Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumatatu, 20 Aprili 2015 16:40

Sura ya Ash-Shua'raa, aya ya 176-187 (Darsa ya 659)

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu. Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur'ani. Hii ni darsa ya 659 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 26 ya Ash-Shua'raa. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 176 hadi 180 ambazo zinasema:


كَذَّبَ أَصْحَابُ الأَيْكَةِ الْمُرْسَلِينَ


Watu wa Mwituni waliwakadhibisha Mitume.


إِذْ قَالَ لَهُمْ شُعَيْبٌ أَلا تَتَّقُونَ


Shuaibu alipo waambia: Je! Hamfanyi mkamchamngu?


إِنِّي لَكُمْ رَسُولٌ أَمِينٌ


Hakika mimi kwenu ni Mtume muaminifu.


فَاتَّقُوا اللَّهَ وَأَطِيعُونِ


Basi mcheni Mwenyezi Mungu, na nit'iini mimi.


وَمَا أَسْأَلُكُمْ عَلَيْهِ مِنْ أَجْرٍ إِنْ أَجْرِيَ إِلاَّ عَلَى رَبِّ الْعَالَمِينَ


Wala sikutakini ujira juu yake. Ujira wangu hauko ila kwa Mola Mlezi wa walimwengu wote.


Kando ya mji wa Madyan lilikuwepo eneo liitwalo Ayka ambalo watu wake walipelekewa Nabii Shuaib, ambaye mbali na kupewa utume kwa ajili ya watu wa mji wake wa Madyan aliamriwa na Mola afanye safari hadi huko Ayka pia ili kuwafikishia watu wito wa uongofu. Ayka maana yake ni vichaka au mwitu; na eneo hilo lilijulikana kwa jina hilo kutokana na kuwa na miti mingi iliyosongana. Watu wa mji wa Ayka walikuwa wakiishi maisha ya raha na uneemevu na walikuwa na mali na utajiri mwingi. Na kama walivyokuwa watu wengine wengi wenye raha, nao pia waliingiwa na ghururi iliyowaghafilisha na kuwafanya wajisahau. Yaliyonukuliwa na Qur'ani kuhusu maneno aliyoyasema Nabii Shuaibu ni sawa na yaliyonukuliwa kutoka kwenye vinywa vya Mitume wengine katika aya zilizotangulia za sura hii. Yaani kuwalingania watu taqwa na kumcha Mungu na kujiepusha na vitendo viovu na vichafu. Na badala yake kutii maamrisho ya Mola yanayoteremshwa na Yeye Mola Mwenyezi kupitia Mitume wake. Aya hizi tulizosoma zinaashiria pia sifa mbili muhimu za Mitume. Ya kwanza ni historia ya wema wao kwa watu ulioambatana na ukweli, mwamana na uaminifu, na ya pili ni kutokuwa na matarajio ya kupata bakhshishi wala malipo yoyote kwa wanadamu wenzao ili wapinzani wasije wakalitumia suala hilo kuwa kisingizio cha kufanya propaganda chafu dhidi yao.
Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya 181 hadi 184 ambazo zinasema:


أَوْفُوا الْكَيْلَ وَلا تَكُونُوا مِنَ الْمُخْسِرِينَ


Timizeni kipimo sawa sawa, wala msiwe miongoni mwa wanao punja.


وَزِنُوا بِالْقِسْطَاسِ الْمُسْتَقِيمِ


Na pimeni kwa mizani iliyo sawa;


وَلا تَبْخَسُوا النَّاسَ أَشْيَاءَهُمْ وَلا تَعْثَوْا فِي الأَرْضِ مُفْسِدِينَ


Wala msiwapunje watu vitu vyao, wala msifanye ufisadi katika ardhi mkafanya vurugu.


وَاتَّقُوا الَّذِي خَلَقَكُمْ وَالْجِبِلَّةَ الأَوَّلِينَ


Na mcheni aliye kuumbeni nyinyi na vizazi vilivyo tangulia.


Baada ya wito jumla wa taqwa na kumcha Mwenyezi Mungu, Nabii Shuaibu aliashiria vitendo muhimu zaidi vya upotofu wa masuala ya kiuchumi uliokuwa umeenea miongoni mwa watu wa Ayka na kuwaambia: kwa nini mnapunja katika uuzaji na kuwatia hasara washitiri na wanunuzi? Kwa nini hamuzitumii mizani na vipimo kwa njia sahihi na mnawapunja watu haki zao? Kwa nini wakati mnaponunua mnadunisha na kudogesha thamani ya mali na bidhaa za watu na kuzitia ila? Eneo la Ayka wapenzi wasikilizaji lilikuwa na hali nzuri ya hewa na lilikuweko kwenye njia ya misafara ya biashara baina ya Hijaz na Sham, hivyo kila mara lilikuwa likitembelewa na misafara ya wafanyabiashara kutoka sehemu mbalimbali. Kwa kuzingatia kuwa katika zama za kale miamala ya biashara ilikuwa ikifanyika kwa kubadilishana bidhaa kwa bidhaa na wala hakukuwepo na matumizi ya pesa, wasafiri waliokuwa wakiwasili katika eneo la Ayka, walikuwa wakiuza baadhi ya bidhaa zao ili kuweza kununua vitu wanavyohitaji. Hivyo wakati watu wa eneo hilo walipokuwa wakinunua bidhaa kwa wasafiri na wageni hao walikuwa wakizitia ila na kasoro na kuzishusha thamani zao; na wakati wao walipokuwa wakiwauzia wageni hao bidhaa zao walikuwa hawavijazi vipimo kama inavyotakiwa au wakitumia mizani zenye walakini kupimia vitu ambazo zikionyesha uzito wa bidhaa ni mdogo kuliko uzito wake halisi. Sehemu ya mwisho ya aya hizi inaashiria upunjaji katika kuuza na kunyonya haki za watu katika miamala ya biashara na kueleza kwamba mambo hayo yanaeneza maovu na ufisadi katika ardhi. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba kuchunga taqwa kuna maana pana inayojumuisha pia kuchunga na kutoa haki za watu. Kwa hivyo kuwanyima au kuwapunja watu haki zao kwa namna yoyote ile ni katika alama za utovu wa taqwa alionao mtu. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa upunjaji katika kuuza ni moja ya maovu makubwa ya kiuchumi na wala hayaishii kwenye vipimo na mizani tu bali unajumuisha kazi, mas-ulia na majukumu yote ya kijamii. Namna yoyote ile ya kutowatimizia watu haki zao ni aina mojawapo ya upunjaji. Kadhalika tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba kuwepo mfumo salama wa uchumi katika jamii ni moja ya malengo yaliyofuatiliwa na Mitume. Kwa sababu ufisadi na utaratibu mbovu wa kiuchumi ni chanzo cha kuharibika watu na kusambaratika mfumo wa kijamii. Wa aidha tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba uadilifu katika nyuga na nyanja zote ikiwemo ya masuala ya uchumi umesisitizwa na kutiliwa mkazo na dini na Mitume wote wa Allah katika zama zote za historia.
Darsa yetu ya leo inahatimishwa na aya ya 185 hadi 187 ambazo zinasema:


قَالُوا إِنَّمَا أَنتَ مِنَ الْمُسَحَّرِينَ


Wakasema: Hakika wewe ni miongoni mwa walio rogwa tu.


وَمَا أَنتَ إِلاَّ بَشَرٌ مِّثْلُنَا وَإِن نَّظُنُّكَ لَمِنَ الْكَاذِبِينَ


Na wewe si chochote ila ni mtu tu kama sisi, na kwa yakini tunakuona wewe ni katika waongo.


فَأَسْقِطْ عَلَيْنَا كِسَفًا مِّنَ السَّمَاء إِن كُنتَ مِنَ الصَّادِقِينَ


Basi tuangushie vipande kutoka mbinguni ikiwa wewe ni miongoni mwa wasemao kweli.


Baada ya Nabii Shuaib (AS) kuwapa maneno ya mantiki yenye hoja na burhani ya wazi kabisa watu wa Ayka ya kuwataka waache kudhulumu na kuwapunja watu haki zao, kilichofanywa na watu hao katika kukabiliana na hoja hizo ni kumtuhumu Nabii Shuaib kuwa ni mtu aliyerogwa na kurukwa na akili kutokana na sihiri na marogo aliyofanyiwa na hivyo kusema maneno yasiyoingia akilini. Lakini baada ya hayo wakaendelea zaidi kumwambia Mtume huyo wa Allah kwamba kwa kuwa unasema maneno yasiyoingia akilini basi itabidi ututhibitishie kuwa wewe ni Mtume kweli, na maneno haya unayoyasema yanatokana na Mwenyezi Mungu; wakati ukweli ni kwamba hakuna tofauti yoyote kati yako wewe na sisi; na wewe ni binadamu tu kama sisi. Kwa hivyo sisi hatukubali kwamba wewe umetumwa na Mwenyezi Mungu mpaka utuonyeshe muujiza na kututeremshia mawe makubwa makubwa kutoka mbinguni yatuangukie vichwani mwetu na kutuangamiza kwa hiyo adhabu unayotuahidi kuwa itatufika. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba uvurumizaji tuhuma ni fimbo na silaha inayotumiwa na watu wasio na hoja wala mantiki na wasioweza kutoa jibu sahihi na la mantiki kwa maneno wanayoambiwa, yaliyojaa burhani na mantiki kamili. Ni sawa na walivyofanya watu wa mji wa Ayka ambao walipokabiliwa na maneno ya mantiki ya Nabii Shuaib (AS) walimjibu Mtume wao huyo kwamba wewe umerogwa na hivyo akili zimekuruka. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa baadhi ya wapinzani wanakuchukulia Mitume kuwa wanadamu kuwa ni udhaifu, wakati hiyo ni miongoni mwa fadhila kwa Manabii hao wa Allah kwamba wanatokana na kiumbe mwanadamu na kwa hivyo wanaweza kuwa na taathira kubwa zaidi kwa watu na kuwa ruwaza na mfano wa kivitendo wa kuigwa na viumbe hao. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 659 ya Qur'ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah atupe mema duniani, na akatupe mema akhera na atulinde na adhabu ya moto.

Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.

 

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)