Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Alkhamisi, 12 Februari 2015 15:19

Sura ya Ash-Shua’raa, aya ya 83-89 (Darsa ya 649)

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu. Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur'ani. Hii ni darsa ya 649 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 26 ya Ash-Shua'raa. Tunaianza darsa yetu hii kwa aya ya 83 na 84 ambazo zinasema:


رَبِّ هَبْ لِي حُكْمًا وَأَلْحِقْنِي بِالصَّالِحِينَ


Mola wangu Mlezi! Nitunukie hukumu na uniunganishe na watu wema.


وَاجْعَل لِّي لِسَانَ صِدْقٍ فِي الآخِرِينَ


Na unijaalie nitajwe kwa wema na watu watakao kuja baadaye.


Katika darsa iliyopita tuliona jinsi Nabii Ibrahim (AS) alivyofanya mlinganisho kati ya Mola wake wa haki na miungu bandia ya washirikina waabudu masanamu wa zama zake ili kuwaonyesha kuwa masanamu hayana chochote yanayoweza kufanya, na kwamba mambo yote yako kwenye mamlaka ya Allah SW. Katika aya hizi tulizosoma na zitakazofuatia Nabii Ibrahim anamwomba Mwenyezi Mungu Mtukufu maombi kadhaa akitanguliza neno "Rabbi" yaani Mola Mlezi, ambalo lenyewe linadhihirisha mawasiliano ya karibu yaliyopo baina ya mja na Mola wake. Nabii huyo anaonyesha na kueleza kuwa Yeye Allah SW si Mungu tu wa walimwengu na viumbe wote, bali pia yu karibu nami kwa kiasi kwamba mimi namwona Yeye kuwa ndiye Mungu wangu na kuweza kuzungumza naye kama hivi. Ee Mola wangu Mlezi! ndivyo asemavyo Nabii Ibrahim na kumwomba Mwenyezi Mungu mambo kadhaa. Moja ni hekima, ambayo ni utambuzi wa hakika ya mambo kwa njia ya elimu na maarifa, vikiambatana na mantiki imara na yenye hoja. Jengine ni kumjaalia awe pamoja na waja wema katika kufanya mambo mema. Mtume huyo, ambaye ni mwenye elimu na maarifa ya mambo na wa mbele katika ufanyaji mambo mema, angali anamwomba Mwenyezi Mungu aendelee kumpa auni na msaada wake katika mambo mawili hayo ya kifikra na kimatendo ili asije akateleza, na pia aweze kufikia daraja aali na za juu za elimu na amali. Ombi la tatu la Nabii Ibrahim kwa Allah ni kutaka kuendelezwa fikra na harakati yake baada yake. Kwa hakika Nabii Ibrahim anamwomba Mola ajaalie njia yake na mafundisho yake ya tauhidi na kumwepekesha Yeye Allah yasisahaulike kwa kuondoka kwake; na jina lake lisifutike katika kumbukumbu. Na anamwomba pia Allah amfanye kuwa ruwaza na kigezo cha kidini kwa watu wa baada yake, kwa jina lake kutajwa kwa wema na njia yake kuendelezwa na watakaomfuatia. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba tumwombe msaada Allah katika mambo yote hususan katika kufikia kwenye ukamilifu wa kielimu na kimaanawi. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa elimu na hekima ni hidaya ya Allah inayotolewa kwa nyoyo safi na zenye utayarifu wa kupokea hidaya hiyo. Wa aidha aya hizi zinatuelimisha kwamba uono, mtazamo na fikra sahihi ndio utangulizi wa kutamka maneno na kutenda matendo ya sawa. Kadhalika tunajielimisha kutokana na aya hizi kuwa kujaaliwa kuwa na hekima na kuwa pamoja na waja wema ni daraja ya juu kabisa ya saada.
Zifuatazo sasa ni aya za 85 na 86 ambazo zinasema:


وَاجْعَلْنِي مِن وَرَثَةِ جَنَّةِ النَّعِيمِ


Na unijaalie katika warithi wa Pepo iliyojaa neema.


وَاغْفِرْ لِأَبِي إِنَّهُ كَانَ مِنَ الضَّالِّينَ


Na umghufirie baba yangu, kwani hakika alikuwa miongoni mwa wapotovu.


Dua ya nne iliyoombwa na Nabii Ibrahim ilihusu ulimwengu wa baada ya kifo. Sisi sote tunatakiwa sambamba na kufanya jitihada kwa ajili ya masuala ya kidunia tufikirie pia kuhusu akhera yetu na kuifanyia idili na juhudi maalumu; na wakati huohuo tumwombe Allah aamiliane nasi kwa upole, kwa uraufu na kwa fadhila zake na kutuingiza kwenye Pepo yake yenye neema zisizohesabika. Kama ambavyo baba huwaachia urithi wanawe konde iliyojaa na kusheheni miti ya matunda, ambapo watoto hao hunufaika na kuneemeka na matunda ya miti hiyo pasina kuyahangaikia wala kuyatokea jasho, Mwenyezi Mungu Mtukufu pia amewaandalia waja wake Pepo isiyoweza kutasawirika wala kuelezeka, ambayo si kitu cha kuweza kupatikana kwa kutegemea amali zetu hafifu tuzifanyazo. Lakini kutokana na fadhila zake, Allah SW atawafanya waja wake wema warithi wa Pepo hiyo.
Dua nyengine ya Nabii Ibrahim (AS) ilikuwa ni ya kumwombea maghufira mlezi wake ambaye alikuwa miongoni mwa washirikina; na Mtume huyo wa Allah alikuwa na matumaini kwamba angemwamini na kuikubali dini ya haki. Kwa sababu hiyo akampa ahadi kwamba atamwombea maghufira kwa Mwenyezi Mungu. Nabii Ibrahim akatekeleza ahadi yake aliyotoa na akafanya hivyo, lakini mlezi wake hakuiamini dini ya haki ya Tauhidi, na kwa hivyo mwishowe Nabii Ibrahim akajibari na kujiweka mbali naye. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba neema zisizohesabika na za milele za peponi ni atiya kubwa mno na adhimu mno kulinganisha na amali zetu chache tunazozifanya; atiya na hidaya ambayo watarithishwa waja wema wa Mwenyezi Mungu. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa kuwaombea dua ya maghufira jamaa na watu wa karibu ni katika sira ya Manabii wa Allah.
Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 649 inahatimishwa na aya za 87, 88 na 89 ambazo zinasema:


وَلا تُخْزِنِي يَوْمَ يُبْعَثُونَ


Na wala usinihizi Siku watapo fufuliwa (wote).


يَوْمَ لا يَنفَعُ مَالٌ وَلا بَنُونَ


Siku ambayo haitafaa mali wala wana.


إِلاَّ مَنْ أَتَى اللَّهَ بِقَلْبٍ سَلِيمٍ


Isipokuwa mwenye kumjia Mwenyezi Mungu na moyo safi.


Dua ya mwisho aliyoomba Nabii Ibrahim inadhihirisha uhisivu wa kuwa na mas-ulia aliokuwa nao juu ya majukumu aliyopewa na Mola Mwenyezi. Majukumu mazito ambayo taksiri na uzembe wowote ufanywao katika utekelezaji wake huwa sababu ya kuaibika na kufedheheka mja Siku ya Kiyama; aibu na fedheha ambayo hakuna kitu wala mtu yeyote anayeweza kuiondoa na kufidia. Ikiwa hapa duniani inayumkinika kufidia kosa la uhalifu kwa mali, pesa na kulipa faini au kukwepa kuingia hatiani kwa kutoa hongo na rushwa, Siku ya Kiyama mtu hatoweza kumiliki pesa na mali za kumwezesha kufanya hivyo; na kama zitakuwepo basi hazitoweza kumfaa katika siku hiyo nzito. Ikiwa hapa duniani wototo huweza kuwasaidia wazazi wao, na kuwa wasaidizi wao katika kazi na shughuli zao, mahusiano yao ya kifamilia yatakatika Siku ya Kiyama na kila mtu atafikiria nafsi yake na kulilia hali yake. Hata mama, ambaye ni dhihirisho la huruma, huba na mapenzi atawasahau wanawe na kufikiria nafsi yake mwenyewe tu. Rasilimali pekee ya mtu siku hiyo ni moyo na amali; amali ambazo tab'an ni zile alizozifanya mtu kwa ajili ya Mwenyezi Mungu na zilizotokana na moyo ulio safi. Yule ambaye moyo wake utakuwa umechafuka kwa shirki, ukafiri na ria, amali zake alizofanya hapa duniani hazitomfikia huko akhera, bali jaza na malipo yake atayapata papa hapa duniani. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba mwanadamu asijikatie na kujiwekea dhamana kwa nafsi yake na amali azifanyazo, bali muda wote awe na hofu juu ya taksiri na kasoro alizonazo katika kutekeleza wajibu wake; na amwombe Mola amuauni na kumnusuru asije akafedheheka Siku ya Kiyama. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa aibu, hizaya na fedheha ya akhera ni moja ya hali ngumu kabisa za Siku ya Kiyama, kwa sababu watu siku hiyo watabainikiwa na kudhihirikiwa na aibu zetu. Ni kama ambavyo aya ya 87 inavyomnukuu Nabii Ibrahim akieleza kwamba moja ya mambo mazito ya Siku ya Kiyama ni kunusurika na fedheha na hizaya. Aidha aya hizi zinatuelimisha kuwa vitu vya kimaada na kidunia kama mali na watoto, na cheo na hadhi havitomfaa wala kumwokoa mtu huko akhera. Wa aidha aya hizi zinatutaka tuelewe kwamba amali njema inayokubaliwa ni ile inayotokana na moyo safi uliotakasika na shirki na uchafu mwengineo wa kiroho. Kwa haya machache wapenzi wasikilizaji tunaifunga darsa yetu hii. Tunamwomba Allah atughufirie madhambi yetu, atutakabalie dua zetu na aufanye mwema mwisho wetu. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh.../

 

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)