Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumatatu, 20 Aprili 2015 16:24

Sura ya Ash-Shua'raa, aya ya 157-166 (Darsa ya 657)

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu. Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur'ani. Hii ni darsa ya 657 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 26 ya Ash-Shua'raa. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 157 hadi 159 ambazo zinasema:


فَعَقَرُوهَا فَأَصْبَحُوا نَادِمِينَ


Lakini wakamuuwa, na wakawa wenye kujuta.


فَأَخَذَهُمُ الْعَذَابُ إِنَّ فِي ذَلِكَ لآيَةً وَمَا كَانَ أَكْثَرُهُم مُّؤْمِنِينَ


Basi ikawapata adhabu. Hakika katika hayo ipo Ishara. Lakini hawakuwa wengi wao wenye kuamini.


وَإِنَّ رَبَّكَ لَهُوَ الْعَزِيزُ الرَّحِيمُ


Na hakika Mola wako Mlezi ndiye Mwenye nguvu Mwenye kurehemu.


Katika darsa iliyopita tulisema kuwa watu wa kaumu ya Thamud walimtaka Nabii Saleh (AS) awaletee muujiza; na kwa irada ya Allah SW ngamia wa muujiza alitoka kwenye jabali. Lakini vigogo wa kaumu hiyo wakamtuma mtu wao mmoja akamuue ngamia huyo kwa kumkata miguu na mikono yake. Wao walikuwa wakihisi kwamba kuwepo ngamia huyo kutawafanya watu wamwamini Nabii Saleh na kuachana na dini na itikadi zao potofu. Ni kwa sababu hiyo ndio maana hawakutaka ishara na muujiza huo wa Mwenyezi Mungu uendelee kubakia mbele ya macho ya watu. Na kwa kuwa karibu watu wote waliridhia kitendo hicho, Qur'ani tukufu iliwahusisha nao wao wote dhambi ya kumuua ngamia huyo.
Kwa kuzingatia kwamba muujiza huo wa ngamia uliletwa kwa ombi lililotolewa na watu wenyewe wa kaumu ya Thamud, baada ya kumuua ngamia huyo ishara za adhabu ya Mwenyezi Mungu zilianza kuwadhihirikia watu hao. Wakati walipoziona ishara za adhabu watu wa kaumu ya Thamud walijuta kwa kitendo walichofanya cha kumuua ngamia wa miujiza. Lakini majuto yao hayakuwa na faida tena, kwa sababu majuto na kutubia wakati wa kuona adhabu ni toba iliyochelewa na isiyo na taathira tena. Matokeo yake adhabu ya Allah iliwashukia watu hao kwa kupigwa na ukelele wa maangamizi ulioandamana na zilzala kali na ya kutisha ambayo ilizisagasaga nyumba za watu wa kaumu hiyo ovu ambazo ziliwaporomokea na kuwaangamiza watu wenyewe. Katika kuhitimisha mazungumzo juu ya kaumu ya Thamud, Qur'ani tukufu imerudia tena maneno yaleyale iliyoyaeleza baada ya kueleza yaliyojiri katika kaumu za Manabii Hud, Nuh na Ibrahim (AS) kwa kubainisha kwamba ishara za ukweli wa Mitume hao ziliwadhihirikia na kuwabainikia watu hao, lakini hawakuwa tayari kuikubali haki bali waliipinga na kuikadhibisha. Yaliyozitokea kila moja kati ya kaumu hizo yalikuwa funzo na ibra kwa wengine, lakini hawakuyazingatia hayo bali waliendelea kufuata mwenendo na njia ileile potofu iliyopitwa na wale waliowatangulia. Wao walikuwa wakidhani kwamba wataweza kumshinda Mwenyezi Mungu na Mtume wake, ilhali Allah SW ni mwenye nguvu zisizoshindika. Tab'an kwa wale wanaotubia toba ya kweli, Yeye Allah ni Mraufu, Mpole na Mrehemevu kwao. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba kufuta ishara za qudra na uwezo wa Allah katika ardhi ni kazi inayofanywa na wapinzani wa Mitume. Iwe kwa kukusudia au bila ya kukusudia, watu hao ambao hufanya hivyo kwa hoja na kisingizio cha kupambana na shirki, huzibomoa na kuzifuta athari na turathi zilizoachwa na mawalii wa Allah. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa kuridhia yanayofanywa na wengine humfanya mtu awe mshirika wa thawabu au adhabu watakayopata watu hao. Imam Ali (AS) amesema: Kwa kuwa watu wote waliridhia kilichofanywa na muuaji kwa hivyo nao walikuwa washirika katika adhabu. Kadhalika tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba ghadhabu za Mwenyezi Mungu zinatushukia kwa sababu ya amali na matendo yetu, vinginevyo Yeye Mola ni mwenye rehma na huruma na sisi waja wake.
Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya za 160 hadi 164 ambazo zinasema:


كَذَّبَتْ قَوْمُ لُوطٍ الْمُرْسَلِينَ


Kaumu ya Lut'i waliwakadhibisha Mitume.


إِذْ قَالَ لَهُمْ أَخُوهُمْ لُوطٌ أَلا تَتَّقُونَ


Alipo waambia ndugu yao, Lut'i: Je! Hamumchimngu?


إِنِّي لَكُمْ رَسُولٌ أَمِينٌ


Hakika mimi kwenu ni Mtume mwaminifu.


فَاتَّقُوا اللَّهَ وَأَطِيعُونِ


Basi mcheni Mwenyezi Mungu na nit'iini mimi.


وَمَا أَسْأَلُكُمْ عَلَيْهِ مِنْ أَجْرٍ إِنْ أَجْرِيَ إِلاَّ عَلَى رَبِّ الْعَالَمِينَ


Wala mimi sikutakini ujira juu yake; ujira wangu hauko ila kwa Mola Mlezi wa walimwengu wote.


Aya hizi zinafanana na maneno yale yale yaliyosemwa na Mitume waliotangulia kutajwa katika sura hii ili kuonyesha kwamba wito na ujumbe mkuu wa Mitume wote ulikuwa mmoja na wala haukuwa na tofauti katika msingi wake. Kumcha Mungu na kujiepusha na mambo maovu yalikuwa ndio maneno ya mwanzo yaliyosemwa na Mitume wote ambayo ni utangulizi wa kuyafanya mambo mema na ya kheri yaenee katika jamii.
Darsa yetu ya leo wapenzi wasikilizaji inahatimishwa na aya za 165 na 166 ambazo zinasema:


أَتَأْتُونَ الذُّكْرَانَ مِنَ الْعَالَمِينَ


Je! Katika viumbe vyote mnawaingilia wanaume?


وَتَذَرُونَ مَا خَلَقَ لَكُمْ رَبُّكُمْ مِنْ أَزْوَاجِكُم بَلْ أَنتُمْ قَوْمٌ عَادُونَ


Na mnaacha alicho kuumbieni Mola wenu Mlezi katika wake zenu? Ama kweli nyinyi ni watu mnao ruka mipaka!


Baada ya katazo jumla la Nabii Lut (AS) la kuwataka watu wake waache kumwasi Mwenyezi Mungu, katika aya hizi tulizosoma, Mtume huyo wa Allah anazungumzia uovu uliokuwa umeenea kwa watu wa kaumu yake; na katika kujaribu kuzizindua dhamiri za nafsi zao akawaambia kwa kuwahoji: Kwani nyinyi hamna wake hata mnakwenda kuingiliana kimwili na wanaume wenzenu? Nini kinaweza kuhalilisha kitendo chenu hiki ghairi ya kuonyesha hulka ya ufuska na uchupaji mipaka ya Mwenyezi Mungu?!
Liwati wapenzi wasikilizaji, ambayo ni mojawapo ya mienendo potofu katika maingiliano ya kimwili, ilikuwa imeenea katika kaumu ya watu wa Nabii Lut na kutambulika kama haki ya kimaumbile kwa wanaume; kiasi kwamba maneno ya Mtume huyo kwa watu hao yalionekana kama kioja na yenye kukinzana na haki na ukweli. Kwa masikitiko ni kwamba katika zama zetu hizi pia liwati na maingiliano ya kimwili ya watu wa jinsia moja yameenea, na si baina ya wanaume tu bali hata wanawake pia. Kwa desturi, watu wanaojihusisha na maingiliano ya kimwili na wenzao wa jinsia moja hufanya hivyo kwa hoja kwamba wao ni wamiliki wa miili yao, na kwa hivyo wana haki ya kuitumia watakavyo na kukidhi matamanio yao ya kijnsia wapendavyo kwa namna yoyote ile ya maridhiano baina ya watu wawili. Ilhali katika utamaduni wa mafundisho ya dini, kimsingi hasa ni kwamba mwanadamu si mmiliki wa nafsi yake, hata awe na haki ya kuamua vyovyote atakavyo kuhusiana na mwili wake na mahitaji ya mwili huo. Mwanadamu mwenyewe ni milki ya Mwenyezi Mungu; na mwili wake ni amana iliyoko mikononi mwake; kwa hivyo anachoweza kufanya kuhusiana na mwili wake ni kile tu alichohalalishiwa na Mola wake; na kama atafanya vingine kinyume na hivyo atakuwa ametenda haramu, hata kama leo hii inashuhudiwa mabunge ya baadhi ya nchi duniani yanahalalisha kisheria kwa wingi wa kura vitendo hivyo vichafu na vya kinyume cha maumbile. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba inatakiwa tuyatambue maovu yaliyoenea katika jamii, na kisha tutumie njia na mbinu mwafaka za ulinganiaji na ukatazaji ili kuzuia yasizagae ndani ya jamii. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa ili kuzuia vitendo viovu na vichafu katika jamii, inatakiwa kwanza kuonyesha njia sahihi za kukidhia mahitaji ya kimaumbile. Kama ambavyo Nabii Lut aliitaja ndoa kuwa ni njia mwafaka na ya kimantiki ya kukidhi mahitaji na ghariza za kijinsia. Wa aidha tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba Mwenyezi Mungu amemwekea mwanadamu njia ya kifitra na kimaumbile ya kutosheleza ghariza zake za kiutu. Na ni kwa sababu hiyo dini zote za tauhidi zinamshajiisha mwanadamu afunge ndoa. Kadhalika aya hizi zinatuonyesha kuwa upotofu wa matamanio ya kijinsia kama maingiliano ya kimwili ya watu wa jinsia moja ni upotokaji na ukengeukaji wa wazi wa kanuni za maumbile na ni namna moja ya uasi na uchupaji mipaka ya thamani za dini na za utu. Kwa haya machache wapenzi wasikilizaji tunaifunga darsa yetu hii. Tunamwomba Allah atuwafikishe kuyatekeleza yale aliyotuamrisha na kutuwezesha kuyaepuka yale aliyotukataza.

Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.

 

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)