Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Alkhamisi, 15 Januari 2015 15:50

Sura ya Ash-Shua’raa, aya ya 49-52 (Darsa ya 644)

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu. Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur'ani. Hii ni darsa ya 644, na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 26 ya Ash-Shua'raa. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 49 ambayo inasema:


قَالَ آمَنتُمْ لَهُ قَبْلَ أَنْ آذَنَ لَكُمْ إِنَّهُ لَكَبِيرُكُمُ الَّذِي عَلَّمَكُمُ السِّحْرَ فَلَسَوْفَ تَعْلَمُونَ لأُقَطِّعَنَّ أَيْدِيَكُمْ وَأَرْجُلَكُم مِّنْ خِلافٍ وَلَأُصَلِّبَنَّكُمْ أَجْمَعِينَ


(Firauni) akasema: Je! Mmemuamini kabla sijakuruhusuni? Bila ya shaka yeye basi ndiye mkubwa wenu aliye kufunzeni uchawi. Basi punde mtajua! Nitakata mikono yenu na miguu yenu kwa kutafautisha, kisha nitakusulubuni nyote.


Katika darsa iliyopita tulisema kuwa wakati wachawi walipoona miujiza ya Nabii Musa walibaini kwamba aliyoyafanya Mtume huyo hayakuwa sawa na mizungu waifanyayo wao ya uchawi na mazingaombwe, bali ni muujiza hasa. Kwa hivyo wote kwa pamoja walimwamini na wakatangaza mbele ya hadhara ya watu uamuzi wao huo wa kumwamini Allah SW, Mola wa Manabii Musa na Harun (AS). Firauni, ambaye lengo lake la kuwakusanya wachawi lilikuwa ni kutaka kumshinda na kumfedhehesha Nabii Musa, aliwaona wachawi hao hao sasa wanamfedhehesha yeye mwenyewe mbele za watu. Na iliyumkinika lahadha yoyote baada ya hapo, watu wengine pia wangemwamini Nabii Musa na kuacha kumtukuza na kumwabudu yeye Firauni. Kwa hivyo taghuti huyo, kwanza akaelekeza tuhuma kwa wachawi kwa kuwaambia:"nyinyi ni wanafunzi wa Musa; na kwa pamoja mmekula njama dhidi yangu; na kisha akatoa vitisho vikali dhidi yao kwa kutangaza kwamba atawatundika na kuwakata mikono na miguu ya upande tofauti ili wafe kwa mateso na machungu, na hilo kuwa funzo kwa wengine kwamba asije mtu mwengine yoyote yule akathubutu kumwamini na kumfuata Musa (AS). Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba katika tawala za kitaghuti watu huwa hawana uhuru wa kuamini. Katika tawala hizo watawala madhalimu hutumia kila mbinu na njia kudhibiti fikra za watu katika jamii. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa maisha na roho za watu huwa hazina thamani yoyote mbele ya watawala majabari na madhalimu. Kwa hiyo mtu yeyote anayechukua hatua kinyume na maslahi yao, damu yake huwa halali kumwagwa.
Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya 50 na 51 ambazo zinasema:


قَالُوا لا ضَيْرَ إِنَّا إِلَى رَبِّنَا مُنقَلِبُونَ


Wakasema: Haidhuru, hakika sisi ni wenye kurejea kwa Mola wetu Mlezi.


إِنَّا نَطْمَعُ أَن يَغْفِرَ لَنَا رَبُّنَا خَطَايَانَا أَن كُنَّا أَوَّلَ الْمُؤْمِنِينَ


Hakika sisi tunatumai Mola wetu Mlezi atatughufiria makosa yetu, kwa kuwa ndio wa kwanza kuamini.


Wachawi waliomwamini Nabii Musa (AS) sio tu hawakutishika na vitisho vikali vya Firauni wala kutetereka katika imani zao, bali nyoyo zao zilikuwa thabiti kwa nuru ya imani, na bila hofu wala kiwewe walimkabili taghuti huyo na kumwambia:"Unatutisha kuwa tutateswa na kuuliwa? Kwani hujui kama sisi tunakupokea kwa mikono miwili kuuawa katika njia ya Mwenyezi Mungu; kwa sababu tunatumai kwamba hilo litakuwa sababu ya sisi kusamehewa makosa yetu ya huko nyuma na tunataraji kupata fadhila na rehma makhsusi za Mola wetu, kwa kuwa watu wa mwanzo kumwamini Musa. Kwa hivyo hilo wewe unaloliona kuwa ni kitisho dhidi yetu, sisi tunalichukulia kuwa ni fakhari na bishara njema kwetu. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba imani inayotokana na elimu na maarifa huwa haiyumbi wala haitetereki kwa vitisho na mashinikizo ya nje, bali vitisho na mashinikizo hayo humzidishia mtu ushujaa na istiqama. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa lililo muhimu zaidi katika jambo ni hatima, na si mwanzo wake. Wachawi, ambao umri wao wote waliutumia katika dhalala na upotofu, wakati walipoona muujiza wa Nabii Musa (AS) walimwamini na kuwa na hatima na mwisho mwema. Na kinyume chake, si hasha Muislamu aliyetumia umri wake wote katika hali ya Uswalihina wa kusali na kufunga, mwisho wake ukawa ni kuondoka duniani akiwa kafiri bila chembe ya imani ndani ya moyo wake.
Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 644 ya Qur'ani inahatimishwa na aya ya 52 ambayo inasema:


وَأَوْحَيْنَا إِلَى مُوسَى أَنْ أَسْرِ بِعِبَادِي إِنَّكُم مُّتَّبَعُونَ


Na tulimpelekea wahyi Musa, kwamba: Nenda na waja wangu wakati wa usiku. Kwa hakika mtafuatwa.


Baada ya tukio la kushindwa Firauni na Nabii Musa (AS), taghuti huyo aliamua sasa kumwaandama mtume huyo wa Allah na watu waliomwamini na kuzuia kuenea kwa watu wengine fikra na mafundisho yake. Kwa upande mwengine Allah SW alimteremshia wahyi Mtume wake kwamba ili kukomboka na madhila ya Firauni, si yeye mwenyewe na ndugu yake tu Harun, bali aondoke pamoja nao katika ardhi ya Misri watu wote wa Bani Israil wanaoishi hapo kama watumwa, na kuwarejesha kwenye ardhi yao ya asili ya Sham. Bani Israil, ambao walishuhudia kwa macho yao ushindi wa Nabii Musa dhidi ya Firauni na wakapata yakini juu ya uwezo wa mtume huyo wa Allah, waliuitikia wito wake, na kila mmoja akafanya kila njia kuhakikisha anafika mjini ili kwa uongozi wa Musa (AS) ajiunge na msafara wa safari ya kukomboka na utumwa na madhila ya Firauni. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba wakati tunapoishi katika jamii chafu na ovu, kama tunao uwezo, basi tubakie ndani ya jamii hiyo na kupambana na dhulma na maovu; la kama hatuwezi basi angalau tuhame na kuhajiri kuelekea mahala pengine ili tusije tukamezwa na mazingira machafu na maovu ya jamii hiyo. Kadhalika tunajielimisha kutokana na aya hii kuwa kuwakomboa watu na madhila na unyongeshaji wa madhalimu ilikuwa moja ya ratiba za Mitume iliyokuwa ikitekelezwa kwa mwongozo wa Mwenyezi Mungu SW. Kwa haya machache wapenzi wasikilizaji tunaifunga darsa yetu hii. Tunamwomba Allah aupe nusra na ushindi Uislamu na Waislamu katika kupambana na mafirauni wa zama hizi. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh.../

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)