamu wa maneno yake na mvuto wa ajabu yalionao, kiasi kwamba hata kama mtu ataisoma mara elfu hahisi kuwa amesoma kitu cha kushosha na kilichopitwa na wakati. Si hayo tu, bali vibwagizo vya maneno yake, mianguko yake ya sauti na mahadhi yake yamejipambanua na maneno mengine yote ya lugha ya kiarabu. Ujumuishaji wa quran wa kila kipengele cha maisha ya mwanadamu vikiwemo vya masuala ya mtu binafsi, familia, jamii, masuala ya kisheria, kiuchumi, kisiasa na kiakhalqi ni wa namna ambayo, ni muhali kwa mwanaadamu yeyote kuweza kuufikia upeo wake. Wapenzi wasikilizaji darsa ya 313 imefikia tamati. Tunamwomba Mwenyezi Mungu aturuzuku kuisoma quran usiku na mchana, kwa namna airidhiayo yeye, na kutuwafikisha kutekeleza kivitendo yaliyomo ndani yake ili tuweze kupata uombezi wa quran siku ya kiyama. Amin. Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)

Hadithi ya Uongofu (39)

Ni matarajio yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji na tunakutana tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. …

Ufeministi, Itikadi na Misingi yake (26)

Assalaamu Alaykum wafuatiliaji wa kipindi hiki na karibuni kuwa nasi katika sehemu nyingine ya kipindi hiki kinachokosoa itikadi ya ufeministi …

Ulaji wa Lishe Bora katika Kipindi Chote cha Maisha

Wataalamu wa Afya wanasema kuwa, awamu mbalimbali za maisha zinahitajia ulaji wa chakula wa aina tofauti. Iwapo wewe ni mtoto, …

Maua mawili ya Mtume wa Allah (31) Sauti

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh Karibuni wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili Radio Tehran na wasomaji wa mtandao …