Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumapili, 15 Disemba 2013 16:13

Surat Yusuf - Aya ya 11-15

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh. Hamdu na sifa zote njema ni za Allah SW ambaye ametupa taufiki ya kukutana tena katika mfululizo mwingine wa Darsa ya Qur'ani. Sura tunayoizungumzia kwa sasa ni ya 12 ya Yusuf na hii ni Darsa ya 358 ambayo tunaianza kwa aya za 11 na 12 ambazo zinasema:
Wakasema: Ewe baba yetu! Una nini hata hutuamini kwa Yusuf? Na hakika sisi ni wenye kumtakia kheri!
Mpeleke kesho pamoja nasi, ale kwa furaha na acheze; na bila ya shaka sisi tutamhifadhi.
Katika darsa iliyopita tulisema kuwa ndugu zake Yusuf kwanza walijiwa na wazo la kutaka kumuua ndugu yao huo kisha wakabadili uamuzi wao na kuamua wakamfiche ndani ya kisima. Hivyo wakapanga jinsi ya kutekeleza njama yao hiyo ya kumtenganisha Yusuf na baba yake kumwendea baba yao Yaaqub AS na kumwambia: "Kwa nini baba unamtenganisha Yusuf na sisi, na huturuhusu tufuatane naye huko jangwani ili wakati sisi tumeshughulika na kazi za kilimo, yeye ajichangamshe kwa michezo?" Naam, kisingizio cha kupata Yusuf fursa ya michezo na burudani kilikuwa hoja madhubuti waliyoitumia kaka zake ili kumfanya baba yao akubali kutengana na mwanawe huyo. Kwani ni ukweli kwamba harakati za michezo na kujichangamsha ni miongoni mwa mahitaji ya kila kijana, na ndiyo maana pamoja na kwamba Yaakub hakupendelea suala hilo lakini hakuweza kukataa ombi hilo la wanawe la kutaka wafuatane na Yusuf huko jangwani. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kuwa tusiwe tayari kukubali kila dai na kutekwa na kuhadaiwa na kila nara na kaulimbiu za kuvutia. Kaka zake Yusuf waliazimia kufanya uovu lakini wenyewe wakajionyesha kuwa ni watu wema na wanaomtakia kheri ndugu yao huyo. Funzo jingine tunalopata hapa ni kuwa husda huweza kumfanya mtu awe tayari kufanya hila hata kufikia hadi ya kumwambia uwongo mtu wake wa karibu kabisa. Halikadhalika inatubainikia kutokana na aya hizi kuwa kijana ni mtu anayehitaji burudani na michezo. Pamoja na hayo tutahadhari wengine wasije wakalitumia vibaya suala hilo.
Tunaendeleza darsa yetu kwa aya ya 13 ambayo inasema:
Akasema: Kwa hakika inanihuzunisha kwamba nyinyi mwende naye, na ninaogopa asije mbwa mwitu akamla nanyi mmeghafilika naye.
Ijapokuwa Nabii Yaaqub alikuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu lakini alikuwa ni baba kwa Yusuf, na hivyo mapenzi ya baba kwa mwanawe yalimfanya asipende kuona Yusuf anatengana naye. Pamoja na hayo Yusuf alikuwa kijana chipukizi ambaye alihitaji kidogo kidogo aanze kujitegemea na kuwa huru; kwa sababu hiyo akawa hana budi kumruhusu afuatane na kaka zake huko jangwani. Ndiyo kusema kuwa kuchelea uwezekano wa mtoto kutokewa na hatari, isiwe sababu ya kumfungia na kumtawisha nyumbani; kwani suala la kumzoesha awe na hali ya kujitegemea ni msingi muhimu katika malezi ambayo wazazi pamoja na kuwapenda watoto wao wanatakiwa wawatayarishiea pia mazingira kwa ajili ya suala hilo. Hata hivyo kila pale wanapohisi kuna hatari fulani wasiache kuwaonya na kuwatahadharisha watoto wao juu ya hali hiyo. Aya hii pamoja na mambo mengine inatufunza kuwa katika malezi ya mtoto, hukta mbili muhimu lazima zizingatiwe kwa pamoja. Moja ni kumtayarishia mtoto mazingira ya kuwa mtu wa kujitegemea na kujenga shakhsia yake, na pili ni kumtanabahisha kila wakati juu ya hatari mbalimbali ambazo ni tishio kwa kijana. Funzo jingine tunalopata katika aya hii ni kuwa kughafilika na hatari kunaweza kusababisha hasara na madhara ambayo si hasha tukashindwa hata kuyafidia.
Ifuatayo sasa ni aya ya 14 ambayo inasema:
Wakasema: Ikiwa mbwa mwitu atamla na hali sisi ni kundi lenye nguvu kabisa, basi bila ya shaka sisi tutakuwa khasarani.
Kaka zake Yusuf ambao walikuwa wameandaa mpango wa kumwondoa ndugu yao mbele ya macho ya baba yao hawakuwa na jibu jingine la kumpa Nabii Yaaqub juu ya hatari inayoweza kumpata Yusuf isipokuwa kutegemea nguvu na uwezo wao wa kimwili na kuifanya kuwa hoja ya kumridhisha baba yao akubali wafuatane na Yusuf huko jangwani. Hali ya kuwa, kuwa na nguvu tu si hoja ya kumfanya mtu awe katika amani. Ni kweli wao walikuwa mashababi wenye nguvu lakini walikuwa na dhamira ya kufanya uovu, suala ambalo alikuwa ameshalihisi Nabii Yaaqub lakini hakuwa na hoja ya kuwathibitishia. Baadhi ya nukta za kuzingatia katika aya hii ni kuwa kwa kawaida vijana huingiwa na ghururi kutokana na nguvu wanazokuwa nazo kiasi cha kutojali sana hatari zinazowakabili, hali ya kuwa wazee wao huwa ni watu wanaochelea sana hatari mbalimbali.
Aya ya 15 ndiyo inayotuhitimishia darsa yetu ya juma hili. Aya hiyo inasema:
Basi walipomchukua na wakakubaliana wamtumbukize ndani ya kisima, tulimfunulia Yusuf: Hapana shaka yoyote utakujawaambia kwa jambo lao hili, na wala wao hawatambui.
Alaa kulli haal kaka zake Yusuf walifanikiwa kumtenganisha ndugu yao na baba yao na kumchukua huko jangwani; na kama walivyokuwa wamedhamiria walimchukua na kumtia ndani ya kisima; tab'an si kumtumbukiza kwenye maji bali walimweka kwenye kuta za kisima katika sehemu iliyo mithili ya rafu ili asiweze kufa kwa kiu na pia awe katika amani ya kutoshambuliwa na wanyama wakali na kutodhurika kwa joto na baridi ya jangwani. Zaidi ya hayo utakapotokea msafara wa wafanya biashara kutoka sehemu nyingine wataweza kumwokoa kwa kumtoa kisimani na kwenda naye huko waendako. Katika lahadha hiyo kutokana na kwamba yamkini Yusuf ambaye bado alikuwa kijana mdogo angeweza kupatwa na hofu ya kuwa peke yake kisimani na hali ya giza ya kisimani humo, Mwenyezi Mungu alimliwaza na kumpa ilhamu kwamba asihofu kwa kutiwa kisimani. Siku itafika ndugu zake hao hao waliomtia kisimani watakuja kwake na yeye atawakumbusha juu uovu huo waliomtendea. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutoka na aya hii ni kuwa wahyi ulio katika sura ya ilhamu, hauwahusu Mitume peke yao, bali hata waja wengine wema na wateule wanaweza kutokewa na hali hiyo. Katika wakati huo Yusuf alikuwa bado hajawa Mtume lakini alipata ilhamu hiyo ya Mwenyeiz Mungu. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa, kuwa na matumaini juu ya mustakbali ndiyo hazina bora kabisa ya kumpa matumaini mtu ya kuendelea na maisha. Kutokana na ilhamu aliyompa Yusuf, Mwenyezi Mungu alimpa kijana huyo matumaini ya maisha. Na pia aya inatutaka tuelewe kwamba katika hali ya shida, tabu na upweke, mtu anatakiwa awe na matumaini ya kupata rehma za Mwenyezi Mungu na katu asivujike moyo wala kukata tamaa. Wapenzi wasikilizaji darsa ya 358 inaishia hapa. Tunamwomba Mola atupe taufiki katika malezi ya watoto wetu na kuwaongoza katika njia ya kheri. Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.

Zaidi katika kategoria hii: « Darsa zaidi za Qur'ani

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)

Hadithi ya Uongofu (39)

Ni matarajio yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji na tunakutana tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. …

Ufeministi, Itikadi na Misingi yake (26)

Assalaamu Alaykum wafuatiliaji wa kipindi hiki na karibuni kuwa nasi katika sehemu nyingine ya kipindi hiki kinachokosoa itikadi ya ufeministi …

Ulaji wa Lishe Bora katika Kipindi Chote cha Maisha

Wataalamu wa Afya wanasema kuwa, awamu mbalimbali za maisha zinahitajia ulaji wa chakula wa aina tofauti. Iwapo wewe ni mtoto, …

Maua mawili ya Mtume wa Allah (31) Sauti

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh Karibuni wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili Radio Tehran na wasomaji wa mtandao …