Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Alkhamisi, 15 Januari 2015 16:25

Sura ya Ash-Shua’raa, aya ya 53-62 (Darsa ya 645)

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu. Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur'ani. Hii ni darsa ya 645, na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 26 ya Ash-Shua'raa. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 53 hadi 56 ambazo zinasema:


فَأَرْسَلَ فِرْعَوْنُ فِي الْمَدَائِنِ حَاشِرِينَ


Basi Firauni akawatuma mijini wakusanyaji.


إِنَّ هَؤُلاء لَشِرْذِمَةٌ قَلِيلُونَ


(Wakieneza): Hakika hawa ni kikundi kidogo.


وَإِنَّهُمْ لَنَا لَغَائِظُونَ


Nao wanatuudhi.


وَإِنَّا لَجَمِيعٌ حَاذِرُونَ


Na sisi sote tuko tayari kwa mapambano.


Katika darsa iliyopita tulisema kuwa Nabii Musa alitakiwa na Allah SW aondoke na Bani Israil Misri na kuelekea nao Sham; hivyo akawapa taarifa ya uamuzi huo watu wa kaumu yake ya Bani Israil waliokuwa wametawanyika huku na kule katika ardhi hiyo ya Misri. Nao Bani Israil wakafanya kila njia kuhakikisha wanafika mjini ili kwa uongozi wa Musa (AS) wajiunge na msafara wa safari hiyo ya kuwakomboa na utumwa na madhila ya taghuti Firauni. Firauni, ambaye alipata habari kuhusu mpango huo aliwaamuru wafanyakazi wake waelekee kila pembe ya Misri, ili mbali na kukusanya kikosi cha kukabiliana na harakati ya Nabii Musa wafanye propaganda pia na kutangaza kwamba Musa na wafuasi wake ni kikundi cha watu dhaifu na wachache hata aweze kukabiliana na Firauni na jeshi lake. Kwa kueneza propaganda hizo walitaka kuwatisha na kuwatia hofu Bani Israil kwamba kama watafanya uasi wataangamia, na pia walitaka kuwahamasisha na kuwatia moyo askari wao kwamba karibuni hivi tutaweka kila kitu sawa kwa kummaliza Musa na wafuasi wake. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba siku zote mataghuti hufanya propaganda za uwongo za kukuza nguvu na suhula walizonazo na kuonyesha kuwa uwezo wa wapinzani wao si lolote si chochote ili kuzuia kuenea wimbi la harakati za wapinzani hao. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa tawala za kidhalimu na za kitaghuti hutumia gharama kubwa kutafuta mapenzi na uungaji mkono wa watu; lakini pamoja na yote hayo chuki na uadui wa watu dhidi yao huzidi kuwa mkubwa siku baada ya siku.
Zifuatazo sasa ni aya za 57, 58 na 59 ambazo zinasema:


فَأَخْرَجْنَاهُم مِّن جَنَّاتٍ وَعُيُونٍ


Basi tukawatoa katika mabustani na chemchem,


وَكُنُوزٍ وَمَقَامٍ كَرِيمٍ


Na makhazina, na vyeo vya hishima,


كَذَلِكَ وَأَوْرَثْنَاهَا بَنِي إِسْرَائِيلَ


Ndio hivyo! Na tukawarithisha hayo Wana wa Israili.


Aya hizi wapenzi wasikilizaji zinasimulia matokeo ya makabiliano kati ya Firauni na jeshi lake na Nabii Musa (AS) na wafuasi wake, makabiliano ambayo hatima yake ilikuwa ni kushindwa Mafirauni na kurithishwa Bani Israil mataji na makasri yao ya ufalme pamoja na konde, mabustani, mali na utajiri usiokadirika waliokuwa nao katika ardhi ya Misri. Awali lengo la Nabii Musa (AS) halikuwa jengine ghairi ya kuikomboa Bani Israil. Lakini Allah SW akajaalia harakati hiyo ihitimike kwa kuanguka watawala wa Misri katika hali ya upeo wa udunifu na udhalilifu; na wale waliokuwa watumwa kushika hatamu za madaraka na utawala, na kumiliki mali na milki zote za kina Firauni. Jambo hilo halikuwa limempitikia katu akilini mwake Nabii Musa mwenyewe wala wafuasi wake seuze kutaka kuchukua hatua kivitendo za kulifanikisha. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba dhulma na uonevu ndio chanzo kikuu cha kuporomoka na kutoweka kwa tawala. Kwa maneno mengine, tawala za kidhalimu hazina mustakabali na wala hazidumu. Kadhalika tunajielimisha kutokana na aya hizi kuwa mojawapo ya kaida na utaratibu wa Allah ni kuyatawalisha matabaka ya wanyonge katika jamii mahala pa watawala wanaojivuna na kutakabari. Wa aidha aya hizi zinatutaka tuelewe kuwa hata kama nguvu za madaraka na utajiri wa mali vitakuwa vikubwa na vingi kiasi gani, lakini kama havitotumiwa kwa njia sahihi na ya sawa vitakuwa balaa na nakama kwa maisha ya wenye mamlaka, mali na utajiri, badala ya kuwa vitu vya neema, raha na starehe kwao.
Aya ya 60, 61 na 62 ndizo zinazotuhatimishia darsa yetu hii. Aya hizo zinasema:


فَأَتْبَعُوهُم مُّشْرِقِينَ


Basi wakawafuata lilipo chomoza jua.


فَلَمَّا تَرَاءى الْجَمْعَانِ قَالَ أَصْحَابُ مُوسَى إِنَّا لَمُدْرَكُونَ


Na yalipo onana makundi mawili, watu wa Musa wakasema: Hakika sisi bila ya shaka tumepatikana!


قَالَ كَلاَّ إِنَّ مَعِيَ رَبِّي سَيَهْدِينِ


(Musa) akasema: Hapana! Hakika Mola wangu Mlezi yuko pamoja nami. Yeye ataniongoza!


Kama alivyokuwa ameamriwa na Allah SW, Nabii Musa aliwachukua Bani Israil na kuondoka nao wakati wa usiku kuelekea upande wa Mto Nile. Kulipopambazuka, Firauni naye pamoja na jeshi lake kubwa aliloliandaa walianza safari ya kuwaandama. Na kutokana na kwamba walikuwa wamepanda farasi wa kivita wenye mwendo wa kasi waliweza kuwafikia haraka sana. Kwa vile Nabii Musa na wafuasi wake hawakuwa na kitu chochote cha kutumia kwa ajili ya kujihami au farasi na nyumbu wa kupanda ili kuweza kukimbia walijiona wameshazingirwa na jeshi la adui na hawakuwa na uwezo wa kufanya kitu chochote. Katika lahadha hiyo na mazingira hayo, Bani Israil walimwendea Musa (AS), na huku wakimwona yeye kuwa ndiye aliyewasababishia hayo walimwambia:" Sasa tumeshanaswa na kuingia mikononi mwa Mafirauni. Na wewe ndiye uliyetuleta hapa; hivi hukufikiria kwamba tutakuja fikwa na hali hii?" Nabii Musa ambaye alichukua hatua hiyo kwa amri ya Mwenyezi Mungu, huku akiwa na yakini na imani kamili ya ahadi ya Mola wake aliwaelekea watu wake na kwa utulivu kabisa akawaambia:" Msiwe na dhana kama hiyo; Yeye Mola aliyeniamuru mimi kufanya hivi, hatotuacha mkono sisi hapa, na karibuni hivi atatuonyesha njia na kutuelekeza nini cha kufanya. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba ikiwa tutatekeleza amri ya Mwenyezi Mungu, basi pale tutakapokuwa kwenye dhiki na mkwamo, Yeye Mola atatufungulia njia na kutuondolea dhiki na mkwamo huo. Hivyo basi tusikate tamaa hata chembe bali daima tutawakali na kumtegemea Yeye Allah. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa ikiwa tutakuwa na imani ya kweli kwa ahadi ya Mwenyezi Mungu hatutohamanika wala kukata tamaa; bali muda wote tutakuwa na matumaini ya kupata fadhila na rehma zake Mola na kuwafanya wengine pia wawe na imani na utulivu wa nyoyo. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 645 imefikia tamati. Tunamwomba Allah azijaze nyoyo zetu imani ya kweli tuwe daima tunatawakali na kumtegemea Yeye tu na si yeyote yule mwenginewe. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh.../

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)