Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumatatu, 18 Mei 2015 15:57

Sura ya Ash-Shua'raa, aya ya 198-209 (Darsa ya 661)

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu. Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur'ani. Hii ni darsa ya 661 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 26 ya Ash-Shua'raa. Tunaianza darsa yetu kwa aya za 198 na 199 ambazo zinasema:


وَلَوْ نَزَّلْنَاهُ عَلَى بَعْضِ الأَعْجَمِينَ


Na lau kuwa tungeli iteremsha juu ya mmoja wa wasio kuwa Waarabu,


فَقَرَأَهُ عَلَيْهِم مَّا كَانُوا بِهِ مُؤْمِنِينَ


Na akawasomea, wasingeli kuwa wenye kuiamini.


Katika darsa iliyopita tulisema kuwa Allah SW amesisitiza nukta hii, kwamba ameiteremsha hii Qur'ani kwa lugha fasaha ya Kiarabu ili itoe indhari na maonyo kwetu. Baada ya maelezo hayo, aya hizi tulizosoma zinaendelea kuelezea moja ya sababu za jambo hilo kwa kusema: taasusbi za kikabila walizokuwa nazo Waarabu wa zama za ujahiliya zilikuwa kubwa kiasi ambacho lau kama hii Qur'ani ingeliteremshwa kwa lugha isiyokuwa ya Kiarabu na kwa kuteremshwa kwa mtu asiyekuwa Mwarabu wasingekubali katu kumwamini na kukubali maneno yake. Wakati huo ambapo kitabu hicho cha Allah kiliteremshwa kwa mtu ambaye ni mzungumzaji wa lugha ya Kiarabu atokaye kwenye ukoo mtukufu na ambaye bishara za kuja kwake zimetajwa kwenye vitabu vya mbinguni vilivyotangulia, watu hao hawakuwa tayari kumwamini seuze kama mambo yote hayo yasingalikuwepo. Imam Jaafar Sadiq (AS) amesema: "Thamani na fadhila walizonazo wasiokuwa Waarabu ni kwamba wameiamini Qur'ani ambayo ni ya lugha ya Kiarabu. Lakini kama Qur'ani ingekuwa ni kwa lugha isiyokuwa ya Kiarabu, baadhi ya Waarabu wasingeiamini." Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba katika tablighi na kuwaandaa watu inapasa kuzingatia na kujali hisia na lugha ya walengwa na wakusudiwa ili kuandaa mazingira ya kuwafanya wawe tayari zaidi kuikubali haki. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa taasubu na ukereketwa wa kikabila, rangi na asili ni miongoni mwa vizuizi vya watu kuikubali haki. Hivyo tujihadhari utashi na hamasa za utaifa zisije zikatuzuia kuikubali haki.
Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya 200 hadi 203 ambazo zinasema:


كَذَلِكَ سَلَكْنَاهُ فِي قُلُوبِ الْمُجْرِمِينَ


Namna hivi tunaingiza katika nyoyo za waovu.


لا يُؤْمِنُونَ بِهِ حَتَّى يَرَوُا الْعَذَابَ الأَلِيمَ


Hawataiamini mpaka waione adhabu iumizayo.


فَيَأْتِيَهُم بَغْتَةً وَهُمْ لا يَشْعُرُونَ


Basi itawafikia kwa ghafla, na hali hawana khabari.


فَيَقُولُوا هَلْ نَحْنُ مُنظَرُونَ


Na watasema: Je, tutapewa muhula?


Wanaosemezwa na Qur'ani wapenzi wasikilizaji si waumini peke yao, bali makafiri na washirikina pia inapasa wayasikie maneno ya haki ili dhima juu yao iondoke wasije wakawa na kisingizio na udhuru wa kutoa kwa sababu ya kutoamini. Na ndiyo maana Allah SW anasema: Sisi tumeiteremsha Qur'ani kwa namna inayowafanya watu wote waielewe na kuifahamu; lakini hulka ya ukaidi, inadi, kutakabari na kufanya maasi na madhambi inawafanya baadhi ya watu wasiyaamini maneno ya haki na kuamua kuyakanusha. Na wengi wao wanashupalia ukafiri wao mpaka kufika hadi ya kusema kumwambia Mtume wao:"Sisi hatuamini mpaka utuonyeshe tuione kwa macho yetu hiyo adhabu unayoahidi kuwa itatufika." Lakini ukweli ni kwamba wakati inapoteremshwa adhabu, huwa hakuna fursa tena ya kuamini. Kwa sababu adhabu huwa inateremshwa ghafla na bila ya taarifa na kuwaangamiza waovu. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba kama nafsi ya mtu haitokuwa na ulainifu na utayarifu wa kuikubali haki, Qur'ani haiwezi kupenya na kuwa na taathira ndani ya moyo wake. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa kuendelea kufanya maovu na madhambi kunafuta athari za uwezekano wa mtu kuongoka na kuifuata haki. Kadhalika tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba tusiingiwe na ghururi kwa kuona Allah SW anatuacha na kutupa muhula, kwani mauti na adhabu yake Mola humshukia mtu ghafla bila ya kutarajia. Wa aidha aya hizi zinatuonyesha kuwa wakati wa kukata roho watu waovu huomba wapewe tena fursa na muhula mwengine.
Zifuatazo sasa ni aya za 204 hadi 207 ambazo zinasema:


أَفَبِعَذَابِنَا يَسْتَعْجِلُونَ


Basi, je, wanaihimiza adhabu yetu?


أَفَرَأَيْتَ إِن مَّتَّعْنَاهُمْ سِنِينَ


Unaonaje kama tukiwastarehesha kwa miaka,


ثُمَّ جَاءَهُم مَّا كَانُوا يُوعَدُونَ


Kisha yakawafikia waliyo kuwa wakiahidiwa,


مَا أَغْنَى عَنْهُم مَّا كَانُوا يُمَتَّعُونَ


Hayatawafaa yale waliyo stareheshewa.


Kama tulivyoona, aya zilizotangulia zimesema, wakati inapoteremshwa adhabu, watu waovu huomba wapewe muhula na fursa nyengine ili wauache mwenendo wao muovu na badala yake waiamini na kuifuata haki. Aya tulizosoma zinasema: Hata kama tutawapa watu hao muhula mwengine mrefu, hawatoamini pia na watayakadhibisha yaliyoahidiwa na Mola. Na katika hali hiyo neema za kimaada za duniani, kama mali na madaraka havitoweza kuwakinga na kuwaepusha wao na adhabu yetu. Naam! Ni namna hivi zilivyo hulka za ukafiri na takaburi za watu waovu na wakaidi, kwamba kila pale wanaposikia kwa kuambiwa na Mtume kuhusu ahadi ya adhabu iliyoahidiwa na Allah, wao hufanya shere na stihzai kwa kumwambia Mtume wao: Kama ni kweli uyasemayo, tuletee hiyo adhabu tuione kwa macho yetu. Lakini wakati wanapoziona ishara za adhabu hapo husema, inawezekana sisi kupewa fursa na muhula mwengine? Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba watu ambao leo wanakadhibisha yaliyoahidiwa na Mwenyezi Mungu, hufika siku wakaomba wapewe muhula na fursa nyengine ili wasalimike na adhabu ya Mola; lakini ombi lao hilo halitokuwa na faida yoyote kwao. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa wakati adhabu ya Mwenyezi Mungu inaposhuka, vitu na suhula zote tunu na adimu za mtu, kama mali, umashuhuri na madaraka aliyonayo huwa havina athari ya msaada wowote kwake. Kadhalika aya hizi zinatutaka tuelewe kwamba kuwa na neema za dunia si hoja ya kuwa kipenzi kwa Mola, wala kielelezo cha kuendelea kupata rehma na neema zake Allah huko akhera.
Darsa yetu ya leo inahatimishwa na aya za 208 na 209 ambazo zinasema:


وَمَا أَهْلَكْنَا مِن قَرْيَةٍ إِلاَّ لَهَا مُنذِرُونَ


Wala hatukuuangamiza mji wowote ila ulikuwa na waonyaji.


ذِكْرَى وَمَا كُنَّا ظَالِمِينَ


Kuwa ni ukumbusho. Wala Sisi hatukuwa wenye kudhulumu.


Aya hizi zinaendelea kuzungumzia maudhui ya aya zilizotangulia kwa kutoa kaida na kanuni jumla kwa kusema: Utaratibu aliouweka Allah ni kwamba hukamilisha dhima kwa waja wake wote; na kwa kuwapelekea Mitume, huwapa indhari na maonyo juu ya hatima ya amali na matendo yao maovu ili watanabahi na kuzinduka. Lakini wanapoamua kuasi na kufanya maovu kwa ujuzi na uelewa, hapo Allah huteremsha adhabu yake na kuwaangamiza. Na jambo hilo ni la uadilifu, wala si uonevu au dhulma kwa waja. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba Mwenyezi Mungu Mtukufu amewatuma wajumbe kwa kila kaumu na umma ili kuwapa watu hao maonyo na indhari. Kadhalika tunajielimisha kutokana na aya hizi kuwa adhabu kabla ya onyo na indhari ni dhulma, na Allah SW katu hawafanyii waja wake dhulma kama hiyo. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 661 ya Qur'ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah atujaalie kuwa waja waumini wa kweli, tunaoshikamana na maamrisho yake na kujiepusha na makatazo yake. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh.

 

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)