Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumatatu, 20 Aprili 2015 16:34

Sura ya Ash-Shua'raa, aya ya 167-175 (Darsa ya 658)

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu. Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur'ani. Hii ni darsa ya 658 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 26 ya Ash-Shua'raa.Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 167 na 168 ambazo zinasema:


قَالُوا لَئِن لَّمْ تَنتَهِ يَا لُوطُ لَتَكُونَنَّ مِنَ الْمُخْرَجِينَ


Wakasema: Kama (hutoacha maneno yako haya) ewe Lut'i! bila shaka utakuwa miongoni mwa wanao tolewa!


قَالَ إِنِّي لِعَمَلِكُم مِّنَ الْقَالِينَ


Akasema: Hakika mimi ni katika wanao kichukia hichi kitendo chenu.


Katika darsa iliyopita tulisema kuwa Nabii Lut (AS) alijenga hoja kwa watu wa kaumu yake za kuwaonyesha kuwa vitendo wanavyofanya vya liwati ni uovu mkubwa na kuwataka waache uovu huo. Aya tulizosoma zinasema: badala ya watu hao kusikiliza nasaha na mawaidha ya Mtume wao na kuacha vitendo vyao vichafu walianza kutoa vitisho dhidi ya Nabii Lut kwa kumwambia, kama hutoacha kutuandama kwa nasaha na mawaidha yako ukaendelea kutughasi na kutusumbua tutakuhamisha kwa kukutoa katika mji wetu huu ili tupate kujitanafasi na kufanya tuyatakayo. Nabii Lut (AS) hakutishika na vitisho vyao bali badala yake aliwakabili na kuwajibu kwa uwazi kabisa kwamba, mimi ninachukizwa na kukirihishwa na vitendo vyenu, na wala sitoacha kuvikemea na kuvipinga. Nukta ya kutaamali na kuzingatia hapa ni kwamba Nabii Lut hakuwaambia watu wake mimi nina uadui na nyinyi au ninakuchukieni nyinyi, bali alisema: Mimi ninachukia vitendo vyenu; ikiwa na maana kwamba endapo mtaacha vitendo hivyo udugu na upendo baina yetu utarudi pale pale. Ni maovu mnayoyafanya ndiyo yanayonifanya nichukue kila hatua niwezayo kupambana nayo na kuzuia yasizagae na kuenea katika jamii. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba kuwahamisha na kuwabaidisha waja wema na walinganiaji haki ni mbinu inayotumiwa na watu wachafu na madhalimu ili waweze kuendelea kufanya maovu na dhulma zao bila ya usumbufu wala wasiwasi wowote. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa haijuzu kukaa kimya na kuyanyamazia maovu. Kama maovu hayo yatakuwa yanafanywa hadharani na bila ya kificho, inapasa watu wadhihirishe na kutangaza hadharani pia jinsi wanavyoudhiwa na kuchukizwa nayo. Na hatua zichukuliwe kwa maneno na vitendo ili kukabiliana na maasi na maovu. Wa aidha aya hizi zinatuonyesha kwamba kwa kuwa Mitume walitawakali na kumtegemea Mwenyezi Mungu tu hawakushtushwa wala kutiwa hofu na vitisho vya maadui wa haki na wala hawakuacha kupambana na dhulma, maovu na upotofu katika mazingira yoyote yale.
Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya 169 hadi 171 ambazo zinasema:


رَبِّ نَجِّنِي وَأَهْلِي مِمَّا يَعْمَلُونَ


Mola wangu Mlezi! Niokoe mimi na ahali zangu na haya wayatendayo.


فَنَجَّيْنَاهُ وَأَهْلَهُ أَجْمَعِينَ


Basi tukamwokoa yeye na ahali zake wote,


إِلاَّ عَجُوزًا فِي الْغَابِرِينَ


Isipo kuwa kikongwe (mkewe Lut'i) aliyekuwa katika walio bakia nyuma.


Baada ya maonyo, indhari na miongozo mtawalia aliyoitoa Nabii Lut (AS), dhima ya Mtume huyo wa Allah kwa watu wake ikawa imeondoka; lakini wapinzani hao wa haki wakala njama dhidi ya Mtume wao huyo. Kwa hivyo Nabii Lut akamwomba Mola wake amuokoe yeye na wafuasi wake na shari ya watu hao waovu. Mwenyezi Mungu aliitakabalia dua ya Mtume wake; hivyo akamwamuru yeye pamoja na wote waliomwamini watoke nje ya mji wakati wa usiku, watu wote watakapokuwa wamelala, ili wasiwepo mjini hapo wakati adhabu itakaposhuka. Tab'an kati ya watu wa nyumbani kwake na wafuasi wake Nabii Lut, mkewe alikuwa mmoja wa watu wapotofu na hakuwa na msaada wowote kwa mumewe ambaye ni Mtume wa Allah katika kupambana na vitendo viovu vya watu wa kaumu yake. Kwa sababu hiyo mke wa Nabii Lut (AS) alibaki pamoja na watu wa kaumu yake, na akafikwa na adhabu iliyowapata watu wengine. Baadhi ya mafunzo ya kuzingatiwa kutokana na aya hizi ni kwamba haijuzu mtu kuendelea kuishi kwenye mazingira machafu na maovu, bali inapasa afikirie njia ya za kujiokoa na kujiondoa kwenye mazingira hayo. Ima airekebishe hali iliyopo au kama hilo haliwezekani basi aiokoe nafsi yake kwa kujiweka mbali na mazingira hayo. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, mbele ya Allah amali za mtu zinatangulia asili na nasaba yake. Hata kama mtu atakuwa mke wa Mtume, lakini kama ni mpotofu naye pia ataangamizwa. Kuwa na uhusiano wa ujamaa na nasaba na Mtume wa Mwenyezi Mungu hakumsaidii mtu kupata nusra na uokovu.
Darsa ya 658 ya Qur'ani inahatimishwa na aya ya 172 hadi 175 ambazo zinasema:


ثُمَّ دَمَّرْنَا الآخَرِينَ


Kisha tukawaangamiza wale wengine.


وَأَمْطَرْنَا عَلَيْهِم مَّطَرًا فَسَاء مَطَرُ الْمُنذَرِينَ


Na tukawanyeshezea mvua (ya mawe), basi ni ovu mno mvua (ya adhabu) ya waliyo onywa.


إِنَّ فِي ذَلِكَ لآيَةً وَمَا كَانَ أَكْثَرُهُم مُّؤْمِنِينَ


Hakika katika hayo ipo Ishara. Na hawakuwa wengi wao wenye kuamini.


وَإِنَّ رَبَّكَ لَهُوَ الْعَزِيزُ الرَّحِيمُ


Na hakika Mola wako Mlezi bila ya shaka ndiye Mwenye nguvu, Mwenye kurehemu.


Baada ya Nabii Lut na watu wa nyumbani kwake pamoja na watu wake waliomwamini kutoka nje ya mji wakati wa usiku, zilzala kubwa na ya kutisha iliukumba mji huo na kuwaangamiza watu wake. Watu hao ambao waliupitisha usiku wao wakiwa wameghariki kwenye bahari ya maovu na madhambi, waliselelea kwenye usingizi wa mghafala na kuamkia kwenye uzinduko wa maangamizi. Na si zilzala tu iliyoutingisha na kuutetemesha mji wa watu wa kaumu ya Nabii Lut na kuzibomoa bomoa nyumba zao zikasawazishika na ardhi, lakini Allah SW aliwateremshia pia mvua ya kokoto iliyowamiminikia na kuwashindilia juu yao. Ilikuwa ni kama kwamba mbingu na ardhi zilikuwa zimewakamia watu waovu na mafasiki wa kaumu hiyo na kudhamiria kuubirua mji huo juu chini, kisha kuwazika chini ya vifusi ili waangamie na kutoweka moja kwa moja. Kuhusu namna kokoto hizo zilivyowamiminikia watu wa kaumu ya Nabii Lut, baadhi ya wafasiri wa Qur'ani wamesema: Ilitokea tufani na kimbunga kikali ambacho kilipeperusha angani kokoto na mawe pamoja, kisha vikawateremkia na kuwafunika watu hao; na kuna waliosema ni volkano iliyokuwa imezimika ambayo iliripuka tena na kuteremsha mvua ya cheche zilizotoka kwenye tanuri la volkano hiyo. Kisha sehemu inayofuatia ya aya, inakariri yale yaliyoelezwa na aya zilizotangulia kuhusu hatima iliyowafika watu wa kaumu za Mitume waliopita, kwamba sababu ya kuteremshiwa adhabu watu hao ni kuwa licha ya kuona alama na ishara za ukweli wa wito wa haki, wengi wao hawakuwa tayari kuamini na wakaamua kula njama dhidi ya Mitume na mawalii wa Allah. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba jamii iliyokitihiri kufanya madhambi na maovu ijiandae kuadabishwa na kufikwa na adhabu ya Mwenyezi Mungu. Adhabu ambayo inaweza kuwajia watu kutokea upande wowote na kwa namna yoyote ile aliyokadiria Mola. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa indhari na maonyo yanahitajika ili kuondoa dhima na jukumu kwa watu; na adhabu huwa haiwashukii watu bila ya kutimizwa hayo kwanza. Wa aidha tunajielimisha kutokana na aya hizi kuwa ulimwengu wa maumbile uko kwenye mamlaka ya qudra na nguvu za Allah SW. Mola Mwenye uwezo wa kuteremsha mvua ya maji kutoka mbinguni ni Mweza pia wa kuteremsha mvua ya kokoto na mawe. Kwa haya machache wapenzi wasikilizaji tunaifunga darsa yetu hii. Tunamwomba Allah atuepushe na madhambi makubwa na madogo, ya siri na ya dhahiri, na atuwafikishe kufanya yale yatakayotuwezesha kupata radhi na rehma zake Yeye Mola.

Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh

 

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)