Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumatatu, 26 Mei 2014 13:40

Sura ya An Nur, aya ya 58-61 (Darsa ya 618)

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu. Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa darsa ya Qur'ani. Hii ni darsa ya 618 na kwa sasa tunaizungumzia sura ya 24 ya An Nur. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 58 na 59 ambazo zinasema:

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لِيَسْتَأْذِنكُمُ الَّذِينَ مَلَكَتْ أَيْمَانُكُمْ وَالَّذِينَ لَمْ يَبْلُغُوا الْحُلُمَ مِنكُمْ ثَلاثَ مَرَّاتٍ مِن قَبْلِ صَلاةِ الْفَجْرِ وَحِينَ تَضَعُونَ ثِيَابَكُم مِّنَ الظَّهِيرَةِ وَمِن بَعْدِ صَلاةِ الْعِشَاء ثَلاثُ عَوْرَاتٍ لَّكُمْ لَيْسَ عَلَيْكُمْ وَلا عَلَيْهِمْ جُنَاحٌ بَعْدَهُنَّ طَوَّافُونَ عَلَيْكُم بَعْضُكُمْ عَلَى بَعْضٍ كَذَلِكَ يُبَيِّنُ اللَّهُ لَكُمُ الآيَاتِ وَاللَّهُ عَلِيمٌ حَكِيمٌ

Enyi mlioamini! Nawakutakeni idhini iliyowamiliki mikono yenu ya kulia na walio bado kubaalighi miongoni mwenu mara tatu - kabla ya Sala ya alfajiri, na wakati mnapovua nguo zenu adhuhuri, na baada ya Sala ya Isha. Hizi ni nyakati tatu za faragha kwenu. Si vibaya kwenu wala kwao baada ya nyakati hizi, kuzungukiana nyinyi kwa nyinyi. Hivyo ndivyo Mwenyezi Mungu anavyokuelezeni Aya zake, na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi Mwenye hikima.

وَإِذَا بَلَغَ الأَطْفَالُ مِنكُمُ الْحُلُمَ فَلْيَسْتَأْذِنُوا كَمَا اسْتَأْذَنَ الَّذِينَ مِن قَبْلِهِمْ كَذَلِكَ يُبَيِّنُ اللَّهُ لَكُمْ آيَاتِهِ وَاللَّهُ عَلِيمٌ حَكِيمٌ

Na watoto wanapofikilia umri wa kubaalighi basi nawatake ruhusa, kama walivyotaka ruhusa wa kabla yao. Hivyo ndivyo anavyokubainishieni Mwenyezi Mungu Aya zake, na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi Mwenye hikima.

Suratun Nur wapenzi wasikilizaji, ambayo ilianza kwa kutaja hukumu ya wanawake na wanaume wanaofanya uchafu wa zina, inaeleza katika aya hizi za karibu ya mwisho wa sura kuhusu hatua za kuchukuliwa ili kuepusha kutokea upotovu wa maingiliano ya kijinsia kwa watoto na kulinda heshima na staha ya familia kwa kusema: Wafanyakazi wa ndani ya nyumba pamoja na watoto, wakubwa na wadogo ambao kwa kawaida huingia na kutoka kila sehemu ya ndani ya nyumba, wanapaswa wachunge mipaka ya faragha ya baba na mama ndani ya nyumba na hivyo wasiwe wakiingia chumbani mwao bila ya ruhusa. Tab'an kwa kuwa watoto wadogo waliokuwa hawajafikia umri wa baleghe huwa na utegemezi zaidi kwa wazazi, na mara nyingi hupendelea kuwa pamoja nao aya hizi zinatilia mkazo maalum kuhusiana na wao kwa kusema: hata watoto hao wadogo pia wanatakiwa waombe ruhusa kwanza ya kuingia chumbani wakati wazazi wao wanapokuwa wamejipumzisha wakiwa katika hali ya faragha. Amri hii na mafunzo haya wanatakiwa wazazi wawape watoto wao tangu utotoni mwao na kuwalea kwa namna ya kuwafanya wajistahi na kuwa wasafi kimaadili. Kutokana na aya hizi tunajielimisha kuwa uhusiano wa mambo ya kunga baina ya mke na mume unatakiwa uwe wa namna itakayochunga heshima na staha kwa watoto na pia kulinda mipaka ya faragha ya wazazi. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa watoto wadogo wanatakiwa wajifunze majumbani na katika mazingira ya familia namna ya kuwa na staha na kuwa wasafi kimaadili. Kadhalika aya hizi zinatuelimisha kwamba mume anatakiwa atenge masaa kadhaa ya mchana na usiku kwa ajili ya mkewe tu, na watoto wanatakiwa wasiwaghasi na kuwasumbua wazazi wao katika nyakati hizo.

Ifuatayo sasa ni aya ya 60 ambayo inasema:

وَالْقَوَاعِدُ مِنَ النِّسَاء الَّلاتِي لا يَرْجُونَ نِكَاحًا فَلَيْسَ عَلَيْهِنَّ جُنَاحٌ أَن يَضَعْنَ ثِيَابَهُنَّ غَيْرَ مُتَبَرِّجَاتٍ بِزِينَةٍ وَأَن يَسْتَعْفِفْنَ خَيْرٌ لَّهُنَّ وَاللَّهُ سَمِيعٌ عَلِيمٌ

Na wanawake wazee wasiotaraji kuolewa, si vibaya kwao kupunguza nguo zao, bila ya kujishaua kwa mapambo. Na wakijihishimu ni bora kwao. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusikia, Mwenye kujua

Hukumu jumla kuhusu hijabu imebainishwa katika aya ya 31 ya sura hii. Aya hii ya 60 inawatoa katika hukumu hiyo wanawake wazee na kueleza kwamba wale wanawake ambao, kutokana na umri mkubwa walionao, hawana hamu tena ya kuolewa na pia hakuna mtu atakayekuwa na hamu ya kutaka kuwaoa, basi wao wanaruhusiwa kuondoa mabaibui na mitandio yao ya kichwa mbele ya wanaume wasio maharimu zao, na si lazima kufunika vichwa na shingo zao. Tab'an hii ni ikiwa hawajavaa mapambo kichwani na shingoni mwao, na wao wenyewe kama hawajajipamba na kujipodoa. Ni wazi kwamba wanawake waliofikia umri wa uzee huwa hawana tena mvuto wa kutamanisha, na kwa hivyo kuvua kwao hijabu hakuna madhara yoyote ya ufisadi wa kimaadili.  Tab'an ni wazi kwamba ikiwa wanawake wa aina hii pia wataamua kuchunga na kufuata sheria ya uvaaji hijabu inayohusu wanawake, na wakaamua kujisitiri kama wafanyavyo wanawake wengine, watakuwa wamejikurubisha zaidi kwenye hali ya staha na usafi wa maadili, na hilo ni jambo lenye kupendeza na lililo bora zaidi kwao. Aya hii inaonesha kwa uwazi kabisa kwamba falsafa na hekima kuu ya hijabu ni kulinda heshima, staha na murua wa wanawake; na bila ya shaka yoyote, kuchunga hijabu ni kwa manufaa ya wanawake wenyewe. Pamoja na hayo, vazi lenye maana ya hijabu kwa mtazamo wa Uislamu ni lile lisilochochea shahawa na kuamsha ghariza na matamanio ya kijinsia. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba sheria za Uislamu zina ulainifu na zinawiyana na udharura na uhalisia wa hali; na kwa hivyo huwa zinabadilika kulingana na mabadiliko ya hali za watu. Kama ambavyo aya hii tuliyosoma inawepesisha hijabu kwa wanawake wazee. Aidha aya hii inatuelimisha kuwa haijuzu kwa wanawake kujitokeza kwenye hadhara ya watu wasio maharimu zao wakiwa wamejipamba na kujipodoa nyuso zao.

Darsa ya 618 inahatimishwa na aya ya 61 ambayo inasema:

لَيْسَ عَلَى الأَعْمَى حَرَجٌ وَلا عَلَى الأَعْرَجِ حَرَجٌ وَلا عَلَى الْمَرِيضِ حَرَجٌ وَلا عَلَى أَنفُسِكُمْ أَن تَأْكُلُوا مِن بُيُوتِكُمْ أَوْ بُيُوتِ آبَائِكُمْ أَوْ بُيُوتِ أُمَّهَاتِكُمْ أَوْ بُيُوتِ إِخْوَانِكُمْ أَوْ بُيُوتِ أَخَوَاتِكُمْ أَوْ بُيُوتِ أَعْمَامِكُمْ أَوْ بُيُوتِ عَمَّاتِكُمْ أَوْ بُيُوتِ أَخْوَالِكُمْ أَوْ بُيُوتِ خَالاتِكُمْ أَوْ مَا مَلَكْتُم مَّفَاتِحَهُ أَوْ صَدِيقِكُمْ لَيْسَ عَلَيْكُمْ جُنَاحٌ أَن تَأْكُلُوا جَمِيعًا أَوْ أَشْتَاتًا فَإِذَا دَخَلْتُم بُيُوتًا فَسَلِّمُوا عَلَى أَنفُسِكُمْ تَحِيَّةً مِّنْ عِندِ اللَّهِ مُبَارَكَةً طَيِّبَةً كَذَلِكَ يُبَيِّنُ اللَّهُ لَكُمُ الآيَاتِ لَعَلَّكُمْ تَعْقِلُون

Si vibaya kwa kipofu, wala si vibaya kwa kiguru, wala si vibaya kwa mgonjwa, wala kwenu nyinyi, mkila katika nyumba zenu, au nyumba za baba zenu, au nyumba za mama zenu, au nyumba za kaka zenu, au nyumba za dada zenu, au nyumba za ami zenu, au nyumba za shangazi zenu, au nyumba za wajomba zenu, au nyumba za dada wa mama zenu, au za mliowashikia funguo zao, au rafiki yenu. Si vibaya kwenu mkila pamoja au mbali mbali. Na mkiingia katika nyumba, toleaneni salamu, ni maamkio yanayotoka kwa Mwenyezi Mungu, yenye baraka na mema. Hivyo ndivyo Mwenyezi Mungu anavyokubainishieni Aya zake mpate kuelewa.

Aya hii wapenzi wasikilizaji imegawika katika sehemu tatu. Sehemu ya kwanza inazungumzia wagonjwa wa kawaida pamoja na walemavu wa viungo kama vipofu na viguru na kueleza kwamba Mwenyezi Mungu Mtukufu amewaondolea dhima ya kufanya kila jambo lenye uzito na tabu watu wagonjwa na walemavu; na amewafanyia wepesi na tahfifu pia katika kutekeleza mambo ya wajibu kama Sala, Saumu, Hija na Jihadi. Kwa hivyo na nyinyi pia muwafikirie na kuwafanyia wepesi maalumu katika maisha ya kifamilia na kijamii. Kisha sehemu ya pili ya aya inazungumzia jamaa wa nasaba na kueleza kwamba hamuhitajii kuomba idhini ya kula na kunywa majumbani kwa wazazi wenu, dada na kaka zenu au shangazi, mama wadogo, ami au wajomba zenu; na ikiwa itatokea mkaweko majumbani kwao na wao wenyewe hawako, hamhitaji ruhusa ya kula kilichomo ndani ya nyumba zao; na Mwenyezi Mungu amekupeni haki hii ya kutumia vyakula vilivyomo majumbani humo kwa kiasi cha ada na desturi. Marafiki na jamaa pia ambao mna mazoea nao ya kuendeana, au wale ambao wamekukabidhini funguo za nyumba zao ili wakati watakapokuwa hawako muwe mkienda kukagua na kutupia jicho, nao pia wanaingia kwenye hukumu hii na kwa hivyo hamhitaji kupewa idhini na ruhusa ya kula vyakula vilivyowekwa ndani ya nyumba zao. Amma sehemu ya tatu ya aya inahusu amri jumla na kwa watu wote kuhusu adabu za kuingia ndani ya nyumba. Iwe ni nyumbani kwake mtu mwenyewe au nyumbani kwa watu; nayo ni kuwatolea salamu kwa ucheshi na uchangamfu wenye nyumba na waliomo humo. Kwa sababu Allah SW amekufanya kutoleana salamu kuwa ndio maamkizi baina ya Waislamu ambako ni kuombeana dua kwa ajili ya uzima na pia huwaepushia balaa waliomo kwenye nyumba. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba wananchi na viongozi wa dola ya Kiislamu wanapaswa kuwaondolea wagonjwa na walemavu kila kitu kinachowapa shida, tabu na uzito; iwe ni katika suala la matibabu na gharama zake, mazingira na hali yao ya ufanyaji kazi au iwe ni katika masuala ya maisha na suhula wanazohitajia. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa jamaa wa nasaba wana haki za baina ya pande mbili. Na moja kati ya hizo ni ya kuwa na ruhusa ya kutumia kwa kiwango cha ada vyakula vilivyomo majumbani mwao. Kadhalika aya hii inatuelimisha kwamba katika Uislamu haki ya marafiki imewekwa kwenye safu moja na ile ya jamaa zake mtu. Na aidha aya inatutaka tuelewe kuwa kuamkiana kwa "Assalamu Alaykum" ni adabu ya mbinguni na iliyobarikiwa, yenye kuleta kheri na baraka katika maisha. Kwa haya machache tunaifunga darsa yetu hii. Tunamwomba Allah atuondolee vinyongo nyoyoni mwetu, atuzidishie mapenzi baina yetu na aufanye mwema mwisho wetu. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh.../

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)