Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumatatu, 20 Aprili 2015 16:19

Sura ya Ash-Shua'raa, aya ya 151-156 (Darsa ya 656)

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu. Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur'ani. Hii ni darsa ya 656 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 26 ya Ash-Shua'raa. Tunaianza darsa yetu kwa za 151 na 152 ambazo zinasema:

وَلا تُطِيعُوا أَمْرَ الْمُسْرِفِينَ


Wala msit'ii amri za walio pindukia mipaka,


الَّذِينَ يُفْسِدُونَ فِي الأَرْضِ وَلا يُصْلِحُونَ


Ambao wanafanya ufisadi ardhini, wala hawaitengenezi.


Katika darsa iliyopita tulisema kuwa Nabii Saleh (AS) alibaathiwa na kupewa Utume ili kwenda kuwalingania na kuwafikishia wito wa uongofu watu wa kaumu yake ya Thamud; na kama walivyofanya Mitume wengine waliomtangulia aliwataka watu wake waache kumwasi Mwenyezi Mungu na badala yake wafuate maamrisho yake Mola. Lakini watu hao walikuwa wameghariki kwenye anasa na starehe na hawakuwa tayari kuuamini na kuufuata wito wa haki aliowalingania Mtume wao Saleh (AS). Baada ya hayo, katika aya hizi tulizosoma Nabii Saleh anawataka watu wa kaumu yake ya Thamud waache isirafu na ubadhirifu na kufurutu mpaka katika mambo wanayofanya na kujiweka mbali na mwenendo wa wafanya isirafu ambayo ni aina mojawapo ya dhulma anayoifanya mtu kwa nafsi yake na kwa wengine pia. Na sababu ni kwamba isirafu na kufurutu mpaka husababisha kuenea maovu na madhambi baina ya watu katika jamii na kufunga njia kwa ajili ya kufanya mambo yenye manufaa na maslaha kwa jamii yenyewe. Katika utamaduni wa Kiislamu, isirafu na kufanya mambo kwa kiwango cha kupindukia mpaka kumekemewa hata katika mambo mema na ya kheri, seuze kufurutu mpaka katika ufanyaji mambo maovu na machafu yanayosababisha jamii kupotoka na kufisidika. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba kama utumiaji wa neema, mali na utajiri hautofanyika kwa kufuata muongozo wa akili timamu na wahyi wa Mwenyezi Mungu husababisha kuenea maovu na ufisadi katika jamii. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa watu wafanya isirafu hawafai kupewa mas-ulia na dhamana muhimu katika jamii au kuwa na mamlaka ya kuongoza jamii, kwa sababu hawana sifa na ustahili wa uendeshaji masuala ya jamii. Wa aidha tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba tusiwe na matumaini ya jamii kutengenea kama itakuwa mikononi mwa wafanya israfu na wanaostarehe wasioguswa na hali za wengine. Jamii itatengenea pale tu itakapoendeshwa kwa kufuata miongozo aali na mafundisho matukufu ya Mitume wa Allah.
Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya za 153 na 154 ambazo zinasema:


قَالُوا إِنَّمَا أَنتَ مِنَ الْمُسَحَّرِينَ


Wakasema: Hakika wewe ni miongoni mwa walio rogwa tu.


مَا أَنتَ إِلاَّ بَشَرٌ مِّثْلُنَا فَأْتِ بِآيَةٍ إِن كُنتَ مِنَ الصَّادِقِينَ


Wewe si chochote ila ni mtu kama sisi. Basi lete Ishara ukiwa wewe ni miongoni mwa wasemao kweli.


Kutokana na uchungu aliokuwa nao kwa watu wake wa kaumu ya Thamud na kwa ajili ya kheri ya dunia na akhera yao, Nabii Saleh (AS) aliwataka wajiweke mbali na madhambi na maovu; lakini jibu la watu hao lilikuwa ni kumtuhumu Mtume wao huyo kuwa ni mtu aliyerukwa na akili; na kwa kuathiriwa na sihiri na marogo anaropokwa maneno yasiyoeleweka. Maneno ambayo hayakuafiki akili na mantiki yao potofu kwa sababu yaliwafungia njia yao ya kujifaragua kwenye mambo ya raha, starehe na anasa. Baada ya wapinzani hao wa haki kudai kwamba ayasemayo Nabii Saleh ni maneno yasiyoingia akilini walisema: Ikiwa maneno haya, kama unavyodai, yanatoka kwa Mwenyezi Mungu, na si maneno yako mwenyewe basi angalau tuonyeshe muujiza ili tuweze kuyaamini na kuyakubali. Kwa sababu wewe ni mtu kama sisi, na hakuna sababu yoyote ya sisi kukufuata wewe na kuacha kufanya tuyatakayo. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba kwa uoni wa wapenda dunia, yeyote anayezungumza chochote au kufanya lolote linalopingana na kukinzana na maslahi yao ya kimaada na starehe zao za kidunia, basi huwa ni mtu aliyerukwa na akili na huanza kumwandama na kumvurumizia kila aina ya tuhuma. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa wapenda dunia huwa siku zote wanawafuata na kuwaiga watu waovu ambao huwa ni kigezo kwao cha kujivunia. Wao huwa hawako tayari kuwafuata watu wema ambao ni waongozaji na warekebishaji wa jamii.
Darsa yetu ya leo inahatimishwa na aya za 155 na 156 ambazo zinasema:


قَالَ هَذِهِ نَاقَةٌ لَّهَا شِرْبٌ وَلَكُمْ شِرْبُ يَوْمٍ مَّعْلُومٍ


Akasema: Huyu ngamia jike; awe na zamu yake ya kunywa, na nyinyi muwe na zamu yenu ya kunywa katika siku maalumu.


وَلا تَمَسُّوهَا بِسُوءٍ فَيَأْخُذَكُمْ عَذَابُ يَوْمٍ عَظِيمٍ


Wala msimguse kwa uwovu, isije ikakushikeni adhabu ya Siku Kubwa.


Kwa kuwa Mitume hulazimika kuonyesha miujiza ili kuthibitisha Utume wao, kwa amri ya Mwenyezi Mungu, kutoka kwenye milima na majabali yaleyale ambayo matajiri wa kaumu ya Thamud walikuwa wakipasua na kujenga makasri na majumba ya fahari alitoka ndani yake ngamia wa ajabu. Kutoka kwake ndani ya jabali ngamia huyo na pia unywaji wake wa maji vilikuwa vya kimiujiza. Kwa sababu alikuwa akinywa maji kwa kiwango ambacho iliwapasa watu wa kaumu ya Thamud watenge maji yote ya matumizi ya siku moja kwa ajili yake yeye tu. Nabii Saleh (AS) aliwatangazia watu kwamba ngamia huyu ameumbwa kwa amri ya Mwenyezi Mungu na si kama alivyo mnyama wa kawaida tu; kwa hivyo muchunge heshima na utukufu wake wala msije mkamdhuru kwa vyovyote vile, bali mwacheni ale na anywe atakavyo na wala musimghasi na kumsumbua kwa namna yoyote ile. Kwani madhara yoyote yatakayomfika mnyama huyu yatafuatiwa na adhabu kali ya Mwenyezi Mungu. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba mamlaka na uwezo wa Allah (SW) katika ulimwengu wa maumbile hauna mpaka wala ukomo; Mwenyezi Mungu ambaye aliigeuza fimbo ya Musa (AS) kuwa nyoka ni mweza wa kumtoa ndani ya jabali mnyama mkubwa mithili ya ngamia. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa ikiwa kumvunjia heshima mnyama tu mwenye utukufu kumewekewa adhabu, je kuwavunjia heshima waja watukufu wa Mwenyezi Mungu kutakuwa na hukumu na adhabu gani? Wapenzi wasikilizaji darsa ya 656 ya Qur'ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah atupe mema duniani, na akatupe mema akhera na atulinde na adhabu ya moto.

Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.

 

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)