Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumatatu, 26 Mei 2014 12:52

Sura ya An Nur, aya ya 53-57 (Darsa ya 617)

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu. Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa darsa ya Qur'ani. Hii ni darsa ya 617 na kwa sasa tunaizungumzia sura ya 24 ya An Nur. Darsa yetu hii inafunguliwa na aya za 53 na 54 ambazo zinasema:

وَأَقْسَمُوا بِاللَّهِ جَهْدَ أَيْمَانِهِمْ لَئِنْ أَمَرْتَهُمْ لَيَخْرُجُنَّ قُل لّا تُقْسِمُوا طَاعَةٌ مَّعْرُوفَةٌ إِنَّ اللَّهَ خَبِيرٌ بِمَا تَعْمَلُونَ

Na wanaapa kwa Mwenyezi Mungu ukomo wa viapo vyao ya kwamba ukiwaamrisha, kwa yakini watatoka. Sema: Msiape! Ut'iifu unajulikana. Hakika Mwenyezi Mungu anazo khabari za mnayoyatenda.

قُلْ أَطِيعُوا اللَّهَ وَأَطِيعُوا الرَّسُولَ فَإِن تَوَلَّوْا فَإِنَّمَا عَلَيْهِ مَا حُمِّلَ وَعَلَيْكُم مَّا حُمِّلْتُمْ وَإِن تُطِيعُوهُ تَهْتَدُوا وَمَا عَلَى الرَّسُولِ إِلاَّ الْبَلاغُ الْمُبِينُ

Sema: Mt'iini Mwenyezi Mungu, na mt'iini Mtume. Na mkigeuka, basi yaliyo juu yake ni aliyobebeshwa, na yaliyo juu yenu ni mliyobebeshwa nyinyi. Na mkimt'ii yeye mtaongoka. Na hapana juu ya Mtume ila kufikisha (Ujumbe) wazi wazi.

Wanafiki ni watu ambao katika dhahiri yao wanajifanya kuwa ni waumini lakini katika batini yao hawana imani yoyote. Na katika mbinu zao wanazotumia ni kupenda sana kuapa na kula yamini. Kila pale wanapohisi kuwa jamii ya Waislamu imeshawatambua na inataka kuwatenga, huyatumia vibaya matukufu ya dini na viapo vikubwa vikubwa kutangaza kwamba sisi tuko tayari kujitolea mhanga roho zetu na mali zetu katika njia ya Mwenyezi Mungu na kutozembea wala kufanya ajizi katika kutekeleza amri ya Allah na Mtume wake. Hata hivyo tajiriba imeonyesha kuwa watu wanaotoa sha'ar za aina hii na kuzungumza kwa mori, jazba na hamasa, pale kweli inapodhihiri kwa kuwadia wakati wa vitendo hukwepa kujitokeza kwenye medani kwa kutumia visingizio mbalimbali ili kuzikimbia tabu na misukosuko. Mwenyezi Mungu Mtukufu anawajibu kuhusiana na mwenendo wao huo wa kindumakuwili kwa kuwaambia:"Hakuna ulazima wa kuapa, nyinyi onesheni katika matendo yenu kuwa ni wenye kutii amri, na mu wakweli katika madai yenu kwamba mumeamini. Msidhani kuwa mnaweza kuwahadaa na kuwadanganya watu na kujitangaza kuwa ni waumini kwa sababu mnayekabiliana naye ni Mwenyezi Mungu aliye mjuzi wa batini zenu; na hakuna chochote kinachoweza kufichika mbele yake. Kisha aya zinaendelea kwa kusisitiza kwamba kumtii Mtume au kuasi maamrisho yake, faida na madhara yake yanakurudiini nyinyi wenyewe na si yeye Mtume. Ikiwa mtamfuata yeye katika matendo, mtahidiwa na kuongozwa kwenye njia ya uongofu, na katika maisha yenu mtasalimika na kuwa mbali na dhalala na upotofu. Lakini kama mtayapa mgongo maamrisho yake, yeye Mtume hana jukumu wala dhima juu yenu, kwani yeye ameshatekeleza wajibu wake kwa kuwatangazia watu wote amri ya Allah kwa ufafanuzi na kwa uwazi kabisa, lakini nyinyi hamjatekeleza wajibu wenu ambao ni kuyakubali na kuyatekeleza mafundisho na maamrisho yake Mola. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba tusihadaiwe na viapo vikubwa vikubwa vya baadhi ya watu kwa sababu hiyo ni katika alama za watu wanafiki na si sifa ya watu waumini. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa Bwana Mtume alikuwa na jukumu la kufikisha hukumu za Allah na si kuwalazimisha na kuwashurutisha watu wazikubali. Aidha aya hizi zinatutaka tuelewe kwamba ni wajibu pia kufuata amri na makatazo ya Bwana Mtume sawa na tunavyotii hukumu na amri za Mwenyezi Mungu SW; na kumkhalifu yeye ni kukhalifu na kuasi hukumu yake Mola.

Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya 55 ambayo inasema:

وَعَدَ اللَّهُ الَّذِينَ آمَنُوا مِنكُمْ وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ لَيَسْتَخْلِفَنَّهُم فِي الأَرْضِ كَمَا اسْتَخْلَفَ الَّذِينَ مِن قَبْلِهِمْ وَلَيُمَكِّنَنَّ لَهُمْ دِينَهُمُ الَّذِي ارْتَضَى لَهُمْ وَلَيُبَدِّلَنَّهُم مِّن بَعْدِ خَوْفِهِمْ أَمْنًا يَعْبُدُونَنِي لا يُشْرِكُونَ بِي شَيْئًا وَمَن كَفَرَ بَعْدَ ذَلِكَ فَأُولَئِكَ هُمُ الْفَاسِقُونَ

Mwenyezi Mungu amewaahidi wale walioamini miongoni mwenu na wakatenda mema, ya kwamba atawafanya makhalifa katika ardhi kama alivyowafanya makhalifa wa kabla yao, na kwa yakini atawasimamishia Dini yao aliyowapendelea, na atawabadilishia amani baada ya khofu yao. Wawe wananiabudu Mimi, wala hawanishirikishi na chochote. Na watakaokufuru baada ya hayo, basi hao ndio mafasiki.

Aya iliyotangulia imetuonyesha kuwa alama ya imani ya kweli ni kuonyesha t'aa na utiifu mutlaki kwa Allah SW na Mtume wake. Aya hii ya 55 inasema: Matunda na tija ya kumtii Mwenyezi Mungu Mtukufu haitodhihirika na kuonekana huko Akhera tu bali hapa duniani pia itakuwa ni kuasisiwa mfumo safi na wa kiadilifu wa utawala ambao utaiokoa jamii na kila aina ya dhulma na machafuko na kuiletea amani na utulivu wa kweli. Hii ni ahadi ya Mwenyezi Mungu SW kwa waumini wake wema. Ahadi hiyo ambayo ilithibiti huko nyuma kwa umma zilizopita za watu wema itathibiti pia kwa kila umati wa watu wema na waumini wa kweli, na Yeye Allah SW atawatimizia ahadi yake, kwa kuwapa nguvu na mamlaka na kuwamakinisha katika ardhi. Kwa mujibu wa hadithi, kielelezo kilichokamilika cha aya hii ni utawala wa ulimwengu mzima wa Imam Mahdi (AS) katika akhiriz zaman. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba kushika hatamu za utawala kwa madhumuni ya kutandika mfumo wa tauhidi ulimwenguni, kuleta amani na kufuta na kuondosha madhihirisho ya ukafiri na shirki ndio ndoto na matarajio ya waumini, na Yeye Mola SW ametoa ahadi ya kuthibiti jambo hilo. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa dini haitenganiki na siasa, bali utawala na siasa vinatakiwa vifanye kazi ya kuilinda dini na waumini walioshikamana na dini. Kadhalika tunajielimisha kutokana na aya hii kuwa ushindi kamili wa waumini, kuasisiwa utawala wa ulimwengu mzima wa waja wema na kuporomoka mihimili ya nguvu za makafiri ni tukio la hakika na lisilo na chembe ya shaka ambalo kwa mujibu wa ahadi ya Allah SW litathibiti na kujiri katika siku za usoni za historia.

Wapenzi wasikilizaji, darsa yetu hii inahatimishwa na aya za 56 na 57 ambazo zinasema:

وَأَقِيمُوا الصَّلاةَ وَآتُوا الزَّكَاةَ وَأَطِيعُوا الرَّسُولَ لَعَلَّكُمْ تُرْحَمُونَ

Na simamisheni Sala, na toeni Zaka, na mt'iini Mtume, ili mpate kurehemewa.

لا تَحْسَبَنَّ الَّذِينَ كَفَرُوا مُعْجِزِينَ فِي الأَرْضِ وَمَأْوَاهُمُ النَّارُ وَلَبِئْسَ الْمَصِيرُ

Usiwadhanie waliokufuru kwamba watashinda katika nchi. Na makaazi yao ni Motoni, na hakika ni maovu kweli marejeo (yao).

Aya hizi zinaendelea kuzungumzia yale yaliyoashiriwa katika aya zilizotangulia na kutilia mkazo kwa mara nyingine tena utekelezaji wa maamrisho ya Allah na Mtume wake na kueleza kuwa kuimarisha mfungamano wao na Mwenyezi Mungu SW kwa njia ya Sala, kuamirisha mahusiano yao na wanyonge na wahitaji kwa njia ya utoaji Zaka, na kujenga uhusiano na kiongozi aliyetumwa na Allah kwa kufuata miongozo na maamrisho yake ni wajibu wa kila muumini wa kweli. Ni wazi kwamba ni kwa kulinda na kudumisha mahusiano haya ndipo fadhila na rehma za Mola kuhusiana na kuasisiwa na kuendelea kudumu utawala wa Kiislamu zitakapowashukia waumini. Na ni jambo lisilo na shaka kuwa kwa hatua hizo zinazochukuliwa na waumini, maadui wa Uislamu nao hawatokaa vivihivi na kukubali hatamu za utawala ziwatoke na kuingia mikononi mwa Waislamu. Kwa sababu hiyo aya zinaendelea kueleza kwamba wanayoyataka maadui hao hayatotimia mbele ya irada ya Allah SW na wala hawatoweza kuzuia kutimia taqdiri ya Mola ya ushindi kwa wafuasi wa haki. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba katika mtazamo wa Uislamu, masuala ya ibada za kiroho hayatenganishiki na yale ya kiuchumi, kisiasa, kiutawala na kijamii. Kadhalika aya hizi zinatuelimisha kuwa kadiri makafiri watakavyokuwa na nguvu na uwezo hila zao za kutaka kuuzuia Uislamu usienee duniani hazitofika popote, na iko siku Uislamu utatawala ulimwengu mzima. Kwa haya machache tunaifunga darsa yetu hii. Tunamwomba Allah aupe nguvu na izza Uislamu na Waislamu na awadhalilishe makafiri na wanafiki. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh.../

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)