Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumatatu, 18 Mei 2015 16:10

Sura ya Ash-Shua'raa, aya ya 210-216 (Darsa ya 662)

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu. Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur'ani. Hii ni darsa ya 662 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 26 ya Ash-Shua'raa. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 210 hadi 212 ambazo zinasema:


وَمَا تَنَزَّلَتْ بِهِ الشَّيَاطِينُ


Wala Mashet'ani hawakuteremka nayo,


وَمَا يَنبَغِي لَهُمْ وَمَا يَسْتَطِيعُونَ


Wala haiwapasi na wala hawaiwezi.


إِنَّهُمْ عَنِ السَّمْعِ لَمَعْزُولُونَ


Hakika hao wametengwa na kusikia.


Aya hizi zinaendelea kuzungumzia maudhui iliyoashiriwa kwenye aya tulizosoma katika darsa iliyopita kuhusiana na tuhuma zisizo na msingi za maadui wa haki dhidi ya Bwana Mtume SAW na kueleza kwamba: watu hao walikuwa wakisema: Muhammad ana mawasiliano na jinni, na yeye ndiye anayemfundisha aya hizi. Neno majnun ambalo limetumiwa mara kadhaa ndani ya Qur'ani tukufu na wapinzani kuhusiana na Mitume wa Allah na kuambatanishwa pia na sifa ya mshairi lina maana ya mtu aliyekumbwa na jini na si kwa maana ya mtu asiye na akili na busara, kwa sababu maana ya mshairi si mtu asiye na akili na busara. Allah SW anazijibu tuhuma hizo za washirikina wa Makka dhidi ya Bwana Mtume kwa kusema: Nyinyi mnayanasibisha maneno haya na mashetani hali ya kuwa maarifa na mafundisho aali ya Qur'ani hayanasibiani wala hayahusiani kwa namna yoyote na fikra na ilhamu za kishetani. Mashetani hawana ustahiki wa kuteremsha maneno yenye maarifa na matukufu kama haya, kama ambavyo hawana uwezo wa kuyateresmsha wao maneno ya Mwenyezi Mungu kwa Mtume na kuleta tashbihi ya kumfanya yeye Mtume asiweze kubaini kama maneno haya yameteremshwa kwake kutoka kwa Mwenyezi Mungu au kutoka kwa mashetani. Isitoshe ni kwamba baada ya kudhihiri Nabii Muhammad SAW mawasiliano baina ya majini na ulimwengu wa mbinguni yalikatika. Ikiwa hapo kabla majini waliweza kuwaendea malaika na kudukua kutoka kwao habari za mbinguni, mawasiliano hayo sasa yameshakatika moja kwa moja. Kwa hivyo hawana uwezo wa kufanya udukuzi wa habari za ghaibu na kuwafikishia watu wenye mahusiano nao. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba Qur'ani ina utakatifu, hifadhi na kinga madhubuti inayoilinda na aina yoyote ile ya upotoshwaji na utiwaji mkono ndani yake. Na kwa hivyo mashetani si uwezo walionao wa kupokea wahyi wala uweza wa kuufikisha kwa mwengine. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa mashetani wanaweza kuwashukia vipenzi na wafuasi wao na kuwafikishia baadhi ya mambo, lakini hawawezi kufanya hivyo kwa Mtume na waja wengine safi na watoharifu. Kadhalika tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba kama hakuna utayarifu wa kiroho na kinafsi, mtu hawezi kuyasikia maneno ya wahyi na kunufaika nayo.
Aya za 213 hadi 216 ndizo zinazotuhitimishia darsa yetu hii. Aya hizo zinasema:


فَلا تَدْعُ مَعَ اللَّهِ إِلَهًا آخَرَ فَتَكُونَ مِنَ الْمُعَذَّبِينَ


Basi usimwombe mungu mwingine pamoja na Mwenyezi Mungu ukawa miongoni mwa watakao adhibiwa.


وَأَنذِرْ عَشِيرَتَكَ الأَقْرَبِينَ


Na uwaonye jamaa zako wa karibu.


وَاخْفِضْ جَنَاحَكَ لِمَنِ اتَّبَعَكَ مِنَ الْمُؤْمِنِينَ


Na inamisha bawa lako (kwa kuwa mnyenyekevu) kwa wanao kufuata katika Waumini.


فَإِنْ عَصَوْكَ فَقُلْ إِنِّي بَرِيءٌ مِّمَّا تَعْمَلُونَ


Na ikiwa watakuasi basi sema: Mimi najitenga mbali na hayo mnayo yafanya.


Katika aya hizi tulizosoma, Allah SW anamhutubu na kumwamuru Mtume wake afanye mambo kadhaa. Amri ya kwanza inahusiana na wapinzani na anamwambia: simama imara katika kukabiliana na washirikina na katu usikubali kuacha njia na fikra yako ya tauhidi na kumwabudu Mola pekee wa haki kwa sababu ya kutaka kuwavuta wao kwenye njia hiyo; kwani ukifanya hivyo nawe pia utafikwa na adhabu kama wao. Amri ya pili inahusiana na jamaa, na kueleza kwamba: katika kufanya da'awa na kuwalingania watu wito wa tauhidi, kabla ya kuwaendea watu wengine, anza kwanza na watu wako wa karibu kwa kuwaonya na kuwapa indhari juu ya shirki na kuabudu masanamu na hatima ya madhambi hayo. Amri ya tatu ni kuhusu waumini na kueleza kwamba: amiliana na wafuasi wako kwa upole na unyenyekevu, na si kama walivyo wafalme, ambao hutoa amri kwa walio chini yao kwa ghururi na takaburi na kujiona bora na walio juu zaidi ya wengine. Muamala na mlahaka wako kwa wafuasi wako unapasa uwe wa huruma na upole. Ni mitihili ya ndege anayewafunika vifaranga wake kwa mbawa zake na kuwashughulikia kwa upole, huba na mapenzi. Amri ya nne ni ya muendelezo wa amri ya pili na inaeleza kwamba: ikiwa jamaa na watu wako wa karibu unaowalingania wito wa tauhidi hawatoyakubali maneno yako na wakaendelea kung'ang'ania imani ya shirki, wewe wawekee wazi msimamo wako kwa kuwatangazia kwamba unachukizwa na unajiweka mbali na kila aina ya shirki. Kama ilivyoelezwa kwenye vitabu ya historia, baada ya kuteremshwa aya hizi Bwana Mtume Muhammad SAW aliwaalika jamaa zake wa karibu, miongoni mwao akiwemo Abu Talib, Abu Lahab na Hamza. Baada ya kumalizika dhifa ya chakula, Abu Lahab aliivuruga hafla hiyo na kutomruhusu Bwana Mtume awafikishie hadhirina wito wake wa Utume. Siku nyengine Bwana Mtume akawaalika tena jamaa zake. Na baada ya kuwakirimu wageni wake hao akawaambia: Mwenyezi Mungu ameniamuru nikulinganieni dini ya tauhidi. Mimi nakutakieni nyinyi kheri yenu ya duniani na akhera; na mimi simjui yeyote aliyewaletea watu wa kaumu yake kitu bora kama kile ambacho mimi nimekuleteeni nyinyi. Yeyote miongoni mwenu atakayenisaidia katika jambo hili atakuwa ndugu yangu, wasii wangu na khalifa wangu. Ghairi ya Ali bin Abi Talib, hakuna mwengine yeyote katika hadhirina aliyesimama kuitikia wito huo. Baada ya hapo Bwana Mtume akasema: Jueni kwamba yeye ni ndugu, wasii na khalifa wangu kati yenu. Yasikilizeni maneno yake na tiini amri yake." Tukio hili ambalo limesimuliwa na akthari ya wanahistoria wa Kiislamu linadhihirisha hali ya upweke aliyokuwa nayo Bwana Mtume kwa jamaa zake, na usaidizi wa Imam Ali (AS) kwa mtukufu huyo na jinsi alivyokuwa pamoja naye bega kwa bega tangu mwanzoni mwa Utume wake. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba kumwendea kumwomba mwengine yeyote ghairi ya Allah, hatima yake ni kudhalilika mtu na kufikwa na adhabu ya Mola. Kwa sababu shirki ilikuwa sababu ya kufikwa na adhabu na kuangamizwa kaumu zilizopita. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa mfungamano wa kiudugu unamfanya mtu awe na mas-ulia makubwa zaidi kwa watu wake. Kama ambavyo mtu ni mas-ul kwa familia yake, ana jukumu na mas-ulia pia katika kuwaongoza na kuwaelekeza kwenye uongofu ndugu na jamaa zake. Kadhalika tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba uhusiano wa kiujamaa haupasi kuwa kizuizi cha kutekeleza mtu jukumu lake hususan la kukataza maovu. Wa aidha aya hizi zinatutaka tuelewe kuwa unyenyekevu, upole na huruma ni sifa wanazopaswa kupambika nazo viongozi na wafanya tablighi katika jamii katika kuamiliana na wafuasi wao na walio chini yao. Vilevile aya hizi zinatuelimisha kuwa viongozi wa jamii wanatakiwa wachukue msimamo kuhusiana na mienendo potofu na kutangaza wazi msimamo wao huo kuhusiana na suala hilo. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 662 ya Qur'ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah atuonyeshe haki na kutupa taufiki ya kuifuata, na atuonyeshe batili na kutuwezesha kuiepuka. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh.

 

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)