Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumatatu, 18 Mei 2015 15:49

Sura ya Ash-Shua'raa, aya ya 188-197 (Darsa ya 660)

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu. Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur'ani. Hii ni darsa ya 660 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 26 ya Ash-Shua'raa. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 188 hadi 191 ambazo zinasema:


قَالَ رَبِّي أَعْلَمُ بِمَا تَعْمَلُونَ


Akasema: Mola wangu Mlezi anajua zaidi mnayo yatenda.


فَكَذَّبُوهُ فَأَخَذَهُمْ عَذَابُ يَوْمِ الظُّلَّةِ إِنَّهُ كَانَ عَذَابَ يَوْمٍ عَظِيمٍ


Basi wakamkadhibisha, na ikawashika adhabu ya siku ya wingu (la moto). Hakika hiyo ilikuwa adhabu ya siku kubwa (na ya kutisha).


إِنَّ فِي ذَلِكَ لآيَةً وَمَا كَانَ أَكْثَرُهُم مُّؤْمِنِينَ


Hakika katika hayo ipo Ishara, lakini hawakuwa wengi wao wenye kuamini.


وَإِنَّ رَبَّكَ لَهُوَ الْعَزِيزُ الرَّحِيمُ


Na hakika Mola wako Mlezi bila ya shaka ndiye Yeye Mwenye nguvu Mwenye kurehemu.


Katika darsa iliyopita tulisema kuwa watu wa eneo la Ayka, mji uliokuwako karibu na Madyan, walimvurumizia Nabii Shuaib (AS) aliyetumwa kwao pia tuhuma za kuwa ni mtu aliyerogwa na kusema maneno yasiyoingia akilini; na kwa hivyo wakamkadhibisha Mtume huyo wa Allah. Lakini si hayo tu bali kwa kutumia lugha ya kejeli na istihzai walimwambia:" Kama unasema kweli kuwa hayo uyasemayo umetumwa na Mwenyezi Mungu, na kwamba kama tutakwenda kinyume na maamrisho ya Mola wako Yeye atatuadhibu, basi tuteremshie papa hapa duniani mawe ya vipande vya mbingu ili itufike hiyo adhabu unayotuahidi." Baada ya maelezo hayo aya hizi tulizosoma zinasema: Nabii Shuaib aliwajibu watu hao kwa kuwaambia: "Mwenyezi Mungu anayaona muyafanyayo, na anajua aamiliane vipi na nyinyi kwa namna aitakayo. Kwamba Yeye Allah atakuadhibuni au la, na au kama atakuadhibuni, adhabu hiyo itakuwaje, mimi sina nafasi yoyote katika hilo." Kisha aya zinaendelea kueleza kwamba Allah SW aliwaangamiza watu hao kwa adhabu kali. Kuhusu namna adhabu ya watu wa Ayka ilivyokuwa imeelezwa katika hadithi kwamba ardhi hiyo ilipigwa na joto kali mno la kuunguza; na kisha baada ya siku chache wingu zito jeusi lilitanda angani likawatia tamaa watu hao ya kunyesha mvua na kupoa moto wa joto lililowapata. Lakini ghafla radi kali ya maangamizi ilipiga kutoka mawinguni, ikatoa moto ulioteketeza miti chungu nzima na kuwaletea moto wa hilaki watu wa mji wa Ayka. Sambamba na radi hiyo tetemeko kubwa na la kutisha la ardhi liliukumba pia mji huo na kuwaangamiza makafiri hao wakaidi na wenye inadi. Na mwishowe, yaliyotokea kwa Nabii Shuaib pamoja na hatima ya watu wa Ayka vikaelezwa na aya zile zile zilizosimulia yaliyojiri katika kaumu za Mitume waliotangulia. Aya ambazo zinasema: Katika kuangamizwa kaumu ya watu hao wabishi na wakaidi kuna ibra, mafunzo na mazingatio makubwa, lakini licha ya watu wengi kuziona ishara hizo hawako tayari kuamini. Ni kama kwamba hawajui kuwa Mwenyezi Mungu Azza wa Jalla ni mwenye nguvu mutlaki na mweza wa kila kitu na huwaangamiza wale wanaosimama kuipinga haki. Tab'an kwa wale wanaotubia na kurejea kwake, Yeye Mola ni Mrehemevu kwao, na huwafungulia mlango wa rehma zake. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba hatutakiwi sisi kuwa na maoni kuhusu namna na kiwango cha adhabu watakayopata waovu na wafanya madhambi. Hata Mitume wa Allah pia walikuwa wakieleza kuwa wao hawajui chochote kuhusu jambo hilo na kwamba elimu yake iko kwa Mwenyezi Mungu mwenyewe SW. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa kupenda dunia na kuabudu mali humfanya mtu asimame kukabiliana na Mitume na kuwakadhibisha, ukadhibishaji ambao hufuatiwa na adhabu kali ya duniani na akhera.
Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya 192 hadi 195 ambazo zinasema:


وَإِنَّهُ لَتَنزِيلُ رَبِّ الْعَالَمِينَ


Na hakika hii ni Uteremsho wa Mola Mlezi wa walimwengu wote.


نَزَلَ بِهِ الرُّوحُ الأَمِينُ


Ameuteremsha Roho muaminifu,


عَلَى قَلْبِكَ لِتَكُونَ مِنَ الْمُنذِرِينَ


Juu ya moyo wako, ili uwe katika Waonyaji,


بِلِسَانٍ عَرَبِيٍّ مُّبِينٍ


Kwa lugha ya Kiarabu iliyo wazi (fasihi).


Baada ya kusimuliwa yaliyojiri katika maisha ya Mitume saba na kuangamizwa watu wabishi, wakaidi na wenye inadi wa kaumu zao, aya hizi tulizosoma zinasema: yale yaliyosimuliwa ndani ya Qur'ani kuhusu maisha na yaliyojiri katika kaumu zilizopita ni maneno ya Mola Muumba yasiyo na chembe ya khurafa wala mambo ya ngano, maneno ambayo yaliteremshwa na malaika mwaminifu Jibril kwenye moyo wa Bwana Mtume Muhammad SAW. Naye Bwana Mtume aliyafikisha maneno hayo kwa watu pasina kuongeza wala kupunguza kitu ili kuwatahadharisha na kuwahofisha na hatari ya kumwasi Mwenyezi Mungu. Aya hizi tulizosoma zinaendelea kwa kusisitiza juu ya kuwa safi Qur'ani na kusalimika na aina yoyote ile ya upotoshwaji. Katika upande mmoja kuna wasita na kiunganishi cha wahyi, yaani Jibril, ambaye ameelezewa kuwa ni mwaminifu, na katika upande mwengine kuna kituo cha kufikia wahyi huo ambacho ni moyo wa Bwana Mtume, ambayo ni roho na nafsi safi na toharifu ya mbora huyo wa viumbe. Na yeye Bwana Mtume alikuwa akiwatamkia watu kilekile ulichokipokea moyo wake. Kwa hivyo Qur'ani tukufu ni kitabu kilichotakasika na hali yoyote ile ya shaka na upotoshwaji kama ambavyo kina ukwasi wa kiwango cha juu kabisa cha fasaha na balagha. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba mfumo wa upangaji hukumu na sheria za dini unawiyana na mfumo wa uumbaji wa ulimwengu wa maumbile na vilivyomo ndani yake. Kwa maneno mengine, Yule mwenye kuteremsha wahyi na kuweka sheria za uongofu za dini kwa ajili ya saada ya wanadamu, ndiye Yeye Yeye Muumba wa ulimwengu na ndiye mwenye kuuendesha kwa tadbiri yake ulimwengu huo wa maumbile. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa Qur'ani ni wahyi ulioteremshwa na Allah SW na imetakasika na aina yoyote ile ya upotoshwaji. Kadhalika tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba kaida na utaratibu aliouweka Allah ni kutuma Mitume wa kutoa maonyo na indhari kwa watu na kuwazindua wale walioghafilika na waliopotoka.
Darsa ya 660 ya Qur'ani inahatimishwa na aya za 196 na 197 ambazo zinasema:


وَإِنَّهُ لَفِي زُبُرِ الأَوَّلِينَ


Na hakika (habari za) hiyo (Qur'ani) zimo katika Vitabu vya kale.


أَوَلَمْ يَكُن لَّهُمْ آيَةً أَن يَعْلَمَهُ عُلَمَاء بَنِي إِسْرَائِيلَ


Je! Haikuwa kwao ni Ishara (ya ukweli wa Qur'ani) kwamba wanayajua haya wanazuoni wa Wana wa Israili?


Aya hizi wapenzi wasikilizaji zinaashiria moja ya hoja za kuthibitisha ukweli wa Qur'ani na kueleza kwamba: Ikiwa washirikina wa Makka wana shaka juu ya ukweli wa Qur'ani wanaweza kuwaendea maulama wa Kiyahudi na kuweza kupitia kwao wao kufahamu Mtume na kitabu alichokuja nacho walivyozungumziwa katika vitabu vilivyotangulia vya mbinguni kikiwemo cha Taurati. Ni wazi kwamba laiti bishara hizo kuhusu Bwana Mtume zingekuwa hazimo ndani ya Taurati iliyokuwepo katika zama zake, na ikawa maulama wa Kiyahudi hawana habari juu ya jambo hilo, kusingekuwa na sababu ya Qur'ani kutoa dai kama hilo na kumtaka Bwana Mtume awaeleze watu jambo hilo. Kwa sababu maulama hao wa Kiyahudi wangemkana na kumwita kidhabi na mwongo. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba bishara za kudhihiri Nabii Muhammad SAW, yaani Mtume wa zama za mwisho wa Allah pamoja na kitabu chake cha Qur'ani zimetajwa katika maandiko ya asili ya vitabu vya mbinguni vilivyotangulia. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa muhtawa na makusudio ya mengi yaliyomo ndani ya aya za Qur'ani yametajwa ndani ya vitabu vya kabla yake, lakini maneno yake ya asili yameteremshwa kwenye kifua cha Bwana Mtume Muhammad SAW. Aidha tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba maulama wa Kiyahudi walikuwa wakiujua ukweli wa Qur'ani lakini hawakuwa tayari kusilimu na kuifuata haki ya Uislamu kwa sababu ya kulinda maslahi yao, vyeo na hadhi zao. Wapenzi wasikilizaji, darsa yetu ya leo imefikia tamati. Tunamwomba Allah atuonyeshe haki na kutuwafikisha kuifuata na atuonyeshe batili na kutuwezesha kuiepuka. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh.

 

 

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)