Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumatatu, 26 Mei 2014 12:45

Sura ya An Nur, aya ya 48-52 (Darsa ya 616)

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu. Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa darsa ya Qur'ani. Hii ni darsa ya 616 na kwa sasa tunaizungumzia sura ya 24 ya An Nur. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 48, 49 na 50 ambazo zinasema:

وَإِذَا دُعُوا إِلَى اللَّهِ وَرَسُولِهِ لِيَحْكُمَ بَيْنَهُمْ إِذَا فَرِيقٌ مِّنْهُم مُّعْرِضُونَ

Na wanapoitwa kwa Mwenyezi Mungu na Mtume wake ili ahukumu baina yao, ndipo kundi moja miongoni mwao linajitenga.

وَإِن يَكُن لَّهُمُ الْحَقُّ يَأْتُوا إِلَيْهِ مُذْعِنِينَ

Na ikiwa haki ni yao, wanamjia kwa kut'ii.

أَفِي قُلُوبِهِم مَّرَضٌ أَمِ ارْتَابُوا أَمْ يَخَافُونَ أَن يَحِيفَ اللَّهُ عَلَيْهِمْ وَرَسُولُهُ بَلْ أُوْلَئِكَ هُمُ الظَّالِمُونَ

Je! Wana maradhi katika nyoyo zao, au wana shaka, au wanahofia kuwa Mwenyezi Mungu na Mtume wake watawadhulumu? Bali hao ndio madhaalimu.

Katika darsa iliyopita tulisoma aya zilizoashiria hatari ya kupenya unafiki ndani ya jamii ya Kiislamu. Aya hizi zinaashiria moja ya alama za kudhoofika imani ya mtu na kutingwa na maradhi ya unafiki na kueleza kwamba kila pale zinapotokea hitilafu baina ya watu wenye maradhi ya unafiki na Waislamu wengine, kama wao watakuwa wako kwenye haki hapo huikubali hukumu inayotolewa na Bwana Mtume SAW na kutii uamuzi wa mtukufu huyo. Lakini kama hukumu ya Bwana Mtume itakuwa na madhara kwao, hapo hugeuka wakakaidi kutii hukumu hiyo japokuwa wanajua kwamba anachofanya mtukufu huyo ni kubainisha hukumu ya Allah.

Leo hii pia kwa mtazamo wa watu wengi wanaojinasibu kuwa ni waumini, kipimo si haki na batili, bali ni maslahi yao binafsi au ya makundi yao ndicho kigezo cha kubainisha usahihi au kutokuwa sahihi matendo yao. Kila kitakachokuwa na manufaa kwao ndio haki na kila kitakachokuwa na madhara kwa upande wao, basi ni batili; na hilo haliafikiani na sifa ya mtu muumini na mwenye t'aa ya kweli. Kisha aya zinaendelea kwa kubainisha chanzo hasa cha tabia hiyo ya kuwa na nyuso mbili na kueleza kwamba, hulka ya ubinafsi na kupenda dunia, baadhi ya wakati hufikia hadi ya kumfanya mtu akipinge na kukikataa kila chenye madhara na yeye, hata kama itakuwa ni hukumu ya Mtume wa Allah. Wakati mwengine baadhi ya watu hufikia hadi ya kutokwa na haya na kuamua bila aibu kumnasibishia dhulma Mwenyezi Mungu na Mtume wake na kudhani kuwa kila kinachofuata matakwa, matashi na maslahi yao ndio haki na uadilifu. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba alama za imani ya kweli ni kutii maamrisho ya Allah na Mtume wake, hata kama maamrisho hayo hayatoafikiana na yatakinzana na matashi na matamanio yetu. Kadhalika tunajielimisha kutokana na aya hizi kuwa kuhukumu kwa uadilifu huwa hakuwafurahishi baadhi ya watu kiasi kwamba hata kama qadhi na hakimu huyo atakuwa ni Mtume na akahukumu kwa uadilifu kuna watu wataiona hukumu yake kuwa ni ya kionevu na hawatoikubali. Aidha aya hizi zinatutaka tuelewe kwamba ni dhulma kumtilia shaka na kumdhania vibaya Allah SW.

Tunaihatimisha darsa yetu hii kwa aya za 51 na 52 ambazo zinasema:

إِنَّمَا كَانَ قَوْلَ الْمُؤْمِنِينَ إِذَا دُعُوا إِلَى اللَّهِ وَرَسُولِهِ لِيَحْكُمَ بَيْنَهُمْ أَن يَقُولُوا سَمِعْنَا وَأَطَعْنَا وَأُولَئِكَ هُمُ الْمُفْلِحُونَ

Haiwi kauli ya Waumini wanapoitwa kwa Mwenyezi Mungu na Mtume wake ili ahukumu baina yao, ila ni kusema: Tumesikia, na tumet'ii! Na hao ndio wenye kufaulu.

وَمَن يُطِعِ اللَّهَ وَرَسُولَهُ وَيَخْشَ اللَّهَ وَيَتَّقْهِ فَأُولَئِكَ هُمُ الْفَائِزُونَ

Na wenye kumt'ii Mwenyezi Mungu na Mtume wake, na wakamwogopa Mwenyezi Mungu na wakamcha, basi hao ndio wenye kufuzu.

Katika aya zilizotangulia tumeona mwenendo mbaya wa watu wanaojidai kuwa ni waumini lakini namna wanavyosimama kukabiliana na hukumu ya Allah na Mtume wake na vipi yale yao yasiyo ya haki wanavyoyadhania kuwa ndio haki na kumwona Bwana Mtume SAW kuwa ni mwenye kuwanyima haki yao. Lakini kinyume na watu hao ambao ni waumini wa maneno matupu, aya hizi tulizosoma zinawataja waumini na wafuasi wa kweli wa Bwana Mtume na kueleza kwamba muumini wa kweli ni yule ambaye anaikubali hukumu ya mtukufu huyo kwa maneno na anayatii yale aliyomwamuru kivitendo. Hapingi wala hakhalifu kwa ulimi wake na wala hazembei na kusuasua katika utendaji wake. Ni wazi kwamba kuwa na moyo na imani kama hiyo kunapatikana chini ya kivuli cha taqwa na kuhofu mtu kuasi amri ya Allah SW na kwa njia hiyo kuweza kufikia saada na uokovu. Kwa kuwa baadhi ya waumini japokuwa wanatii amri za Allah, lakini wanafanya hivyo kwa kulazimika tu na bila ya kupenda, aya zinaendelea kueleza kwamba ikiwa utiifu wa mja kwa amri za Mola utafanyika huku moyo wa mja huyo ukiwa na hofu na t'aa ya kweli kwa Mola Muumba, hilo litamfanya aifaulu na kuishinda mitihani migumu ya maisha na kupata saada ya duniani na Akhera. Kwa mujibu wa hadithi, Imam Ali (AS) ambaye daima alikuwa mtiifu kwa maamrisho ya Allah na Mtume wake ni miongoni mwa misdaqi na mifano halisi ya wakusudiwa wa aya hizi, ambaye alifuzu na kupata saada kubwa. Miongoni mwa mafunzo ya kuzingatiwa katika aya hizi ni kwamba saada na uokovu unapatikana chini ya kivuli cha utiifu kwa maamrisho ya Allah SW. Kwa kupima kiwango cha utiifu wetu kwa maamrisho ya Mwenyezi Mungu Mtukufu na Mtume wake ndipo tutakapoweza kujua ukubwa wa imani zetu. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa suala muhimu kwa mja muumini ni kutimiza wajibu wake, iwe kufanya hivyo ni kwa manufaa yake au kwa madhara yake. Na pia tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba hali ya haya na hisia ya aibu anayokuwa nayo mtu ndani ya nafsi yake pamoja na hofu ya kuasi na kukhalifu amri ya Mola humlinda na matukio na mitihani mbalimbali ya maisha na kumfikisha kwenye ghaya na lengo kuu la  kupata saada ya duniani na Akhera. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 616 ya Qur'ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah atujaalie kuwa miongoni mwa waumini wa kweli ambao imani zao zinathibitishwa na matendo yao. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh.../

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)