Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumatatu, 20 Aprili 2015 16:07

Sura ya Ash-Shua'raa, aya ya 137-150 (Darsa ya 655)

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu. Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur'ani. Hii ni darsa ya 655 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 26 ya Ash-Shua'raa. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 137 hadi 140 ambazo zinasema:

 

إِنْ هَذَا إِلاَّ خُلُقُ الأَوَّلِينَ


Haya si chochote ila ni mtindo wa watu wa tokea zamani.


وَمَا نَحْنُ بِمُعَذَّبِينَ


Wala sisi hatutaadhibiwa.


فَكَذَّبُوهُ فَأَهْلَكْنَاهُمْ إِنَّ فِي ذَلِكَ لآيَةً وَمَا كَانَ أَكْثَرُهُم مُّؤْمِنِينَ


Wakamkanusha; nasi tukawaangamiza. Hakika bila ya shaka katika haya ipo Ishara. Lakini wengi wao hawakuwa wenye kuamini.


وَإِنَّ رَبَّكَ لَهُوَ الْعَزِيزُ الرَّحِيمُ


Na hakika Mola wako Mlezi ndiye Mwenye nguvu Mwenye kurehemu.


Katika darsa iliyopita tulisikia jibu walilotoa watu wa kaumu ya Aad kwa Mtume wao Hud (AS); kwani wakati nabii huyo wa Allah alipowataka wamche Mwenyezi Mungu na kuacha mambo maovu, wao walimwambia: usijisumbue na kujitaabisha bure, ukituaidhi au usituaidhi hakuna tofauti yoyote kwetu kwani mawaidha na maonyo yako hayana athari yoyote kwetu sisi. Baada ya hayo, aya hizi zinaendelea kunakili maneno ya watu wa kaumu hiyo ya Aad ambao katika kutetea matendo yao maovu walitoa hoja ya kushika njia na mwenendo waliofuata wazee wao waliotangulia na wakamwambia Nabii Hud: wewe unatukosoa na kutulaumu bure sisi na kudhani kuwa tuko kwenye upotofu. Sisi tunafuata njia ile ile waliyopita wazee wetu waliotutangulia ambayo ilikuwa njia sahihi na ya sawa; na kinyume na usemavyo wewe wala hatutoadhibiwa kwa sababu hakuna baya tulilofanya. Katika aya tulizosoma, Qur'ani tukufu inajibu kwa kusema: wao walidai aliyosema Hud (AS) ni uongo na wakaukadhibisha wito na ujumbe wake wa Utume, na kwa hivyo walifikwa na adhabu na kuangamizwa papa hapa duniani. Kwa sababu wengi wao hawakuamini wala hawakutaka kuitambua haki. Kisha aya zinaendelea kwa kueleza kwamba hayo yaliyowafika watu hao ni somo kwa watu la kupata funzo na ibra na ni alama ya qudra na nguvu za Allah Jalla fii ulaah ambayo inapasa kuzingatiwa na watu wa kaumu mbalimbali. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba mwenendo wa wazee waliopita si hoja ya kuonyesha kuwa njia waliyokuwa wakifuata ni ya haki, kama ambavyo kufuata na kuiga kibubusa na bila hoja mila, ada na desturi zilizoachwa na wazee hao na kung'ang'ania kwa taasubi juu ya mambo yaliyofanywa na wao si jambo la mantiki wala linalokubaliwa na akili timamu. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa tusitetee mambo yasiyo ya sawa tunayoyafanya kwa hoja ya kushika njia na mwenendo tuliorithi kwa waliotutangulia ili kujivua na dhima na mas-ulia juu ya matendo yetu.
Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya 141 hadi 145 za sura yetu ya Ash-Shua'raa ambazo zinasema:


كَذَّبَتْ ثَمُودُ الْمُرْسَلِينَ


Kina Thamud waliwakadhibisha Mitume.


إِذْ قَالَ لَهُمْ أَخُوهُمْ صَالِحٌ أَلا تَتَّقُونَ


Alipo waambia ndugu yao Saleh: Je! Hamumchimngu?


إِنِّي لَكُمْ رَسُولٌ أَمِينٌ


Hakika mimi kwenu ni Mtume muaminifu.


فَاتَّقُوا اللَّهَ وَأَطِيعُونِ


Basi mcheni Mwenyezi Mungu, na nit'iini mimi.


وَمَا أَسْأَلُكُمْ عَلَيْهِ مِنْ أَجْرٍ إِنْ أَجْرِيَ إِلاَّ عَلَى رَبِّ الْعَالَمِينَ


Wala sikutakini ujira juu yake. Ujira wangu hauko ila kwa Mola Mlezi wa walimwengu wote.


Baada ya aya zilizotangulia kusimulia yaliyojiri katika maisha ya Manabii, Nuh, Ibrahim, Musa na Hud (AS), aya hizi tulizosoma zinazungumzia habari za Nabii Saleh (AS) na jinsi alivyowalingania watu wa kaumu yake ya Thamud wito wa uongofu. Njia na mbinu aliyotumia Nabii Saleh ilikuwa sawa na ile iliyotumiwa na Mitume wengine ya kusisitiza juu ya misingi mitatu muhimu. Wa kwanza ni kuacha kumwasi Allah AS, wa pili ni kumfuata Mtume wao ambaye ni mtu mkweli na mwaminifu ili kupata saada ya duniani na akhera, na wa tatu ni kuwatanabahisha kwamba Mitume hawatarajii wala hawategemei chochote kwa watu, bali kazi wanayoifanya ni kwa ajili ya Mwenyezi Mungu tu, si watu wanaowalingania! Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba muhtawa, njia ya ulinganiaji na ujumbe wa Mitume wote ulikuwa mmoja. Wajumbe hao wa Allah waliwalingania watu kumwabudu Mungu mmoja tu wa haki na kuwatahadharisha na hatari ya kumwasi Mola. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa mtu anayeweza kubeba jukumu la kufikisha wito na risala ya Allah ni yule ambaye rekodi yake ya huko nyuma inaonyesha kwamba alikuwa mkweli na mwaminifu. Kwa hivyo wafanya tablighi na wafikishaji wa wito wa dini ambao ni waendelezaji wa njia ya Mitume wanapaswa wapambike na sifa hizo.
Darsa yetu hii wapenzi wasikilizaji inahatimishwa na aya ya 146 hadi 150 ambazo zinasema:


أَتُتْرَكُونَ فِي مَا هَاهُنَا آمِنِينَ


Je! Mtaachwa salama usalimina katika haya yaliyopo hapa?


فِي جَنَّاتٍ وَعُيُونٍ


Katika mabustani, na chemchemi?


وَزُرُوعٍ وَنَخْلٍ طَلْعُهَا هَضِيمٌ


Na konde na mitende yenye makole yaliyo wiva.


وَتَنْحِتُونَ مِنَ الْجِبَالِ بُيُوتًا فَارِهِينَ


Na mnachonga majumba milimani kwa ustadi.


فَاتَّقُوا اللَّهَ وَأَطِيعُونِ


Basi mcheni Mwenyezi Mungu, na nit'iini mimi.


Katika aya hizi tulizosoma Nabii Saleh (AS) anawapa indhari na tanbihi kali watu wa kaumu yake kwa kuwaambia, vipi mnadhani kwamba mtaishi milele katika dunia hii na kuendelea daima dawamu kufaidika na raha na neema zake? Vipi mnafikiria kuwa haya mabustani na mashamba ya mitende iliyonawiri na kustawi itabakia mikononi mwenu milele ili kufaidika na neema za matunda yake? Imekuwaje mumekuwa watumwa wa matumbo yenu na wa anasa na starehe za dunia kiasi hiki, na licha ya kufaidika na neema za Mwenyezi Mungu lakini kila wakati mnamwasi Yeye Mola? Basi angalau acheni kumwasi na mcheni Mwenyezi Mungu. Na kama mnataka saada ya duniani na akhera basi yasikilizeni maneno yangu, kwa sababu mimi sisemi chochote kitokanacho na mimi mwenyewe, bali ninakubainishieni maneno ya Mwenyezi Mungu Mola wenu. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba tuzitumie na kunufaika nazo neema za dunia, lakini tujihadhari zisije zikaziteka nafsi zetu, kwa sababu hivyo si vitu vya kudumu wala vyenye kubaki milele. Kadhalika tunajielimisha kutokana na aya hizi kuwa raha, uneemevu na ukunjufu wa maisha vinapokithiri mno huweza kuwa sababu ya kupoteza taqwa na kutumbukia kwenye maovu; na jamii yenye raha na ustawi mkubwa mno wa maisha inahitajia indhari na ukumbusho wa kila mara. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 655 ya Qur'ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah ajaalie neema alizotupa na anazoendelea kutupa ziwe sababu ya kumdhukuru na kumshukuru, na si kumwasi na kumkufuru.

Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.

 

 

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)