Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumatatu, 09 Machi 2015 12:06

Sura ya Ash-Shua'raa, aya ya 110-115 (Darsa ya 652)

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu. Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur'ani. Hii ni darsa ya 652 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 26 ya Ash-Shua'raa. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 110 na 111 ambazo zinasema:

 

فَاتَّقُوا اللَّهَ وَأَطِيعُونِ

 

Basi Mcheni Mwenyezi Mungu, na nit'iini mimi.


قَالُوا أَنُؤْمِنُ لَكَ وَاتَّبَعَكَ الأَرْذَلُونَ


Wakasema: Je! Tukuamini wewe, hali wanao kufuata ni watu duni?


Katika darsa iliyopita tulisema kuwa Nabii Nuh (AS) alikuwa akiwalingania kila mara watu wa kaumu yake kumcha Mwenyezi Mungu na kujiepusha na madhambi; akawa anawaonyesha njia sahihi ya maisha na kuwataka wamtii yeye kwa sababu ni Mtume na Mjumbe wa Mwenyezi Mungu. Aya hizi tulizosoma pia zimeanza na wito huohuo, lakini jibu la wapinzani wa haki lilikuwa ni kusema: watu waliokuzunguka na kukuamini wewe Nuh ni wanyonge na mafakiri; si watu wenye pesa wala hadhi yoyote. Ni watu walio chini ya mamlaka yetu sisi na hawana nafasi yoyote ndani ya jamii. Basi vipi unatuweka sisi na wao katika daraja moja na kututaka tufuate dini yako kama wafanyavyo wao? Maana ya maneno hayo ni kwamba kipimo na kigezo cha kuwa na thamani mtu mbele ya watu hao kilikuwa ni cheo, hadhi, mali na umashuhuri wake; na kwa kuwa wafuasi wa Nabii Nuh (AS) hawakuwa na sifa hizo, kwa mtazamo wa watu hao hawakuwa na thamani yoyote. Hali ya kuwa mbele ya Allah (SW) na Mtume wake Nuh (AS) thamani ya mtu ni usafi wake wa kiroho, taqwa na uchaji Mungu wake, ambavyo vilionekana kwa wingi zaidi katika tabaka la watu wenye hali duni, na kwa uchache mno miongoni mwa matajiri na wenye mali walioghafilishwa na neema hiyo. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba mali na vyeo ni vitu vyenye madhara na mitihani; miongoni mwao ni kuingiwa na ghururi na kiburi na kuwadunisha watu wanyonge na mafakiri. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, mizani ya kupimia haki na ukweli ni haki yenyewe si watu walioikubali au kuikanusha. Si sawa hata kidogo kuikubali au kuikataa haki kwa hoja na kisingizio cha kuwa inafuatwa au inapingwa na kundi fulani la watu. Kadhalika tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba katika mafundisho ya Mitume, watu wote wana hali moja na sawa, wala hakuna ubaguzi au upendeleo kwa yeyote kati yao.
Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya za 112 na 113 za sura yetu ya Ash-Shua'raa ambazo zinasema:


قَالَ وَمَا عِلْمِي بِمَا كَانُوا يَعْمَلُونَ


Akasema: Nayajuaje (mimi) waliyo kuwa wakiyafanya?


إِنْ حِسَابُهُمْ إِلاَّ عَلَى رَبِّي لَوْ تَشْعُرُونَ


Hisabu yao haiko ila kwa Mola wangu Mlezi, laiti mngeli tambua!


Baada ya wapinzani wa haki kutoa visingizio vya kuwataja wafuasi wa Nabii Nuh kuwa ni watu duni na dhalili katika jamii, Mtume huyo wa Allah aliwajibu watu hao kwa kuwaambia: wajibu wangu mimi ni kuwalingania watu wa matabaka yote ya jamii kuifuata haki na kujiepusha na batili. Kwamba ni kundi na tabaka gani linaamini na lipi haliamini, hilo haliko kwenye mamlaka yangu. Aidha kuhusu kwamba watu hao huko nyuma walikuwaje na walifanya nini, hilo pia haliko kwenye mamlaka yangu mimi. Muhimu ni kwamba wao sasa wameiamini haki. Kama nyinyi mtatafakari kidogo tu basi mtafahamu kuwa hisabu ya amali na matendo yao iko kwa Mwenyezi Mungu; si kwangu mimi. Kwa hivyo msilifanye suala la hali yao ya huko nyuma kuwa kisingizio cha upinzani wenu wa kuipinga na kuikataa haki.
Kimsingi ni kwamba katika utamaduni wa mafundisho ya dini sisi hatuna haki ya kujasusi na kupeleleza mambo ya watu na kukashifu na kufichua kasoro na udhaifu wao. Wajibu wetu sisi ni kuwahukumu watu kutokana na dhahiri yao, na ikiwa mtu ataamini hatuwezi kuikataa imani yake na kutaka kumsimanga kwa sababu ya matendo yake ya huko nyuma. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba elimu ya Mitume juu ya hali za huko nyuma na za sasa za watu inategema irada ya Allah SW, na si kwamba elimu yao juu ya mambo ya ghaibu inatokana na irada yao wenyewe tu. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa hisabu ya amali za watu iko kwa Mwenyezi Mungu, si kwetu sisi, na kila mtu ni mas-ul wa amali zake si amali na matendo ya wenzake. Sisi hatuna haki ya kuhukumu kuhusu hali za Siku ya Kiyama za watu.
Aya za 114 na 115 ndizo zinazotuhatimishia darsa yetu hii. Aya hizo zinasema:


وَمَا أَنَا بِطَارِدِ الْمُؤْمِنِينَ


Wala mimi si mwenye kuwafukuza katu Waumini.


إِنْ أَنَا إِلاَّ نَذِيرٌ مُّبِينٌ


Sikuwa mimi ila ni Mwonyaji aliye dhaahiri.


Wapinzani wa Nabii Nuh (AS) walitoa sharti la kuwafanya wawe tayari kumwamini Mtume huyo, nalo ni kwamba lazima ajiweke mbali na waumini wanyonge na mafakiri ndipo wao pia watamwamini. Tab'an maneno hayo pia yalikuwa ni kisingizio tu kwani si hasha kwamba hata kama Nabii Nuh angejiweka mbali na waumini, wapinzani hao wangetafuta kisingizio kingine na wala wasingeamini. Kwa hivyo Nabii Nuh aliyakataa matakwa yao hayo yasiyo na msingi na akawaambia: kazi na wajibu wangu mimi ni kuelimisha na kubainisha haki na ukweli. Mimi sitaki kujikusanyia mali na utajiri wala kutaka jaha na umaarufu hata niamue kuwafukuza wanyonge na mafakiri na kutaka niwavute maashrafu na matajiri. Nukta ya kuvutia hapa ni kwamba kwa mujibu wa aya za Qur'ani katika zama nyenginezo pia Mitume walikutana na matakwa kama haya yasiyo na msingi ya watu matajiri kwamba kama unataka tukuamini basi wafukuze na ujiweke mbali nao watu duni na mafakiri. Lakini jibu la Mitume wote hao lilikuwa ni kukataa takwa hilo na kuwaambia watu hao kwamba wao ni mas-ul wa kuwaelimisha na kuwaelekeza kwenye uongofu watu wa matabaka yote ya jamii. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba inapasa kusimama imara kukabiliana na matarajio hewa ya wapinzani na kutokuwa tayari kuwapoteza waumini kwa sababu ya kuwavuta na kuwaleta wao kwenye dini. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa katika mafundisho ya Mitume thamani ya mtu ni imani yake, si mali na utajiri wake wala hadhi na cheo chake katika jamii. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 652 ya Qur'ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah atujaalie kuwa miongoni mwa waumini wa kweli wanaothibitisha imani zao kwa matendo yao.

Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.

 

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)