Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Alkhamisi, 12 Februari 2015 15:26

Sura ya Ash-Shua’raa, aya ya 90-101 (Darsa ya 650)

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu. Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur'ani. Hii ni darsa ya 650 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 26 ya Ash-Shua'raa.Tunaianza darsa yetu kwa aya za 90, 91, 92 na 93 ambazo zinasema:


وَأُزْلِفَتِ الْجَنَّةُ لِلْمُتَّقِينَ


Na Pepo itasogezwa kwa wachamngu.


وَبُرِّزَتِ الْجَحِيمُ لِلْغَاوِينَ


Na Jahannamu itadhihirishwa kwa wapotovu.


وَقِيلَ لَهُمْ أَيْنَ مَا كُنتُمْ تَعْبُدُونَ


Na wataambiwa: Wako wapi mlio kuwa mkiwaabudu


مِن دُونِ اللَّهِ هَلْ يَنصُرُونَكُمْ أَوْ يَنتَصِرُونَ


Badala ya Mwenyezi Mungu? Je! Wanakusaidieni, au wanajisaidia wenyewe?


Aya hizi, ambazo baada ya aya zilizotangulia zilizozungumzia maisha ya Nabii Ibrahim, ima zinaendelea kununkuu maneno ya Mtume huyo au maneno ya Allah SW kwa kuzungumzia Pepo na Moto. Kwanza zinayapambanua makundi mawili ya watu wa peponi na motoni, kwa moja kuwa la watu wachamungu na jengine la wapotovu, ili kubainisha na kuonyesha kwamba kinachomuelekeza mtu peponi ni taqwa na uchamungu, na kinachowafanya watu wa motoni wafikwe na adhabu ni kufuata kwao dhalala na upotofu. Wakati watu wa motoni watakapobaini kwamba vile walivyokuwa wakiviabudu duniani havina uwezo wa kuwasaidia na kuwaokoa na adhabu ya moto watasononeka na kuungulika mno. Siku hiyo watafahamu kwamba wao walikuwa kwenye dhalala na upotofu lakini walikuwa wakiwadhani waumini kuwa ndio waliopotoka. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba Pepo na Moto vitamdhihirikia mtu wakati faili la amali zake litakuwa limeshafungwa na hakutokuwa na chochote atakachoweza kukifanya. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa cheo na hadhi ya muumini mwenye kumcha Mola wake ni ya juu, kwa kiasi ambacho Pepo huandaliwa na kuwekwa tayari kwa ajili yake. Kadhalika aya hizi zinatutaka tutafakari, kwamba masanamu au watu, ambao hawana uwezo wa kujilinda hata nafsi zao wenyewe, vipi wataweza kuwa walinzi na watetezi kwetu sisi Siku ya Kiyama.
Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya za 94, 95, 96, 97 na 98 ambazo zinasema:


فَكُبْكِبُوا فِيهَا هُمْ وَالْغَاوُونَ


Basi watavurumizwa humo wao na hao wapotovu,


وَجُنُودُ إِبْلِيسَ أَجْمَعُونَ


Na majeshi ya Ibilisi yote.


قَالُوا وَهُمْ فِيهَا يَخْتَصِمُونَ


Watasema, na hali ya kuwa wanazozana humo:


تَاللَّهِ إِن كُنَّا لَفِي ضَلالٍ مُّبِينٍ


Wallahi! Kwa yakini tulikuwa katika upotovu ulio dhaahiri,


إِذْ نُسَوِّيكُم بِرَبِّ الْعَالَمِينَ


Tulipo kufanyeni ni sawa na Mola Mlezi wa walimwengu wote.


Kama ilivyoelezwa katika aya nyengine za Qur'ani, Siku ya Kiyama Allah SW atayahudhurisha masanamu yaliyokuwa yakiabudiwa ili waabudu masanamu hayo na washirikina waweze kuona wao wenyewe kwamba vile walivyokuwa wakivitukuza, wakivipa heshima, wakiviabudu na hata kuviwekea nadhiri hapa duniani, siku hiyo havitakuwa na uwezo wa kufanya lolote. Wakati masanamu yatakapovurumizwa motoni kwa amri ya Mwenyezi Mungu Azza wa Jalla hayatokuwa na uwezo wa kujiokoa, seuze kuwa na uwezo wa kuwasaidia waliokuwa wakiyanyenyekea na kuyaabudu. Lakini mbali na masanamu na waabudu masanamu hayo, shetani na jeshi lake pia watavurumizwa motoni, ambapo makundi yote hayo yatakuwa yakigombana na kutuhumiana wao kwa wao. Kinyume na anga ya upendo, huba na urafiki itakayotawala peponi, chuki, hasama na uadui ndivyo vitakavyotawala huko motoni. Ni hali ya kuchukiana watu wa motoni wao kwa wao, hisia za majuto kwa waliyoyatanguliza huko nyuma hapa duniani na kukiri kuwa walikuwa wamepotoka na kufuata njia ya batili. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba usuhuba na urafiki ambao ulianzishwa hapa duniani baina ya watu kwa msingi wa kufanya madhambi na mambo ya upotofu utakuwa sababu ya kugombana na kuchukiana watu hao Siku ya Kiyama. Watu wa motoni watahasimiana na kugombana wao kwa wao. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa dhamiri ya nafsi ya mtu itazinduka na kuamka Siku ya Kiyama na kumlaumu sana mtu mwenyewe, lakini lawama hizo na majuto atakayopata mtu hayatokuwa na faida ghairi ya kujisikitikia mtu nafsi yake.
Tunaihatimisha darsa yetu hii kwa aya za 99, 100 na 101 za sura hii ya Ash-Shua'raa ambazo zinasema:


وَمَا أَضَلَّنَا إِلاَّ الْمُجْرِمُونَ


Na hawakutupoteza ila wale waovu.


فَمَا لَنَا مِن شَافِعِينَ


Basi hatuna waombezi.


وَلا صَدِيقٍ حَمِيمٍ


Wala rafiki wa dhati.


Kile ambacho mwishowe washirikina na waabudu masanamu watasema ni kwamba sababu ya sisi kupotoka ni watu waovu waliotuvuta sisi katika njia hii na kutufanya tuhasirike na kuharibikiwa. Ni watu ambao waliutumia vibaya utajiri na mamlaka yao, wakatufanya na sisi tuwafuate, tukidhani kwamba njia waifatayo wao itatufikisha sisi pia kwenye saada. Lakini leo tumefahamu kuwa tulifuata upotofu. Kwa sababu hakuna mtu wa kutushufaia na kutuombea, wala rafiki wa kutusaidia. Si masanamu na tulivyokuwa tukiviabudu vinaweza kutuombea, na si katika waumini ambako tunaye rafiki wa dhati anayeweza kutufanyia jambo la kuwa sababu ya sisi kuokoka. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba Siku ya Kiyama kila mtu atamtupia mwenzake mzigo wa lawama. Washirikina na wale waliofuata upotovu watawashtaki viongozi wao waliowaongoza katika njia ya upotofu. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa Siku ya Kiyama itakuwepo shufaa na uombezi, lakini hautowajumuisha washirikina. Bwana Mtume SAW na Maimamu (AS) maasumu watawaombea waumini tu ambao watastahili kushufaiwa. Wa aidha tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba Siku ya Kiyama pia mtu atahitajia rafiki mzuri. Hivyo tufanye urafiki na watu ambao watakuwa washirika na wasaidizi kwetu hapa duniani na huko akhera pia; na marafiki kama hao hawapatikani ila katika watu waumini. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 650 ya Qur'ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah atujaalie kuwa miongoni mwa wale watakaoshufaiwa na Bwana Mtume, Maimamu maasumu na waja wateule wa Allah. Atujaalie pia kuwa na marafiki watakaokuwa sababu ya kufuzu na kufaulu hapa duniani na huko akhera. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh.../

 

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)