Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumatano, 28 Januari 2015 10:09

Sura ya Ash-Shua’raa, aya ya 78-82 (Darsa ya 648)

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu. Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur'ani. Hii ni darsa ya 648 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 26 ya Ash-Shua'raa. Tunaianza darsa yetu hii kwa aya ya 78, 79 na 80 ambazo zinasema:


الَّذِي خَلَقَنِي فَهُوَ يَهْدِينِ


Ambaye ameniumba, na Yeye ndiye anayeniongoa,


وَالَّذِي هُوَ يُطْعِمُنِي وَيَسْقِينِ


Na ambaye ndiye anayenilisha na kuninywesha.


وَإِذَا مَرِضْتُ فَهُوَ يَشْفِينِ


Na ninapo ugua ni Yeye ndiye anaye niponesha.


Katika darsa iliyopita tulisimulia mazungumzo yaliyojiri kati ya Nabii Ibrahim (AS) na waabudu masanamu wa kaumu yake. Katika mazungumzo hayo, Mtume huyo wa Allah alitumia mbinu ya mantiki kuonyesha kuwa masanamu wanayoyaabudu watu wake hayana nafasi yoyote katika maisha ya wanadamu; lakini jibu pekee walilotoa watu hao kukabiliana na hoja za Nabii Ibrahim lilikuwa ni kwamba wanachofanya wao ni kuqalidi na kufuata yale yaliyokuwa yakifanywa na wazee na wakubwa wao waliowatangulia. Katika darsa yetu ya leo tunaendelea kusikia hoja za Nabii Ibrahim (AS) kwa waabudu masanamu ambaye aliwaambia: miungu yenu nyinyi ndio hiyo tuliyoiona; lakini Mungu wangu mimi ni yule aliyeniumba na kuniongoza. Yeye amenipa mimi akili na uwezo wa kufikiri ili niweze kupambanua kati ya njia sahihi na isiyo sahihi ya kufuata. Yeye ameniwezesha mimi kujua jema na baya ili niweze kufuata njia sahihi ya uongofu. Na si kwamba amenionyesha njia tu ya uongofu, bali ni Yeye ndiye anayenikidhia mahitajio yangu ya kimaada pia. Ni yeye Allah ndiye anayeniruzuku kila nilacho na kila ninachokinywa. Ameniwekea pia njia na nyenzo za tiba na kunifunza jinsi ya kuzitumia ili nipate ahueni na uzima pale nisibiwapo na maradhi. Kwa hivyo hali yangu ya huko nyuma, ya sasa na ya usoni, kiwiliwili changu na roho yangu na uzima wangu na kuumwa kwangu, yote hayo yako kwenye mamlaka Yake. Yeye haniachi mkono mimi katika hali yoyote ile, bali hunikidhia mahitaji yangu hata bila ya mimi mwenyewe kujua. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba baada ya neema ya kuumbwa, uongofu ndiyo neema ya pili kubwa kabisa ya Allah kwa wanadamu. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa dawa ni njia na wenzo wa tiba; lakini athari yake katika kumponya na kumuondolea maradhi mgonjwa inatokana na Mwenyezi Mungu. Yeye Mola ambaye ni Ash Shaafii, yaani Mponyaji, ameviumba viwiliwili vyetu kwa namna ambayo vinaweza kujikinga na maradhi na pia kukifanya kipate uzima tena kiungo kinachoathiriwa na ugonjwa. Ni Yeye pia aliyeiumba dawa pamoja na elimu na njia za kutengezea dawa hiyo kutokana na akili aliyompa mwanadamu. Kwa hiyo kila kitu kinatokana na Yeye Allah.
Aya za 81 na 82 ndizo zinazotuhitimishia darsa yetu hii. Aya hizo zinasema:


وَالَّذِي يُمِيتُنِي ثُمَّ يُحْيِينِ


Na ambaye atanifisha, na kisha atanihuisha.


وَالَّذِي أَطْمَعُ أَن يَغْفِرَ لِي خَطِيئَتِي يَوْمَ الدِّينِ


Na ambaye ndiye ninaye mtumai kunighufiria makosa yangu Siku ya Malipo.


Katika aya zilizotangulia Nabii Ibrahim aliashiria nafasi ya Allah SW katika maisha ya mwanadamu katika dunia hii; na katika aya hizi anazungumzia mamlaka ya Mola katika ulimwengu wa baada ya kifo ili kuwafahamisha waabudu masanamu kwamba uhai wangu na kufa kwangu; na aidha dunia yangu hii na ulimwengu wangu ule wa akhera, yote hayo yako kwenye mamlaka yake Yeye Mola. Kama ambavyo hapo kabla mimi sikuwepo, na Yeye Allah akanileta hapa duniani, ni Yeye pia ndiye atakayeichukua roho yangu na kuiondoa katika dunia hii. Hata hivyo hatima yangu haitoishia hapo, bali Allah SW atanipa uhai tena katika ulimwengu mwengine na kunilipa thawabu kwa mema niliyofanya na adhabu kwa mabaya niliyotenda hapa duniani. Mungu wangu mimi ni Mungu mwenye huruma. Si katika dunia hii tu anatoa neema zake kwa waja wake, lakini huko akhera pia atawarehemu kwa rehma zake; nami nina matumaini kwamba atanisamehe kwa uraufu, rehma na fadhila zake kwa kila taksiri, kasoro na makosa niliyofanya hapa duniani. Wapenzi wasikilizaji, tunavyoamini sisi Waislamu, Mitume ni waja waliohifadhika na kufanya madhambi; na katu hawaasi amri za Mwenyezi Mungu Mtukufu. Lakini wao wenyewe hujihisi ni waja wenye taksiri na makosa mbele ya Allah; na kwa hivyo humwomba Mola awasamehe kwa kuhisi wana ila na dosari katika kutekeleza jukumu zito walilopewa la kufikisha wito na risala ya Allah. Kwa maneno mengine, nia na makusudio yao ni kuwaelimisha na kuwafikisha watu kwenye uongofu. Lakini katika utekelezaji, takwa hilo huwa haliwezi kuthibiti kirahisi kutokana na vikwazo na vizuizi vingi vinavyojitokeza. Kwa hali hiyo Mitume huhofu kwamba labda kuna taksiri ambayo imetokana na wao, katika uchukuaji hatua za kuondoa vikwazo na vizuizi hivyo ili kuweza kuufikisha wito wa Allah kwa watu. Kwa sababu hiyo wanamwomba Mola awasamehe ikiwa kuna kasoro, upungufu na taksiri yoyote ile iliyotokea. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba katika mtazamo wa dini juu ya ulimwengu mauti sio mwisho wa mwanadamu bali ni mwanzo wa maisha mengine ya kiumbe huyo. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa tusitegemee na kujiaminisha kwa amali zetu njema. Kwani hakuna mtu yeyote asiyehitajia rehma na msamaha wa Allah SW. Hata Mitume pia wanatarajia rehma na maghufira ya Mola na si kutegemea na kujiaminisha kwa amali zao njema na za kheri walizofanya. Aidha aya hizi zinatuonyesha kwamba, kuwa na matumaini ya kupata maghufira na msamaha wa Allah ndio mwenendo wa Mitume na Manabii. Wa aidha aya hizi zinatutaka tuelewe kwamba mahitaji ya kimaada na kimaanawi ya mwandamu, kuanzia mwanzo hadi mwisho wa maisha yake yanadhaminiwa na kukidhiwa na Mwenyezi Mungu SW. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 648 ya Qur'ani imefikia tamati. Tunamwomba Mola atusamehe madhambi yetu, atutakabalie amali zetu na aufanye mwema mwisho wetu. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh.../

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)