Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumatatu, 09 Machi 2015 12:21

Sura ya Ash-Shua'raa, aya ya 128-136 (Darsa ya 654)

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu. Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur'ani. Hii ni darsa ya 654 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 26 ya Ash-Shua'raa. Tunaianza darsa yetu hii kwa aya ya 128 hadi 130 ambazo zinasema:


أَتَبْنُونَ بِكُلِّ رِيعٍ آيَةً تَعْبَثُونَ


Je! Mnajenga juu ya kila mnyanyuko jengo la kufanyia upuuzi?


وَتَتَّخِذُونَ مَصَانِعَ لَعَلَّكُمْ تَخْلُدُونَ


Na mnajenga majengo ya fakhari kama kwamba mtaishi milele!


وَإِذَا بَطَشْتُم بَطَشْتُمْ جَبَّارِينَ


Na mnapo tumia nguvu mnatumia nguvu kwa ujabari.


Katika darsa iliyopita tulisema kuwa Nabii Hud (AS) alipewa Utume na kutumwa kwa watu wa kaumu ya Aad, na kila mara alikuwa akiwapa miongozo na maonyo watu wake hao ya kuifuata haki na kujiepusha na batili. Aya tulizosoma zinasema: wapinzani wa Nabii Hud walikuwa watu matajiri na wapenda raha na starehe, ambapo katika kujifaharisha na kujionyesha kwa neema walizojaaliwa, walijenga majengo marefu katika sehemu zenye miinuko licha ya kutohitajia kuishi kwenye majengo hayo, bali walikuwa wakienda huko kwa ajili ya starehe na kufanya mambo ya anasa tu. Katika hayo majumba na makasri waliyojijengea, watu wa kaumu ya Aad walifanya israfu na mambo ya kifahari kana kwamba wataishi katika dunia hii milele na wala hawatofikwa na mauti.
Baada ya kutaja maradhi ya kukumbatia dunia na kupenda jaha, ambazo zilikuwa miongoni mwa sifa mbaya za watu wa kaumu yake ya Aad, Nabii Hud (AS) anaashiria sifa na hulka nyengine chafu ya watu hao na kuwaambia kwamba: nyinyi si watu mnaosameheana wala wenye wema, uraufu na upole baina yenu, na wakati mnapokasirishwa na mtu mnakuwa mithili ya watu makatili na majabari, mkachupa mipaka na kuwadhulumu watu. Kaumu ya Aad wapenzi wasikilizaji ilikuwa ya watu makatili na wasio na huruma, na ilipotokea mtu kufanya kosa dogo tu alipewa adhabu kubwa na kali mno. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba kila jambo lenye sura ya kujionyesha na kujifakharisha linakemewa katika utamaduni wa mafundisho ya dini, hata kama litakuwa na thamani ya kisanaa. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa kujenga majumba ya fahari yaliyo mithili ya makasri huufanya moyo wa mtu utekwe na kuikumbatia dunia na kughafilika na akhera. Hali ya kuwa yawe yawavyo, makasri hayamfanyi mtu abaki milele duniani. Kadhalika tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba ujengaji nyumba na majengo – kama yalivyo mambo mengine ya kidunia – unaweza ukawa na madhara yake, ambayo inapasa kujiepusha nayo, kama vile israfu na ubadhirifu, kujifaharisha na kujionyesha na kuingiwa na ghururi na kujisahau kwa kuipenda dunia.
Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya 131 hadi 134 ambazo zinasema:


فَاتَّقُوا اللَّهَ وَأَطِيعُونِ


Basi mcheni Mwenyezi Mungu, na nit'iini mimi.


وَاتَّقُوا الَّذِي أَمَدَّكُم بِمَا تَعْلَمُونَ


Na mcheni aliye kupeni haya mnayo yajua.


أَمَدَّكُم بِأَنْعَامٍ وَبَنِينَ


Amekupeni wanyama wa kufuga na watoto.


وَجَنَّاتٍ وَعُيُونٍ


Na mabustani na chemchemi.


Baada ya Nabii Hud (AS) kukosoa tabia na mwenendo usiopendeza wa watu wa kaumu yake, katika aya hizi anawatajia neema mbalimbali ambazo Allah SW amewapa watu hao na kuwataka wasimwasi Mola huyo aliyewaneemesha kwa hayo, bali wafuate maneno anayowaambia yeye Mtume wao ili wapate saada na uokovu. Neema anazozitaja Nabii Hud ni neema zenye kuonekana na kuhisika ambazo zilikuwa zimewazunguka kila upande watu wa kaumu yake. Chemchemi zilizofurika na kutiririka maji, mabustani na konde za miti ya matunda, anuai za mazao ya kilimo, mifugo ikiwemo ya nyama hoa waliokuwa wakiwazalishia chakula chao na pia kuwatumia kama vitenda kazi na vyombo vya uchukuzi; na kwa upande mwengine ni kizazi cha watoto aliowajaalia Mola ambao ni rasilimaliwatu inayohitajika kwa ajili ya kazi ya ulimaji na upandaji mazao na uchungaji na usimamizi wa mifugo yao. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba kutokuwa na taqwa na uchamungu ndio sababu ya maovu na matatizo yote ya mtu binafsi na jamii. Na ndio maana wito na agizo la kwanza la Mitume wote kwa watu wao lilikuwa ni kuwataka wachunge taqwa na kumcha Mwenyezi Mungu. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa kumcha Mwenyezi Mungu ni aina fulani ya ushukurivu kwa neema mbalimbali ambazo Yeye Mola amempa mja. Ikiwa hatuwezi kufanya jambo lolote la kuonyesha ushukurivu kwa neema chungu nzima za Allah basi angalau tusiasi na kukhalifu maamrisho yake Mola.
Darsa yetu wapenzi wasikilizaji inahatimishwa na aya ya 135 na 136 ambazo zinasema:


إِنِّي أَخَافُ عَلَيْكُمْ عَذَابَ يَوْمٍ عَظِيمٍ


Hakika mimi ninakukhofieni adhabu ya Siku Kubwa.


قَالُوا سَوَاء عَلَيْنَا أَوَعَظْتَ أَمْ لَمْ تَكُن مِّنَ الْوَاعِظِينَ


Wakasema: Ni mamoja kwetu, ukitupa mawaidha au kutokuwa miongoni mwa watoao mawaidha.


Katika aya hizi, Nabii Hud (AS) anazungumza kwa huruma na upendo, ambayo ni sifa maalumu ya Mitume wote na kuwaambia watu wapinzani wa kaumu yake kwamba: ninayoyasema mimi ni yenye faida kwenu nyinyi wenyewe wala hayanifaidishi mimi kwa chochote. Mimi sitaki chochote katika mali zenu wala sitaki ukubwa na kujikweza mbele yenu. Mimi nahofia hatima yenu; kwani kutokana na maasi yote haya mnayofanya mtafikwa na adhabu kali. Hata hivyo watu hao ambao mali na madaraka vilikuwa vimewalevya na kuwatia batra, badala ya kutaamali na kuzingatia maneno ya Nabii Hud na kuaidhika nayo, kwa jeuri na dharau walimjibu kwa kumwambia: usijisumbue na kujitaabisha bure, maneno yako haya yanaingia kwenye sikio moja na kutokea sikio jingine na wala hayana athari yoyote ndani ya nyoyo zetu. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba tunatakiwa tuwape indhari na maonyo watu waliojawa na ghururi na kutingwa na mghafala na hali ya kujisahau, hata kama neno la haki halitokuwa na taathira yoyote kwao. Aidha aya hizi zinatuelimisha kuwa ikiwa nafsi za watu hazina utayarifu wala hazilaiki kuikubali haki, basi hata maneno ya waja bora na wateule wa Allah hayatokuwa na taathira yoyote kwao na wala hawatoyakubali. Darsa ya 654 wapenzi wasikilizaji imefikia tamati. Tunamwomba Allah atujaalie kuwa washukurivu wa neema zake, tuzijuazo na tusizozijua.

Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.

 

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)