Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumanne, 17 Februari 2015 13:12

Sura ya Ash-Shua’raa, aya ya 102-109 (Darsa ya 651)

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu. Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur'ani. Hii ni darsa ya 651 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 26 ya Ash-Shua'raa. Tunaianza darsa yetu hii kwa aya ya 102 hadi 104 ambazo zinasema:


فَلَوْ أَنَّ لَنَا كَرَّةً فَنَكُونَ مِنَ الْمُؤْمِنِينَ


Laiti tungepata kurejea tena tungeli kuwa katika Waumini.


إِنَّ فِي ذَلِكَ لآيَةً وَمَا كَانَ أَكْثَرُهُم مُّؤْمِنِينَ


Hakika katika haya ipo Ishara, lakini wengi wao hawakuwa wenye kuamini.


وَإِنَّ رَبَّكَ لَهُوَ الْعَزِيزُ الرَّحِيمُ


Na hakika Mola wako Mlezi ndiye Mwenye nguvu Mwenye kurehemu.


Katika darsa iliyopita tulinukuu maneno yatakayosemwa na watu wa motoni, ambao wataonyesha majuto kwa kuwafuata watu waovu na wafanya madhambi, na kuwataja wao kuwa ndio wasababishaji wa wao kufikwa na yatakayowafika. Katika aya hizi tulizosoma Mwenyezi Mungu Mtukufu anayaelezea matakwa yao watu hao ambayo ni ya kutamani warudishwe tena duniani huku wakisema, yalaiti ungekuwepo uwezekano wa sisi kurudi duniani kwa mara nyengine na kuwa kwenye kundi la waumini. Hivi sasa tumefahamu kuwa njia tuliyokuwa tukifuata sisi duniani haikuwa njia ya sawa na hivyo tumeziangamiza nafsi zetu. Hata hivyo kutaasafu na kusikitika kwao hakutokuwa na faida huko, kwa sababu hakutokuwepo tena njia ya kurudi duniani. Qur'ani tukufu imeyajibu maneno ya watu hao kwa kusema: duniani zilikuwepo ishara chungu nzima za kuwaelekeza wao kwenye uongofu, lakini hawakutaka kuitafuta na kuikubali haki na ukweli. Pamoja na kwamba Allah aliwarefushia umri wao ili waiache njia ya batili na kuifuata haki, lakini wao waliutumia vibaya muhula huo waliopewa na kuendelea kufuata njia na mwenendo potofu. Kwa hivyo wanayoyasema leo ni maneno matupu, kwani hata kama watarudi tena duniani hakuna dhamana kwamba wataiamini na kuifuata haki. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba Siku ya Kiyama ni siku ya masikitiko na majuto; lakini majuto hayo hayatokuwa na faida yoyote wala hautokuwepo uwezekano wa kufidia kitu. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa ikiwa watu watafanya ukaidi na hawatotaka kuikubali haki, aya na ishara zote kubwa zilizopo za Mola Mwenyezi za kuwaelekeza wao kwenye uongofu hazitofaa kitu. Kadhalika tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba Mwenyezi Mungu Mtukufu ni Mwenye rehma na huruma lakini pia ni Mwenye nguvu na izza, na kwa hivyo atawaadhibu vikali watu wanaosimama kuipinga haki kwa sababu ya inadi na ukaidi.
Tunaiendeleza darsa yetu hii kwa aya ya 105, 106 na 107 ambazo zinasema:


كَذَّبَتْ قَوْمُ نُوحٍ الْمُرْسَلِينَ


Kaumu ya Nuhu waliwakadhibisha Mitume.


إِذْ قَالَ لَهُمْ أَخُوهُمْ نُوحٌ أَلا تَتَّقُونَ


Alipo waambia ndugu yao, Nuhu: Je! Hamchimngu?


إِنِّي لَكُمْ رَسُولٌ أَمِينٌ


Hakika mimi kwenu ni Mtume muaminifu.


Baada ya aya zilizotangulia kuzungumzia habari za Nabii Ibrahim (AS), aya tulizosoma zinasimulia yale yaliyojiri katika maisha ya Nabii Nuh (AS). Bila ya shaka kwa mtazamo wa kihistoria, Nabii Nuh aliishi katika zama za kabla ya Nabii Ibrahim, na Qur'ani imemtaja Nabii Ibrahim kuwa ni mfuasi wa dini ya Nabii Nuh, lakini kwa kuwa Qur'ani si kitabu cha historia, na mtazamo wake kuhusiana na yaliyojiri kwa watu waliotangulia si mtazamo wa kihistoria kwa hivyo haijifungi na msingi wa kutanguliza na kufuatiza maudhui kwa kuzingatia zama. Jina la Nabii Nuh limetajwa ndani ya Qur'ani mara 43; na Allah SW amemsalia na kumtakia rehma maalumu mtume wake huyo. Watu wa kaumu ya Nabii Nuh walimkadhibisha mtume wao huyo, lakini Qur'ani inasema: Kaumu yake iliwakadhibisha Mitume wote, kwa sababu Mitume wote wana lengo moja; na kumkadhibisha yeyote kati yao ni sawa na kuwakadhibisha wote. Kila Mtume katika zama zake, alikuwa mtu mwaminifu, msema kweli na mwenye heshima, na watu walikuwa wakimjua mja huyo mteule kwa sifa hizo. Lakini hulka na tabia ya uasi, inadi na ukaidi waliyokuwa nayo watu ilikuwa sababu ya kuyakataa maneno ya haki ya Mitume wao na badala yake kuendelea na raha na starehe zao na kufikiria jinsi ya kulinda manufaa na maslahi yao binafsi. Mitume walikuwa wakizungumza na watu wao kwa kutumia mbinu ya uulizaji na lugha ya upole, upendo na ya udugu na wakiwauliza: kwa nini hamumuonei haya Muumba wenu na kuacha mambo maovu? Lakini watu hao hawakuwa tayari kusikiliza mawaidha na nasaha hizo na kuamua kujitenga na Mitume wao ambao walikuwa wakiwahurumia na kuwaonea uchungu wao. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba Mitume wote wa Allah walikuwa na lengo moja; na kumkadhibisha yeyote miongoni mwao ni sawa na kuwakanusha na kuwakadhibisha wote. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa tabia na akhlaqi za Mitume kwa watu wa zama zao hazikuwa za kujikweza bali walikuwa wakijitangaza na kujitambulisha kuwa ni ndugu kwa watu wao na si mabwana na wakubwa wao. Wa aidha aya hizi zinatufunza kwamba inatakiwa kutumia mbinu ya uulizaji ili kuamsha dhamiri zilizolala na kughafilika za nafsi za watu, na si mbinu ya uamrishaji. Kadhalika aya hizi zinatuelimisha kuwa Mitume walikuwa watu wenye rekodi safi na wenye kutajwa kwa wema na watu wa zama zao; lakini pamoja na yote hayo akthari ya watu hawakuwa tayari kuwaamini na kuifuata haki waliyowalingania.
Tunaihatimisha darsa yetu hii kwa aya za 108 na 109 ambazo zinasema:


فَاتَّقُوا اللَّهَ وَأَطِيعُونِ


Basi Mcheni Mwenyezi Mungu, na nit'iini mimi.


وَمَا أَسْأَلُكُمْ عَلَيْهِ مِنْ أَجْرٍ إِنْ أَجْرِيَ إِلاَّ عَلَى رَبِّ الْعَالَمِينَ


Na sikutakini juu yake ujira, kwani ujira wangu hauko ila kwa Mola Mlezi wa walimwengu wote.


Katika aya hizi tulizosoma limetajwa na kukaririwa tena suala la taqwa na kumcha Allah SW. Kwa sababu mtu huyaendea madhambi pale anapomsahau Mwenyezi Mungu ambaye ametuneemesha kwa neema na fadhila zake zisizohesabika. Kwa hivyo ni kama kwamba Nabii Nuh (AS) anakusudia kuwaambia watu wa kaumu yake kwamba: vipi mnamwasi Mwenyezi Mungu ilhali mnakula riziki yake asubuhi na jioni na mko hai na mnaishi kwa irada na kutaka kwake Yeye Mola? Kisha baada ya kuwaeleza hayo akawaonyesha njia ya kujiweka mbali na madhambi na kuifikia haki na kuwaambia: mimi nimetumwa na Mwenyezi Mungu ili kuja kukuelekezeni katika njia ya uongofu; kwa hivyo kama mtayasikiliza maneno yangu hilo ni kwa faida yenu wenyewe. Kwa sababu mimi sifaidiki kwa vyovyote kutokana na amali zenu; mimi sitafuti umaarufu, jaha, mali wala utajiri na wala sikuombeni nyinyi chochote. Ikiwa nitatekeleza wajibu wangu sawasawa Allah SW ndiye atakayenipa malipo yangu na kunifanya nisiwe mhitaji kwa mwengine yeyote yule. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba katika kuwaelimisha na kuwaaidhi watu baadhi ya mambo kama taqwa na kumkumbuka Mwenyezi Mungu yanapasa yausiwe na kukaririwa kila mara ili wasije wakaghafilika na kupotoka. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa wafanya tablighi ya dini na wale wanaowalingania watu kushikamana na mafundisho ya dini, hawatakiwi kuwa na matarajio ya kupata malipo ya kimaada kwa watu, bali wafanye kazi yao hiyo kwa ikhlasi na kwa ajili ya Allah na kutawakali kwake Yeye Mola. Ni katika hali hiyo ndipo maneno yao yatakuwa na taathira zaidi ndani ya nyoyo za watu. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 651 ya Qur'ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah aijaze taqwa ndani ya nyoyo zetu na atuwafikishe kuzifanya kwa ikhlasi amali na matendo yetu. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh.../

 

 

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)