Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumatatu, 09 Machi 2015 12:13

Sura ya Ash-Shua'raa, aya ya 116-127 (Darsa ya 653)

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu. Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur'ani. Hii ni darsa ya 653 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 26 ya Ash-Shua'raa. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 116 hadi 118 ambazo zinasema:


قَالُوا لَئِن لَّمْ تَنتَهِ يَا نُوحُ لَتَكُونَنَّ مِنَ الْمَرْجُومِينَ


Wakasema: Kama hutakoma ewe Nuhu, bila ya shaka utapigwa mawe.


قَالَ رَبِّ إِنَّ قَوْمِي كَذَّبُونِ


Akasema: Mola wangu Mlezi! Hakika watu wangu wamenikadhibisha.


فَافْتَحْ بَيْنِي وَبَيْنَهُمْ فَتْحًا وَنَجِّنِي وَمَن مَّعِي مِنَ الْمُؤْمِنِينَ


Basi amua baina yangu na wao uamuzi, na uniokoe mimi na walio pamoja nami katika, Waumini.


Katika darsa iliyopita tulisema kuwa wakati Nabii Nuh (AS) alipowalingania watu wa kaumu yake wito wa Tauhidi na kuwataka wamche Allah SW wapinzani wa Mtume huyo walitumia kisingizio cha hadhi ya chini ya kijamii waliyokuwa nayo wale walioamini kusema kwamba wafuasi wa Nuh ni watu wanyonge, mafakiri na wa tabaka la chini; na kwa sababu ya kuwepo wao, sisi hatutoamini.
Aya tulizosoma hivi punde zinaelezea ukubwa wa ghadhabu na hasira za wapinzani wa Nabii Nuh ambao walimtishia Mtume wao huyo kwamba watamshambulia kwa mawe mpaka aache hayo anayoyatangaza ya kuwalingania watu; na pia awaache wao kama walivyo wajifanyie watakavyo. Lakini Nabii Nuh ambaye alikuwa amepoteza matumaini kwa wapinzani hao kumwamini na kuifuata haki, aliamua kumuelekea Mola na kumwomba ahukumu baina yake na wale walioikufuru haki kwa kumwokoa yeye na waliomwamini na kuwaepusha na shari ya wapinzani hao vichwa ngumu na wakaidi. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba kutoa vitisho vya kupiga, kutusi na hata kuua ni moja ya silaha za wapinzani wa Mitume na mawalii wa Allah katika zama zote za historia. Hata hivyo waja hao wateule wa Mwenyezi Mungu hawakuvihofu vitisho hivyo na wala hawakuacha kushikamana na njia ya haki waliyokuwa wakiilingania kwa watu. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa tumfanye Allah kuwa kimbilio letu wakati tunapokabiliwa na shari ya madhalimu wenye nguvu na madaraka, na kumwomba Yeye Mola atufungulie njia ya nusra ya kuokoka na kuepukana na shari yao.
Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya 119 hadi 122 ambazo zinasema:


فَأَنجَيْنَاهُ وَمَن مَّعَهُ فِي الْفُلْكِ الْمَشْحُونِ


Basi tukamwokoa yeye na walio kuwa pamoja naye katika marikebu iliyo sheheni.


ثُمَّ أَغْرَقْنَا بَعْدُ الْبَاقِينَ


Kisha tukawagharikisha baadaye waliobaki.


إِنَّ فِي ذَلِكَ لآيَةً وَمَا كَانَ أَكْثَرُهُم مُّؤْمِنِينَ


Hakika katika haya ipo Ishara, lakini si wengi wao walio kuwa Waumini.


وَإِنَّ رَبَّكَ لَهُوَ الْعَزِيزُ الرَّحِيمُ


Na hakika Mola wako Mlezi ndiye Yeye Mwenye nguvu Mwenye kurehemu.


Kama ilivyoelezwa katika aya nyengine za Qur'ani, Mwenyezi Mungu Mtukufu alimwamuru Nabii Nuh atengeneze jahazi kubwa na kutia ndani yake jozi moja moja ya dume na jike la kila aina ya wanyama na kisha kupanda humo yeye pamoja na wafuasi wake waliomwamini. Ulipowadia muda wa kufikwa na adhabu kaumu ya Nabii Nuh, kwa amri ya Allah Jalla Jalaaluh, maji yalichimbuka kutoka ardhini na mvua za mafuriko zikamiminika kutokea mbinguni na kusababisha gharika isiyotasawirika. Safina ya Nuh (AS) ilipasua na kukata mawimbi makubwa ya maji, ama wale wote waliomkadhibisha na kuikufuru haki waligharikishwa na kuangamizwa. Bila ya shaka kuokolewa waumini na kugharikishwa makafiri kwa namna hiyo ni moja ya alama na ishara ya wazi ya qudra na uwezo wa Allah, lakini akthari ya kaumu zilizofuatia baada ya Nabii Nuh hazikuamini; kama ambavyo licha ya kuona ishara za Mwenyezi Mungu watu wa Nabii huyo waliikana na kuikadhibisha haki na kufikwa na adhabu ya Mola. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba Allah SW ni mwenye kupokea na kuitika dua za manabii na mawalii wake, na haikhalifu ahadi yake ya kuwapa nusra na msaada wake. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa kujitenga na njia ya Mitume ni sababu ya kuhilikishwa na kuangamizwa watu. Wa aidha tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba kaida na utaratibu aliouweka Allah ni kuipa msaada haki na kuwaokoa waumini, na kuitokomeza batili na kuwaangamiza makafiri.
Zifuatazo sasa ni aya za 123 na 124 ambazo zinasema:


كَذَّبَتْ عَادٌ الْمُرْسَلِينَ


Kina A'd waliwakanusha Mitume.


إِذْ قَالَ لَهُمْ أَخُوهُمْ هُودٌ أَلا تَتَّقُونَ


Alipo waambia ndugu yao, Hud: Je! Hamumchimngu?


Baada ya Nabii Nuh, Qur'ani tukufu inaashiria risala na wito wa Tauhidi uliolinganiwa na Nabii Hud (AS) ambaye alitumwa kwa watu wa kaumu ya A'd. Kaumu hii ilikuwa ikiishi kusini mwa Bara Arabu katika ardhi ya Ahqaf ambayo ilikuwa sehemu ya nchi ya Yemen. Aya tulizosoma zinasema: watu wa kaumu ya A'd, kama walivyokuwa wa kaumu nyenginezo walimkadhibisha Mtume wao na hawakuwa tayari kuukubali wito wa haki aliowalingania, japokuwa wito wa Mitume wote akiwemo Nabii Hud (AS) haukuwa kitu kingine ghairi ya kumwabudu Mungu mmoja tu wa haki na kumcha Yeye Mola kwa kujiweka mbali na maasi na mambo maovu. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba kwa kuwa kimsingi, lengo la wito wa Mitume wote lilikuwa moja, kwa hivyo kumpinga na kumkadhibisha Mtume mmoja ni sawa na kuwapinga Mitume wote. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa Mitume walikuwa wakijichukulia kuwa ni ndugu wa watu wa kaumu zao na si wakuu au mabwana kwao, suala ambalo linaonyesha khushuu, unyenyekevu, upole, upendo na huruma waliyokuwa nayo manabii hao kwa watu wao.
Darsa yetu ya leo inahatimishwa na aya ya 125 hadi 127 ambazo zinasema:


إِنِّي لَكُمْ رَسُولٌ أَمِينٌ


Hakika mimi kwenu ni Mtume muaminifu.


فَاتَّقُوا اللَّهَ وَأَطِيعُونِ


Basi mcheni Mwenyezi Mungu, na nit'iini mimi.


وَمَا أَسْأَلُكُمْ عَلَيْهِ مِنْ أَجْرٍ إِنْ أَجْرِيَ إِلاَّ عَلَى رَبِّ الْعَالَمِينَ


Wala sikutakeni juu yake ujira, kwani ujira wangu hauko ila kwa Mola Mlezi wa walimwengu wote.


Mitume wa Allah walijulikana katika kaumu zao kuwa ni watu wakweli na waaminifu; na mwenendo wao huo ulikuwa hoja na kipimo tosha cha kuwafanya watu wa kaumu zao waukubali wito wa haki waliowalingania. Kwa mujibu wa aya tulizosoma Nabii Hud (AS) alikariri wito na ujumbe ule ule wa Nabii Nuh (AS) kwa kuwaambia watu wake, enyi watu! msimwasi Mwenyezi Mungu na nifuateni mimi ili nikujulisheni njia sahihi ya maisha na kukuelekezeni kwenye fanaka na saada. Lakini wapinzani wa Nabii Hud, ambao hawakuwa tayari kuikubali haki walitoa kila aina ya visingizio ili kuukataa na kuupinga wito wake. Ili kufuta baadhi ya visingizio vya watu hao, Mtume huyo wa Allah aliwaeleza bayana kwamba: mimi sitegemei wala sitarajii chochote kwenu nyinyi; hivyo msidhani kwamba ninatafuta mali, au umaarufu na cheo. Mwenyezi Mungu amenifanya mkwasi kwenu, na matarajio yangu mimi ni kupata fadhila na rehma zake Yeye duniani na akhera. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba kuacha kukhalifu amri za Allah na kuwatii na kuwafuata mawalii wake Mola ndilo sharti la watu kupata saada ya duniani na akhera. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kwamba ikhlasi na kutokuwa na tamaa na matarajio ya kitu ndio siri ya mafanikio katika kutekeleza mas-ulia na majukumu ya kidini. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 653 ya Qur'ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah atuonyeshe haki na kutupa taufiqi ya kuifuata, na atuonyeshe batili na kutuwezesha kuiepuka.

Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.

 

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)