Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumatano, 28 Januari 2015 09:49

Sura ya Ash-Shua’raa, aya ya 63-68 (Darsa ya 646)

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu. Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur'ani. Hii ni darsa ya 646, na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 26 ya Ash-Shua'raa. Tunaianza darsa yetu hii kwa aya ya 63 hadi 66 ambazo zinasema:


فَأَوْحَيْنَا إِلَى مُوسَى أَنِ اضْرِب بِّعَصَاكَ الْبَحْرَ فَانفَلَقَ فَكَانَ كُلُّ فِرْقٍ كَالطَّوْدِ الْعَظِيمِ


Tukampelekea wahyi Musa tukamwambia: Piga bahari kwa fimbo yako. Basi ikatengana, na kila sehemu ikawa kama mlima mkubwa.


وَأَزْلَفْنَا ثَمَّ الآخَرِينَ


Na tukawajongeza hapo wale wengine.


وَأَنجَيْنَا مُوسَى وَمَن مَّعَهُ أَجْمَعِينَ


Na tukamwokoa Musa na walio kuwa pamoja naye wote.


ثُمَّ أَغْرَقْنَا الآخَرِينَ


Kisha tukawazamisha hao wengine.


Katika darsa iliyopita tulisema kuwa Firauni, akiwa ameandamana na jeshi lake kubwa lililojizatiti kwa silaha na zana chungu nzima za kivita alimfuata Nabii Musa (AS) pamoja na wafuasi wake. Wakati walipofika kwenye ukingo wa Mto Nile, Nabii Musa na wafuasi wake walijikuta wamezingirwa na jeshi la taghuti huyo. Mbele yao yaliwakabili mawimbi makubwa ya maji, na nyuma yao kulikuwa na jeshi lililojizatiti kwa silaha. Wafuasi wa Musa (AS) waliingiwa na hofu na wasiwasi mkubwa kiasi cha kuvunjika moyo na kukata tamaa baada ya kuhisi hakuna njia tena ya kuokoka na kujitoa kwenye makucha ya Mafirauni. Lakini Nabii Musa (AS) ambaye alikuwa ametawakali na kumtegemea Allah, yeye alijua kwamba ahadi ya Mola ya kuokoka Bani Israil ni ya uhakika na isiyo na shaka. Hivyo aliwatuliza na kuwapa moyo watu wake kwa kuwaambia:"Wao hawatoweza kutushinda katu. Yeye Mola aliyeniamuru mimi nikuchukueni na kukuondoeni Misri atatuonyesha njia ya kutokea." Baada ya kujiri hayo, katika aya hizi tulizosoma Mwenyezi Mungu SW anamwambia Mtume wake Musa (AS): Ile fimbo ambayo uliitupa mbele ya Firauni ikageuka joka kubwa, ipige sasa kwenye mto Nile wenye mawimbi makali uone jinsi zitakavyopasuka na kujitokeza njia mbalimbali ndani ya maji, na mawimbi ya maji hayo kupandana moja juu ya jengine na kufanyika mlima mkubwa." Nabii Musa alifanya kama alivyoamriwa akaipiga fimbo yake baharini. Tahamaki ghafla bahari ikapasuka na mawimbi yakaanza kurundikana kwa kasi, na baina yao zikajitokeza njia kadhaa. Kwa amri ya Nabii Musa, Bani Israil waliingia ndani ya Mto Nile na kuvuka salama usalimini kupitia njia hizo zilizojitokeza. Katika lahadha hiyo, japokuwa Firauni na watu wake waliuona waziwazi na kwa macho yao muujiza huo lakini hawakuwa tayari kuacha kiburi na ghururi waliyokuwa nayo, hivyo wakaamua kumwandama Nabii Musa na wafuasi wake. Walijitosa ndani ya Mto Nile pasina kutambua kwamba dakika za mwisho za uhai wao zinakaribia ukingoni. Mara baada ya mtu wa mwisho katika wafuasi wa Musa (AS) kutoa mguu wake nje ya njia ya Mto Nile, kwa amri ya Allah SW maji ya mto huo yakarejea kwa mara nyengine tena kwenye hali ile ile ya mwanzo ambapo dhoruba ya mawimbi makubwa ya maji ilimsomba Firauni na jeshi lake, na huo ukawa ndio mwisho wa Mafirauni waliokuwa wamejawa na ghururi, kiburi na majivuno. Firauni, ambaye alidai na kujitangazia uungu huku akijitapa na kujivuna kwa nguvu za mamlaka na utajiri wa mali, hakuwa amewaza wala kufikiria kamwe kama iko siku atakuja kutingwa namna hiyo ndani ya Mto Nile na kugharikishwa na kuzamishwa kwenye maji ya mto huo yeye na jeshi lake lote. Kwa hakika Firauni alijionea kwa macho yake wakati fimbo ya Nabii Musa ilipogeuka nyoka. Lakini kama wakati ule hakuweza kufahamu kwamba aliyofanya Musa (AS) yalikuwa tofauti kabisa na yanayofanywa na wachawi, sasa alishuhudia mwenyewe jinsi njia kavu za kupita zilivyojitokeza katikati ya mawimbi makubwa ya Mto Nile; kwa nini hakuweza kutambua ukweli wa Utume wa Nabii Musa? Kama hakuwa na nia asilani ya kumwamini Musa (AS) basi baada ya kuona miujiza kama hiyo angalau angeghairi kuendelea na safari ya kumwandama Mtume huyo wa Allah na wafuasi wake na kuwaacha kama walivyo badala ya kuhatarisha maisha yake na ya watu wa jeshi lake. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba kwa irada ya Allah SW, maumbile na sababu za kimaumbile kama maji na udongo hutiishwa na kuwa chini ya mamlaka ya waja wake maalumu Mola Mwenyezi. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa irada ya Allah inashinda juu ya vitu vyote. Kwa irada yake Mola kuna siku fimbo hugeuka nyoka, na kuna siku huwa sababu ya bahari kukauka na kufunguka njia kwa ajili ya waumini. Tab'an kama inavyoashiria aya ya 60 ya Suratul Baqarah kuna siku pia fimbo huwa sababu ya kuchimbuka chemchemi za maji ardhini. Wa aidha aya hizi zinatuelimisha kwamba ikiwa Mwenyezi Mungu mwenyewe ataona ni jambo lenye maslaha atawaokoa watu wanaoinusuru dini yake hata wanapokuwa kwenye hali ngumu kabisa ya mkwamo.
Tunaihatimisha darsa yetu hii kwa aya za 67 na 68 ambazo zinasema:


إِنَّ فِي ذَلِكَ لآيَةً وَمَا كَانَ أَكْثَرُهُم مُّؤْمِنِينَ


Hakika bila ya shaka katika hayo ipo Ishara; lakini wengi wao si wenye kuamini.


وَإِنَّ رَبَّكَ لَهُوَ الْعَزِيزُ الرَّحِيمُ


Na kwa hakika Mola wako Mlezi ndiye Mwenye nguvu Mwenye kurehemu.


Katika sehemu ya mwisho ya kisa cha Nabii Musa (AS) na Firauni katika sura hii ya Ash-Shua'raa Mwenyezi Mungu Mtukufu anamhutubu Bwana Mtume SAW na Waislamu kwamba: Katika kadhia ya kughariki Firauni na jeshi lake kwenye Mto Nile kuna ibra na mafunzo mengi kwa watawala madhalimu na pia kwa madhulumu wanaokandamizwa. Watawala madhalimu wanatakiwa wapate funzo kwamba ikiwa Allah SW ataamua, basi mataji na viti vyao vya enzi vitaporomoka ndani ya kutwa moja tu na hakuna jeshi lolote litakaloweza kuwaokoa. Na amma watu wanaodhulumiwa, wao pia wanapata funzo muhimu kwamba ikiwa watasimama chini ya uongozi wa mmoja wa viongozi wa dini kwa lengo la kujikomboa na kujitoa kwenye makucha ya madhalimu basi Mwenyezi Mungu atawaokoa kwa kuwapa auni na msaada wake. Hii ni kaida na utaratibu wa Allah SW kwa waja wake. Hata hivyo licha ya kuwepo ishara na ibra zote hizi akthari ya watu hawakuwa tayari kuitafuta hakika na haki na kuiamini, pamoja na kwamba katika kadhia hii Mwenyezi Mungu Azza wa Jalla amedhihirisha waziwazi qudra na nguvu zake mutlaki kwa madhalimu na fadhila na rehma zake makhsusi kwa waumini na wafuasi wa Nabii Musa (AS). Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba kama nia ya mtu ni kutaka kuitambua haki basi ajue kuwa ishara na athari za Allah katika ulimwengu wa maumbile ziko wadhiha na wazi kabisa kumtosheleza na kumfikisha kwenye yakini. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa kaida na utaratibu wa Allah katika zama zote za historia ni kuipa auni na nusra haki na kuifuta na kuiangamiza batili. Wa aidha tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba Allah anaelezea tarikh na historia ya waliotangulia ili kumliwaza Bwana Mtume na waumini na kuwapa somo la subira na istiqama. Kwa haya machache wapenzi wasikilizaji tunaifunga darsa yetu hii. Tunamwomba Allah atujaalie kuwa miongoni mwa wanaoaidhika na kupata ibra na mafunzo kutokana na historia za waliotutangulia. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh.../

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)