Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumatatu, 26 Mei 2014 13:44

Sura ya An Nur, aya ya 62-64 (Darsa ya 619)

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu. Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa darsa ya Qur'ani. Hii ni darsa ya 619 ambapo leo tutahatimisha tarjumi na maelezo ya sura ya 24 ya An Nur. Tunaianza darsa yetu hii kwa aya ya 62 ambayo inasema:

إِنَّمَا الْمُؤْمِنُونَ الَّذِينَ آمَنُوا بِاللَّهِ وَرَسُولِهِ وَإِذَا كَانُوا مَعَهُ عَلَى أَمْرٍ جَامِعٍ لَمْ يَذْهَبُوا حَتَّى يَسْتَأْذِنُوهُ إِنَّ الَّذِينَ يَسْتَأْذِنُونَكَ أُوْلَئِكَ الَّذِينَ يُؤْمِنُونَ بِاللَّهِ وَرَسُولِهِ فَإِذَا اسْتَأْذَنُوكَ لِبَعْضِ شَأْنِهِمْ فَأْذَن لِّمَن شِئْتَ مِنْهُمْ وَاسْتَغْفِرْ لَهُمُ اللَّهَ إِنَّ اللَّهَ غَفُورٌ رَّحِيمٌ

Hakika Waumini wa kweli ni wale waliomuamini Mwenyezi Mungu na Mtume wake; na wanapokuwa pamoja naye kwa jambo la kuwakhusu wote hawaondoki mpaka wamtake ruhusa. Kwa hakika wale wanaokuomba ruhusa, hao ndio wanaomuamini Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Na wakikuomba ruhusa kwa baadhi ya kazi zao, mruhusu umtakaye miongoni mwao na uwaombee maghufira kwa Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kughufiria, Mwenye kurehemmu.

Katika darsa iliyopita tulisoma aya zilizoelezea baadhi ya adabu za jinsi ya kulahilikiana na kusuhubiana Waislamu wao kwa wao. Aya hii inahusu jinsi Waislamu wanavyotakiwa wasuhubiane na Bwana Mtume Muhammad SAW na kueleza kwamba moja ya alama ya imani ya kweli juu ya Allah na utiifu wa kweli kwa mtume wake ni kwamba wakati nyinyi Waislamu mnapokuwa katika kazi muhimu za jamii ni kutofanya jambo lolote bila ya ruhusa na amri yake yeye Mtume; na kama mtakuwa katika ufanyaji kazi unaohitajia mahudhurio yenu kwa pamoja na mkawa pamoja na Mtume basi msiende popote bila ya ruhusa yake na wala msitengane na wenzenu. Bila ya shaka aya hii haihusiani na zama za Bwana Mtume tu, bali mtu yeyote atakayekuwa kiongozi wa haki wa jamii ya Kiislamu na akashika uongozi huo kwa ustahiki, inapasa waumini wamtii na wala watu wasichukue hatua yoyote katika masuala ya kijamii bila ya muongozo na maelekezo yake.

Ni wazi kwamba viongozi wa dini huwa wanachukua maamuzi kwa kuzingatia maslaha ya mtu binafsi na jamii kwa ujumla; na amri na idhini wanayotoa ni kwa msingi wa kutekeleza wajibu wa kidini na kufikisha risala ya Allah. Kwa hivyo huwa wanawaombea maghufira kwa Mola wale watu wanaoomba idhini kwao ili Yeye Allah awasamehe na kuwarehemu kutokana na taksiri na kasoro zinazotokana na matendo yao. Katika tafsiri za Qur'ani imeelezwa kuwa moja ya sababu za kuteremshwa aya hii ni kisa cha sahaba Handhalah ambaye katika usiku wa arusi yake, Bwana Mtume pamoja na masahaba wengine walikuwa wanatoka nje ya mji wa Madina kuelekea kwenye vita vya Uhud. Handhalah aliomba ruhusa kwa Mtukufu huyo ili usiku huo awahi kushiriki kwenye sherehe ya arusi yake kisha asubuhi mapema akaungane na Waislamu wenzake kuelekea kwenye vita vya Jihadi. Kwa hivyo usiku ule akaingia ndani lakini wakati wa kutoka asubuhi, akawa na haraka ya kukimbilia kwenye Jihadi kiasi kwamba hakuwahi kukoga josho la janaba. Akiwa katika hali hiyo alielekea eneo la Uhud na kuingia kwenye uwanja wa vita. Na hatimaye Handhalah akauawa shahidi katika medani ya Jihadi. Alipozungumzia hali ya sahaba wake huyo, Bwana Mtume SAW alisema:" Malaika wa mbinguni wamemkosha josho hilo na kumpeleka peponi". Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba katika mas-ulia na majukumu ya kijamii kuna ulazima wa kuchunga nidhamu za utaratibu uliowekwa ili kulinda mshikamano uliopo na kuweza kufikia lengo lililokusudiwa. Kuchunga nidhamu na taratibu hizo ni utekelezaji wa maamrisho ya dini na ni miongoni mwa alama za imani ya kweli. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa katika kazi za kijamii ambazo maamuzi yake yanapitishwa kwa msingi wa kushauriana na kufuata fikra ya pamoja, haitakiwi mtu kujiamulia mambo kivyake na kuzingatia mawazo yake binafsi tu. Kadhalika tunajielimisha kutokana na aya hii kwamba jamii ya Kiislamu inatakiwa daima iwe tiifu kwa amri ya kiongozi wa Kiislamu na kutoacha kutekeleza majukumu yake bila ya ruhusa na idhini yake. Wa aidha aya hii inawataka viongozi wa jamii ya Kiislamu wawe watu wanaozingatia uhalisia wa mambo na wanaobadilika kimantiki katika utekelezaji wa sera zao, na pia wawe wapole kwa watu na kuwakubalia nyudhuru zao.

Darsa ya 619 inahatimishwa na aya za 63 na 64 ambazo zinasema:

لا تَجْعَلُوا دُعَاء الرَّسُولِ بَيْنَكُمْ كَدُعَاء بَعْضِكُم بَعْضًا قَدْ يَعْلَمُ اللَّهُ الَّذِينَ يَتَسَلَّلُونَ مِنكُمْ لِوَاذًا فَلْيَحْذَرِ الَّذِينَ يُخَالِفُونَ عَنْ أَمْرِهِ أَن تُصِيبَهُمْ فِتْنَةٌ أَوْ يُصِيبَهُمْ عَذَابٌ أَلِيمٌ

Msifanye wito wa Mtume baina yenu kama wito wa nyinyi kwa nyinyi. Hakika Mwenyezi Mungu anawajua miongoni mwenu wanaoondoka kwa kificho. Basi na watahadhari wanaokhalifu amri yake, usije ukawapata msiba au ikawapata adhabu yenye kuumiza.

أَلا إِنَّ لِلَّهِ مَا فِي السَّمَاوَاتِ وَالأَرْضِ قَدْ يَعْلَمُ مَا أَنتُمْ عَلَيْهِ وَيَوْمَ يُرْجَعُونَ إِلَيْهِ فَيُنَبِّئُهُم بِمَا عَمِلُوا وَاللَّهُ بِكُلِّ شَيْءٍ عَلِيمٌ

Jueni kuwa hakika ni vya Mwenyezi Mungu vilivyomo mbinguni na ardhini. Hakika Yeye anajua mlionayo. Na siku mtakaporudishwa kwake atawaeleza waliyoyafanya. Na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa kila kitu.

Aya hizi zinaendelea na maudhui iliyozungumziwa katika aya iliyotangulia kuhusu kutoondoka Waislamu katika kazi wanayofanya bila ya ruhusa ya Bwana Mtume, na kueleza kwamba kila pale Mtume anapokuiteni kufanya jambo msitafute fursa na upenyo wa kujificha mbele ya macho yake na kuamua kuondoka taratibu na kukwepa kufanya hilo mlilopaswa kulitekeleza. Jueni kwamba kukhalifu amri ya Mtume na kukwepa kutekeleza amri zake kuna mwisho mbaya kwenu duniani na Akhera. Kwa upande wa duniani mtaandamwa na matatizo na masaibu kuanzia mtu binafsi na jamii pia na kufikwa na mitihani na mabalaa makubwa; na huko Akhera kuna adhabu kali inayokungojeni kutokana na kuasi amri ya Mtume.

Inakuwaje nyinyi Waislamu mnaichukulia amri ya Mtume kuwa ni sawa na amri za watu wengine na kuamua kuikhalifu na kukwepa kuitekeleza? Lakini kama mnaweza kwa hila zenu kujificha mbele ya macho ya Mtume, vipi mnadhani mtaweza kujificha na kumkwepa Mwenyezi Mungu jalla fii ulaah, aliyekizunguka na Mwenye kukiona kila kitu? Yeye Allah anayaona yote myatendayo muda wote na ni Mjuzi na Mwelewa wa hali zenu zote za dhahiri na za batini. Na sio nyinyi tu bali viumbe vingine na vitu vingine vyote katika ulimwengu wa maumbile viko chini ya udhibiti wake Yeye na hakuna chochote kifichikacho kwake. Yeye Allah SW, ambaye hivi sasa ni Mwenye kuyashuhudia na kuyaona matendo na amali zenu hapa duniani, Siku ya Kiyama ndiye atakayekuwa hakimu wenu ambapo atakuonyesheni madaftari ya amali zenu na kuainisha hatima ya kila mmoja wenu kulingana na yale mliyoyafanya.

Aya ya mwisho ya Suratun Nur inasisitiza mara tatu kuhusu elimu na ujuzi wa Allah SW juu ya amali na matendo ya mwanadamu ili mtu yeyote yule asije akadhani kwamba anaweza kufanya jambo lolote lile kwa kificho au ataweza kukimbilia mahali ambako elimu ya Mwenyezi Mungu Mtukufu haiwezi kupafikia. Ni wazi kwamba mtu ambaye anaamini kwa yakini kuwa ulimwengu wote ni hadhara yake Mola, na amali anazofanya mja muda wote ziko chini ya uangalizi wa Yeye Allah SW, imani hiyo itakuwa na taathira kubwa kwa mtu huyo ya kumfanya ajihadhari asifanye maasi mbele ya hadhara ya Mola wake. Hakuna shaka kwamba imani na itikadi hiyo ni kinga imara na ngao madhubuti ya kumlinda mtu na madhambi na upotofu. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba Bwana Mtume na mawalii wengine wa Allah ni watu watakatifu na wenye kuheshimika ambao heshima na utukufu wao unapasa kulindwa katika kila hali. Tuyataje majina yao kwa heshima, na wito wao tusiuchukulie kuwa sawa na wito wa mtu mwengine yoyote; hivyo tuuitikie kwa heshima na taadhima. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa kukhalifu amri ya Allah au wito wa Mtume kunamletea mtu matatizo na masaibu duniani na Akhera. Salama ya duniani na Akhera inapatikana kwa kutii maamrisho ya dini. Kadhalika aya hizi zinatuelimisha kwamba kuamini kuwa Mwenyezi Mungu Mtukufu ni mjuzi na mtambuzi wa yote anayoyafikiri na anayoyatenda mja, humzuia mtu kufanya mambo machafu na maovu. Wapenzi wasikilizaji darsa ya 619 imefikia tamati na kutuhitimishia pia tarjumi na maelezo ya sura ya 24 ya Annur. Inshaa Allah tuwe tumeelimika, tumeaidhika na kunufaika na yote tuliyojifunza katika sura hii, amin. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh.../

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)