Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumatatu, 18 Mei 2015 16:16

Sura ya Ash-Shua'raa, aya ya 217-227 (Darsa ya 663)

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu. Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur'ani. Hii ni darsa ya 663 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 26 ya Ash-Shua'raa. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 217 hadi 220 ambazo zinasema:


وَتَوَكَّلْ عَلَى الْعَزِيزِ الرَّحِيمِ


Na umtegemee (Mwenyezi Mungu) Mwenye nguvu Mwenye kurehemu.


الَّذِي يَرَاكَ حِينَ تَقُومُ


Ambaye anakuona unapo simama,

وَتَقَلُّبَكَ فِي السَّاجِدِينَ


Na mageuko yako kati ya wanao sujudu.


إِنَّهُ هُوَ السَّمِيعُ الْعَلِيمُ


Hakika Yeye ndiye Mwenye kusikia Mwenye kujua.


Katika darsa iliyopita tulisema kuwa kutokana na maneno na mwenendo muovu wa wapinzani wa haki dhidi ya Bwana Mtume Muhammad SAW, Allah SW alimwamuru Mtume wake kushikamana na mambo manne ambayo tuliyazungumzia katika darsa hiyo ya 662. Amma amri na agizo la tano linalokamilisha maagizo hayo manne limo katika aya tulizosoma zinazoeleza kwamba pamoja na jitihada na subira tawakal na umtegemee Mwenyezi Mungu, kwani Yeye ni Mwenye kushinda kila kitu; kwani atakapo Yeye jambo liwe basi hakuna yeyote awezaye kusimama dhidi ya irada yake na kulizuia. Katika habari za Mitume waliotangulia umeona ni vipi tuliwaangamiza kina Namrudi na Firauni licha ya nguvu na mamlaka yote waliyokuwa nayo; na badala yake tukamwezesha Musa kushika hatamu za madaraka na utawala. Kama ambavyo kaumu zilizopita zilizoasi na kukufuru tuliziangamiza na tukawaokoa Mitume na wale waliowaamini. Kisha aya zinaendelea kueleza kwamba: Wewe unakuwa chini ya uangalizi wake Mola katika hali zote; iwe ni wakati unaposali na kufanya ibada ukiwa pamoja na waumini, au wakati unaposimama kufanya da'wa kuwaita washirikina kwenye wito wa tauhidi na kumwabudu Yeye Mungu wa haki. Katika hali zote hizo Yeye Allah ni Mwelewa wa uyasemayo na uyafanyayo, na daima atakupa auni na msaada wake. Kwa hiyo endelea kushikamana na njia yako hiyo huku ukitawakkal kwake Yeye na kumtegemea Yeye tu, na simama imara na kuwa madhubuti mbele ya wapinzani wa haki. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba badala ya kutegemea mali na vyeo vyetu au nguvu, madaraka na utajiri wa wengine, tutawakkal kwa Mwenyezi Mungu ambaye ni Mwenye nguvu, Mrehemevu, Mwenye kusikia na Mwelewa wa kila kitu, na ambaye yuko juu ya nguvu na mamlaka yote ya ulimwengu. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa mawalii wa Allah daima huwa chini ya uangalizi wake Mola, iwe wanapokuwa kwenye hali ya harakati na mapambano au katika hali na kusujudu na kufanya ibada nyenginezo.
Tunaiendeleza darsa yetu hii kwa aya za 221 hadi 223 ambazo zinasema:


هَلْ أُنَبِّئُكُمْ عَلَى مَن تَنَزَّلُ الشَّيَاطِينُ


Je! Nikwambieni nani wanawashukia Mashet'ani?


تَنَزَّلُ عَلَى كُلِّ أَفَّاكٍ أَثِيمٍ


Wanamshukia kila mzushi mkubwa mwingi wa dhambi.


يُلْقُونَ السَّمْعَ وَأَكْثَرُهُمْ كَاذِبُونَ


Wanasikiliza (yanayosemwa na Mashetani); na wengi wao ni waongo.


Aya hizi zinaashiria tena tuhuma za maadui wa Uislamu za kudai kuwa Qur'ani inatokana na ilhamu za mashetani kwa Bwana Mtume na kueleza kwamba: shetani huwashukia watu waongo na waovu na kuwashajiisha kueneza maovu na madhambi. Na wao wanamsikiliza yeye na kufanya mambo yanayotokana na uongo na uzushi. Hali ya kuwa nyinyi washirikina wa Makka hamna kumbukumbu nyengine katika historia ya maisha ya Bwana Mtume ghairi ya kumjua kwa sifa za wema, ukweli na uaminifu. Kwani nyinyi mumewahi tangu huko nyuma kusikia neno hata moja la uongo kutoka kinywani mwake mpaka hivi sasa mnamtuhumu kuwa anayokuambieni ni uongo na kuyanasibisha maneno yake na shetani? Isitoshe wito anaokulinganieni hauna kingine ndani yake ghairi ya kukutakeni mufanye mema na kuwa wasafi wa roho na kujiepusha dhulma na maovu, wakati shetani huwa kila mara anataka kueneza uchafu, maovu na ufasiki na kuwachochea watu kwa njia ya kuwatia wasiwasi wayafanye mambo hayo. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba nyoyo chafu ni mashukio mazuri ya kujazwa wasiwasi na uchochezi wa shetani. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa kusema uwongo ni chanzo cha kufanya maovu na madhambi mengine mengi; na masikio ndilo dirisha analopenyea shetani na kuingiza maneno yake ndani ya moyo wa mtu.
Wapenzi wasikilizaji darsa ya 663 inahatimishwa na aya za 224 hadi 227 ambazo ndizo zinazotukamilishia pia tarjumi na maelezo ya sura yetu hii ya Ash-Shua'raa. Aya hizo zinasema:


وَالشُّعَرَاء يَتَّبِعُهُمُ الْغَاوُونَ


Na watungaji mashairi, ni wapotofu ndio wanaowafuata.


أَلَمْ تَرَ أَنَّهُمْ فِي كُلِّ وَادٍ يَهِيمُونَ


Je! Huwaoni kwamba wao wanatangatanga katika kila bonde?


وَأَنَّهُمْ يَقُولُونَ مَا لا يَفْعَلُونَ


Na kwamba wao husema wasiyo yatenda?


إِلاَّ الَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ وَذَكَرُوا اللَّهَ كَثِيرًا وَانتَصَرُوا مِن بَعْدِ مَا ظُلِمُوا وَسَيَعْلَمُ الَّذِينَ ظَلَمُوا أَيَّ مُنقَلَبٍ يَنقَلِبُونَ


Isipo kuwa wale walio amini, na wakatenda mema, na wakamkumbuka Mwenyezi Mungu kwa wingi, na wakajitetea wanapo dhulumiwa. Na punde watajua walio dhulumu ni mgeuko gani watakao geuka.


Aya hizi zinatoa jibu kwa tuhuma nyengine za wapinzani wa haki kwa kusema: Bwana Mtume si mshairi, na maneno anayoyasema si udhanifu na ubunifu wa kishairi bali yanatokana na hakika na ukweli. Katika zama za Nabii wa rehma Muhammad SAW, kulikuwepo na washairi wengi waliokuwa wakiishi katika eneo la Hijazi. Aghalabu ya mashairi yao yalikuwa ya kuhamasisha taasubi za kijahilia, kushajiisha ashiki za udhanifu, starehe, anasa na ulevi pamoja na vita vya kikabila na mfano wa hayo; na mshairi yeyote aliyeweza kubainisha mambo hayo kwa njia ya usanifu wa kusisimua zaidi, mashairi yake yalikuwa yakichaguliwa katika tamasha la kila mwaka la mashairi katika mji wa Makka na kubandikwa kwenye ukuta wa al Kaaba. Ni wazi kwamba watu waliokuwa wakijishughulisha kusanifu, kuhifadhi na kusoma mashairi kama hayo walikuwa mbali kabisa na mafundisho ya dini za tauhidi, na walikuwa wametawaliwa na fikra za udhanifu na mambo ya kubuni. Na kikawadia shairi halisanifiwi kwa msingi wa hoja na mantiki bali hulenga zaidi kuleta tamthili na tashbihi na kuipa nguvu zaidi hisi ya udhanifu na ubunifu. Washairi hufikia kwenye kilele cha usanifu wao katika kuwasifu au kuwaponda watu; na kwa kawaida huwa wanatia chumvi katika kufanya hivyo. Kwa desturi, washairi ni watu wa usemaji na usanii, si watu wa kazi na matendo; ni watu wa majlisi na vikao vya dhifa na tafrija; si watu wa mapambano katika medani, na ndiyo maana mashairi yao yanaafikiana zaidi na majlisi za tafrija na si katika medani za vita na mapambano. Pamoja na yote hayo wako miongoni mwa washairi watu makini na wazuri. Washairi ambao, mashairi yao yanazingatia ukweli na uhalisia, na wao wenyewe ni watu wa fikra na matendo. Kwa sababu hiyo Qur'ani tukufu imewapambanua watu hao na kusema, ila wale washairi waumini na wafanyao amali njema, ambao mashairi yao yanawaelekeza watu katika kumkumbuka na kumdhukuru Mwenyezi Mungu na kuihamasisha jamii kusimama kupambana na dhulma mpaka madhalimu watambue kuwa muda si muda wataangamizwa kwa ushindi wa waumini dhidi yao. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba sanaa huwa na thamani pale msingi wake unapotokana na fikra sahihi na lengo lake likawa ni kuwahudumia watu na kurekebisha jamii; na si sanaa kuwa chombo cha kueneza fikra potofu na vishawishi vya kishetani. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa katika mtazamo wa Uislamu shairi huwa na thamani kama litakuwa linahuisha na kueneza katika jamii thamani za kimaadili na mafundisho ya kidini, si kuwaelekeza vijana kwenye pumbao na upuuzi. Kadhalika tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba Qur'ani imekemea kuwapotosha watu na kuwashughulisha na mambo ya kipuuzi na yasiyo na maana, iwe ni kwa kutumia shairi, hadithi, filamu, hotuba au kitu kingine chochote kile; isipokuwa katika aya tulizosoma imeashiria shairi kutokana na uzuri, mvuto na taathira maalumu liliyonayo. Wapenzi wasikilizaji darsa ya 663 ya Qur'ani imefikia tamati, na tumehatimisha pia tarjumi na maelezo ya sura ya 26 ya Ash-Shua'raa. Tunamwomba Allah atujaalie kuwa wenye kunufaika kiimani na kimatendo na yote tuliyojifunza katika sura hii. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh.

 

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)