Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumatano, 28 Januari 2015 10:00

Sura ya Ash-Shua’raa, aya ya 69-77 (Darsa ya 647)

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu. Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur'ani. Hii ni darsa ya 647, na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 26 ya Ash-Shua'raa. Tunaianza darsa yetu kwa aya za 69, 70 na 71 ambazo zinasema:


وَاتْلُ عَلَيْهِمْ نَبَأَ إِبْرَاهِيمَ


Na wasomee khabari za Ibrahim.


إِذْ قَالَ لِأَبِيهِ وَقَوْمِهِ مَا تَعْبُدُونَ


Alipo mwambia baba yake na kaumu yake: Mnaabudu nini?


قَالُوا نَعْبُدُ أَصْنَامًا فَنَظَلُّ لَهَا عَاكِفِينَ


Wakasema: Tunaabudu masanamu, nasi tutaendelea kuyanyenyekea.


Katika darsa iliyopita tulikamilisha kuzungumzia sehemu moja ya kisa cha maisha ya Nabii Musa (AS) kama kilivyosimuliwa katika sura hii ya Ash-Shua'raa. Kuanzia aya tulizosoma kinasimuliwa kisa cha maisha ya Nabii Ibrahim, ambaye baada ya Nabii Musa, ndiye Mtume ambaye jina lake limetajwa mara nyingi zaidi ndani ya Qur'ani tukufu. Kama ilivyoelezwa katika vitabu vya historia pamoja na Taurati iliyopo hivi sasa jina la baba yake Nabii Ibrahim ni Tarakh, na mtu aliyetajwa katika aya tulizosoma kwamba ni baba yake, kwa hakika hakuwa baba yake halisi bali alikuwa mkuu na mlezi wake ambaye jina lake lilikuwa ni Azara. Tab'an katika utamaduni wa mataifa mengi duniani imezoeleka kwamba wakubwa wa kielimu na wa masuala ya kimaanawi hupewa lakabu ya baba, ambapo Wakristo wanamwita mkubwa wao wa kidini Papa yenye maana ya baba. Washirikina na waabudu masanamu wa Makka walikuwa wakimjua Nabii Ibrahim, na hata amali ya Hija waliyokuwa wakiitekeleza kila mwaka wakiitaja kuwa ni ukumbusho ulioachwa na Mtume huyo. Na ni kwa sababu hiyo Mwenyezi Mungu Mtukufu anamwambia Bwana Mtume Muhammad SAW kwamba: wasomee watu hawa habari za maisha ya Nabii Ibrahim na uwakumbushe kwamba tangu mwanzo wa maisha yake alikuwa akipambana na shirki ya kuabudu masanamu. Japokuwa alikuwa ndio kwanza kijana chipukizi lakini ili kuwazindua na kuwatoa kwenye usingizi wa mghafala jamaa zake na watu wake wa karibu, mja huyo mteule wa Allah aliibua masuali kadhaa ili kuwafanya watu wake watumie akili zao kutafakari na kuliweka kwenye mizani ya akili zao na kulipima suala hili, kwamba je kuabudu masanamu ni jambo la sawa au la? Japokuwa yeye alikuwa akijua wanachokiabudu lakini alitaka wao wenyewe walikiri jambo hilo ili iwe njia ya kuwatupia maswali mengine juu ya suala hilo. Ni kawaida ya kila mtu kutetea jambo analolifanya na kuonyesha kuwa ni sahihi na lenye kuingia akilini. Walipojibu swali la Nabii Ibrahim kwamba ni nini wanachokiabudu, waabudu masanamu wa kaumu ya Mtume huyo nao pia walijibu waziwazi kuwa: sisi sio tu tunayaabudu masanamu bali pia tunayatukuza na tunayahitajia kwa muda wetu wote.
Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba tutalii na kusoma historia ya waliotutangulia hususan shakhsia wakubwa ili kupata funzo kutokana na yale yaliyojiri katika maisha yao na kuwafanya wao kigezo na mfano wa kufuata katika maisha yetu ya leo. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa badala ya kutumia njia ya mkato kupambana na upotofu wa kifikra na kiitikadi, tutumie mbinu ya maswali na majibu ili kuwafanya watu watafakari na kuweza wao wenyewe kulifikia jibu mwafaka. Wa aidha aya hizi zinatuelimisha kwamba badala ya kufuata kibubusa na bila ya hoja mila, itikadi na desturi zilizozoeleka kwa jamaa na watu wetu wa karibu au mambo yaliyoenea katika jamii, tukae na kutafakari sisi wenyewe na kuchagua njia sahihi ya kufuata. Kadhalika aya hizi zinatuelimisha kuwa katika kupambana na dhalala na upotofu tusiwe na hofu kwa sababu ya uchache wetu wa kiidadi, kwani Nabii Ibrahim alisimama peke yake kupambana na waabudu masanamu.
Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya 72, 73 na 74 ambazo zinasema:


قَالَ هَلْ يَسْمَعُونَكُمْ إِذْ تَدْعُونَ


Akasema: Je! Yanakusikieni mnapo yaita?


أَوْ يَنفَعُونَكُمْ أَوْ يَضُرُّونَ


Au yanakufaeni, au yanakudhuruni?


قَالُوا بَلْ وَجَدْنَا آبَاءَنَا كَذَلِكَ يَفْعَلُونَ


Wakasema: Bali tumewakuta baba zetu wakifanya hivyo hivyo.


Kwa kuwa Nabii Ibrahim (AS) alitaka waabudu masanamu wafahamu wao wenyewe kwamba wanayoyafanya ni mambo ya upuuzi na yasiyo na faida, aliendelea kujadiliana nao kwa kuwatupia maswali mengine, ambayo kwa kawaida humpitikia kila mtu, nayo ni kwamba, hayo masanamu mnayoyaabudu yanasikia mnayoyaambia, au yanaelewa shida na mahitaji yenu ili kuweza kukukidhieni? Na au je masanamu haya yanao uwezo kweli wa kukunufaisheni au kukudhuruni nyinyi kwa namna yoyote? Kama si hivyo mnayatukuza, mnayasujudia na au kuyachinjia na kuyafanyia makafara kwa jambo gani? Ajabu ni kwamba majibu ya watu wake kwa maswali yote hayo yalikuwa ni kuungama ukweli. Kwani walikuwa wakijua kwamba masanamu yao hayakuwa na uwezo wa kufanya lolote lenye athari kwao wao. Lakini hoja pekee waliyotoa kuwa sababu ya wao kuabudu masanamu ilikuwa ni kufuata wazee wao waliowatangulia. Waliwafuata watu wao hao kutokana na taasubu na ukereketwa wa kikaumu tu. Yaani kama kwamba wazee wao waliotangulia walikuwa wakamilifu wa akili, ambao walijua kila kitu pasina kukosea katika jambo lolote. Hali ya kuwa kufuata kibubusa mila, ada na desturi za waliotangulia, baadhi ya wakati huwazuia watu kutumia akili zao kwa njia sahihi na kuwafanya wawe na fikra yabisi na mgando na hivyo kulemaa na kubaki nyuma. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba tunayepaswa kumwabudu ni yule mwenye uelewa wa hali zetu na awezaye kukidhi mahitaji yetu. Na huyo si mwengine ila ni Allah SW. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa katika zama zote za historia ujinga na ujahili kwa upande mmoja, na ufuataji mambo kibubusa na bila ya kutumia akili kwa upande mwengine vimesababisha upotofu wa kifikra na kimatendo katika jamii za wanadamu.
Wapenzi wasikilizaji, darsa yetu ya leo inahatimishwa na aya za 75, 76 na 77 ambazo zinasema:


قَالَ أَفَرَأَيْتُم مَّا كُنتُمْ تَعْبُدُونَ


Akasema je! Mmewaona hawa mnao waabudu


أَنتُمْ وَآبَاؤُكُمُ الأَقْدَمُونَ


Nyinyi na baba zenu wa zamani?


فَإِنَّهُمْ عَدُوٌّ لِّي إِلاَّ رَبَّ الْعَالَمِينَ


Hakika hao ni maaadui zangu, isipo kuwa Mola Mlezi wa walimwengu wote.


Baada ya mazungumzo na majadiliano ya kimantiki aliyofanya na waabudu masanamu, mwishowe Nabii Ibrahim (AS) aliwaambia watu wa kaumu yake kuwa: kwa hiyo mmeona sasa kwamba nyinyi na baba zenu mmekuwa mukikiabudu kitu ambacho hakiwezi kukufanyieni lolote na wala hakichangii chochote katika maisha yenu ya duniani. Lakini mimi ninamwabudu Mola wa walimwengu na ninachukia kumwabudu asiyekuwa Yeye, kwa sababu kumwabudu yeyote na chochote kile ghairi yake Yeye Allah kutakuwa sababu ya kuharibikiwa, na hakutoniletea kitu kingine mimi isipokuwa hasara na madhara. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba imani na itikadi juu ya Muumba na Mola wa ulimwengu inapasa itokane na fikra na akili na si kwa kudhani na kukalidi. Kiujumla ni kwamba kukalidi na kufuata vivi hivi tu katika usuli na misingi ya itikadi ni jambo linalokatazwa na lisilokubalika. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa kufanywa mijadala na midahalo kati ya wafuasi wa fikra na itikadi mbalimbali kwa madhumuni ya kubainisha hakika na ukweli wa mambo ni jambo lenye udharura. Kujadiliana na watu kwa kuchunga misingi ya mantiki na ya akhlaqi ni katika njia na taratibu zilizokuwa zikitumiwa na Mitume. Wa aidha tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba miungu na maabudu bandia na wa kubuni ni maadui wa saada na ukamilifu wa kiutu wa mwanadamu. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 647 ya Qur'ani imefikia tamati. Tunamwomba Mola atuonyeshe haki na kutupa taufiqi ya kuifuata na atuonyeshe batili na kutuwezesha kuiepuka. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh.../

 

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)